Msuya: Waambieni wananchi ukweli

 

 WAZIRI Mkuu mstaafu, Cleopa David Msuya (92), ametoa siri ya namna ya kudumu madarakani na Watanzania pasipo migogoro; kuwaeleza ukweli.

Katika mazungumzo yake na Gazeti la Dunia, Msuya alisema jambo kubwa alilojifunza kwenye utumishi wake wa umma uliodumu kwa takribani nusu karne, ni kwamba kama watu wakiambiwa ukweli na kuelewa, viongozi hawatakuwa na kitu cha kuhofia.

“Nimejifunza sana kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Mwanzoni mwa miaka ya 1980, tulipitia wakati mgumu sana kiuchumi. Yeye aliita wazee hapa Dar es Salaam na kuwaeleza kwamba hali ni ngumu na tunatakiwa kufunga mikanda.

“Wananchi walimsikia Rais wao akisema hivyo na kwa kweli walimwona naye akiwa amefunga mkanda. Matokeo yake ni kwamba wananchi nao walifunga mikanda kweli kweli na tukapita katika wakati ule mgumu.

“Miaka ya 1980 ilikuwa migumu kwa nchi nyingi za Kiafrika kwa sababu ya masharti yaliyoanza kuwekwa kwetu na vyombo vya fedha vya kimataifa. Wengi wa viongozi katika nchi ambazo raia wake hawakuambiwa nini hasa kinaendelea, waliishia kuondolewa madarakani kwa kuuawa, kupinduliwa au kukimbia. Sisi ukweli wa Baba wa Taifa ulitusaidia,” alisema Msuya.

Msuya alizungumza na Gazeti la Dunia mwezi uliopita akiwa nyumbani kwake Upanga jijini Dar es Salaam na mazungumzo yake yote yatarushwa kupitia podcast ya The Ezekiel Kamwaga Show baadaye mwezi huu.

Msuya ni Mtanzania pekee hadi sasa kuwahi kuwa Waziri Mkuu chini ya marais wawili tofauti; Julius Nyerere na Ali Hassan Mwinyi, na katika mazungumzo yake hayo alikiri kwamba nafasi ya Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha ni nafasi ngumu kwa mtu yeyote anayekabidhiwa majukumu hayo.

Alisema Tanzania ni nchi kubwa; ikiwa na ukubwa sawa na nchi za Kenya, Uganda na Malawi zikiunganishwa kwa pamoja, na kwamba kazi ya kuwa kiongozi wa mawaziri kwenye kuongoza nchi kubwa namna hiyo na yenye changamoto tofauti si ndogo.

Msuya alikuwa akijibu swali la endapo kuwa kwake Waziri Mkuu – kama ilivyo kwa wanasiasa wengine wote waliowahi kushika wadhifa huo kwenye Serikali ya Tanzania, kilikuwa ni kikwazo kilichosababisha asiweze kuwa Rais wakati alipotaka kuwania nafasi hiyo mwaka 1995.

“Kwanza naamini nafasi ya Urais si nafasi ambayo kila mtu anaweza kuipata. Kuna sababu nyingi zinazosababisha mtu awe au asiwe Rais na si sababu moja tu kwamba labda uliwahi kuwa Waziri Mkuu au Waziri wa Fedha.

“Lakini ni kweli kwamba kama ukiwa Waziri Mkuu na ukatimiza majukumu yako vizuri, uwezekano wa wewe kupishana na mawaziri wenzako au wanasiasa wengine ni mkubwa kuliko ukiwa kwenye majukumu mengine.

“Sasa huwezi kutimiza majukumu uliyopewa na mkubwa wako huku kichwani ukiwaza unataka Urais. Unamwona Rais Samia? Nani alijua kwamba siku moja atakuja kuwa Rais wa Tanzania? Ushauri wangu kwa wanasiasa ni kwamba wao wafanye kazi. Kama Urais utakuja, uje tu,” alisema.

Katika mchakato wa kutafuta mgombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1995, Msuya aliingia katika tatu bora akiwa na Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete – na kumekuwa na maneno ya wachambuzi wengi kwamba ni kura za wafuasi wa Msuya ndizo zilimpa ushindi Mkapa dhidi ya Kikwete wakati huo.

“Mkapa alipigiwa kura na kushinda kwenye mchakato ule kwa sababu waliompigia kura waliona anafaa kupigiwa kura. Hakukuwa na suala la watu wa Msuya kuhamia kwa Mkapa. Hayo ni maneno ya watu tu”, alisema.

Katika mahojiano ya takribani saa nzima, Msuya alizungumzia pia suala la utoaji huduma muhimu kama afya na elimu, akisema kimsingi kinachotakiwa kufanywa si kutoa huduma hizo bure bali kuhakikisha kila mtu anachangia kwa kadri ya uwezo wake lakini wale wasio nacho pia wananufaika.

“Unajua kimsingi hakuna kitu kinaitwa elimu bure. Hii ni kwa sababu kuna gharama. Unaingia gharama kujenga majengo, kufundisha na kulipa watumishi, kununua vifaa vya kazi na mambo mengine. Hapo maana yake hakuna bure.

“Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba wenye uwezo wanalipia huduma na wasio na uwezo nao wanapata huduma kama kawaida hata kama hawana uwezo wa kuhudumia. Ndivyo inavyotakiwa kuwa,” alisema.

Picha kwa Hisani ya Gazeti la Mwananchi

Mwisho