Ya kina Mwalimu, ‘Jibwa Kubwa’ na ‘Top Pen’

Picha: Chen Boda, aliyepata kuwa “Top Pen” wa Chama cha Kikomunisti cha China. Picha kwa hisani ya Memoires de Guerre

 

Na Ahmed Rajab

 

SI kwamba najaribu kujipendekeza kwa muasisi na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Dunia ambaye siku hizi amejipa lakabu ya ‘Top Pen’. Lakini nataka kuyaanza makala haya kwa kusema kwamba kati ya lakabu ambazo Ezekiel Kamwaga amejipa hii ya ‘Top Pen’ ndiyo yenye kumsibu.

 

Kabla ya kuitumia lakabu hiyo Kamwaga alijibandika lakabu mbili nyingine ninazozikumbuka: ‘The Sunak’ na baadaye ‘The Wolf’.

 

Amenambia mwenyewe kwamba aliipachika lakabu ya Sunak katika majina yake baada ya Rishi Sunak kuibuka kuwa waziri mkuu wa Uingereza. Tukio hilo lilimsisimua sana kwa sababu hakufikiria kwamba angeweza kumuona mtu mwenye asili ya Kihindi kuwa waziri mkuu wa Uingereza katika uhai wake na zaidi kwamba alikuwa Uingereza wakati tukio hilo la kihistoria lilipotokea.

 

Kwa hivyo, ni wazi kwamba zilikuwa jazba za kumuona asiye mzungu, kama yeye, akiiongoza Uingereza na hayakuwa mazingatio ya kiitikadi yaliyomfanya amkumbatie hivyo Sunak.  Tukio hilo lilimhamasisha kwa sababu lilipotokea ndipo alipozidi kutanabahi kwamba katika dunia ya leo, na katika nchi zenye mifumo ya demokrasia licha ya mapungufu yao, mtu anaweza akapanda ngazi katika jamii bila ya kuzuiwa au kurudishwa nyuma na rangi ya ngozi yake.

 

Mfano mwingine kabla ya Sunak ni wa Barack Hussein Obama, aliyechaguliwa Rais wa 44 wa Marekani mwaka 2009 na kwa mara ya pili miaka mine baadaye.  Obama, ambaye baba yake alikuwa Mwafrika aliyehamia Marekani kutoka Kenya, alifanikiwa kuwa katika kilele cha uongozi wa nchi ambayo tangu iasisiwe Julai 4, 1776, ilikuwa, na mpaka leo iko, chini ya udhibiti wa Wamarekani wenye asili ya kizungu.

 

Ama ile lakabu ya ‘The Wolf’ (yenye maana ya Mbwa wa Mwitu) Mhariri wetu anasema alipewa zamani na sahibu yake mmoja baada ya kusoma kitabu kimoja kuhusu unyama wa majambazi wa mafia. Kitabu hicho kinamtaja mtu aitwaye Ezekiel ‘The Wolf’ Rubirosa.

 

Kubandikwa lakabu na watu ni jambo ambalo binafsi lilinikuta tangu utotoni.  Nadhani ni majaaliwa ya wengi wenye mijuso ya duara.  Lakabu hizo hazikuniganda kwa sababu sikukasirika.  Nina hakika kwamba lau ningekasirika ningefanyiwa tashititi na lakabu hizo zingeniganda.

 

Nilipokuwa skuli wanafunzi wenzangu wakiniita ‘China’ na wapo ambao hadi leo wanaona raha kuniita hivyo.  Lakabu nyingine ya ‘Baby Mao’ niliitwa na Frene Ginwala, kabla hakuwa spika wa kwanza wa bunge la Afrika Kusini baada ya kuanguka kwa utawala wa makaburu.

 

Lakabu ya tatu ya ‘Sukarno’ alinibandika mtangazaji mwenzangu wa BBC Zeyana Seif. Alikuwa akinifananisha na Ahmed Sukarno, aliyekuwa Rais wa mwanzo wa Indonesia na lakabu yane ‘Chu Teh’ (au kwa tahajia, yaani maandishi, ya kisiku hizi Zhu De) ni jina ambalo kiongozi mmoja wa kihistoria wa Zanzibar Komredi Ali Sultan Issa akipenda kuniita kila alipokuwa akiona raha kunichokoza.

 

Zhu De aliyewahi kuwa Amiri Jeshi wa majeshi ya China alianza kushirikiana na Mao Zedong tangu 1928.

 

Waswahili tunapenda kutaniana kwa kuitana majina ya kuchekesha.  Tabia hiyo imekuwa sehemu ya utamaduni wetu licha ya kuwa kuna Hadithi kadhaa za matamshi ya Mtume Muhammad (SAW) zenye kuwakataza Waislamu wasiitane majina yenye kuwakebehi wenzao.

 

Hata kwenye Qur’ani kuna aya nzima isemayo: ‘Na msitukanane na msiitane majina mabaya.’  Uswahilini lakini ile tabia ya kuchekana, na hata ya kujicheka, hupindukia mipaka na kuchukua sura isiyopendeza.

 

Tabia ya watu wenyewe kujibandika majina ya bandia ni tabia waliyoizoea sana washairi wa Uswahilini.  Katika utamaduni wa Kifaransa majina kama hayo wanayojibandika waandishi huitwa ‘nom de plume’ (jina la kalamu).  Mara nyingi jina halisi la mwandishi huwa halijulikani, mara nyingine hujulikana, ingawa au angalau na wachache.

 

‘Jina la kalamu’ ni tafauti na ‘jina la vitani’ (nom de guerre) kama lile la ‘Tatu’ ambalo mwanamapinduzi wa Cuba Che Guevara alijibandika alipokuwa katika medani ya mapigano Zaire wakati wa enzi za dikteta Mobutu Sese Seko.

 

Katika medani ya siasa tumewaona wanasiasa wengi wa kimataifa wakibandikwa majina yasiyo yao na mahasimu zao.  Uingereza, kwa mfano, waziri mkuu wa zamani Boris Johnson alifupishiwa jina lake na kuitwa kwa utani ‘BoJo’ na wasiompenda kabisa wakimwita Boris ‘Big Dog’ Johnson (yaani Boris ‘Jibwa Kubwa’ Johnson).

 

Barani Afrika, wananchi wa nchi kadhaa wakiwaita viongozi wao majina ya kuwaenzi kama, kwa mfano, Dr Kwame Nkrumah, Rais wa kwanza wa Ghana, aliyekuwa  akiitwa Osagyefo yaani ‘mwokozi’.  Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania, akiitwa Mwalimu, kiongozi wa upinzani Seif Sharif Hamadi akiitwa Maalim na mwanasiasa wa zamani wa Zanzibar, Sheikh Ali Muhsin Barwani, aliyekuwa mmoja wa wakuu wa chama cha Zanzibar Nationalist Party (Hizbu) akiitwa ‘Zaim’ (yaani Kiongozi, kwa Kiarabu).

Na kuna baadhi ya viongozi wa siasa katika nchi mbali mbali waliojipachika majina yenye kuwasifu.

 

Bila ya shaka kila mtu ana haki na uhuru wa kujiita atakavyo au kukataa kuitwa kwa jina alilopewa alipozaliwa.  Mfano mzuri ni wa Malcolm Little, aliyelikana jina hilo alilopewa alipozaliwa na badala yake akachagua lile la Malcolm X.  Baadaye, baada ya kwenda Makkah na kutimiza nguzo ya tano ya Uislamu ya kufanya hijja alitaka aitwe el-Hajj Malik el-Shabbaz.

 

Lakabu ya ‘Top Pen’ unaweza kuifasiri kwa Kiswahili kuwa ‘Kalamu ya Juu’ au ‘Kalamu Adhimu’ lakini miye naona tafsiri ifaayo ni ‘Kalamu ya Upeo’.  Huo ni upeo wa fikra, umahiri, mantiki na ufasaha.  Ni kalamu ambayo pia ina macho mawili: ya uchunguzi na uchambuzi.  Ina uchu wa kutafiti kwa ujasiri na ari ya kuchambua kwa kina yale yanayojiri katika jamii.

 

Bila ya shaka sisi wasomaji wa hiyo kalamu tuna haki ya kutafautiana nayo. Si lazima tuukubali uchambuzi wake.  Lakini kalamu hiyo itakuwa imetimiza wajibu mkubwa endapo angalau itatufanya tuyatafakari maandishi yake.

 

Sidhani kama kwa kutumia lakabu ya ‘Top Pen’ Kamwaga amekuwa akijikweza.  Nafikiri anajaribu kumuigiza mtu wa mwanzo aliyejipa lakabu hiyo.  Naye ni Chen Boda aliyekuwa kigogo wa Chama cha Kikomunisti cha China wakati wa enzi za Mwenyekiti Mao Zedong.

 

Chen alikuwa mwandishi habari, profesa na mwananadharia wa kisiasa. Katika miaka ishirini ya mwanzo tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China Chen Boda ndiye aliyekuwa akiaminiwa kuwa mfafanuzi mkuu wa “Fikra za Mao”, yaani Umao.  Alikuwa mshiriki mkubwa wa Mao katika miaka ya mwisho ya mwongo wa 1930 akiwa mwandishi wa hotuba za Mao pamoja na makala ya kinadharia.  Naye ndiye aliyekuwa akiongoza propaganda za Wakomunisti wa China.

 

Yale yaitwayo ‘Mapinduzi ya Kitamaduni’ yalipoanza China mwaka 1966, Mao alimteua Chen awe Mwenyekiti wa Kundi la Mapinduzi hayo na akampa dhamana ya kuongoza vuguvugu hilo la kimapinduzi.

 

Chen na mke wa Mao, Jiang Qing, ndio waliokuwa wakiiongoza propaganda nzima ya serikali ya Kikomunisti ya China.  Lakini heshima yake ilianza kuporomoka pale yeye na wenzake wa Kundi la Mapinduzi ya Kitamaduni walipoanza kufuata siasa kali za mrengo wa kushoto.

Baada ya kufifia kwa Mapinduzi ya Kitamaduni, serikali iliyokuwa madarakani kufuatia kifo cha Mao ilimpandisha Chen kizimbani kwa mashitaka ya kushirikiana na lile lililokuwa likiitwa ‘Kundi la Wane.’ Alihukumiwa kifungo cha miaka 18 jela, lakini kwa sababu ya ugonjwa aliachiwa muda mfupi baadaye.  Alifariki Septemba 1989, akiwa na umri wa miaka 85.

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; X:@ahmedrajab

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.