Lamata: Taa ya Tamthilia za Nyumbani

Na Ezekiel Kamwaga

MWAKA 2017 alijitambulisha kupitia tamthilia ya Kapuni iliyorushwa na kituo cha DSTV. Tangu wakati huo, Leah Richard Mwendamseke, amekuwa akifyatua tamthilia ambazo zimekuwa sehemu ya maisha ya Watanzania – sasa akitamba na ile ya Jua Kali.

Kwa wengi, Mwendamseke ni alama ya tamthilia za Kitanzania na safari yake haikuwa rahisi. Yeye ni mwongozaji wa tamthilia katika tasnia ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikitawaliwa na wanaume. Kufika hapa tulipo, ambapo mchango wa sekta ya sanaa na burudani umeanza kuonekana hata katika bajeti ya serikali, Lamata kafanya kazi kubwa. Huu ni mwaka mwingine ambao Leah amezidi kujidhihiri kama mwongozaji bora zaidi nchini.