Na Ezekiel Kamwaga
MWANZONI mwa mwaka huu, Kiongozi wa Chama wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alikuwa pengine mwanasiasa aliyekuwa akishambuliwa zaidi mitandaoni kuliko mwingine. Mashambulizi hayo yalitokana na ushiriki wake katika Kikosi Kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mapitio ya sheria za uchaguzi zilizopo nchini.
Kikosi kazi hicho hakikuwa kinaungwa mkono na chama kikuu cha upinzani nchini CHADEMA kwa sababu zake na kuwa kwake kwenye timu hiyo, halikuwa jambo rahisi kisiasa kwake. Kimsingi, ACT Wazalendo chini ya uongozi wake, kiliunga mkono ajenda ya maridhiano ya kisiasa ya Rais Samia kuanzia siku ya kwanza.
Ni kazi ya kikosi hicho na wadau wengine ndiyo imefanikisha kuandaliwa kwa Sheria za Uchaguzi zinazoweza kuufanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kuwa huru zaidi pengine kuliko chaguzi zozote zilizopita hapa nchini. Mwanzoni mwa mwaka huu, ilikuwa rahisi zaidi kwa Zitto kujitoa kwenye mchakato mzima ili kuepuka kashfa, lawama na mashambulizi dhidi yake binafsi na chama chake. Lakini aliamua kufuata njia ngumu zaidi lakini sasa uamuzi wake huo umeonekana wa manufaa kwa nchi.
Lakini mwaka 2023 ndiyo Zitto ametangaza rasmi kutowania tena nafasi ya Kiongozi wa Chama kwenye chama chake. Katika historia ya vyama vya upinzani nchini, yeye anakuwa Kiongozi wa pili mkuu wa chama kuachia nafasi yake kumwachia miwngine – wa kwanza akiwa Mabere Marando kwa Augustine Mrema, takribani miaka 30 iliyopita.
Tofauti ya Zitto na Marando ni kwamba Mbunge huyo wa zamani wa Rorya alifanya hivyo kumpa nafasi mwanasiasa aliyeonekana kuwa na nguvu kisiasa wakati huo ili kukipa chama nafasi zaidi ya kukua. Zitto anaachia ngazi kwa kufuata Katiba ya chama hicho inayotaka nafasi hiyo ishikwe na mtu mmoja kwa vipindi visivyozidi viwili. Hii ni hatua mpya katika uwanda ambao uongozi katika vyama vya upinzani huonekana kama ni wa kudumu.
Kama Zitto na ACT Wazalendo ingesusia pia mchakato wa maridhiano ya kisiasa kupitia TCD na Kikosi Kazi, huenda leo tusingekuwa tumefika tulipo. Kazi ya TCD na Kikosi Kazi pasipo baraka ya vyama viwili vikuu vya upinzani nchini ingepata shida kuwa na uhalali. Lakini Zitto alifanya uamuzi ambao bila shaka umefikisha maridhiano ya kisiasa hapa yalipo sasa.