Pichani: Ismail Haniyey, aliyekuwa Kiongozi wa Kisiasa wa Chama cha Hamas cha Palestina. Picha kwa hisani ya Getty Image
Na Ahmed Rajab
WATU wengi wanaposikia mvuvumko wa Hamas ukitajwa, sura ya mwanzo inayowajia ni ya Ismail Haniyeh, aliyekuwa kiongozi wa kisiasa wa chama hicho na aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Palestina baada ya chama chake kushinda uchaguzi mkuu wa Bunge la Palestina mwaka 2006.
Sura za vigogo wengine wa Hamas, kwa mfano, kiongozi wake aliye Gaza, Yahya Sinwar au kaimu wake, Khalil al-Hayya, au za makamanda wa kijeshi wa kundi hilo, kama vile Mohamed Dief au kaimu wake Marwan Issa huwa haziwajii watu wengi.
Kwa takriban miaka 20 sasa kwa wengi sura ya Hamas imekuwa ile ya Haniyeh, aliyeuawa usiku wa manane wa kuamkia Jumatano Julai 31, jijini Tehran, Iran, saa chache baada ya kuhudhuria sherehe ya kuapishwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian.
Tuliokuwa tukiangalia sherehe hiyo kwenye televisheni tulimuona Haniyeh akikumbatiwa na Pezeshkian. Miongoni mwa wageni kutoka nje ya Iran waliohudhuria sherehe hiyo alikuwa Mahmoud Thabit Kombo, waziri mpya wa mambo ya nje wa Tanzania.
Kwenye makala niliyoyaandika humu miezi kadhaa iliyopita chini ya kichwa cha maneno “Netanyahu na wenzake ni chui wa karatasi” nilieleza hamu kubwa niliyokuwa nayo ya kukutana na Haniyeh, nilipozuru Gaza Mei 2009.
Mwandishi wa Kipalestina Nahedh Abdelwahed, aliyekuwa na maingiliano na viongozi wa Hamas, alifanya juu chini kunisaidia nimfikie Haniyeh. Bahati mbaya juhudi zake hazikufua dafu. Ujumbe aliopewa anipe na ofisi ya Haniyeh ulikuwa wa kusikitika kwamba huo haukuwa wakati muwafaka wa kukutana na Haniyeh.
Hali ya usalama ilikuwa bado tete miezi michache baada ya majeshi ya Israel kulivamia na kulitwanga eneo la ukanda wa Gaza. Waisraeli walikuwa wakimuandama Haniyeh. Naye, kwa usalama wake, hakuwa akitulia mahala pamoja. Hata ilikuwa haijulikani usiku atalala wapi.
Aliyenitia mori hasa wa kutaka nikutane na Haniyeh alikuwa Serene Assir, aliyekuwa mwanahabari wangu siku hizo nilipokuwa mkuu wa chumba cha habari cha Ofisi ya Mashariki ya Kati na Asia ya lililokuwa Shirika la Habari la Umoja wa Mataifa, IRIN. Siku hizi binti huyo mwenye asili ya Lebanon ni naibu wa mkuu wa ofisi ya Asia na Pacific ya Shirika la Habari la AFP huko Hong Kong. Siku hizo akituletea ripoti kutoka Cairo na kutoka Beirut.
Safari moja, miezi kadhaa kabla ya mimi kwenda Gaza, alikwenda yeye na alibahatika kukutana na Haniyeh. Aliporudi alinipa picha aliyopiga na Haniyeh. Na, kwa mara ya kwanza, nilimuona akivaa buibui jeusi akimhoji Haniyeh.
Nilivutiwa na haiba ya Haniyeh. Pamoja na kuwa mwanasiasa mshupavu alikuwa pia mhitimu wa shahada ya fasihi ya Kiarabu aliyosomea katika Chuo Kikuu cha Kiislamu huko Gaza. Moja ya sababu zilizonifanya nitake kuonana naye ilikuwa kutaka tuzungumze kuhusu fasihi ya Kiarabu. Nikijua pia kwamba alipokuwa mwanafunzi alikuwa shabiki mkubwa wa soka akichezea timu ya Jumuiya ya Kiislamu ya chuoni kwake.
Sawa na viongozi wengine wa Hamas, Haniyeh alikuwa ameuhifadhi kwa moyo msahafu mzima. Na alikuwa akisoma Kuruani kwa sauti nzuri na kwa mahadhi yenye kuvutia. Kuna video kadhaa mitandaoni zinazomuonesha akiswalisha.
Haniyeh akitambua vilivyo jinsi Waisraeli walivyokamia kumuua. Na, kwa hakika, walijaribu mara kadhaa kumtoa roho wakashindwa. Safari moja aliponea chupu chupu asiuliwe pamoja na Sheikh Ahmed Yassin, aliyekiasisi chama cha Hamas pamoja na Abdel Aziz Rantisi mwaka 1987.
Haniyeh alijiunga na chama hicho mara baada ya kuhitimu masomo yake ya chuo kikuu mwaka huo wa 1987 na aliwahi kukamatwa mwaka huo na pia 1988 na kufungwa na Waisraeli.
Alihukumiwa kifungo kirefu cha miaka mitatu mwaka 1989 na alipofunguliwa 1992 wakuu wa kijeshi wa Israel waliokuwa na mamlaka katika maeneo ya Wapalestina walimfukuza na kumhamishia kusini mwa Lebanon pamoja na viongozi wakuu wa Hamas kama Rantisi, Mahmoud Zahhar na Aziz Duwaik pamoja na wanaharakati 400.
Mwaka mmoja baadaye, Haniyeh aliruhusiwa kurudi Gaza na akawa mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu. Baada ya Sheikh Ahmed Yassin kufunguliwa kutoka gerezani mnamo 1997, Haniyeh aliteuliwa kuiongoza ofisi yake. Hapo ndipo alipozidi kuwa karibu na Yassin na umaarufu wake ulizidi kupanda.
Wakati nilipokuwa Gaza nikitaka kukutana naye, viongozi waliomtangulia, kina Yassin na Rantisi, walikwishauliwa na Waisraeli. Yassin aliuliwa kwa makombora ya ndege ya kivita huko Gaza tarehe 6, Septemba, 2003.
Rantisi naye aliuliwa hivyo hivyo kwa makombora ya ndege ya kivita 17, Aprili, 2004. Mkewe, Jamila, aliyekuwa na shahada ya uzamivu ya udaktari wa falsafa katika lugha ya Kiingereza, aliuliwa 19 Oktoba, mwaka jana, katika shambulio la Israel dhidi ya Gaza.
Hamas ni chama cha kisiasa chenye muelekeo wa Kiislamu; wafuasi wake wanafuata madhehebu ya Sunni. Kama nilivyoandika kwenye makala niliyoyadhukuru Hamas si shetani wa Fatah, chama kikuu cha Wapalestina kilichokuwa kikiongozwa na Yasser Arafat na sasa na Mahmoud Abbas. Wala si shetani wa Israel iliyolizingira eneo la ukanda wa Gaza kwa muda wa miaka 17 sasa na iliyonyakua na kulishikilia kwa nguvu eneo kubwa la Palestina.
Ismail Haniyeh alizaliwa Gaza miaka 62 iliyopita kwenye kambi ya wakimbizi ya Al-Shati. Hii leo kambi hiyo imegeuzwa kifusi kwa mashambulizi yaliyofanywa na Israel tangu Oktoba mwaka jana. Lakini kwao hasa Haniyeh ni mji ambao siku hizi unaitwa Ashkelon ulio ndani ya taifa ambalo tangu 1948 linaitwa Israel.
Wazazi wake walikuwa wakimbizi baada ya mji wao kutekwa katika vita vya mwaka huo, vilivyokuwa vya mwanzo baina ya Waarabu na Wayahudi katika Palestina.
Mauaji ya Haniyeh yamezusha maswali kadhaa. Baadhi yao yanajibika, baadhi mtu anaweza kukisia namna ya kuyajibu na kuna yanayotuweka gizani.
Tunachokijua ni kwamba Haniyeh aliuliwa pamoja na mlinzi wake muhtasi, aitwaye Wasim Abu Shaaban. Pia tunajua kwamba waliuliwa wakiwa katika nyumba waliyofikia katika sehemu za kaskazini mwa Tehran wakiwa wageni wa serikali ya huko. Kwa kawaida nyumba hiyo hukaliwa na maveterani wa majeshi ya Iran.
Inavyosemekana ni kwamba Haniyeh na mlinzi wake waliuliwa kwa kombora lililorushwa kutoka angani nje ya Iran. Inayotuhumiwa kwa shambulizi hilo ni Israel, hasa idara yake ya ujasusi ya Mossad.
Swali linalozuka ni: Idara hiyo ya ujasusi ilijuaje Haniyeh na mwenzake walikuwa katika chumba gani kwenye jengo hilo? Inavyodhaniwa ni kwamba Israel ilipandikiza programu ya kijasusi ndani ya ujumbe wa WhatsApp aliopelekewa Haniyeh kwenye simu yake.
Programu hiyo iliiwezesha idara ya kijasusi ya Israel kujua ni wapi hasa ndani ya nyumba alikokuwako Haniyeh. Alipozungumza kwa simu na mwanawe ndipo idara ya ujasusi ya Mossad ilipojua wapi hasa alipokuwako.
Programu hiyo ya kijasusi ina uwezo wa kuiingilia simu ya mtu, ikayaona mazungumzo yake ya maandishi, picha na mahala alipo. Inaweza pia kuitumia kamera ya simu pamoja na kipaza sauti bila ya mwenye simu kujua.
Israel ingeweza kumuua Haniyeh nchini Qatar, alikokuwa akiishi tangu 2017, au Uturuki, alikokuwa akenda mara kwa mara, au Misri alikokuwa akihudhuria mikutano inayohusika na mashauriano ya kusitisha mapigano Gaza. Lakini haikufanya hivyo.
Israel ilifanya umaluuni wa kusudi kumuulia Iran, nchi yenye wafuasi wengi wa madhehebu ya Shi’a. Lengo ni kutaka kuchochea fitina baina ya Masunni na Mashia na pia kuifanya Iran ilaumiwe kwamba haina usalama ulio imara au kwamba ilihusika kumtosa Haniyeh.
Kabla ya kumuua Haniyeh, Israel ilimuua kamanda wa Hezbollah Sayyed Fouad Shukr (Hajj Mohsen), mjini Beirut. Inavoonesha ni kwamba Israel imedhamiria kuvikuza vita vyake dhidi ya Hamas na kuyaingiza makundi na nchi nyingine.
Tangu Oktoba 7 mwaka jana, Israel iliwaua watoto watatu na wajukuu watano wa Haniyeh katika Gaza. Jamaa zake wengine w karibu wasiopungua 60 nao pia wameuliwa. Mauaji yake bila ya shaka yatatatiza mashauriano ya kusitisha mapigano Gaza na kuachiwa kwa mateka wa Israel waaoshikwa na Hamas.
Hamas na Hezbollah wameahidi kulipiza kisasi kwa mauaji ya Haniyeh na Shukr. Iran nayo imekwishasema kwamba lazima italipiza kisasi mauaji ya Haniyeh yaliyofanywa kwenye ardhi yake, ingawa haikusema lini na vipi italipiza kisasi. Hofu iliyopo ni kwamba karibu eneo zima la Mashariki ya Kati litawaka moto na Israel huenda isiweze kujinusuru bila ya msaada wa Marekani.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab
Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.