Na Ezekiel Kamwaga
SIKU moja tukiwa New Delhi, India, kwenye ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alifanya mkutano na waandishi wa habari wa Tanzania tuliokuwa pale. Nakumbuka alipomaliza mkutano, nilikwenda kumshika mkono na kumkumbatia, nikamueleza kwamba nimefurahi kwa kilichotokea.
Bashe alikuwa ametoka kueleza waandishi wa habari kuhusu makubaliano ya Tanzania na India kwenye biashara ya mbaazi na korosho ambayo ikifanyika, nchi yetu itaingiza mabilioni ya shilingi. Wakati ule kulikuwa na mjadala mkubwa nchini kuhusu umuhimu wa ziara za viongozi nchi za nje na dili na India ilikuwa na thamani kubwa kuliko ziara zote za viongozi wa Tanzania nchi za nje.
Mwanasiasa huyu amejibanaisha kama kiongozi ambaye kila analofanya wizarani kwake lina lengo la kuboresha maisha ya wakulima na biashara kwa Watanzania. Ubunifu wa Building Better Tomorrow (BBT) ni miongoni mwa miradi ambayo inaweza kunasibishwa moja kwa moja na utawala wa Rais Samia.
Kwa muda mrefu, Wizara ya Kilimo ilikuwa haina waziri anayeonekana kufahamu umuhimu wa wizara hiyo kwa watu wetu na uchumi wetu. Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, Wizara ya Kilimo inaonekana imepata mtu anayejua nini kinahitajika kufanywa. Mwaka 2023 umetuonyesha kwamba Bashe walau ana nia ya kuacha alama wizarani hapo.