Na Ahmed Rajab
UHUSIANO baina ya Tanzania na Comoro unatazamiwa kupaa na kukua baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Saidi Yakubu kuwa balozi mpya wa nchi yake visiwani Comoro. Yakubu aliyehitimu shahada ya sheria nchini Uingereza kabla ya kurudi Tanzania na kufanya kazi bungeni na baadaye kuwa katibu mkuu katika wizara ya utamaduni, sanaa na michezo, anasifika kwa utendaji kazi wake.
Waliowahi kufanya kazi naye wameliambia Gazeti La Dunia kuwa Yakubu si mtu aliyezubaazubaa, wa kumangamanga, kama wasemavyo vijana siku hizi. Ni mtu mahiri, mwenye kujiandaa kabla ya kupambana na jukumu lolote lililo mbele yake. Si mtu wa kupigana, au wa kushindana, na vivuli.
Na kuna vivuli vingi katika ngazi hizo za juu za utumishi wa umma vinavyoweza kumbabaisha mtu.
Ninavyoyaandika haya ninayakumbuka aliyowahi kunambia sahibu yangu mmoja mwenye uzoefu mkubwa wa siasa za barani Afrika, hasa za nchi zilizowahi kutawaliwa na Ufaransa. Yeye aliifananisha Comoro na kisiwa cha Corsica cha Ufaransa kinachodhibitiwa na majambazi wa Mafia. Alinambia kwamba ni muhali mtu kuupata ukweli wa yanayojiri Comoro ikiwa huna mtu wa ndani mwenye kuielewa mikondo ya kisiasa ya visiwani humo. Wengi wanayajua ya juujuu tu lakini ya ndani yanawakwepa. Hiyo ni changamoto kubwa atayokumbana nayo Yakubu.
Pengine balozi huyo mteule tayari anazijua baadhi ya changamoto atazokabiliana nazo Moroni, mji mkuu wa Comoro. Ninasema haya kwa sababu hivi ninavyoyaandika makala haya, ninaviona visiwa hivyo vikiwa katika hali ya taharuki. Mwenyeji mkuu wa Yakubu, yaani Rais Azali Assoumani, kwa vitendo vyake amejitia kile ambacho Wacomoro wanachokiita ‘msajaja’, ni kama amejitia kitanzi. Matokeo yake ni kwamba amekuwa rahisi kupigwa mishale kutoka kila upande.
Wapinzani wake wameungana kumpinga, Marekani, ikijaribu kuipiku Ufaransa, inampiga vita. Ufaransa, iliyokuwa mkoloni wa visiwa hivyo, imekuwa na kigeugeu juu ya Azali, na wananchi wanazidi kupaza sauti za kumkataa.
Siku ya siku ya Azali inawadia, Yakubu akiwa anajitayarisha kufunga safari kuelekea Moroni.
Siku yenyewe ni 26 Mei ambapo Azali anatazamiwa kuapishwa kwa muhula mwingine wa miaka mitano ya urais. Gavana wa kisiwa kikubwa cha Ngazidja (Grand Comoro), Ibrahim Mze Mohamed, anayemuunga mkono Azali, anatarajiwa naye kuapishwa siku tatu kabla ya hapo.
Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI) ilitangaza kwamba katika uchaguzi uliofanywa Januari 14, mwaka huu, Rais huyo aliibuka na ushindi wa asilimia 63. Wapinzani wanabisha. Wanasema kwamba wana ushahidi ya kwamba uchaguzi huo ulikuwa wa bandia.
Wapinzani wanasema uhuni mkubwa ulifanywa wa kufakamiza makaratasi ya kumpigia kura Azali ndani ya masanduku ya kura. Wanadai pia kwamba hata hivyo Azali alitokea watatu na hakuwa mshindi.
Matokeo ya uchaguzi yalipotangazwa Januari 17, palizuka maandamano katika sehemu kadhaa za Moroni. Wanajeshi waliingia mitaani kupambana na waandamanaji walioweka vizuizi barabarani na kuichoma moto nyumba ya waziri mmoja wa zamani.
Azali amesema kuwa amewaalika marais sita kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwake. Ingawa hadi ninavyoyaandika haya hakuyataja bado majina ya marais aliowaalika inatazamiwa sana kwamba miongoni mwao ni Marais Samia na William Ruto wa Kenya.
Azali ana usuhuba mkubwa na Tanzania na Kenya lakini nchini mwake anaonekana kuwa ni tatizo. Kwa muda wa miaka 25 amekuwa katika safu ya mbele ya siasa za Comoro na kwa kipindi kikubwa amekuwa akizidhibiti. Lakini kabla ya kuanza kuzicheza siasa Azali alikuwa jeshini alikokuwa na cheo cha kanali baada ya kupata mafunzo ya kijeshi Morocco (alikofunzwa uaskari wa mwavuli) na Ufaransa.
Mzaliwa huyu wa Mitsoudjé, mji wa kusini mwa kisiwa cha Ngazidja, alilitumia jeshi kujitumbukiza katika siasa aliponyakua madaraka kwa kumpindua Rais Tadjidine Ben Said Massounde mnamo Aprili 30, 1999. Hapo ndipo alipoanza kuyaonja madaraka na kuuona utamu wake. Mapinduzi hayo yalikuwa takriban ya ishirini kufanywa visiwani humo tangu vijitangazie uhuru kutoka Ufaransa 1975.
Azali alichaguliwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2002 baada ya wapinzani wake wakuu, Mahamoud Mradabi na Said Ali Kemal kususia duru ya pili ya uchaguzi. Mradabi na Kemal walilalamika kwamba duru ya kwanza ilikuwa na mizengwe.
Azali alichaguliwa tena 2016, 2019 na Januari mwaka huu. Alipata heshima pia ya kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa mwaka mmoja kutoka Februari mwaka jana hadi Februari mwaka huu. Katika muda wote wa utawala wake, Azali amekuwa akituhumiwa kutawala kwa mabavu na kuwafunga wapinzani wake, hasa Rais wa zamani, Sayyid Ahmed Abdalla Sambi.
Hivi karibuni amemtia ndani Mohamed Daoud ‘Kiki”, mmoja wa wagombea urais watano waliochuana naye mwaka huu. Washindani hao wote watano wameungana kupinga kuapishwa kwa Azali. Kwa kama wiki mbili sasa wapizani hao wamekaa kimya na kimya hicho kimemtia wahka mkubwa Azali. Kulikoni? Amekuwa akijiuliza na bado hajalipata jibu.
Azali anahangaishwa pia na harakati zinazofanywa nje ya nchi na mwanasheria kijana Said Larifou. Si wengi wenye kujua kwamba Mcomoro huyo ndiye aliyewaongoza mawakili waliomtetea Ousman Sonko, aliyekuwa mpinzani mkuu wa Rais wa zamani wa Senegal Macky Sall, na ambaye sasa ni waziri mkuu wa nchi hiyo.
Sonko ndiye aliyewahamasisha vijana wa Senegal wamchague Bassirou Diomaye Faye awe Rais wa nchi yao katika uchaguzi wa Machi mwaka huu. Angeupigania yeye uchaguzi huo wa urais lakini sheria ilimzuia kwa vile alikuwa amepatikana na hatia ya jinai na aliwataka wananchi wenzake wamchague Diomaye Faye akisema: ‘Diomaye ni Sonko.’
Zamani Larifou aliwahi kuwa chanda na pete na Azali na aliwahi kuwa msemaji wake wa mambo ya sheria. Baadaye alimgeukia Azali, akafungwa Comoro na hata aliwahi kupigwa risasi wakati wa maandamano ya uchaguzi mwaka 2019. Larifou, anayejulikana mitaani kwa jina la chama chake ‘Ridja’ (Tumekuja), amepata umaarufu wa ghafla katika duru za wanamajumui wa Afrika kwa namna alivyokuwa akimtetea Sonko, Senegal.
Ana jina katika duru za mrengo wa kushoto katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi, hasa Guinea, Mali na Senegal, ingawa hajawahi kuwa pamoja na wanamajumui wa Afrika au wafuasi wa siasa za kisoshalisti katika Reunion, Ufaransa, Madagascar au kwingineko katika ukanda wa Afrika Mashariki. Mahasimu wake wanamtuhumu kwamba akishirikiana na Wafaransa dhidi ya maslahi ya wananchi wa Reunion na Mayotte na kwamba akiwaunga mkono waliokuwa wakitaka kujitenga katika kisiwa cha Anjouan (Nzuwani).
Hivi sasa Larifou, aliyezaliwa Foumbouni, kusini mwa Ngazidja, amejitosa kuwasaidia wapinzani wa Azali.
Tukiuacha msuguano huo unaoendelea baina ya Azali na wapinzani wake, labda changamoto kubwa kabisa atayoikabili balozi mteule Yakubu, ni suala la Mayotte, kisiwa chane cha Comoro ambacho bado kinatawaliwa na Ufaransa. Inasikitisha kuiona Tanzania iliyokuwa mstari wa mbele kusaidia ukombozi wa Comoro ikiwa sasa imepwaya na kuonekana kana imeridhia Mayotte iendelee kutawaliwa na Ufaransa kinyume na msimamo wa Umoja wa Afrika.
Kuna wasemao kwamba Ufaransa ina nguvu na ushawishi mkubwa juu ya Tanzania na kwamba nchi hizo zimekuwa na uhusiano madhubuti tangu zilipolitambua jimbo la Biafra lilipojitenga na Nigeria 1967. Rais wa Ufaransa wa wakati huo alikuwa Charles de Gaulle na wa Tanzania alikuwa Mwalimu Julius Nyerere. Inasemekana kwamba Rais wa tano wa Ufaransa Jacques Chirac ndiye hasa aliyeitaka Tanzania iwe ‘inaiangalia’ Comoro.
Katika miaka ya karibuni pamekuwako na ushirikiano baina ya Baraza la Biashara la Tanzania na Ufaransa (FTCC), kwa upande mmoja, na Mayotte, kupitia Shirika la Maendeleo la Kifaransa, ADIM. Na mwanzoni mwa wiki hii Manispaa ya Mji wa Mayotte wa M’Tsangamouji na Manispaa ya Jiji la Zanzibar zilitiana saini mkataba wa udugu baina yao.
Mkataba huo una azma ya kuwaunganisha vijana wa miji hiyo katika mambo ya michezo, utamaduni, afya, elimu na mazingira. La kuhuzunisha ni kwamba Baraza la Manispaa la Zanzibar lilipokuwa likitiana saini mkataba huo lilikuwa, kwa hakika, likiidhinisha ukoloni wa Ufaransa katika kisiwa cha Mayotte. Ajabu ya mambo ni kwamba hata Meya wa M’Tsangamouji, Said Maanrifa Ibrahima, alihudhuria hafla ya utiaji saini akiwa amevaa bendera ya Ufaransa.
Pengine utajiuliza: kwa nini Ufaransa inaking’ang’ania kisiwa cha Mayotte? Kwa nini imewekeza sana kisiwani humo? Na kwa nini kila rais wa Comoro aliyejaribu kuidai Mayotte aliuawa?
Nathubutu kusema kwamba si Tanzania peke yake iliyo gizani kuhusu Mayotte na yanayojiri huko. Afrika nzima haisikii wala haioni yanayotokea kwenye kisiwa hicho. Umuhimu wa Mayotte kwa Ufaransa ni wa kimkakati. Ufaransa, ikishirikiana na Ujerumani, ina kambi kubwa ya jeshi la wanamaji kisiwani humo. Kambi hiyo ina mfumo wa kielektroniki na iko kama mita 100 hadi 200 chini ya mlima wa volkano.
Umuhimu wa kambi hiyo, yenye kuendeshwa na idara za kijasusi za Ufaransa na Ujerumani, ni uwezo wake wa kuyanasa mawasiliano ya eneo zima la Mashariki ya Kati pamoja na ya Afrika.
Visiwa vya Comoro ni vidogo, siasa zake ni chafu lakini juu ya hayo bado wako wengi wenye kuvitapia. Sababu ni utajiri wake wa baharini ukiwa pamoja na akiba za mafuta ambayo bado hayajaanza kuchimbwa. Hofu iliyopo ni kwamba askari wa kukodiwa, mamluki, kutoka nchi za Magharibi wangali wamekaa chonjo na mtandao wao mpana. Wanatumai watapata fursa nyingine ya kuucheza mchezo waliouzoea Comoro wa kuziingilia siasa za huko.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; @ahmedrajab/X.
Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.