“Baba yenu ni Doto, Uwaziri umekuja na utaondoka”

Picha: Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko (kulia), akisalimiana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika mojawapo ya matukio ya kiserikali hivi karibuni.

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

DESEMBA 30, mwaka 1978, mapacha walizaliwa katika familia moja ya wakulima huko Bukombe. Wazazi hawakuwa na uwezo wa kuhudumia mapacha hao peke yao huku wakiendelea na shughuli zao za kutafuta riziki kama kawaida; ikabidi jukumu la kuwalea liangukie kwa dada wa mapacha hao. Huyu ndiye dada ambaye ilibidi akatishwe maisha yake ya shule ili hatimaye Kulwa na Doto Biteko – Naibu Waziri Mkuu mpya wa Tanzania, wapate mtu wa kuwalea.

 

Kwenye mazungumzo na marafiki zake, Biteko ambaye cheo chake rasmi cha sasa ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, hueleza kuhusu kuzaliwa kwake huku na makuzi yake kulivyomjenga kwenye maisha yake ya sasa. Kwanza, kwamba Mungu hakutaka awe mpweke na ndiyo maana alimpa mtu wa kuishi naye angali tumboni mwa mama yake na pili kwamba kufika alipofika sasa kuna mchango wa watu wengine.

 

Ukifanikiwa kumtembelea nyumbani kwake – iwe Bukombe au Dar es Salaam, huwezi kukosa wageni wenye masuala mbalimbali ambayo wanaomsubiri ili aweze kuwatatulia. Nilipomuuliza siku moja anapokeaje changamoto hiyo ya kuwa mtu wa wageni – alinipa jibu moja rahisi; kwamba “Kama Mungu amekupa watu wa kukuletea shida na changamoto zao, Mungu huyohuyo atakupa namna ya kutatua shida na changamoto hizo”.

 

Kupanda kisiasa kwa Doto Mashaka Biteko kwenye kipindi cha takribani muongo mmoja tu uliopita ni miongoni mwa hadithi za kisiasa ambazo pengine zinawezekana Tanzania peke yake. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipomtangaza kuwa Naibu Waziri Mkuu wiki mbili zilizopita, swali kubwa ambalo watu walianza kujiuliza lilikuwa ni kwa nini na ni nani hasa mwanasiasa huyu? Makala haya yatajaribu kujibu swali hili kwa ufupi.

 

Ni nani huyu Biteko?

 

Wakati hayati Rais John Magufuli alipomteua Biteko kuwa Naibu Waziri wa Madini mwaka 2017, si watu wengi walikuwa wakimfahamu. Kuondoa wananchi wa Bukombe waliomchagua kuwa mbunge wao kwa mara ya kwanza mwaka 2015, watu aliosoma na kufanya nao kazi na watu waliofahamu duru za kibunge, ni wachache walikuwa wanamfahamu.

 

Lakini ndani ya Bunge, tayari jina lake lilikuwa limeanza kuwa maarufu. Ingawa ilikuwa mara yake ya kwanza kuingia bungeni, alipata nafasi ya kugombea na kushika wadhifa wa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini. Michango ya kamati yake – katika wakati ambapo Tanzania ilianza kufanyia marekebisho ya kisheria na uhusiano wake na kampuni za kimataifa za sekta ya uziduaji, kulifanya awe katika viti vya mbele kabisa kushuhudia kinachoendelea.

 

Mwaka 2018, akateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Madini na Januari 2019 Magufuli akampandisha cheo kuwa Waziri kamili. Akaendelea na wadhifa huo baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na Rais Samia akamwacha hapo hadi alipofanya mabadiliko ya karibuni ya baraza la mawaziri. Lakini ni nini hasa Doto – msomi wa kiwango cha shahada ya uzamivu (PhD) amefanya katika wizara hiyo tangu awe waziri mwaka 2019?

 

Kuna mengi. Lakini mawili yana ushahidi wa takwimu. La kwanza ni kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa. Wakati akianza kuwa waziri, mchango ulikuwa chini kidogo ya asilimia nne. Mwaka jana, mchango ulikuwa umefikia kiwango cha asilimia 7.3 na kulikuwa na matarajio ya kufikia asilimia 10 kufikia mwaka 2025.

 

Lakini hadithi ya kusisimua zaidi ipo katika ukuaji wenyewe. Kwa muda mrefu, kulikuwa na malalamiko kwamba sekta ya madini hapa nchini imetawaliwa na wachimbaji wakubwa ambao ni kampuni za kigeni. Chini ya Biteko, mchango wa wachimbaji wadogo kwenye sekta hiyo umeongezeka karibu mara mbili – kutoka chini ya asilimia 20 hadi zaidi kidogo ya asilimia 40.

 

Na ukuaji huo unahusu kuongezeka kwa masoko ya mauzo ya madini ambayo yamepunguza biashara ya magendo ya bidhaa hiyo na kupunguza kero kwa wachimbaji wadogo. Ilikuwa bahati kwa Wizara ya Madini kupata waziri ambaye alikuwa anajua taabu na adha ambazo wachimbaji wadogo walikuwa wanazipata na akafanya uamuzi wa muhimu wa kusaidia kundi hilo. Chini yake pia, Tanzania imefanikiwa kujenga viwanda vya uchenjuaji wa madini na hivyo kuongeza thamani hapahapa nchini.

 

Na amefanya hivyo pasipo kelele nyingi wala kufokafoka ambao ndiyo umekuwa utaratibu wa wanasiasa wengi vijana wa miaka ambayo yeye ameibuka kisiasa. Hakuna hata video moja iliyowahi kusambaa mitandaoni ikimuonyesha Doto akimfokea au kumdhalilisha mtumishi au mwekezaji kwenye eneo lake la kazi. Wala hakuna nyingine inayomuonyesha akijitapa kwamba ni yeye ndiye aliyefanya hiki au kile kwenye wizara yake.

 

Kuna mchapo mmoja mashuhuri kwenye Wizara ya Madini kumhusu waziri huyu. Mara baada ya kifo cha Magufuli, baadhi ya watumishi wa wizara hiyo walifikia hatua ya kufanya maombi maalumu na kufunga ili kwamba wakati Rais Samia atakapofanya mabadiliko, asimwondoe Biteko kwenye wadhifa wake huo. Labda maombi yao yalisikilizwa na jambo hilo likafanikiwa. Sijajua wafanyakazi hao wamepokeaje uteuzi huu wa sasa lakini walichofanya kinaonyesha kiwango cha uhusiano alichojenga na wenzake pale alipopokuwa.

 

Historia yake tangu akiwa chuoni ni historia ya uongozi. Wakati akisomea Ualimu katika Chuo cha Butimba, alikuwa Kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi. Alipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), alikuwa pia Kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi. Alikuwa pia kiranja enzi akiwa mwanafunzi katika shule za ngazi za chini alikopitia.

 

Kwa watu wanaomfahamu vizuri, wanajua kwamba kwanza kabisa Doto ni mwalimu. Mwalimu kwa maana ya mtu anayejua kuelekeza walio chini yake na pia anayejua ni wakati gani wa kuwa mkali na upi wa kuwa mpole. Kubwa zaidi, kama ambavyo walimu wengi watakwambia, Doto ni mtu anayependa kujifunza kila kukicha. Ndiyo sababu haikuwa ajabu kwamba alisoma na kufanikiwa kupata PhD yake wakati tayari akiwa ameingia kwenye siasa. Tangu awali, alikuwa na lengo la kufikia hatua hiyo ya kielimu kabla hajavuka miaka 45.

 

Biteko na Unaibu Waziri Mkuu

 

Uteuzi wake wa kushika wadhifa huu umemfanya Doto kuwa Mtanzania wa tatu kushika wadhifa huo. Wa kwanza akiwa Dk. Salim Ahmed Salim na wa pili akiwa hayati Augustine Lyatonga Mrema. Ni muhimu, kabla ya kuangalia kwa Biteko, kutazama mazingira na nyakati zilizosababisha kuwepo kwa wadhifa huo ambao si wa kikatiba.

 

Baadhi ya wakongwe wa siasa niliowahi kuzungumza nao miaka ya nyuma, uteuzi wa Salim ulikuwa “tactical” – kwa maana kwamba ni uamuzi uliochukuliwa kukidhi siasa za wakati huo. Ilikuwa inajulikana kwamba Dk. Salim alikuwa ndiye kipenzi cha Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere, na wengi wakitarajia ndiye angekuwa Rais baada yake. Mwinyi hakuwa akipewa nafasi mbele ya Salim.

 

Kwa sababu hiyo, cheo chochote ambacho Mwinyi angempa Salim bado kingeonekana ni cha chini. Wakati ule, cheo kikubwa baada ya Rais kilikuwa ni Waziri Mkuu. Lakini Salim asingeweza kuwa Waziri Mkuu kwa sababu Tanzania isingeweza kuwa na Rais na Waziri Mkuu kutoka Zanzibar. Ikabidi Mwinyi aibue cheo cha Naibu Waziri Mkuu ili walau mwanadiplomasia nguli huyo walau awe na cheo cha juu ya mawaziri wengine wa kawaida.

 

Uteuzi wa Mwinyi, kwa mara nyingine tena, kumfanya Mrema kuwa Naibu Waziri Mkuu pia ulikuwa na sababu. Miaka ya mwisho ya urais wa Mwinyi iligubikwa na tuhuma kadhaa za ufisadi na nchi kuwa na Rais mpole. Mrema alikuwa ndiye waziri kipenzi cha Watanzania wakati ule na tabia yake ya ukali ilitoa ahueni kwa serikali iliyokuwa inaonekana inaendeshwa kwenye autopilot.

 

Biteko anaweza kuwa amepewa wadhifa huo kwa sababu kadhaa. La kwanza, ambalo liko wazi zaidi, linahusu unyenyekevu na utiifu kwa mamlaka. Kama kuna kitu ambacho kimeanza kuonekana wazi kwenye utawala wa Rais Samia ni kuwa anajali sana watu wanaozungumza kwa ulimi mmoja kuhusu utawala wake. Ukitazama vizuri, utaona watu ambao wamemzungumzia vizuri Rais na baadaye wakapata vyeo.

 

Kwa hiyo la kwanza ni kwamba inaonekana Biteko ni mtu ambaye hajawahi kumzungumza vibaya Rais na utii na unyenyekevu wake kwa ofisi namba moja hauna shaka. La pili linahusu utendaji wake. Kote alikopita – kuanzia Uenyekiti wa Kamati ya Bunge na Uwaziri, Biteko ametimiza majukumu yake ipasavyo kwa kutimiza malengo yaliyowekwa.

 

Wizara ya Nishati ina mambo makubwa mawili yaliyo mbele yake; suala la Mradi wa LNG ulioko Lindi na Bwawa la Mwalimu Nyerere. Miradi hii miwili ni muhimu sana kwa Serikali ya Awamu ya Sita. Ni miradi ambayo itaongeza mapato ya serikali kwa kuingiza fedha za kigeni nyingi na pili kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme ambayo ni jambo kubwa kwa taifa letu.

 

Kama fedha za kigeni zitaanza kuingia kwa sababu ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa LNG na Bwawa la Nyerere kuanza uzalishaji huku Reli ya SGR ikiwa inaanza kazi, Rais Samia atakuwa na kazi ndogo kuwashawishi Watanzania wamchague tena kumalizia ngwe yake ya pili ya urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Si ajabu kwamba Doto ameongezwa hadhi kwa kuwa Naibu Waziri Mkuu kwa sababu wizara yake inashikilia walau theluthi moja ya kura za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi ujao.

 

Doto pia anatoka katika kundi wanalotoka asilimia kubwa ya Watanzania. Anaweza kujijenga na kuwa mtetezi na mnyanyuaji wa kundi la wanyonge na wavuja jasho – kazi ambayo Mrema alitakiwa kuifanya wakati wa Mwinyi. Lakini Biteko hana makeke wala tabia za kiaskari za mtangulizi wake huyo. Anachoweza kufanya – na ambacho ameonesha tayari kuwa anaweza kukifanya, ni kuonesha matokeo kwa kufanikisha uwepo wa umeme wa uhakika kwa wananchi na kuongeza mapato ya serikali kupitia nishati.

 

Doto hajawahi kusahau alikotoka. Mmoja wa rafiki zake alipata kunisimulia kuhusu mazungumzo ambayo Naibu Waziri Mkuu amekuwa akiwausia watoto zake kila apatapo nafasi. Msemo wake mashuhuri kwao ni kwamba “Baba yenu ni Doto, Uwaziri umekuja kama mgeni, kuna siku utaondoka.” Ujumbe pekee anaoufikisha kwa watoto wake ni kuwa yeye atabaki kuwa baba yao lakini uwaziri ni jambo la kupita.

 

Changamoto ya simu ya Magufuli

 

Mwaka 2020, pacha wa Biteko, Kulwa, aliamua kujitosa kuwania ubunge wa Jimbo la Busanda. Katika kinyang’anyiro cha ndani ya CCM, alifanikiwa kuibuka wa kwanza na ilitarajiwa chama kitampitisha kuwa mgombea ubunge wake kwenye uchaguzi huo. Hata hivyo, majina yalipotoka, Kulwa alikatwa na mtu aliyekuwa wa tatu alipewa nafasi hiyo.

 

Usiku mmoja katika nyakati hizo, Biteko alipokea simu ya Magufuli. Rais huyo, akizungumza kwa lugha ya Kisukuma – pengine akifahamu ndiyo lugha ya kwanza ya Doto na pengine atamwelewa vizuri zaidi, alimweleza kwa kina kwa nini CCM ilichukua uamuzi iliouchukua dhidi ya pacha wake. Naibu Waziri Mkuu hajapata kunieleza kwa kina kuhusu maelezo ya Magufuli kwake lakini nimewahi kumsikia Magufuli mwenyewe akieleza kwa wananchi kwa nini chama kilifanya hivyo.

 

Magufuli alisema kwamba kwanza hakuamini katika jambo la kuwa na watu wawili – Kulwa na Doto, kuongoza katika eneo moja na kueleza linaweza kuwa chanzo cha uongozi wa kindugu katika nchi. Lakini pili, alieleza kwamba kama Doto na Kulwa walizaliwa siku moja na eneo moja – iweje mmoja aongoze kwingine na mwingine kwingine? Kwa Magufuli, mbunge mzuri alitakiwa kuwa yule anayeongoza pale alipozaliwa – hasa kwa yale majimbo ya vijijini.

 

Hii ndiyo changamoto ambayo Biteko itabidi awe nayo kwenye wadhifa wake mpya. Kwa upande mmoja – yeye ni waziri mwenye Wizara anayopaswa kuifanyia kazi na matokeo yake kuonekana. Kwa upande mwingine, yeye pia ni mratibu wa shughuli za serikali ikimaanisha kwamba anahusika – kwa namna zaidi ya moja, kwenye utendaji wa serikali nzima.

 

Wenzake, kwenye Baraza la Mawaziri, watakuwa wanamwangalia kwa macho mawili; kama mwenzao lakini pia wa kwanza kati yao. Kama akitumia fimbo zaidi kuliko karoti, atajijengea maadui wa kudumu sasa na katika miaka ijayo kwenye maisha yake ya kisiasa. Kama akitumia karoti kuliko fimbo – kuna hatari ya yeye kuwa kuonekana kama Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; mtu rahimu lakini ambaye haonekani kama madaraka ya Waziri Mkuu yanamkaa barabara.

 

Ni matumaini yangu kwamba Doto anafahamu hili. Bahati nzuri, tangu awali kabisa, anafahamu kwamba Mungu hajawahi kutaka awe mpweke tangu tumboni mwa mama yake na kwamba mafanikio yake huwa yanachangiwa na watu wengine wa pembeni. Dada yake alighairishwa elimu yake kwa sababu yake.

 

Mara hii, Rais – ambaye kwa sadfa pia, ni mwanamama, naye kamwamini kwa kumpa majukumu ambayo anadhani anayamudu. Wahenga walisema mzigo mzito mpe Mnyamwezi – inawezekana walikuwa wanamaanisha Msukuma pia.