Siasa za ujenzi wa Ikulu

Maelezo ya picha: Mwonekano wa Ofisi mpya za Ikulu, Chamwino, Dodoma. Picha kwa hisani ya Ikulu.

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

WAKATI unapoingia kwenye eneo ilikojengwa Ikulu mpya ya Chamwino mkoani Dodoma, kuna vitu viwili unaviona haraka; kwanza ni ukubwa wa eneo husika – eneo lina ekari zaidi ya 8,000 na pili ni upekee wa jengo lenye ofisi hizo.

 

Majengo huwa yanazungumza lugha yake na linapokuja suala la mamlaka, ujenzi wa kitu chochote chenye uhusiano na utawala huwa na tabia zake. Profesa Maurice Amutabi aliandika katika andishi lake la mwaka 2016, Colonial Architecture and Urbanism in Africa; “Nyakati za ukoloni, watawala walikuwa wakihakikisha kuwa majengo yao yanakuwa makubwa zaidi na marefu zaidi kuliko ya wale wanaowatawala”.

 

Nikiwa kwenye tukio la uzinduzi wa Ikulu ya Chamwino juzi, nilimkumbuka Garth Myers na kitabu chake cha Verandahs of Power pale alipohoji kama kuna tofauti za kimamlaka kati ya utawala wakati wa ukoloni na utawala baada ya ukoloni. Hii ni kwa sababu, kama utaangalia vizuri, watawala waliofuata baada ya ukoloni, walikaa katika majengo na ofisi zilezile walizokuwa wakitumia wakoloni wakati wa ukoloni.

 

Mjadala wowote unaohusu ujenzi wa Ikulu ya Chamwino ni mjadala unaozungumzia tabia za mamlaka na wale walio madarakani. Katika historia ya Tanzania, Rais wa Awamu ya Tano, hayati John Magufuli, anaweza kuwa ndiye mwenye ushawishi zaidi kuhusu ujenzi wa Ikulu na namna ilivyo.

 

Sina shaka kwamba kama Rais wa Tanzania angekuwa ni kati ya Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete au Samia Suluhu Hassan, na wakafanya uamuzi wa kujenga Ikulu Chamwino, sidhani kama ingekuwa hii ambayo tumeiona sasa iliyojengwa kwa ushawishi na mawazo ya Magufuli.

 

Kitabia, Magufuli alikuwa mjenzi. Namna yake ya kufanya kazi na kuonyesha uwezo na nguvu yake ilikuwa kupitia ujenzi wa vitu. Baada ya kufanya uamuzi wa kuhamia Dodoma, ilikuwa lazima ajenge Ikulu mkoani humo na kama nilivyomnukuu Amutabi hapo awali; kwa wenye mamlaka, majengo yao ni lazima yawe makubwa na marefu kuliko mengine kwenye eneo husika.

 

Kuna hoja kwamba pengine Ikulu ya Dodoma ingekuwa na dizaini tofauti na ile iliyojengwa Dar es Salaam nyakati za ukoloni. Mawazo hayo yanafanana na Waghana wakati walipoamua kujenga Ikulu nyingine jijini Accra kutokana na kuihusisha Ikulu ya zamani ya Christianborg na ukoloni pamoja na biashara ya watumwa. Ikulu mpya ya sasa ya Ghana ina muundo wa stuli iliyokuwa inatumiwa na watawala wa kabila la Ashanti.

 

Hoja hii ina mashiko lakini kuna upande mwingine wa shilingi. Upande huo ni ukweli kwamba utawala una alama zake. Kwa miaka mingi, Watanzania na watu wengi duniani wamekuwa wakihusisha majengo ya Ikulu na taswira kama za Ikulu ya Dar es Salaam au White House ya Marekani. Vichwani mwa watu hao ni kwamba mamlaka inakaa kwenye majengo ya namna hiyo.

Suala hili la taswira lina mifano ya nchi nyingine pia. Wakati akiwa Rais wa Ivory Coast, Rais Felix Houphoeut Boigny aliamua kujenga Kanisa Katoliki kubwa katika eneo la Yamoussoukro nchini kwake. Mchoro na muundo wa kanisa hilo ulifanana na ule wa kanisa kubwa maarufu kwa jina la Basilica lililopo Vatican. Rais huyo ni kama alikuwa anawaambia watu kwamba hawahitaji kwenda Vatican kusali kwenye Basilica, bali wanaweza kufanya hivyo wakiwa kwao.

 

Kubadilisha mchoro na mwonekano kunaweza kufanya watu wakabaki na taswira ya Ikulu kuwa ni ile tu waliyoizoea na si nyingine mpya. Kwa jicho lingine, pengine hiyo ndiyo ilikuwa sababu kubwa ya kwa nini watawala wengi wa Afrika na Asia walikwenda kuishi na kufanya kazi katika ofisi zilezile walizokuwa wakifanyia kazi wakoloni. Hata kwenye makazi, watawala wapya walihamia kulekule walikokuwa wakiishi watawala waliowabadili.

 

Kama akina Nyerere, Kwame Nkrumah, Kenneth Kaunda na wengine wangeamua kwenda kufanya kazi kwenye ofisi nyingine tofauti na zile walizokuwa wakifanyia kazi Gavana na watumishi wengine, pengine wananchi wasingeona kuwa tuko huru. Kwa maana nyingine, tafsiri ya Uhuru, tafsiri ya mamlaka, ilijionyesha pia kwenye majengo.

 

Kama Rais Samia atapokea wageni wake akiwa Ikulu ya Chamwino au Magogoni, taswira itakayorushwa kwa wananchi itabaki kuwa ileile na hakuna itakayodogosha nyingine. Kwa watu wengine, hii inaweza isiwe na maana sana lakini kwa wanasiasa wa aina ya Magufuli, suala la ujenzi na uonyeshaji wa nguvu ya mamlaka vinakwenda namna moja.

 

Si Ikulu pekee

 

Ni muhimu kutazama ujenzi wa Ikulu ya Chamwino kwa kuangalia muktadha wa kisiasa wa Tanzania wakati wa utawala wa Rais Magufuli. Ni wakati huohuo ambapo nchi yetu imeanza ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Reli ya Mwendokasi, ununuzi wa ndege na ujenzi wa miundombinu mingine kama barabara na vivuko.

 

Ni kama vile Rais Magufuli alikuwa akitoa ujumbe kwamba Tanzania inajitawala na imeanza kufuata njia yake yenyewe kujitafutia maendeleo. Nakumbuka katika shughuli ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi, alizungumzia ukweli kwamba Ikulu ya Dodoma itajengwa na Watanzania wenyewe na kwamba alikataa msaada kutoka nchi za kigeni waliotaka kutoa msaada wa ujenzi.

 

Kwa Magufuli, ilikuwa aibu kwa Tanzania kujengewa Ikulu na wageni na ujenzi wa ofisi mpya kwake lilikuwa suala la uzalendo. Hii ni sababu inayofanya mjadala kuhusu thamani ya ujenzi huo kuwa mgumu kwa sababu uzalendo hauna bei. Zipo nyakati ambazo uzalendo wa Watanzania kwa nchi yao ulisababisha tuingie vitani dhidi ya Uganda. Vita ni gharama kubwa na nchi yetu ilitaabika mno baada ya vita lakini kuna mambo hayana bei.

 

Ujenzi wa Ikulu mpya ya Ghana mwaka 2008 uligharimu kati ya dola milioni 30 hadi milioni 45 kulingana na chanzo chako cha habari. Lakini aliyekuwa Rais wa Ghana, John Agyekum Kuffour, alijenga hoja kuwa anapata shida kulala kwenye jumba ambako babu zake walikuwa wanafungwa minyororo na kuteswa. Hakutaka kulala kwenye nyumba ambayo waliyoijenga lengo lao lilikuwa kupora utajiri wa taifa lake.

 

Mbadala wake, Rais John Atta Mills, hakuwa anapendezwa na Ikulu hiyo mpya. Yeye alitoka chama tofauti na Kuffour na aliamini ujenzi wa jengo hilo ulikuwa ni upotevu wa fedha nyingi. Badala ya kuendeleza jina la Golden Jubilee lililopendekezwa na Kuffour likiadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Ghana, Mills aliliita Flagstaff House – jina la jengo la zamani lililokuwepo kwenye eneo hilo kabla ya ujenzi wa Ikulu mpya.

 

Kuffour alilalamika hadharani kuhusu mabadiliko hayo. Nakumbuka alitumia lugha ya “baba wa kambo kubadilisha jina la mtoto asiyemzaa”, akimaanisha inakuwaje jengo alilojenga yeye libadilishwe jina na Rais ambaye hakuhusika wakati linajengwa? Bahati nzuri ni kwamba Rais aliyembadili Mills, John Mahama, alirejesha jina la zamani na mambo yamepoa nchini Ghana hivi sasa.

 

Rais Samia na Ikulu mpya

 

Ni vigumu kujua Rais Samia ana mawazo gani kuhusu ujenzi wa Ikulu ya Chamwino. Sijui ana mawazo gani kuhusu dizaini iliyotumika na ukubwa wa eneo lenyewe. Lakini kuna vitu vichache naviona kutokana na tukio la uzinduzi nililolishuhudia juzi.

 

Kubwa zaidi ni kwamba ameamua urais wake utakuwa na sifa kubwa mbili; mwendelezo na mabadiliko (continuity and change). Kwamba ataendeleza mambo yote ambayo mtangulizi wake – Magufuli, aliyaanzisha na atafanyia mabadiliko mambo anayoona yanahitaji mabadiliko.

 

Kwa wafuatiliaji wa masuala ya Tanzania, inafahamika sasa kwamba ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao ulikuwa umefikia asilimia 37 wakati anaingia madarakani, sasa umezidi asilimia 80 na ni wazi – kama mambo mengine yataenda kama yalivyopangwa, ataukamilisha kwa wakati.

 

Ujenzi wa reli ya SGR unaendelea kwa spidi zaidi na tayari viongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) wameanza kuzungumzia uwezekano wa kuanza kutumika kwa reli hiyo katika awamu hii ya kwanza ya utawala wa Rais Samia.

 

Rais Samia anafanya hayo huku akiendelea na jitihada za kuleta maridhiano ya kisiasa Tanzania Bara na Zanzibar, akifungua uchumi wa nchi na kuongeza nguvu katika diplomasia ya uchumi kwa kutafuta masoko mapya kwa bidhaa za Tanzania.

 

Ingawa hakuwa na usemi kwenye kutenga eneo la Ikulu mpya na muundo wa jengo la ofisi hiyo, sasa ana uwezo wa kuamua matumizi bora ya eneo hilo kubwa. Kwenye hotuba yake alizungumza kuhusu ndoto za kuwa na uwanja wa ndege mdogo, viwanja vya michezo tofauti ikiwamo gofu na mambo mengine.

 

Kazi rahisi zaidi kwake ilikuwa kusema Ikulu hiyo haina maana na eneo ni kubwa sana na kupeleka lawama kwa mtangulizi wake. Inaonekana ameamua kufuata njia ngumu zaidi – njia ya kiungwana. Baada ya kukamilisha ndoto ya mtangulizi wake, kazi kubwa sasa ya Rais Samia itakuwa ni kuweka ndoto zake kwa kusikiliza na kuamua kuhusu matumizi ya kimkakati ya eneo ilikojengwa Ikulu mpya ya Chamwino. Hizo, ndizo siasa za ujenzi wa Ikulu.