Rais Julius Nyerere akiwa na Henry Kissinger jijini Dar es Salaam mwaka 1976. Picha kwa Hisani ya Cambridge University Press
Na Ahmed Rajab
DAKTA Henry Kissinger aliyefariki dunia Kent, Connecticut, Marekani, Novemba 29 mwaka huu alikuwa mwingi wa mengi. Alikuwa msomi wa hali ya juu, gwiji wa diplomasia, mshauri wa siasa za kimataifa na mwanasiasa.
Kabla ya kuzivaa siasa, Kissinger alikuwa akisomesha katika Chuo Kikuu cha Harvard, kimoja kati ya vyuo vikuu ‘babu kubwa’ duniani. Miongoni mwa wanafunzi wake alikuwa kijana kutoka Uganda, Mahmood Mamdani, ambaye sasa ni profesa aliyebobea wa sayansi ya siasa.
Uzoefu wa Kissinger wa siasa za kimataifa ndio uliomchongea akawa anasakwa na marais na mawaziri wakuu wa nchi nyingi waliokuwa wakitaka wafaidike kwa ushauri wake.
Mwenyewe Kissinger alikuwa akizipalilia sifa hizo. Kwa vile alikuwa na hulka ya kupenda kutukuzwa, alikuwa akizikuza sifa hizo na wakati huo huo akizikana tuhuma za kwamba alikuwa mhalifu wa vita. Sina shaka kwamba historia ya karne ya 20 itamhukumu kwa mauaji ya halaiki ya watu katika Vietnam, Cambodia, Laos na Pakistan ya Mashariki, ambayo leo ni Bangladesh.
Kissinger alikula chumvi nyingi; alipofariki alikuwa na umri wa miaka mia. Bado bongo lake lilikuwa likifanya kazi. Na mwenyewe akiendelea kufanya kazi, akichupa kwa ndege kwenda huku na huku, akiwashauri viongozi wa mataifa kadhaa. Mwezi Julai mwaka huu, akiwa tayari amekwishatimia miaka mia, aliizuru China na alionana na Xi Jiping pamoja na waziri wa ulinzi wa nchi hiyo, Li Shangfu.
Li alilalamika kwamba kuna baadhi ya watu Marekani walioyafuja ‘mawasiliano ya kirafiki’ baina ya China na Marekani kwa sababu walikuwa hawataki Marekani ipatane na China. Kwa kiwango kikubwa uhusiano kati ya Marekani na Jamhuri ya Watu wa China ulijengwa kwa juhudi kuu za kidiplomasia za Kissinger alipokuwa waziri wa mambo ya nje chini ya Rais Richard Nixon. Aliushika wadhifa huo pia chini ya Gerard Ford, Rais aliyemfuatia Nixon.
Kuanzia siku hizo Kissinger amekuwa akivuma katika medani za siasa za kimataifa. Wenye kumjua wamelisifu bongo lake kwa namna mbili. Kuna wasemao kwamba lilikaa kama mchwa na kuna wasemao kwamba lilikaa kama tembo kwa kukumbuka mambo. Bila ya shaka kumbukumbu zake zikimsaidia alipokuwa akizichambua siasa za kimataifa na migongano ya madola makuu.
Nakumbuka jinsi alivyokuwa akisifiwa katika nchi za Magharibi kwa umahiri wake. Nakumbuka pia jinsi Mwenyekiti Mao Zedong wa China alivyonukuliwa baada ya kukutana naye kwa mara ya mwanzo. Mao alimponda kidogo Kissinger kwa kusema kwamba hakuwa mahiri hivyo.
Kissinger alikuwa na mvuto wa aina yake. Alikuwa mfupi, kitipwatipwa kidogo, macho yake yalikuwa kama ya bundi, na alikuwa na sauti nene ya kivivuvivu.
Kissinger alikuwa na ujanja wa sungura na aliutumia katika diplomasia. Ndio maana akipenda kufanya mambo chini kwa chini, kuichonga na kuiendesha diplomasia yake bila ya ulimwengu kujua. Kwa mfano, alipokuwa akijaribu kuanzisha mawasiliano na China, iliyokuwa siku hizo ikiongozwa na Mao, Kissinger akimtumia Jenerali Yahya Khan, kiongozi wa kijeshi wa Pakistan, iliyokuwa na uhusiano mzuri na China.
Mwaka 1971 alipokuwa mkutanoni Pakistan, Kissinger alijitia ugonjwa ili kuubabaisha ulimwengu. Ukweli ni kwamba alipanda ndege kwa siri, akavuka mpaka akaingia China alikofanya mazungumzo na viongozi wa huko. Mazungumzo hayo hatimaye yalimwezesha Rais Richard Nixon aizuru China 1972, akiwa Rais wa mwanzo wa Marekani kufanya hivyo.
Aprili 25, 1976, saa moja na dakika tano za Magharibi Kissinger alijikuta Ikulu, Dar es Salaam. Alibaki hapo hadi saa mbili na robo za usiku. Muda mfupi akaingia Mwalimu Julius Nyerere akiwa na Joseph Butiku, katibu wake muhtasi. Baada ya kulahikiana huku wakipigwa mapicha, Nyerere alimjulisha Kissinger kwa mama yake na familia yake. Baada ya hapo, akaingia naye ndani ya ofisi yake kwa mazungumzo ya faragha.
Nimenukuu mazungumzo haya kutoka katika nyaraka za siri za Marekani zilizoruhusiwa kutolewa hadharani, Foreign Relations of the United States, 1969–1976, Volume XXVIII, Southern Africa.
Kissinger: ‘Nimefurahi sana kupata fursa hii ya kukutana nawe.’
Angetaka angezuia hapo. Lakini aliendelea na akamlazia Nyerere kwa kumwambia kwa nini alijawa na furaha hiyo:
Kissinger: ‘kwa sababu hakuna watu wengi upande huu wa dunia wanaoweza kuyaongoza matukio kifalsafa. Ni rahisi kuyashughulikia masuala ya sasa. Lakini bila ya kuwa na ufahamu wa kifalsafa, unakuwa unayatanzua masuala yanayokukabili wakati huu tu.’
Nyerere: ‘Sawa.’
Baada ya hapo Kissinger akaanza kufafaruka. Alimwambia Nyerere kwamba kabla ya kuyasikiliza maoni yake kuna mambo mawili aliyotaka kuyataja. Kwanza alimtaka Nyerere asiziamini ripoti za magazetini kwamba dhamira ya safari yake ya Afrika ilikuwa kuunda chama cha ukombozi kitachodhaminiwa na Marekani au kuusaidia utawala wa wazungu wa Rhodesia [Zimbabwe ya leo].
Kuhusu Rhodesia alimhakikishia Nyerere kwamba alikuwa tayari kutumia nguvu za Marekani kusaidia ukombozi wa Rhodesia ili Smith [waziri mkuu Ian Smith wa Rhodesia] na Vorster [waziri mkuu John Vorster wa Afrika ya Kusini] wauelewe kinaganaga msimamo wa Marekani. Pili, Marekani haitaki kuona mapande Afrika. Muungano wa Sovieti na Marekani zisiwe na mapande Afrika, kwa sababu iwapo kutakuwako mapande basi Afrika itakuwa uwanja wa migogoro kutoka nje.
Kissinger: ‘Sipendi kufanya ziara za kirafiki, lakini napenda kuona matokeo [kutokana na ziara].’
‘Niko tayari kukubali makosa tuloyafanya. Tulikuwa na Vietnam, Mashariki ya Kati, Watergate; hatukuweza kufanya kila kitu wakati mmoja.’
Kwa ufupi, Kissinger akaendelea kumwambia Nyerere kwamba Marekani iko tayari kufanya kazi naye kuhusu Afrika.
Nyerere: ‘Bwana Waziri, ninashukuru sana sana kupata fursa hii ya kukutana nawe. Tutakutana tena usiku na nitakuwa na fursa ya kusema haya rasmi mbele ya rafiki zangu. Tumefurahi sana kupata fursa hii ya kujadiliana nawe faraghani kuhusu matatizo yetu.’
Kissinger alimsikiliza kwa makini Nyerere alipokuwa akiuchambua ukoloni wa Rhodesia na utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini.
Nyerere: ‘Wakati mwingine tuna matatizo yetu, wakati mwingine matatizo ya kazi, na kwa nchi kama Tanzania, kuna wakati huwa taabu kuupata uhuru. Na tunauhitaji na kuuthamini msaada na walau uelewa wa madola makubwa. Kwa hivyo tunaithamini sana fursa hii.’
Kissinger: ‘Msaada wa aina gani unaufikiria?’
Nyerere: ‘Katika Kusini mwa Afrika. Tutaeleza maoni yetu. Mambo yanabadilika. Kilichohitajika mwaka ’75 huenda kisihitajike leo. Tunataka utawala wa Rhodesia uwekewe shinikizo; tunataka shinikizo juu ya Vorster kuhusu Namibia, na hatimaye tunataka mageuzi katika Afrika Kusini. Hatuwezi kuishi na Afrika Kusini kama ilivyo sasa.’
Halafu Nyerere akamuuliza Kissinger ni nini Marekani inachoweza kusaidia si kwa mujibu wa uwezo wake, lakini kwa mujibu wa mfumo wake, kwani alisema anajua Marekani haiwezi kutoa silaha kwa ajili ya shughuli za ukombozi.
Kissinger: ‘Bila shaka tuko tayari kuwa na uelewa, na tuko tayari kufanya zaidi ya hayo, kuangalia msaada gani tunaweza kuutoa. Ni dhamira yangu kuwa na mawasiliano na viongozi kama wewe…Sisi tutaangalia kwa kuuzingatia Muungano wa Sovieti; nyiye mtaangalia kwa kuzingata Afrika huru. Lakini niko hapa kujifunza.Tunaamini kwamba bila ya utawala wa walio wengi, hapawezi kupatikana amani na maendeleo ya Afrika huru. Nchi nyingine zinaweza kushiriki. Viongozi kama wewe mnajua namna ya kuyatumia madola makubwa kwa maslahi yenu. Lakini ni tatizo kwetu kwa nchi kama Angola ambako kuna majeshi ya kigeni. Lakini azma yetu ni kuzuia hali kama hizo zisizuke.
Utawala wa Rhodesia hauwezi kudumu tukiwa na umoja na tukifanya kazi kwa dhati. Namibia pia. Bila ya shaka tatizo la Afrika Kusini ni gumu zaidi.
Nyerere: Hayo ndo maoni yangu. Kusini mwa Afrika ni eneo zima — Ureno, Afrika Kusini — lakini hatuwezi kulitatua tatizo hilo zima kwa mpigo mmoja.
Baada ya kusema hayo Nyerere akamueleza Kissinger kwamba Rhodesia na Namibia ndizo zilizokuwa vipaumbele vya zile zilizokuwa zikiitwa nchi za mstari wa mbele.
Nyerere aliongeza kwamba ingawa suala la Afrika Kusini lilikuwa gumu lakini hata hivyo wao wataendelea kusema kwamba lengo ni kuwa na utawala wa walio wengi nchini humo.
Kissinger alikubaliana na Nyerere na akamwambia alikuwa na azma ya kuyasema hayo kwenye mkutano ataokuhudhuria Lusaka.
Kissinger: ‘Natumai nitasema mambo unayokubaliana nayo. Nitakupa nakala [ya hotuba]. Utaona kwamba naichambua Rhodesia zaidi kuliko Namibia, na Namibia zaidi kushinda Afrika Kusini…Nitazitaka nchi zilizo jirani ziufunge mpaka wao na Rhodesia. Unaonaje?”
Nyerere: ‘Hiyo ni fikra nzuri kabisa. Barabar. Seretse Khama [Rais wa Bostwana] anapiga hesabu za gharama.’
Kissinger: ‘Nitazitaka zifanye hivyo ingawa sitozitaja kwa majina, na nitaahidi msaada wa Marekani.’
Nyerere: ‘Barabar.’
Kissinger: ‘Nitasema kwamba Afrika Kusini inaweza kujithibitisha kwamba ni nchi ya Kiafrika kwa kutoiunga mkono Rhodesia. Na nitazungumza kuhusu kuzipa misaada nchi za Kiafrika.’
Nyerere: ‘Barabar’.
Kissinger: ‘Unamuonaje Machel [Samora Machel, Rais wa Msumbij]? Nikitaka kukutana naye, lakini unaonaje nikikutana naye kwenye mkutano wa UNCTAD?’
Katika mkutano wao wa mwanzo Kissinger na Nyerere walipatana. Walikaa kama sungura wawili wakipanga nani aseme nini hadharani.
Kissinger: ‘Kesho utakutana na waandishi wetu wa habari, na nimefurahi. Itasaidia ikiwa hotuba yangu haitoonekana kama imeshinikizwa nawe. Bora ionekane kuwa ni uamuzi wetu wenyewe.’
Nyerere: ‘Barabar. Ninaelewa.’
Kissinger: ‘Unaweza kusema umeridhika, au una matumaini, au chochote kile.’
Vipi Msumbiji?
Nyerere: ‘Tulisaidia kuijenga Frelimo [chama cha ukombozi wa Msumbiji]. Sisi na China.’
Kissinger: ‘Na umeona hatukupinga.’
Saa mbili kasoro dakika mbili, walielekea kwenye chumba kikubwa cha mkutano, ambako Nyerere aliwajulisha wenzake kwa Kissinger na aliofatana nao. Nyerere aliwakaribisha mvinyo lakini Kissinger alikataa.
Nyerere: ‘Hunywi mvinyo!’
Kissinger: ‘Naam. Sinywi.’
Nyerere: ‘Mimi nilikuwa sinywi. Mpaka ulipopatikana ushindi Msumbiji. Sikuwa na maingiliano na Ureno. Nilikuwa siujui mvinyo wa Kireno. Halafu Samora [Machel] akagundua misururu ya chupa za mvinyo katika ghala. Akaniletea. Kwa hivyo, watakupeni. [Vicheko]
Kwa vile Samora ndiye aliyeniletea, ninaiita ‘Samora.’ [Vicheko] Husema: ‘Niletee Samora.’ [Vicheko]
Kissinger: ‘Huwezi kujua jinsi nilivyotaka kukutana nawe.’
Nyerere: ‘Miye pia.’
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; @ahmedrajab/X
Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.