Mzigo wa Rais Samia, Mbowe na Zitto

Na Ezekiel Kamwaga

KUTOKANA na kuimarika kwa mahusiano ya kisiasa baina ya vyama vitatu vikubwa vya siasa nchini Tanzania; Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT Wazalendo, maswali yameibuka – nani anapata nini kwenye maridhiano haya ya kisiasa?

Ninawafahamu wanasiasa wawili wabunge wa CCM ambao wamezungumza nami wakionesha wasiwasi mkubwa kwamba maridhiano haya yanamaanisha wao kukosa ubunge kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Kwao, maridhiano haya hayana faida.

Ninawafahamu pia wanasiasa kadhaa wa vyama vya upinzani ambao wanaona vyama vya upinzani – hasa Chadema, vinakosea kwa kuonekana kuwa karibu na chama ambacho kimetumia takribani miaka sita iliyopita kutesa viongozi na wanachama wake.

Ninawafahamu pia wanachama wa ACT Wazalendo ambao bado hawakubaliani na hatua ya chama chao kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na CCM huko Zanzibar – wakati vidonda na machungu waliyopitia baadhi ya viongozi na wafuasi wake baada ya uchaguzi wa mwaka 2020 vikiwa havijauka.

Lakini viongozi watatu wa vyama hivyo; Rais Samia Suluhu Hassan wa CCM, Freeman Mbowe wa Chadema na Zitto Kabwe wa ACT Wazalendo, wanaendelea na safari yao ya kutafuta maridhiano ya kisiasa.

CCM inafaidika nini na maridhiano? Chadema wanafaidika nini na maridhiano? ACT Wazalendo inafaidika nini kupitia kuimarika huku kwa uhusiano baina ya wadau wa kisiasa nchini Tanzania?

Maana ya Maridhiano

 Kwa tafsiri ya kawaida, maridhiano ni hatua ya pande zinazosigana kwa jambo fulani kuamua kuondoa tofauti zao kwa ajili ya maslahi mapana zaidi kuliko tofauti zao. Maslahi hayo yanaweza kuwa ni utaifa wao au jambo lolote kubwa linalowaunganisha pamoja.

Katika muktadha wa maridhiano ya sasa, ni wazi kwamba maslahi mapana ni Tanzania/Zanzibar. Kwamba, viongozi wa kisiasa wameona Tanzania/ Zanzibar ni kubwa kuliko tofauti zao na kwamba namna pekee ya kuishi na kukua pamoja ni kusahau yaliyopita na kujenga msingi imara wa usawa na maelewano ya kudumu huko mbele ya safari.

Mara zote ninapofanya uchambuzi wa masuala ya maridhiano barani Afrika, huwa ninapenda sana kutumia lenzi iliyotumiwa na wasomi wawili maarufu wa siasa za Afrika; Miles-Blessing Tendi na Nic Cheeseman. Wawili hawa wanaamini kwamba kufanikiwa kwa maridhiano kwenye nchi za Afrika, mambo mawili ni lazima yawe sawa; uhusiano wa tabaka la watawala na uwezo wa kudhuriana miongoni mwa tabaka la watawala.

Kama wale walio katika tabaka la watawala wana uhusiano mzuri, uwezekano wa kuwepo kwa maridhiano ni mkubwa kuliko kukiwa hakuna uhusiano. Pia, kama watu wa tabaka hilo wana uwezo wa kuumizana kupitia vurugu, ni rahisi pia kwa maridhiano kutokea.

Jambo la muhimu kufahamu hapa ni kwamba maridhiano kamili hayawezi kutokea kama mojawapo ya mawili hayo linakosekana. Ipo mifano ya kutosha barani Afrika kuonyesha namna kukosekana kwa kimoja au vyote viwili kulivyosababisha maridhiano kuwezekana.

Chukulia mfano wa Angola. Baada ya Uhuru iliopata kutoka kwa Wareno mwaka 1975, taifa hilo liliingia kwenye mapambano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Upande mmoja Jeshi la MPLA chini ya Agostinho Neto na upande mwingine Jeshi la UNITA chini ya Jonas Savimbi.

Savimbi na Neto hawakuwahi kuaminiana. Bahati mbaya kwa Angola ni kwamba wote wawili walikuwa na majeshi na hivyo uwezo mkubwa wa kuumizana. Katika hali ya namna hii ambapo wahusika hawaaminiani na wote wana majeshi, mwafaka pekee itakuwa ni kupigana vita hadi mshindi apatikane. Hicho ndicho kilichotokea Angola.

Zimbawe ni mfano tofauti. Chama tawala cha ZANU PF na washindani wake; chama cha MDC, bado hawajaaminiana na kuchangamana vya kutosha. Lakini ZANU ina uwezo wa kuumiza MDC lakini MDC haina uwezo huo. Matokeo yake ni ZANU PF kubaki madarakani kinguvu kwa vile viongozi wake hawana hofu ya kuumizwa kama watabaki madarakani kinguvu.

Mfano wa Kenya ndiyo unaeleza jambo la tatu kuhusu maridhiano. Nchini Kenya, viongozi walio madarakani na walio kwenye upinzani wanajuana na kufahamiana vema. Rais William Ruto kwa vipindi tofauti amewahi kufanya kazi kwa karibu na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, na kabla yake alikuwa swahiba wa karibu wa Raila Odinga.

Wanasiasa wengine maarufu wa Kenya kama vile Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula wamewahi kufanya kazi wakati mmoja na akina Ruto, Raila na Uhuru. Hii maana yake ni kwamba tabaka la watawala la Wakenya linaaminiana na kujuana.

Kwa upande mwingine, vurugu za nchini Kenya za mwaka 2008, zilionyesha kwamba uwezo wa kudhuriana kisiasa na kiuchumi miongoni mwa vinara wa siasa za Kenya ni mkubwa. Kama ambavyo Ruto angeweza kudhuru mali na maisha ya wafuasi wa Raila kwenye eneo la Bonde la Ufa, ndivyo hivyo Raila angeweza kudhuru mali na wafuasi wa Ruto kwenye eneo la Nyanza.

Kwa sababu ya kuaminiana na kujuana, ni rahisi kwa Ruto na Raila kuzungumza – kama ambavyo imejionyesha wiki hii kwenye kuzuia maandamano yaliyopangwa kufanyika Aprili 3, 2023, na pia kufikia maridhiano kwa vile hakuna anayefaidika na vurugu.

Maridhiano kwa Tanzania na Zanzibar

 Siasa za Tanzania zina tofauti na zile za Kenya kwa sasa. Tofauti kubwa ya kwanza ni kwamba CCM ina uwezo mkubwa wa kudhuru viongozi na wafuasi wa upinzani kuliko wapinzani kuidhuru CCM. Historia ya uchaguzi nchini tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi inaonyesha namna chama tawala kinavyoweza kutumia dola kwa maslahi yake kila inapobidi ili kukifanya kizidi kubaki madarakani.

Jambo la pili ni kwamba kuaminiana na kufanya kazi pamoja miongoni mwa tabaka la watawala kulifika pazuri kuelekea mwaka 2015 lakini hali ilivurugika sana kati ya mwaka 2015 hadi 2021 kutokana na aina ya siasa zilizokuwa zinafanywa na Rais John Magufuli.

Ilianza kuwa kawaida, kwa mfano, kumwona Zitto – wakati huo akiwa kiongozi wa Chadema, akifanya kazi kwa karibu na aliyekuwa Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, kupitia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwenye kuisimamia serikali.

Wakati wa kashfa ya Escrow, wabunge wa upinzani na wale wa CCM waliungana na kuwa kitu kimoja kwenye kutaka uwepo uwajibikaji miongoni mwa wahusika wa Sakata hilo.

Kilele cha uhusiano baina ya tabaka la watawala wa Tanzania Bara ilikuwa ni ukweli kwamba kufikia mwaka 2016, Kamati Kuu ya Chadema ilikuwa na mawaziri wakuu wawili; Frederick Sumaye na Edward Lowassa – ikiwa ni chama pekee cha upinzani kufikia hatua hiyo kwenye historia ya Tanzania.

Hata Mwafaka wa Zanzibar wa mwaka 2010, ulitokana na kuwepo kwa mazungumzo ya chini kwa chini kupitia Kamati Maalumu iliyoundwa kwanza na Rais Jakaya Kikwete ikiwashirikisha vigogo wa CCM na Chama cha Wananchi (CUF) – mmoja wa wajumbe akiwemo Samia wakati huo.

Kufikia mwaka 2010, kulikuwa na kufahamiana na kuaminiana vya kutosha miongoni mwa vinara wa siasa za Zanzibar kiasi kwamba haikuwa vigumu sana kuunda SUK kwa mara ya kwanza mwaka 2010. Hata SUK ya sasa ni matokeo ya maelewano ya awali miaka 13 iliyopita.

Mvurugano uliotokea kati ya 2016 -2021, uliondoa hali ya kuaminiana na kufanya kazi pamoja iliyoanza kujengwa kwenye siasa za Tanzania. Kwa kufuata uzoefu wa kwingineko barani Afrika, hakuna namna ambayo maridhiano yanawezekana pasipo wakubwa kufahamiana na kufanya kazi pamoja.

Hii ndiyo hatua ambayo Samia, Mbowe na Zitto wanaipitia wakati huu. Hizi picha, vicheko na kauli zisizo za kiadui ni hatua muhimu kwenye kurejesha hali ya uhusiano iliyokuwepo kuelekea mwaka 2015.

Freeman Mbowe anafahamu kwamba Chadema ilipata kura nyingi kuliko wakati mwingine wowote kwenye historia yake kupitia uchaguzi wa mwaka 2015. Atakuwa pia anafahamu kwamba kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 – uliofanyika katika mazingira ya uhusiano mbovu zaidi miongoni mwa tabaka la watawala kuwahi kutokea nchini Tanzania, Chadema haikufua dafu.

ACT Wazalendo ni chama kipya cha kisiasa lakini kwa sasa uti wa mgongo wake kisiasa – hasa Zanzibar, unajengwa na waliokuwa viongozi wa CUF walioshiriki kwenye SUK kati ya 2010-2015.

Viongozi hao wa zamani wa CUF, na Zitto, wanafahamu kwamba upinzani ulipata kura nyingi zaidi katika historia yake ikiwa ndani ya SUK na maelewano baina ya tabaka la watawala wa Zanzibar yakiwa yanaridhisha.

Kwa upande wa Rais Samia, imani yake kwenye maridhiano inajengwa na msingi kwamba hata katika nyakati ambazo upinzani ulifanya vizuri nchini Tanzania, CCM ilibaki madarakani kwa kura na kutokana na faida nyingine ilizonazo kama chama kilicho madarakani.

Jambo la msingi zaidi kwa Mbowe na Zitto ni kwamba bila maridhiano wananchi ndiyo wanaoumia zaidi lakini pale ambapo uhusiano baina ya watawala unakuwa wa kuaminiana, upinzani unakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kufanya vizuri kuliko ikiwa vinginevyo.

Taasisi imara zitategua mtego wa pili

Hakuna uwezekano wa Chadema au ACT Wazalendo – walau katika siku za karibuni, kuunda majeshi au vikundi vya kigaidi kwa ajili ya kutoshana nguvu za kuumizana na CCM. Tanzania pia haina siasa za kikabila – kama Kenya, kusema inaweza kutumia ukabila kuitishia CCM.

Namna pekee ambayo upinzani unaweza kufanya kupambana na uwezo wa CCM kutumia dola kuvikandamiza na kuviumiza ni kupitia kujenga taasisi imara za uchaguzi zitakazohakikisha mshindi halali anatangazwa.

Katika nchi ambazo upinzani umeingia madarakani dhidi ya chama tawala, sifa moja kubwa ya nchi husika ni uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mahakama. Tumeona namna Mahakama ilivyoingia na kuamua kuhusu Uchaguzi wa Kenya mwaka 2017 na 2022.

Tumeona pia namna Tume za Uchaguzi za Ghana na Malawi zilivyosimama kidete mara kadhaa kuhakikisha vyama vilivyopata ushindi kwenye uchaguzi ndivyo vyama vinavyotangazwa kushinda.

Kwa vyovyote vile, hatua inayofuata kwa vyama vya ACT Wazalendo na Chadema ni kuhakikisha kwamba sheria rafiki za uchaguzi zinakuwa mezani kufikia uchaguzi wa mwaka 2025. Muhimu zaidi ni marekebisho ya kuhakikisha Tume za Taifa za Uchaguzi za NEC na ZEC zinakuwa na mfumo na aina ya watu waadilifu wasioweza kufanya mambo yaliyo kinyume na haki.

Jambo ambalo wakosoaji wa Mbowe na Zitto hawawezi kulisema hadharani ni kwamba ili kufikia hatua ya kutengeneza Tume ya Uchaguzi na Mahakama Huru ni muhimu kwanza kuwe na maridhiano baina ya watawala.

Kama hakuna kuaminiana na kuelewana miongoni mwa watawala, si kazi rahisi kwa walio madarakani kukubali jambo lolote litakalohatarisha kuendelea kwao kubaki walipo. Kama kuna maelewano baina ya watawala lakini Tume za Uchaguzi zinaongozwa na watu wa aina ya Mzee Jecha, hali ya uchafuzi wa uchaguzi itabaki kuwa hii iliyopo.

Nani anapata nini?

Ni rahisi kuona Rais Samia anapata nini kupitia maridhiano yanayoendelea hapa nchini. Jambo la muhimu kuliko yote ni kwamba limesaidia kusafisha taswira ya Tanzania iliyokuwa imeanza kuchafuka kutokana na utawala wa Magufuli.

Kusafishika kwa kwa taswira kutasababisha kuongezeka kwa watu, taasisi na kampuni za kigeni zitakazotaka kuja kuwekeza, kufanya biashara na kutalii hapa nchini.

 Ziara ya hivi karibuni ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, nchini Tanzania ilielezwa kama alama mojawapo ya mafanikio kwa aina ya siasa za maridhiano anazofanya Rais Samia tangu aingie madarakani.

Kwa uhusiano huo na dunia, Rais Samia anajua serikali yake itaweza kupambana na changamoto zinazomkabili nchini kwake hivi sasa – masuala kama ajira, elimu na afya. Kwa upande mwingine, anafahamu kwamba chama chake kina mtaji wa kutosha kushindana na hoja za wapinzani.

Kama alivyopata kusema Rais mstaafu wa Marekani; ”It’s the economy, stupid”. Kwamba, endapo hali ya uchumi kwa wananchi itakuwa nzuri, hakuna mgombea atakayeshindwa uchaguzi. Kwa maneno na matendo ya Rais Samia, endapo CCM itafanikiwa kutatua kero za wananchi, kitaendelea kubaki madarakani pasipo kutumia mabavu na ukatili.

Hatari pekee kwa mwenendo wa Rais Sami ani endapo mabadiliko yake anayoendelea kiuchumi hayatazaa matunda ama kutokana na changamoto za ndani au nje ya nchi. Kama maridhiano yatashindwa kuongeza ajira na kupunguza makali ya maisha – wahafidhina ndani ya CCM na Chadema watataka kufuata njia nyingine – bila shaka wakisukumwa kufanya hivyo na wananchi.

Hatari iliyopo kwa Mbowe na Zitto ni kwamba endapo Rais Samia atachanga karata zake vizuri kiuchumi, upinzani utaendelea kuwa upinzani kwa muda mrefu kutoka sasa. Na wahafidhina kwenye vyama vyao watalaumu kwamba ni viongozi wao ndiyo waliowaingiza huko.

Huo ndiyo mzigo ambao Rais Samia, Mbowe na Zitto wanaubeba sasa katika kipindi hiki. Hakuna ajuaye nani atavuna mabua na nani atavuna mahindi.

Lakini kwa sasa, angalau wananchi ndiyo wameshinda. Na faida iko kwa Rais Samia. Angalau kwa sasa maana siasa ni bando kama lilivyo lile la kwenye simu. Lina muda wa kuanza na kumalizika matumizi yake.

Picha kwa Hisani ya Ikulu

Mwisho.