Na Ezekiel Kamwaga
MWAKA jana, marais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Xi Jin Ping wa China walifanya mabadiliko katika mabaraza yao ya mawaziri na kuwapa nafasi wanasiasa wawili ambao ndiyo wasaidizi wao wakuu kwenye masuala ya diplomasia na uhusiano wa kimataifa.
Julai mwaka 2023, Rais Xi alimteua mwanadiplomasia mbobezi, Wang Yi, kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo. Miezi miwili baadaye, Rais Samia akamteua January Makamba kushika nafasi hiyohiyo kwa upande wa Tanzania.
Wawili hawa wanapishana kiumri kwa takribani miaka 20 January akiwa na umri wa miaka 50 wakati mwenzake huyo akiwa na umri wa miaka 70. Pia, ingawa hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa mbunge huyo wa Bumbuli kushika wadhifa huo, hii ilikuwa mara ya pili kwa Wang kupewa wadhifa huo.
Kuna mengi yanayowafananisha wawili hawa. Wote walianza ajira zao serikalini kupitia wizara ya mambo ya nje ya nchi zao. Wote wamepata elimu yao ya juu kupitia vyuo vikuu vilivyoko nchini Marekani – Wang Yi akisomea Chuo Kikuu cha Georgetown wakati January akisoma kwenye Chuo Kikuu cha George Mason na wote wamepata kuongoza idara za Uhusiano wa Kimataifa kwenye vyama vyao vya siasa, CCM kwa January na CCP kwa Yi.
Wang anachukuliwa kuwa mmoja wa wanadiplomasia wabobezi duniani hivi sasa. Kwa umahiri, huwa anawekwa kwenye kundi moja na Sergei Lavrov wa Russia. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, yeye ndiye amekuwa taswira ya China mpya inayofuata mwelekeo wa Rais XI.
Katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari mara baada ya kuteuliwa na Xi kwa mara ya kwanza, Yi aliweka wazi mambo makubwa mawili ambayo angependa kuona yanatokea wakati yeye akiwa Waziri wa wizara hiyo. La kwanza ni kuhakikisha sauti ya China inasikilizwa na kuheshimiwa duniani na pili ni kuona mapendekezo ya China kuhusu mwenendo dunia yakisikilizwa pia.
Kwa kufanya hivyo, alieleza Yi wakati ule, China ingefuata mwongozo alioupa jina la “Two Guidances”. Kwamba mosi, China ingehakikisha mfumo wa uendeshaji wa dunia (The World Order) unakuwa wa haki na sawa na pili usalama wa dunia unatunzwa kwa malengo yanayofanana kidunia.
Akasema matarajio yake ni kuona China inakuwa kiongozi wa dunia kwenye mambo hayo mawili. Katika kipindi chake hiki, tumeshuhudia China ikiwa na msimamo tofauti na mataifa ya Magharibi katika masuala tofauti ikiwemo matumizi ya nishati mbadala, vita vya Ukraine na Gaza na kuongoza kufanyika mabadiliko kwenye mfumo wa uendeshaji mambo ndani ya Umoja wa Mataifa.
Tangu awe Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January ameonyesha pia kupitia maelekezo ya Rais Samia, sauti ya Tanzania kwanza itasikika na pili itatoa uongozi kwa dunia kwenye masuala kadhaa.
Hakuna mfano mzuri wa mwenendo huu wa Tanzania kama suala la nishati safi. Wiki moja tu iliyopita, suala la matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kuokoa mazingira na maisha ya watu ambalo lilianzia Tanzania, lilikuwa ajenda kuu kwenye mkutano uliofanyika Paris, Ufaransa, ambako Samia alikuwa mwenyekiti mwenza wa mkutano huo.
Kwenye duru za kidiplomasia, huo ulikuwa ushindi mkubwa kwa taifa kama Tanzania kupata kwanza kuwa na ajenda duniani ambayo championi wake ni Rais wake na pia kupata fursa ya kusikilizwa. Haijalishi mkutano wa aina hiyo umefanyikia wapi lakini kidiplomasia, malengo makuu mawili; kusikika na kuongoza kwa Tanzania, yalifikiwa.
January pia, kwenye mikutano tofauti ya kidunia, kuanzia Copenhagen, Delhi na kwingineko, amekuwa akisisitiza mabadiliko ya mfumo wa dunia ulio wa haki na unaofanya kazi kwa mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea.
January uso kwa uso na Wang
Nilikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakisubiri kwa hamu nini kitatoea wakati wawili hawa watakapokutana kikazi kwa mara ya kwanza. Kwa bahati nzuri, nilipata bahati ya kuwa Beijing, China, wakati wawili hao walipokutana kwa mara ya kwanza.
Wang alifika katika eneo la mkutano wake takribani dakika 16 kabla ya mkutano wao. January aliwasili dakika chache kabla akitokea kwenye mkutano mwingine na Rais wa Benki ya EXIM nchini China. Lakini hawakukutana moja kwa moja kwa sababu ilipangwa wakutane saa tano kamili kwa saa za China.
Wang alipofika kwanza alikutana na maofisa wa China waliokuwepo kwenye eneo la mkutano na walikuwa wakipitia kwa pamoja ratiba ya mazungumzo ya siku hiyo. Katika wakati huohuo, January naye alikuwa amenyamaza kimya akipitia nyaraka za mazungumzo yake katika chumba cha kusubiria akiwa na ujumbe wake.
Ilipotimu saa tano kamili, wawili hawa walikutanishwa na kusalimiana kwa bashasha – kwa kushikana mikono. Baada ya dakika mbili za kupiga picha, wote waliingia katika eneo lililoandaliwa kwa ajili ya mkutano wao.
Wang alifungua mazungumzo kwa kueleza historia fupi ya Tanzania. Kipekee kabisa alizungumzia kuanza kwa uhusiano wa nchi hizo mbili miaka 60 iliyopita, mchango wa Tanzania kwenye kurejesha heshima ya China kimataifa kupitia kurejeshewa kiti chake UN na ujenzi wa reli ya TAZARA.
Ingawa anazungumza kwa ufasaha lugha za Kijapani na Kiingereza, Wang alizungumza kwa Kichina karibu muda wote huku mkalimani akifanya kazi yake. Nilibaini vitu kadhaa kwenye mazungumzo yake.
Mosi, alizungumza huku muda wote macho yake akiwa kayaelekeza kwa January na aliyabadili wakati akisoma alichoandika kwenye karatasi zake. Na alikuwa akizungumza taratibu na kwa msisitizo.
Pili, ni wakati January akiwa anazungumza. Wang alikuwa akitoa ishara za mikono, kutikisa kichwa na mwili kila alipokuwa akikubaliana na kinachosemwa na mwenzake huyo. Ilikuwa rahisi kujua iwapo amefurahishwa au hajafurahishwa na kilichokuwa kinasemwa na mwenzake. Na kwa ujumla, alionekana kufurahia muda wote.
Somo lilikuwa kwamba kwenye mazungumzo ya namna ile, ni muhimu kwa mwenzako kujua kwamba uko naye kwenye mazungumzo yenu. Na kwa sababu anakijua Kiingereza, alikuwa akionyesha mtazamo wake hata kabla mkalimani hajafanya kazi ya ukalimani.
Lingine la muhimu ni uwezo wa kujibu hoja zilizoibuliwa hapo hapo kwenye mkutano. January, pamoja na kueleza msimamo wa Tanzania kuhusu China, alizungumzia pia kuhusu hali ya Chuo cha Diplomasia cha Dkt. Salim Ahmed Salim na namna alivyotaka China na Tanzania zishikiriane kukiongezea hadhi na mwonekane wake. Wang alijibu palepale kuwa taifa lake liko tayari.
Jambo la tatu lilikuwa ni namna Wang alivyozungumzia suala la mvua za mafuriko zilizotokea Tanzania na namna zilivyowagusa. Alisema China itatoa mchango mdogo tu wa dola 500,000 (zaidi ya shilingi bilioni 1.3) kwa ajili ya kusaidia waathirika wake. Ilibidi January azungumze mwishoni kwa kusema kwamba ingawa muda wake wa kuzungumza ulikuwa umepita, kwa mila na desturi za Tanzania, asingeweza kuacha kushukuru kwa msaada huo wa watu wa China.
Katika muda wote wa mazungumzo yao yaliyochukua zaidi ya saa moja, si January wala Wang aliyegusa kikombe cha maji wala biskuti na keki zilizokuwa mezani kwao. Wote walikuwa wakitazamana na kuzungumza bila kukwepesha macho au kuondoka ndani ya notes walizokuwa wameandaa.
Mwishoni, wawili hao walirejea katika ajenda iliyo moyoni mwao ambayo ni kutengeneza mwongozo mpya wa kuendesha dunia. Kupitia kile kinachoitwa Dar es Salaam Consensus, ambao ni mwongozo ulioandaliwa na wasomi wa Afrika na China kuhusu kujenga mfumo mpya wa dunia usiobagua mataifa masikini, wawili hao walikubaliana kuwa chou cha Dk. Salim kinaweza kuwa taasisi kinara ya kusimamia utekelezaji wake.
Wang alimaliza mkutano kwa kutoa mwaliko kwa Rais Samia kuhudhuria mkutano wa Afrika na China wa FOCAC uliopangwa kufanyika Septemba mwaka huu. Lakini kwa msisitizo, akamwambia January akiweza aende mapema kabla ya Rais ili wapate muda wa kuzungumza mawili matatu.
Mkutano wa January na Wang ulikuwa darasa zuri la saa tatu kwenye masuala ya diplomasia na uhusiano wa kimataifa.