Rais Macky Sall wa Senegal akiwatembeza Rais mteule wa Senegal, Diomaye Faye (kushoto kwake) na Ousmane Sonko (kulia kwake) kwenye Ikulu ya Dakar hivi karibuni. Picha kutoka mtandao wa Quest France.
Na Zitto Kabwe
Mtandao wa Viongozi wa Upinzani katika Bara la Afrika (Pan African Opposition Leaders Solidarity Network) umepoteza wanachama wake wawili wiki iliyopita baada ya uchaguzi nchini Senegal. Wanachama hao ni Kiongozi wa Chama cha Wazalendo wa Senegal (PASTEF) Ousman Sonko na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bassirou Diomaye Faye, ambao sasa wamekuwa viongozi wa taifa lao.
Wananchi wa Senegal walijitokeza kwa wingi tarehe 25 Machi 2024 kupiga kura ya mabadiliko ya kisiasa katika nchi yao na kumchagua Faye kuwa rais katika duru la kwanza la uchaguzi. Hakuna mgombea yeyote wa kutoka upinzani aliyewahi kushinda uchaguzi nchini humo katika duru la kwanza. Mwaka 2000, Abdoulaye Wade alimshinda Rais Abdou Diof katika duru la pili na vilevile Rais anayeondoka madarakani, Macky Sall alimshinda Rais Wade mwaka 2012 katika duru la pili.
Mtandao wetu wa viongozi wa upinzani uliundwa mahususi kushughulikia masuala ya viongozi wa upinzani ambao wanapata changamoto za kisiasa zinazowazuia kufanya shughuli zao ikiwemo kufungwa jela kwa makosa ya kubambikizwa.
Kesi ya kwanza ambayo tulianza kushughulika nayo ni kesi ya Ousman Sonko aliyefungwa huko Senegal na baadaye Bassirou Diomaye Faye ambaye pia aliswekwa jela. Tuliendesha kampeni ya kutaka wawili hao waachiliwe huru ili waweze kuendesha chama chao cha PASTEF kwa uhuru na kushiriki uchaguzi.
Kabla sijaendelea na aya zinazofuata ni vema nieleze kuwa pamoja na suala la Sonko na Faye, mtandao wetu pia hivi sasa unashughulika na kesi za wanasiasa wengine wawili. Mmoja ni mwanamama Reckya Madougou ambaye alikuwa mgombea urais wa chama cha upinzani nchini Benin mwaka 2020. Reckya alibambikiwa kesi ya ugaidi na hivi sasa anatumikia kifungo cha miaka 20 jela.
Chama chake cha Les Democrats ndiyo chama kikubwa zaidi cha upinzani nchini Benin ambapo Rais Patrice Talon anakihofia sana katika mkakati wake wake wa kutaka kubadili katiba na kugombea muhula wa tatu. Mtandao wetu unaendelea na kampeni ya kutaka Reckya aachiliwe huru na ashiriki katika siasa za nchi yake bila bugudha.
Suala lingine tunashughulika nalo ni suala la Burundi ambapo kiongozi wa upinzani nchini humo, Agathon Rwasa, ameporwa chama chake kwa mara ya pili sasa. Mtandao wetu unapaza sauti kuhakikisha kuwa Rwasa anapata haki ya kuongoza chama chake ambacho ndiyo chama kikuu cha upinzani nchini Burundi kikiwa na karibu theluthi ya wabunge katika Bunge la nchi hiyo.
Chama cha PASTEF pia kilifutwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Senegal mwezi Novemba mwaka 2023. Ousman na Bassirou walitolewa jela siku kumi kabla ya uchaguzi na yaliyofuata ni historia. Kesho Bwana Diomaye Faye anakula kiapo rasmi kuwa Rais wa Senegal. Hatujajua bado Ousman Sonko atakuwa nani. Tutagusia kidogo katika makala haya.
Rais Bassirou Diomaye Faye alikuwa mgombea wa urais kuziba nafasi ya Sonko. Serikali ya Rais Sall iliona kuwa njia bora ya kumzuia Sinko kugombea urais ni kumfungulia mashtaka na kisha kumfunga jela. Sonko na chama chake walifahamu mpango huo na kuamua kuwa na mgombea mbadala.
Hivyo dakika chache baada ya Sonko kuhukumiwa jela kwa makosa yanayomzuia kuwa mgombea urais, walitoa video iliyorekodiwa siku 40 kabla ambayo iliyomwonyesha Sonko akitoa maelekezo kwa wananchi wa Senegal kuwa ikitokea amezuiwa kugombea urais basi wamwunge mkono Faye.
Alitamka maneno “Diomaye mooy Sonko” “Sonko mooy Diomaye” kwa lugha ya Wolof ambayo ndio lugha inayozungumzwa zaidi nchini Senegal. Maneno hayo yalikuwa na maana kuwa Diomaye ni Sonko na Sonko ni Diomaye.
Niliingia Jijini Dakar siku ya uchaguzi. Hali ya mji wa Dakar ulikuwa shwari kabisa. Wenzangu katika msafara walifika siku moja kabla na hivyo waliweza kushiriki zoezi la kutazama wananchi walivyopanga mstari na kupiga kura na hatimaye matokeo kutangazwa katika vituo vya kupigia kura.
Kama ilivyo hapa nchini, matokeo ya uchaguzi hutangazwa kwenye vituo vya kupigia kura mara baada ya kura kuhesabiwa na kisha jumla ya kura kupelekwa kwenye majumuisho. Baada ya kuungana na wenzangu tulizunguka mitaa ya Dakar jioni mara baada ya kupata futari katika hoteli niliyofikia ya Radison Blu pembezoni mwa Bahari ya Atlantiki. Mji ulikuwa umetulia lakini ilipofika saa tatu usiku mji ulilipuka kwa nderemo. Matokeo ya awali yalikuwa yameshaonyesha ushindi wa dhahiri wa kijana wa miaka 44 Diomaye Faye.
Ilikuwa ni kama Senegal imeshinda mashindano ya ubingwa wa Afrika. Mitaa ilijaa bodaboda zikiwa na bendera ya Taifa la Senegal (sio bendera za vyama vya siasa). Vijana waliendesha boda na magari kwa kasi katika barabara kuu. Televisheni zilikuwa zinaonyesha matokeo kutoka vituoni moja kwa moja na kufanya majumuisho. Baadhi ya wagombea wa urais walianza kutoa pongezi kwa Bassirou Diomaye Faye kwenye mitandao yao kama X na Instagram kwa ushindi. Ilikuwa ni sherehe kubwa na furaha zisizo na kifani.
Siku ya pili ilipofika mchana tayari aliyekuwa mgombea wa chama tawala na Rais anayemaliza muda wake Macky Sall walishakubali matokeo. Ilikuwa ni mapinduzi ya raia dhidi ya “status quo”.
Jioni ya siku hii tulikutana na rais mteule alipokuja kuhutubia taifa katika moja ya kumbi za hoteli tuliyokuwa tumefikia. Tulipata nafasi fupi sana ya kusaliamiana naye. Alikuwa ametulia akionekana kuwa anatambua matumaini makubwa aliyobeba mabegani mwake. Hotuba yake iliwahakikishia wananchi mabadiliko lakini vilevile iliwahakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa Senegal wataendelea kuwa taifa nguzo katika Kanda ya ECOWAS na Umoja wa Afrika.
Kabla ya Faye kufika eneo la mkutano, nilipata nafasi ya kuzungumza na timu yake tukiwa tunapata futari. Ni timu ya vijana wadogo ambao huu ni uchaguzi wao wa mara ya kwanza. Walijawa na hasira ya mabadiliko. Mmoja wa kvjana niliyokutana nao aliniuliza kwanini sizungumzi lugha ya Wolof maana hakuwa anataka kuongea Kiingereza wala Kifaransa. Nikacheka nikamwambia Tanzania tunatumia lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo Wolof ya Tanzania hivyo naye ajifunze Kiswahili, Akacheka pia. Lakini hii ni ishara ya mabadiliko watu wa Senegal wanataka.
Faye ameahidi kufanya mageuzi makubwa ya mahusiano ya Senegal na Ufaransa kiuchumi. Nchi nane za Afrika Magharibi zinatumia sarafu moja iitwayo CFA Franc ambayo inalazimisha akiba yote ya fedha za kigeni ya nchi hizi iwekwe katika Benki Kuu ya Ufaransa. Hii ni moja ya alama ya ukoloni wa Ufaransa kwa nchi hii na kwamba nchi hizi hazina uhuru wa kiuchumi kwani haziwezi kutekeleza sera yeyote ya sarafu yake.
Sonko na Diomaye wamekuwa wakipambana kuondoa doa hili. Wachambuzi wengi wa mambo wanadhani kuwa baada ya kuingia madarakani uongozi mpya utaenda kwa tahadhari kubwa katika suala hili.
Rais Faye anaingia madarakani katika kipindi ambacho Senegal inakwenda kuingia katika nchi zinazozalisha mafuta na gesi duniani. Katika kampeni aliahidi kupitia upya mikataba ya mafuta na gesi. Mapato ya Fedha za kigeni kutoka Mafuta na Gesi yanaweza kuchochea ukuaji wa uchumi wa Senegal kiasi cha kuifanya kuwa nchi ya kwanza Afrika kwa kasi ya kukua uchumi ifikapo mwaka kesho, 2025.
Ni namna gani Rais Faye na kiongozi wake wa chama watashughulika na uwekezaji katika eneo hili ni jambo linasubiriwa kwa hamu na wafuatiliaji wa mambo na wananchi wa Senegal.
Changamoto mbili kubwa naziona zikimkabili Faye. Moja ni suala la ajira kwa vijana. Ni dhahiri vijana wa Senegal walichoka kuona mageuzi ya kiuchumi hayawanufaishi kwani gharama za maisha zimeongezeka na pia hakuna ajira kwa vijana wengi wanaoingia kwenye nguvu kazi ya taifa hilo. Kura kwa upinzani ilikuwa ni kura ya kuchoshwa. Ni vipi Rais mpya atakabaliana na hili ni suala linaumiza vichwa vya wengi.
Suala la pili ambalo linaweza kusaidia kutuliza hali katika la kwanza hapo juu ni nafasi ya Ousman Sonko katika serikali. Nilizungumza na waziri mmoja wa zamani wa Serikali ya Sall ambaye alijiondoa serikalini kupinga Rais wake kutaka muhula wa tatu. Katika mazungumzo yetu aliniambia kuwa Senegal ina mitume wawili – Ousman Sonko na Sadio Mane.
Kwamba hawa ni watu ambao wakiwaeleza wasenegali lolote wanafuata. Mahusiano ya Sonko na ‘kijana wake’ ambaye sasa amekuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama yatakuwaje? Wengi wanatarajia kuwa Sonko atakuwa Waziri Mkuu mwenye mamlaka makubwa ili aweze pia kutumika kuwatuliza vijana wakiona mambo yanachelewa.
Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa wawili hawa lazima watagombana au kugombanishwa. Wengine wanasema ukamaradi wao tangu wakiwa wafanyakazi wa mamlaka ya mapato ya nchi yao na wakiongoza chama cha wafanyakazi wa mamlaka ya mapato unadhitisha kuwa hawatagombana bali wataongoza taifa lao kwa pamoja. Muda ni jawabu.
Kwa sisi ndugu watazamaji kutoka nchi za Afrika Mashariki na hasa Tanzania, tunapaswa kuitazama Senegal kama mfano. Ushindi wa Faye unaweza kutumika kama chanzo cha hamasa kwa wanademokrasia na vyama vya upinzani nchini Tanzania, ukionyesha kwamba mabadiliko yanawezekana kupitia njia za amani na za kidemokrasia.
Hii inaweza kuchochea wito wa mageuzi ya kisiasa na kuheshimiwa kwa kanuni za kidemokrasia nchini Tanzania. Hata hivyo kuna mafunzo makubwa sana na haswa funzo la kuaminiana kama wana mageuzi. Bila kuaminiana vuguvugu la PASTEF lisingedumu tangu lianze mwaka 2014. Ousman Sonko kama kiongozi, licha ya kupata kiti kimoja tu bungeni katika uchaguzi wake wa kwanza wa wabunge, aliendelea kupambana na kujenga mahusiano na wana mageuzi wengine.
Vilevile Diomaye Faye, mwaka mmoja na nusu tu uliopita alishindwa kura ya udiwani katika kata ya nyumbani kwao, lakini wenzake waliendelea kumwamini kiasi cha kumweka kuwa mgombea Urais kuziba nafasi ya Sonko. Kama kuna jambo moja la kujifunza kutoka Senegal ni wana mageuzi kuaminiana.
Zitto Kabwe ni Kiongozi wa Chama (KC) mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo nchini Tanzania. Ana shahada ya kwanza ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na ya Uzamili aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Bucerus nchini Ujerumani.