Ajali ya Kariakoo, angani na Rio: Saa 15 za kwanza

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

DAKIKA chache baada ya ndege iliyombeba Rais Samia
Suluhu Hassan kupaa angani kwenda Brazil kuhudhuria
mkutano aliopewa heshima ya kualikwa wa Nchi Tajiri
Duniani wa G20, habari zilianza kusambaa mitandaoni
kuhusu kuanguka kwa jengo la biashara katika eneo la
Kariakoo jijini Dar es Salaam.

 

Kwa bahati nzuri, ndani ya ndege hiyo kubwa ya Shirika
la Ndege la Tanzania (ATC) aina ya Dreamliner maarufu
kwa jina la Hapa Kazi Tu, kuna huduma ya internet na
abiria tuliokuwa ndani ya ndege hiyo na katika
mitandao ya kijamii, tulikuwa tunafuatilia kilichokuwa
kinaendelea.

 

Kama mwandishi wa habari na mwanafunzi wa
masuala ya siasa, jana nilipata fursa kubwa ya
kuangalia kwa karibu ni nini hutokea wakati tukio kama
la Kariakoo linapotokea katika wakati ambao Mkuu wa
Nchi, Serikali na Amiri Jeshi Mkuu, akiwa angani.

 

Nilichokiona jana kilikuwa ni “masterclass” ya nini hasa
kinatakiwa kufanyika. Kwa macho yangu, nilishuhudia
viongozi viongozi wa serikali na wateule wengine wa
Rais tuliokuwa nao kwenye ndege kwenda alipo Rais –na sasa ninafahamu kwamba alifanya hivyo baada ya
kuwa amezungumza na viongozi wa serikali na vyombo
vya dola ili kupata picha ya nini kinaendelea.

 

Ni mpaka baada ya kuwa amezungumza kupata picha
ya nini kilichotokea na kushauriana na baadhi ya
wateule na wasaidizi wake aliokuwa nao angani, ndipo
sasa aliandika ujumbe ule kwenye mitandao ya kijamii
wa kutoa pole na maelekezo ya nini kinatakiwa
kufanyika.

 

Nimeambiwa kwamba Rais katika muda wote wa safari
ya kwenda Brazil alikuwa akipewa taarifa tofauti na
taasisi tofauti – wakiwemo watu binafsi kuhusu
kinachoendelea. Hata zile sauti za watu waliokuwa
wakizungumza na vyombo vya habari kuomba msaada
wa serikali na Rais, yeye binafsi alizisikiliza pia.

 

Wakati abiria wengine tukisinzia njiani na kupiga soga
kwenye ndege, Rais alikuwa kwenye mazungumzo ya
mara kwa mara ama na watu walio kwenye eneo la
tukio au mawaziri Kitila Mkumbo na Saada Mkuya –
Waziri wa Fedha wa Zanzibar ambaye yupo katika
msafara, kujaribu kutafuta namna bora ya kufanya.

 

Jana, nilimshuhudia Rais anayependa watu wake.
Nilimshuhudia Rais anayeumizwa na kadhia
zinazowakumba watu wake. Na nilimshuhudia Rais anayesikiliza watu wa aina zote – wataalamu wa fani
tofauti lakini na raia wa kawaida kabisa. Jana, lilikuwa
darasa zuri sana kwangu kuhusu unyenyekevu wa
kiuongozi.

 

Kwa kusoma taarifa za vyombo vya habari na marafiki
zangu wa Tanzania ambao nimezungumza nao,
naamini ndiyo sababu katika historia ya miaka 30
iliyopita ya maafa na majanga hapa nchini, kazi ya
uokoaji iliyofanyika jana na kuendelea leo imefanyika
kwa kasi na weledi mkubwa.

 

Kuna picha zilisambaa za askari wanajeshi wakiwa
wanashangiliwa na wananchi baada ya kufika kwenye
eneo la tukio. Kwa mujibu wa taratibu za Tanzania,
wanajeshi huwa wanatoka kambini kwa ruhusa
maalumu ya Amiri Jeshi Mkuu ambaye kwa sasa ni Rais
Samia.

 

Kuna vifo vitano vimetokea na napenda kutoa pole kwa
wafiwa lakini kuna mambo mawili matatu yaliyofanyika
ambayo si ya kawaida kwenye matukio ya maafa na
ajali hapa kwetu.

 

Sikumbuki mara ya mwisho kwa serikali kutoa msaada
wa kitaalamu wa kupeleka hewa ya oksijeni kwa watu
wanaohitaji na kuiweka katika mahali ambapo kulisaidia kuongeza muda wa kuishi wa watu ambao
maisha yao yaliokolewa.

 

Ninakumbuka jinsi Watanzania tulivyokuwa
tunaitazama meli ya MV Bukoba ikizama na maisha ya
watu pasipo kuwa na msaada wowote. Wakati ule,
kuna mtu mmoja aliamua kuchomelea sehemu moja ya
meli ili kuokoa watu na badala yake ndiyo akaifanya
izame.

 

Tunakumbuka bado tukio la ajali ya ndege ya Precision
Air ambako hadi leo taswira ya uokoaji inabebwa na
watu binafsi kama kijana Majaliwa ambaye alifanya
kazi kubwa wakati ule.

 

Safari hii, kwenye tukio la kubomoka kwa jengo la
Kariakoo, sifa kubwa zitakwenda kwa serikali na kwa
vyombo vyake vilivyofanya kazi kubwa ya uokoaji.
Lakini, aliyeongoza yote hayo alikuwa Rais Samia akiwa
zaidi ya futi 40,000 kutoka usawa wa bahari.

 

Ninafahamu pia kwamba hata tulipofika Rio majira ya
saa kumi jioni, shughuli yake ya kwanza aliyoifanya
Mhe Rais ilikuwa ni kutaka kujua nini kinaendelea Dar
es Salaam.

 

Kwa utulivu ule niliouona angani jana, nina matumaini
kwamba ushiriki wa kihistoria wa Tanzania kwenye G20
mwaka huu utakuwa wa mafanikio makubwa.

 

Huu ni mkutano wa nchi tajiri duniani ambazo
zinamiliki asilimia 85 ya uchumi wote duniani. Katika
taifa kama letu ambalo linahitaji uhusiano na wakubwa
ili ikalimishe miradi yake ya kimkakati na kupeleka
duniani ajenda muhimu kama ya matumizi ya nishati
safi kwenye maisha yetu, hakuna fursa kubwa kama
kukutana na kujadiliana na wadau wa G20.

 

Sisi tulio Rio – na zaidi kwa Rais Samia, yanayoendelea
Kariakoo yako vichwani na mioyoni mwetu. Lakini,
nimeshuhudia pia kwamba Tanzania iko tayari
kuunguruma na kuweka hoja zake mezani kwenye G20.