Membe ambaye hujawahi kumsikia

Caption. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, akitoa mhadhara kuhusu masuala ya kitaifa na kimataifa wakati alipozungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Tusiime jijini Dar es Salaam mnamo Machi 30, 2015. Picha kutoka Ofisi Binafsi ya Membe.

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

BERNARD Kamillius Membe (69) aliyefariki dunia Mei 9 mwaka huu, alikuwa mtu maarufu nchini Tanzania. Alikuwa maarufu zaidi wakati alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kati ya mwaka 2007-2015; akiweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa pili kushika wadhifa huo kwa muda mrefu zaidi – akizidiwa na Jakaya Kikwete tu aliyehudumu kwa muda wa miaka 10 kati ya mwaka 1995-2005.

 

Kwa Watanzania wengi, Membe alikuwa mwanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyekihama chama hicho kwa kipindi kifupi na kuhamia chama cha upinzani cha ACT Wazalendo wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Anajulikana kama mmoja wa makachero wachache ambao walifahamika kwa taaluma hiyo iliyogubikwa na usiri.

 

Watanzania wanamkumbuka kama mmoja wa wanasiasa waliopewa nafasi kubwa ya kumrithi Kikwete wakati alipomaliza muda wake wa uongozi mwaka 2015. Wanamkumbuka kama kiongozi jasiri aliyekuwa tayari kukosoa hadharani vitendo visivyo vya kidemokrasia na kiungwana vilivyokuwa vinafanyika wakati wa utawala wa hayati Rais John Magufuli. Wengi pia wakimfahamu kama mwanadiplomasia na mwanamikakati mbobezi.

 

Katika wakati huu ambapo Watanzania wanaomboleza msiba wake, nimeamua kuandika kidogo kuhusu masuala 10 ambayo hayajazungumzwa sana wakati huu wa uhai – na kifo chake, lakini kwa sababu ya muda mchache niliokaa naye na kuwa na marafiki ambao baadhi ni rafiki zake pia, nilikuwa nayafafahamu kwa ama kumsikia mwenyewe akiniambia au kuambiwa na watu wake wa karibu.

 

  1. Shabaha ilimpa ajira Usalama wa Taifa

 

Membe aliajiriwa na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) mara tu baada ya kumaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria mnamo mwaka 1976 na mara moja alipelekwa katika Ofisi ya Rais, Ikulu. Niliwahi kumuuliza ilikuwaje akaajiriwa usalama moja kwa moja?

 

Alinieleza kwamba kilichompa kazi TISS haraka ni uwezo mkubwa wa kulenga shabaha kwa kutumia bunduki aliounyesha wakati akiwa JKT. Membe alikuwa na faida kwamba baba yake mzazi alikuwa mwindaji aliyetumia bunduki, hivyo yeye alianza kuiona na kujifunza kutumia silaha hiyo wakati angali mdogo.

 

Alipokuwa JKT, mara nyingi alikuwa akiwa kinara kwenye mazoezi ya kulenga shabaha. Jambo hilo liliwavutia wakubwa waliokuwa wakiangalia vijana wanaofaa kwa kazi za jeshi na usalama kwenye mafunzo hayo na hapo ndipo uwezo wake ulipoonekana.

 

Kwenye mazungumzo na rafiki zake wengine, nilipata kuambiwa kuhusu baadhi ya rekodi za kulenga shabaha alizowahi kuziweka na niliwahi kuambiwa kwamba alikuwa na umahiri unaolingana na wale wanaojulikana kama wadunguaji (snipers).

 

  1. Urafiki wake na Rais Mnangagwa

 

Rais wa sasa wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa, ni kachero mbobezi wa taifa hilo. Ambacho hakijulikani na wengi ni kwamba kwa mara ya kwanza alikutana na Membe kwenye mafunzo maalumu ya ujasusi yaliyoandaliwa na shirika la Scotland Yard la Uingereza kwenye miaka ya 1980.

 

Kukutana huko ndiko kulikofanya wawe marafiki kiasi kwamba – ingawa Mnangagwa hajawahi kutamka hadharani, Membe alikuwa mmoja wa watu aliowasiliana nao wakati akitoroka makucha ya vyombo vya dola kukimbilia uhamishoni nchini Afrika Kusini enzi za hayati Rais Robert Mugabe; kabla ya baadaye kibao kubadilika na yeye kugeuka kuwa Rais.

 

Ndiyo sababu, haikuwa ajabu kwamba mojawapo ya taasisi ambazo Membe alikuwa akifanya nazo kazi, zilikuwa moja ya taasisi zilizoangalia na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa Zimbabwe wa mwaka 2019 uliomweka rasmi Mnangagwa madarakani. Kila walipokutana, Membe na Mnangagwa walikuwa wakiitana “Comrade”.

 

  1. Uwezo wa kuandika kwa mikono yote miwili

 

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Membe alipewa mwaliko wa kutembelea Shule ya Sekondari ya Tusiime jijini Dar es Salaam. Wakati akifanya muhadhara kuhusu masuala ya uhusiano wa kimataifa, wanafunzi walishangaa kumwona akiandika ubaoni kwa kubadilisha mikono. Membe alikuwa akijulikana kwa uwezo wa kuandika kwa kutumia mikono yote miwili.

 

Ilikuwaje? Membe alizaliwa akiwa anatumia mkono wa kulia. Wakati akiwa shule ya msingi, rafiki yake waliyekuwa wakikaa dawati moja, alikuwa akitumia mkono wa kushoto kuandika. Ili kwenda sawa na rafikiye, Membe akaanza kujifunza kuandikia mkono wa kushoto. Miaka mingi baadaye, Membe akawa na uwezo wa kuandika kwa kutumia mikono yote.

 

  1. Shabiki wa Yanga

 

Jambo moja ambalo sikuwahi kulielewa kuhusu Membe ni ushabiki wake kwa klabu ya Yanga. Kwa tabia zake, mazungumzo yake na umahiri wake kwenye kutimiza majukumu, Membe alikuwa na sifa zote za kuwa shabiki wa Simba. Lakini, mpaka anafariki dunia, alikuwa shabiki mzuri wa Yanga. Alipenda pia mieleka na mchezo wa ndondi.

 

  1. Nusura awe Padri

 

Baada ya kumaliza masomo yake kwenye Shule ya Sekondari Namupa, Membe alikwenda kuanza masomo ya Upadri katika Shule ya Peramiho wakati akisubiri matokeo yake ya kwenda Kidato cha Tano. Matokeo yalipotoka kwamba amefaulu kwenda Seminari ya Itaga, aliamua kuachana na Upadri na kuendelea na masomo ya kawaida ya Kidato cha Tano na Sita.

 

  1. Mkanda mweusi kwenye Karate

 

Kachero huyu alikuwa amejifunza pia Sanaa za Mapigano na alikuwa amefikia kiwango cha kuwa na mkanda mweusi kwenye mchezo wa Karate. Kwa hiyo, kama mlikuwa vitani na – kwa bahati mbaya, alikukosa kwa risasi, mngekutana mkono kwa mkono pia ingekuwa hatari kupigana naye.

 

  1. Kulala muda mchache

 

Watu walio karibu naye, walikuwa wanajua kwamba ungeweza kuchati naye hadi usiku wa manane. Kwa maelezo yake mwenyewe, alipata kunieleza kwamba kwa kawaida hawezi kulala zaidi ya saa nne hadi tano kwa siku. Kwa utaratibu wake, kulala saa sita usiku ilikuwa ni kulala mapema.

 

  1. Alimtabiria Majaliwa makubwa mwaka 2015

 

Kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Membe alifanya tukio moja linalokumbukwa kwenye jimbo la Ruangwa mkoani Lindi. Kwenye kilele cha kampeni hizo, watu wa Ruangwa wanakumbuka mambo mawili kwenye hotuba ya Membe.

 

Mosi, kilikuwa kitendo cha kuzungumza – kwanza kwa lugha ya Kimwera; lugha ya asili ya watu wa Ruangwa, na baadaye Kiswahili, maneno ambayo tafsiri yake ilikuwa kwamba watu wa Ruangwa wamchague aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM wa jimbo hilo, Kassim Majaliwa, kwa sababu “anapendeka na atakuwa Waziri Mkuu. Pili, baada ya kutamka maneno hayo ilinyesha mvua kubwa ya takribani dakika 10 na kachero huyo hakushuka jukwaani.

 

Baada ya Majaliwa kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Waziri Mkuu, maneno hayo ya Membe yalitimia.

 

  1. Chakula

 

Membe alikuwa na tabia moja ambayo simfahamu mtu mwingine niliyewahi kumwona akiwa nayo. Kama amekaa muda mrefu bila kula, alikuwa akipenda kunywa soda au juisi kwanza kabla ya kula chakula. Alikuwa akiamini kwamba mtu mwenye njaa anahitaji sukari kwanza. Kwenye chakula, alikuwa mpenzi wa ugali, samaki na mboga za majani.

 

  1. Mahaba na bunduki

 

Membe alikuwa mtu mwenye mahaba na bunduki. Popote pale ulipomwona hadharani akiwa nchini, alikuwa anatembea na bunduki yake. Kama haikuwa mwilini au mguuni, basi ingekuwa kwenye kibegi alichokuwa anatembea nacho.

 

Sitasahau tukio moja mwaka 2018 wakati aliponionyesha bastola moja mpya iliyokuwa ndani ya briefcase yake aliyoniambia ndiyo kwanza alikuwa ameinunua wiki hiyo. Kwa maelezo yake, alikuwa na utaratibu wa kununua bastola za aina ile kila aliposikia kuna toleo jipya limetoka. Mimi si mtu wa bunduki na bastola lakini aliniambia mpaka jina. Kama kumbukumbu yangu iko sahihi, ilikuwa ya aina ya Colt. Damu ya mwindaji kutoka kwa baba yake ilimsababishia mahaba makubwa na silaha hiyo.

 

Naamini kadri Watanzania wanavyoendelea kumwomboleza mwanasiasa huyu maarufu, taarifa zaidi kumzidi zitazidi kutolewa na watu waliomfahamu zaidi na kuwa karibu naye. Kwenye makala haya, nilitaka walau kueleza upande wake ambao haukuwa ukijulikana sana kwa wengi.

 

TANBIHI: Natumia nafasi hii kuwashukuru baadhi ya marafiki wa Membe – , hasa msaidizi wake binafsi wa zamani, Allan Kiluvia, ambao walinipa sehemu ya taarifa zilizofanikisha andishi hili