Kazini kwao kuna kazi
Na Ezekiel Kamwaga
UTANGULIZI
WAKATI mwaka mpya unapoanza, vyombo vya habari vimekuwa na utamaduni wa kufanya tafakuri kuhusu masuala tofauti yaliyotokea katika mwaka uliokwisha na yapi ya kutarajia katika mwaka mpya.
Kwa mara ya kwanza mwaka huu, Gazeti la Dunia linafanya uchambuzi wa kuangalia wanasiasa wa kuangaliwa zaidi katika mwaka 2025.
Tumeamua kuchagua wanasiasa kwa sababu kuu mbili; Mosi kwamba huu ni mwaka ambao Tanzania inatarajiwa kufanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani na pili ni kupunguza idadi ya watu wanaoweza kuingia kwenye orodha hii.
Na tumeamua kuandika watu 10 tu kwa sababu walau ni namba isiyo kubwa sana lakini pia si kidogo pia. Ni rahisi kufanya uchambuzi kwenye namba ya namna hii kuliko idadi kubwa zaidi au ndogo zaidi.
Namba zilizotumika kwenya makala haya, hazina uhusiano wowote na ukubwa wa ushawishi.
Tusome.
- Tundu Lissu
LOLOTE litakalotokea baada ya uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Januari 21 mwaka huu, Makamu Mwenyekiti wake wa sasa, Tundu Lissu, atakuwa mwanasiasa muhimu wakati huu.
Endapo atashindwa na Freeman Mbowe kwenye kinyang’anyiro hicho, hakuna ajuaye atachukua hatua ipi – mwenyewe akisema atabaki kwenye chama kama asipofukuzwa.
Lakini endapo atashinda kwenye uchaguzi huo, maana yake ni kwamba chama hicho itabidi kingie kwenye mabadiliko ya kukifanya chama hicho kiendane na taswira ya kiongozi wake mpya.
Endapo ataamua kuhama chama hicho, kwa vyovyote litakuwa jambo la kufuatiliwa kuona atahamia kwenye chama kipi. Kama atashinda au kushindwa uchaguzi, kama atabaki au kuhama CHADEMA, Lissu ataendelea kugonga vichwa vya vyombo vya habari mwaka huu.
- Hussein Bashe
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuhusu upungufu wa mvua mwaka huu ambao unaweza kusababisha mavuno hafifu ya chakula kwa wakulima.
Mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan alizungumzia pia uwezekano wa kuwepo kwa mvua hafifu msimu huu na kuna dalili za upungufu wa uzalishaji chakula.
Katika mwaka wa uchaguzi, bei za juu za vyakula au upungufu wa vyakula sokoni na majumbani kunaweza kukawa jambo litakalotawala mijadala ya uchaguzi.
Ndiyo sababu, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ni mtu muhimu mwaka huu. Kama atafanikisha nchi kuingia kwenye uchaguzi ikiwa haina shida ya chakula wala bei za vyakula hazijapaa, itamaanisha nafasi nzuri kwa CCM kushinda kwenye uchaguzi.
Kama nchi ikienda kwenye uchaguzi wakati watu wakilia na bei za juu za vyakula, maana yake ni kuwa CCM itaingia kwenye uchaguzi ikiwa kwenye kuepa mashambulizi. Huu ndiyo mzigo wa Bashe mwaka huu.
- Zitto Kabwe
Mwaka jana, Zitto aliachia nafasi ya Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo baada ya kumaliza muda wa kikatiba wa vipindi viwili aliyotakiwa na Katiba kufanya hivyo.
Ingawa viatu vyake vimevaliwa na Dorothy Semu, Zitto anabaki kuwa mwanasiasa muhimu ndani ya chama chake. Kwa sababu Semu tayari ametangaza azma ya kuwania Urais kwenye uchaguzi wa mwaka huu, ni wazi kuwa Zitto ataelekeza nguvu zake kwenye ubunge.
Kama kinachoendelea CHADEMA kinaweza kusababisha mpasuko kwenye chama hicho – ni Zitto kwa sababu ya historia yake ya nyuma na chama hicho, anaweza kuwa kete muhimu.
Na kama chama chake kitafanya vizuri kwenye uchaguzi wa Zanzibar na kupata viti vingine Tanzania Bara baada ya uchaguzi wa mwaka huu, tunaweza kuwa tunazungumzia Waziri Mkuu Kivuli ajaye baada ya uchaguzi wa mwaka huu.
Kwa vyovyote vile, jina la Zitto litarindima mwaka huu kwa sababu tofauti kutokana na hali ya kisiasa inayoendelea sasa.
- Mwigulu Nchemba
Miongoni mwa matokeo yaliyoshtua wengi barani Afrika mwaka jana, yalihusu kushindwa kwenye uchaguzi kwa chama tawala cha Botswana Democratic (BDP) baada ya kukaa madarakani tangu mwaka 1966.
Kuna sababu kadhaa zilizofanya BDP ishindwe uchaguzi lakini mojawapo ya sababu inayotajwa zaidi ni ukweli kwamba ingawa uchumi wa Botswana kwa maana ya Pato la Taifa (GDP) unaonekana mzuri, hali ya uchumi kwa watu si ya kuridhisha kama zamani.
Vijana wa Botswana wanalalamikia tatizo la ukosefu wa ajira linaloelezwa kuwa juu kuliko wakati mwingine wowote kwenye historia ya taifa hilo lakini raia pia wanalalamikia kupanda kwa gharama za maisha.
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, atakuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba hali ya afya ya uchumi ya nchi iko vizuri – ikimaanisha ajira zaidi na kupungua kwa makali ya maisha kwa wananchi.
Kama alivyopata kusema aliyepata kuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton, “Its economy, stupid”. Katika mwaka wa uchaguzi, uchumi wa nchi ndiyo jambo mpira huu kwa sasa uko miguuni wa Mwigulu. Atasikika sana kwa namna atakavyokuwa anaucheza.
- Innocent Bashungwa
Jambo la muhimu kuliko yote katika taifa ni kwa watu kuona wako sehemu salama na wanaweza kuishi pasi na hofu. Wasomi maarufu wa Sayansi ya Siasa kama Hobbes na Fukuyama kimsingi wanaeleza kuwa watu walikubali kuwa na serikali ili walindwe.
Serikali za Kenya na Nigeria zimewahi kuingia katika matatizo makubwa kwa sababu wananchi wake walianza kuhisi hawako salama ndani ya nchi yao.
Kama Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa, atakuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha raia wanakuwa salama ndani ya mipaka ya nchi yao.
Katika mwaka wa uchaguzi, matukio ya utekaji na watu kupotea kama yaliyotokea mwaka jana, yatakuwa yanapaziwa sauti mara dufu na kwa kuangalia mfano wa matukio ya kikosi cha SARS nchini Nigeria wakati wa utawala wa Rais Muhamadu Buhari, ni wazi Bashungwa atakuwa na kibarua kizito kuhakikisha raia wanahisi kuwa salama.
- Othman Masoud Othman (OMO)
Kwa mara ya kwanza tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, uchaguzi mkuu wa Zanzibar unafanyika bila ya uwepo wa Maalim Seif Sharif Hamad – pengine mwanasiasa mashuhuri zaidi wa visiwa hivyo kwenye kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Badala yake, upinzani utaongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ambaye tayari ametangaza nia yake ya kuwania urais wa visiwa hivyo mwaka huu.
Ni matarajio ya wengi kwamba tofauti na uchaguzi wa mwaka 2020, mwaka huu Zanzibar itashuhudia uchaguzi utakaofanana na walau ule wa mwaka 2015 au 2010 na ni wazi jina la OMO litasikika kuliko wakati mwingine wowote.
Huu ni uchaguzi wake wa kwanza kushiriki kama mwanasiasa na mgombea na wengi wanataraji kuona namna atakavyofaa viatu vikubwa vya hayati Maalim Seif kwenye uchaguzi huu.
- Abdallah Ulega
Wabunge watatu mashuhuri wa Tanzania wamefanya tafiti binafsi kuhusu hali ya kisiasa nchini na jambo moja limeibuka kama mojawapo ya kero kubwa zaidi nchini – ubovu wa barabara.
Tatizo hili limesababishwa na mambo mawili makubwa, mosi mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana za masika na El Nino ambazo zimesababisha athari kubwa kwenye baadhi ya barabara na madaraja na pili ni uwezo mdogo wa kibajeti wa TANROADS na TARURA kwenye kushughulika na changamoto hizo.
Kama Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, atakuwa na kazi kubwa na pengine atasikika sana akizungumzia kuhusu utatuzi wa kero za miundombinu kwa sababu kama litabaki kama lilivyo, linaweza kuwa mwiba kwa chama tawala kwenye mwaka wa uchaguzi.
- Dkt. Hussein Mwinyi
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, atakuwa anatetea kiti chake katika uchaguzi wa Zanzibar ambako kwa kawaida upinzani huwa ni mkali.
Tegemea taarifa nyingi kutoka visiwani kuhusu mambo anayoendelea kuyafanya kuboresha maisha ya Wazanzibari.
Utamu wa siasa za Zanzibar mwaka huu ni kwamba utakutanisha washindani wawili ambao vyama vyao vina mwelekeo tofauti ambao kimsingi mmoja ni tiba dhidi ya mwingine.
Pmaoja na mambo mengine, ACT Wazalendo wataendelea kuzungumzia masuala ya mamlaka kamili ambalo ni suala la kihisia kwa Wazanzibari. Kwa upande wa Mwinyi, itabidi aendelea kuwashawishi wapiga kura kwamba urais wake ni wa vitendo zaidi kuliko maneno matupu.
Tofauti na uchaguzi wa mwaka 2020, ni wazi kwamba Rais Mwinyi sasa atasikika zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 2020.
- Mahmoud Thabit Kombo
Hali ya kiulinzi na kiusalama duniani kwa ujumla hivi sasa ni tete. Hata hivyo, hali inaonekana kuelekea kuwa ngumu miongoni mwa majirani wa Tanzania mwaka huu.
Nchini Msumbiji, hali imelegalega kufuatia uchaguzi wake mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana. Hotuba ya wiki hii ya Rais Paul Kagame mbele ya mabalozi wa nchi za kigeni nchini kwake, inaonyesha kwamba hali haitakuwa shwari Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa sababu ya uchaguzi wa mwaka huu, kurunzi la mataifa makubwa pamoja na asasi za kimataifa za masuala ya demokrasia na utawala bora litamulikwa kuelekea upande wa Tanzania.
Kuna maslahi ya kuimarisha TAZARA na kuangalia fursa za Ukanda wa Lobito. Kuna namna ya kuishi na Marekani ya Donald Trump huku tukiendeleza uhusiano wetu wa kihistoria na China ambao uhasimu wake na Marekani unakua.
Kwa vyovyote, kazini kwa Kombo kutakuwa na kazi nyingi mwaka huu na ni wazi tutasikia mengi kutoka kwake.
- Samia Suluhu Hassan
Zaidi ya kofia tatu alizonazo – za Ukuu wa Nchi, Ukuu wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Samia Suluhu Hassan, atakuwa na kofia nyingine mwaka huu, ya mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hii itakuwa mara yake ya kwanza kuwania urais – ingawa ameshiriki kama mgombea mwenza wa urais, mara mbili huko nyuma.
Ili kukihakikishia ushindi chama chake, Rais Samia atakuwa na majukumu kadhaa ya kuhakikisha chama au serikali yake haiingia kwenye matope mwaka huu.
Atakuwa mchapa kazi namba moja, mkemea rushwa na uzembe kinara, mpenda watu, mtatua kero na bila shaka atahakikisha uchumi wa nchi unaendelea na ukuaji wake, raia wakiwa salama, na kuiepusha serikali yoyote na kashfa yoyote ya rushwa inayoweza kuwapa wapinzani pumzi ya kupigania kwenye uchaguzi huu.
Kama chama tawala kikongwe zaidi barani Afrika hivi sasa, Samia ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, atakiongoza chama chake kupambana na wimbi kubwa la mabadiliko linaloendelea duniani ambapo vyama vingi tawala vinapata taabu kushinda uchaguzi.
Kazi yake kubwa mwaka huu itakuwa ni kuhakikisha kwamba CCM yake inavuka kwa kishindo wimbi hili kubwa linaloendelea duniani la watu kuchukia serikali zilizo madarakani au vyama vilivyodumu madarakani kwa muda mrefu.
Ndiyo mtihani wake mkubwa mwaka huu.
Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.

















































































































































