Mtungaji: Mohammed Ghassani
Wachapishaji: Zaima Publishers
Uhakiki na Ahmed Rajab
KITABU hiki, kilichozinduliwa Oktoba 26, mwaka 2024 kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha SOAS, London, ni cha aina ya pekee. Hakina mfanowe katika fasihi ya Kiswahili — si ya kale, si ya kisasa. Ni vitabu viwili ndani ya kimoja. Kila kitabu kati yavyo kikiwa na uzito wake na nyuzi zenye kuviungaisha — kama si kwa maudhui yao basi kwa hisia zao au vichocheo vya hisia vinavyoyafanya maudhui yao yawe mamoja au yenye kuhusiana.
Kila kitabu kati ya hivyo viwili ni mkusanyiko. Cha kwanza, “Mbegu za Tikiti,” ni mkusanyiko wa mashairi — diwani yenye kuzungumzia mambo mengi lakini yote yakijikita juu ya suala pevu la Palestina. “Tikiti” la kwenye isimu ya sehemu hiyo, tikiti maji, linaashiria Palestina, kwa vile tunda hilo linanasibishwa na taifa hilo kama vile zao la karafuu linavyonasibishwa na taifa la Zanzibar.
Uhusiano wa tikiti na Palestina, kama nilivyogusia, ni wa kiashiria na unatia mizizi juu ya utambulisho wa kitamaduni na wa kisiasa wa Wapalestina. Tikiti maji, na hasa rangi zake — nyekundu, kijani, nyeupe na nyeusi –— zinashabihi rangi za bendera ya Palestina. Kwa sababu hiyo, tikiti maji limekuwa mithili ya nembo ya uzalendo wa Kipalestina na mapambano ya Wapalestina ya kujikomboa kutoka ukandamizwaji wa Israel.
Hayo hudhihiri zaidi pale bendera ya Palestina inapozuiwa au inapopigwa marufuku isipeperushwe na Wapalestina au na wenye kuwaunga mkono. Nyakati nyingine huwa ni alama mbadala za kitaifa za Wapalestina — na si bendera pekee — zinazozuiwa au kupigwa marufuku.
Nakumbuka katika miongo ya 1960 na 1970, wakati watawala wa Israel walipokuwa wakizidi kukandamiza uchapishwaji wa habari kuhusu Palestina na mapambano yao, aghalabu Wapalestina wakifanya ujanja kwa kutumia tikiti au tikiti maji kuashiria taifa lao la Palestina.
Matumizi hayo ya tikiti, badala ya bendera rasmi ya Wapalestina au alama nyingine za dhahiri za Wapalestina, yaliwapa taabu wakuu wa Israel waliokuwa na dhamana ya kudhibiti uchapishaji wa habari. Uhusiano baina ya tikiti na utambulisho wa Wapalestina umedumu tangu siku hizo. Hivi sasa, kwa Wapalestina, tikiti limekuwa ishara yenye nguvu ya kitamaduni.
Kuna wasanii wawili maarufu katika fasihi ya Wapalestina ambao hawakulitumia tikiti kuashiria Palestina katika maandishi yao, licha ya kwamba wameandika sana kuhusu maudhui ya utambulisho wao Wapalestina, mapambano na ukombozi. Nao ni mshairi Mahmoud Darwish na mwana riwaya Ghassan Kanafani.
Darwish aliyepata umaarufu mkubwa kwa tungo zake kuhusu hali za Wapalestina, uhamisho, au hasa ujiakazi, kufukuzwa kwa nguvu Wapalestina kutoka makwao na hamu yao ya kurudi, ametumia alama kadhaa nyingine kama vile mizaituni, ardhi na ndege lakini hakutumia tikiti.
Kanafani, aliyekuwa mwanahabari, mwana riwaya na mwandishi wa hadithi fupi, naye pia hakulitumia tikiti.
Tunda hilo limekuwa likitumiwa zaidi na washairi na waandishi wengine pamoja na wasanii wenye kujishughulisha na sanaa za kuona, kama vile uchoraji, uchongaji wa sanamu na upigaji picha.
Nitawataja wachache hapa.
Kulikuwako mchoraji wa vibonzo wa Kipalestina, Naji al-Ali, aliyejipatia umaarufu kwa “Handala,” mhusika mashuhuri aliyembuni kwenye vibonzo vyake. Al-Ali alikuwa akitumia taswira ya tikiti katika vibonzo kuashiria uzalendo wa Kipalestina na mapambano ya Wapalestina. Mithili na afanyavyo Mohammed Ghassani katika diwani yake ya “Mbegu Za Tikiti”, Al-Ali alikuwa akilitumia tikiti kuwasilisha ujumbe wa kisiasa.
Sliman Mansour, mchoraji maarufu wa Kipalestina, amelitumia tikiti kuashiria utambulisho wa Wapalestina. Tikiti kwake ni taswira ya kitamathali au tamathali ya kuona inayowakilisha bendera ya Palestina na mapambano ya ukombozi.
Kamal Boullata, mchoraji wa Kipalestina na mwanahistoria wa sanaa, naye pia amekuwa akilitumia tikiti katika kazi zake za sanaa zenye maudhui ya uhamisho, utambulisho na mapambano.
Mpiga picha Rania Matar, mwanamke aliyezaliwa Lebanon lakini mwenye asili ya Kipalestina, amelitumia sana tikiti katika picha alizozipiga zikionyesha maisha ya wanawake na watoto katika Mashariki ya Kati, uvumilivu wao na nguvu zao za kupambana na maisha magumu yanayopitia sulubu kubwa na mazongezonge. Matar amelitumia tikiti kama tamathali ya utambulisho wao wa kitamaduni.
Ni nadra kusoma diwani ya mashairi inayoukuna moyo wako kwa mkusanyiko wa tungo zake na, wakati huohuo, inayokufanya utafakari, kwa mapana na marefu, kwa mengine yaliyomo ndani ya diwani hiyo. Mfano mzuri ni haya mashairi yaliyomo katika sehemu ya mwanzo ya kitabu hiki iitwayo “Dafina ya Mkiwa.” Hii ni hazina kweli, ni hazina yenye utajiri na thamani kubwa. Inaweza kuwa ni hazina ya kimajazi ya shakhsiya — au ya nafsi — yake mwenyewe mkiwa. Katika shairi moja, ‘Sina Sinani’, huyo yatima Ghassani analalama:
“Sina fedha sina mali, sina mbele sina nyuma, Wallahi sina sinani
Si kauli si amali, si wa kheri si wa jema, hiulizwa siungami
Si wa moja si wa mbili, si wa kamba si wa chuma, si wa mimu si wa nuni
Sina kitu sina hali
Lakini nina asili
Dhuluma isokubali
Ingatendwa na Jabari, na mbabe wa dunia!”
Hicho ni kipande tu cha shairi zima lenye kusema mengi kuhusu ukakamavu wa mtungaji wa kuwa na asili ya kutokubali dhuluma.
Sehemu ya pili ya kitabu cha Ghassani, ambayo ni ndogo kwa ukubwa, haina pambo la umbo la tungo za Kiswahili. Ni mkusanyiko wa insha zilizoandikwa kwa lugha nyepesi lakini yenye kubeba mambo mazito au maudhui magumu. Ni nathari yenye kumbukumbu nyingi na maelezo yaliyokamilika anayoyaelekeza moyoni mwake.
Ghassani ni msimulizi mwerevu wa kumbukumbu – naziwe kumbukizi za Wapalestina na dhuluma walizofanyiwa au za taifa lake na harakati zake za kuurejesha utaifa wake au kumbukizi zake mwenyewe binafsi zinazoipumbaza nafsi yake, kama kwa mfano anavyokumbuka alivyolelewa na baba yake au anapozungumza na “wakati”.
Ladha na utamu wa kumbukumbu hizo zinamfanya msomaji ajihisi kana kwamba ameketi katika pembeya ya historia.
Kitabu hichi kimezidi kupaishwa kwa utangulizi mwanana na ulioshiba uchambuzi wa yaliyomo kitabuni. Utangulizi huo, ulioandikwa na msomi wa Kimarekani Nathalie Arnold Koenings, ni wa aina ya pekee. Umekihakiki kitabu kizima kiasi cha kuyafanya mate ya makala haya yakauke. Pasiwe na cha ziada cha kuongeza.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com/ X@ahmedrajab
Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.