Na Ezekiel Kamwaga
NAMBA zinazungumza kuliko maneno. Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, alimteua Gilead Teri, kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Wakati anapewa nafasi hiyo, wastani wa miradi ya uwekezaji iliyokuwa inarekodiwa na kituo hicho kwa miaka mitatu ya nyuma ilikuwa takribani 56. Katika mwaka wake wa kwanza tu, miradi imefika 158 – takribani mara tatu ya wastani wa miaka mitatu kabla yake.
Si Watanzania wengi walikuwa wanamfahamu Teri kabla ya majukumu yake mapya. Kimsingi, kitabia, kituo hicho kilikuwa kinaongozwa na watumishi waandamizi wa serikali waliolelewa na kukulia kwenye mifumo hiyo. Mifano mizuri zaidi ni Samuel Sitta na Emmanuel ole Naiko. Terri ni kijana mdogo ambaye hajafikisha hata miaka 40 lakini tayari ameanza kuonyesha tofauti na athari kubwa kwenye taasisi.
Nimezungumza naye mara kadhaa na unamuona kama mtu ambaye hajadhamiria kukaa na kuridhika na mafanikio. Tamaa yake ni kuona Tanzania inavutia miradi ya uwekezaji itakayobadili maisha ya wengi katika kipindi cha muda mfupi na wa kati.
Teri ni mfano mwingine kuwa Tanzania ina vijana wa kutosha wanaohitaji tu kupewa nafasi na kuonyesha vipaji na uwezo wao. Unaweza kuonyesha tofauti kwa kuongeza namba tu za miradi. Lakini kuongeza miradi mara tatu ya kawaida – katika mazingira ya kutoka kwenye COVID 19, Vita ya Ukraine na matatizo ya uchumi duniani, ni wazi kuwa Gilead Teri anafanya vitu vikubwa.