Ancien Regime, Abdul Nondo na watu kutekwa

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

 

KATIKA uchambuzi wake wa nini kilisababisha Mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789, Alexis du Tocqueville aliandika kitu cha tofauti na wengine walioandika kuhusu mapinduzi yale. Alisema mapinduzi yale hayakuwa tukio la mara moja bali ni hitimisho la miaka mingi ya kuharibika kwa mfumo wa utawala wa taifa hilo.

 

 

Katika andishi lake maarufu la mwaka 1856, L’Ancien Régime et la Révolution (The Old Regime and the French Revolution), Tocqueville alitumia muda mrefu kuisaili jamii ya Wafaransa kiundani kuelekea kwenye mapinduzi.

 

 

Tukio la hivi karibuni la kutekwa kwa Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo na mengine yanayoendelea kuigubika jamii yetu katika siku za karibuni yamenifanya kusaili upya jamii yetu katika kutafuta sababu ya imekuwaje tumefika hapa.

 

 

Katika uchambuzi wangu huu, nimezingatia nguzo kuu mbili za muhimu – kwamba Tanzania ni nchi inayofuata mfumo wa kidemokrasia na pili taifa lolote duniani lina misingi au tabia fulani ambazo ndizo huliweka pamoja. Misingi, au kwa lugha nyingine reli hizo zikianza kung’oka – na mara nyingi hung’oka taratibu, taifa taratibu huanza kumeguka pia.

 

 

Historia ya watu kutekwa, kupotezwa na kuuawa ndani ya Tanzania ina umri wa zaidi ya nusu karne. Matukio ya awali kabisa kuhusu watu kupotezwa na kutekwa yalianzia Zanzibar katika miaka iliyofuatia Mapinduzi yam waka 1964. Wapo viongozi kama Abdullah Kassim Hanga na wengine ambao walipotezwa katika mazingira ambayo hayajawahi kuwekwa wazi hadi leo.

 

 

Hakuna mtu yeyote aliyewahi kuchukuliwa hatua kwa matukio ya kikatili yaliyotokea Zanzibar wakati ule ingawa wahusika wanajulikana. Na wala hakujawahi kufanyika uchunguzi au maridhiano ya watu kusameheana kwa yaliyotokea. Kama hakuna uwajibikaji wa matukio ya namna hiyo, maana yake ni kwamba yatamea na kuwa ya kawaida.

 

 

Tangu wakati huo – na hata takribani muongo mmoja tu uliopita, matukio ya watu kukamatwa bila kufuata sheria, kuteswa na hata kupoteza maisha, yamekuwa yakitokea nchini na kwa bahati mbaya hakuna hatua mahususi za uwajibikaji zimekuwa zikichukuliwa kwa wahusika.

 

 

Kitu ambacho kimebadilisha hali sasa hivi ni uwepo wa mitandao ya kijamii na kuimarika kwa mawasiliano ya haraka. Katika tukio lililomhusisha Wakili Alphonce Lusako wiki hii, ujumbe wake wa kuwa yuko hatarini kutekwa, ulisambaa katika makundi sogozi mengi dakika chache tu baada ya kujirekodi.

 

 

Kuna vitu kama kamera za CCTV ambazo zinaweza wazi ushahidi na teknolojia nyingine. Inawezekana kabisa kwamba hivi sasa inaonekana matukio ni mengi zaidi kwa sababu mchezo mzima umebadilishwa na teknolojia.

 

 

Kati ya mwaka 2016 na 2020, matukio haya ya kihalifu yalifikia katika kiwango cha juu kabisa. Kwa mara nyingine tena, wahusika hawakuwajibishwa.

 

 

Katika taifa ambalo ni dola pekee ndiyo yenye “escalation dominance” – yaani uwezo wa kuumiza usio na ushindani, kama uwajibikaji hakuna, uwezekano ni kukua na kukua kwa tabia za kuumiza wanyonge. Kama kungekuwa na taasisi nyingine nje ya dola yenye uwezo wa kujibu mapigo, pengine wahusika wangejiuliza mara mbili kabla ya kutekeleza majukumu yao.

 

 

Kwa hiyo tumefika hapa kwa sababu huko nyuma hatukufanya tuliyotakiwa kufanya kama nchi ya kidemokrasia. Tumeachia kansa imekua kiasi kwamba sasa uwazi na teknolojia vinaanika ugonjwa wetu hadharani. Kinachoendelea sasa si kitu kilichoibuka ghafla. Ni mtoki ambao sasa umepasuka na kutoa usaha.

 

 

Utamaduni wa siasa za kistaarabu

 

 

Demokrasia ina udhaifu mmoja mkubwa wa kimfumo. Kwamba kwa sababu sote tuna haki sawa, kuna uwezekano hata wa watu wenye tabia zisizo za kidemokrasia, wabaguzi na wengine wa namna hiyo kupata madaraka.

 

 

Lakini kama nchi, kuna tabia ambazo huwa viongozi wanazikemea kila zinapotokea kwa lengo la kuilinda demokrasia na udhaifu wake huo.

 

 

Kwa mfano, Tanzania tumekubaliana kwamba hata Rais akiwa mzuri kiasi gani, muda wake wa kukaa madarakani ni miaka 10 tu. Lakini, kwenye kampeni zetu za kutafuta madaraka, hatutatweza wengine, hatutatesa wengine na hatutatumia lugha za kibaguzi.

 

 

Demokrasia yetu, hasa ya vyama vingi katika miaka yake ya awali, ilijengwa katika misingi ambayo baadhi ya wasomi wa sayansi ya siasa kama Tali Mendelberg wameipachika jina la “Norm of Equality”. Kwamba unaweza kumshambulia mshindani wake bila kumuumiza moja kwa moja.

 

 

Mfano mzuri wa hili ni kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitumia mbinu ya kuonyesha matukio ya mauaji ya kimbari ya Rwanda na kwingine kwenye vita barani Afrika kuwatia hofu wananchi kuwa upinzani ukiingia madarakani nchi itaingia vitani.

 

 

Majukwaani, viongozi na wagombea wa CCM hawakuwaita wapinzani kwa majina mabaya wala kusema waziwazi kwamba wataingiza nchi vitani. Ila walitumia luninga kupitisha ujumbe ambao hauzungumziki majukwaani kwa sababu ya utamaduni wetu kisiasa tulioujenga.

 

 

Lakini kuanzia mwaka 2010, imekuwa jambo la kawaida kwa wafuasi wa CCM na vyama mbadala kupingana kwa kuitana majina ya kutweza utu majukwaani na mitandaoni. Kwa mara ya kwanza, majina kama “mbogamboga na nyumbu” yakaanza kuwa rasmi.

 

 

Waswahili wanasema kama unataka kuua mbwa, unahitaji kwanza kumpa jina baya. Washindani wa kisiasa walipoanza kuitana majina mabaya ya kuondoa ubinadamu, na thamani zao kama wanadamu zikaanza kushuka.

 

 

Kama mimi nakuona wewe sawa na nyumbu, ng’ombe au mbogamboga tu, nitajali nini kuhusu uhai au haki zako za kiraia? Kama hoja yako dhidi ya mpinzani wako kisiasa au mtu ambaye mnapishana kisiasa ni kumwita chawa au msaliti, utajali nini kuhusu usalama wake?

 

 

Kama kupishana kwetu kwa hoja maana yake ni usaliti, si ajabu tukashuhudia kiongozi mkubwa wa upinzani nchini, Tundu Lissu, akishambuliwa kwa risasi mchana kweupe akiwa katika kutimiza majukumu yake.

 

 

Kama wapinzani wako ni nyumbu tu, una sababu gani ya kuruhusu washinde uchaguzi – mwaka 2019 na 2020, ili waongoze wanadamu?

 

 

Sijasahau hadi leo, namna aliyekuwa mgombea urais wa upinzani kupitia UKAWA mwaka 2015, Edward Lowassa, alivyodhalilishwa kwa maneno mabaya sana kwa sababu ya hali yake ya kiafya kwenye kampeni zile. Baadhi ya matamshi mabaya zaidi yalitamkwa hadharani na viongozi wakubwa kabisa wa nchi yetu.

 

 

Misingi ya demokrasia ya Tanzania ilijengwa katika tunu zetu za taifa ambayo kubwa kuliko zote ni kuamini katika utu. Unapoamini katika utu, huwezi kubagaza mshindani wala kutumia lugha za kibaguzi. Kama unajali kuhusu utu, huwezi kuteka na kutesa washindani. Huwezi kumnyima ushindi katika mahali ambapo amestahili kushinda. Ukiondoa utu katika siasa zetu, unaondoa msingi muhimu wa demokrasia yetu.

 

 

Hofu yangu

 

 

Kutekwa na kuteswa kwa Abdul Nondo kuliniumiza kwa sababu moja kubwa; kwamba huyu ni kijana mdogo ambaye mara zote amejipambanua kwa kujenga hoja na kufanya siasa za kiungwana. Kumuumiza Nondo ni kuumiza siasa za kistaarabu.

 

 

Ustaarabu unapokuwa umeondoka katika nchi ya kidemokrasia, kinachofuata ni hatari. Kwa waliongalia maneno yaliyozungumzwa na mwandishi mwenzangu Sammy Awami katika picha jongefu iliyosambazwa kwenye mtandao wa twitter wiki hii, watu wanaweza kuamua kujilinda wenyewe.

 

 

Hofu yangu ni kwamba kujilinda huko kutaibuka kuwa suala zima la nani anaweza kuwa na “escalation dominance” kubwa kuliko wengine. Kama ikitokea huku nje kuna watu wana uwezo wa kujilinda na kuiumiza dola wakitaka, huo utakuwa mwisho wa Tanzania kwa namna tunayoiona leo.

 

 

Kwa ridhaa yetu, tumeipa dola nguvu ya kuwa na bunduki, pingu, mabomu ya machozi, magereza na mengine ili kujenga jamii ya haki na inayofuata sheria. Uhusiano wetu, kama ambavyo Thomas Hobbes ameandika kwenye Leviathan, ni yenyewe kulinda watu nasi kuendelea na shughuli zetu pasi na woga. Escalation dominance ikiondoka kwa dola, hatutakuwa na nchi.

 

 

Nini kifanyike?

 

 

Tanzania ni nchi ya kidemokrasia. Nimezungumza kuhusu udhaifu mkubwa wa demokrasia hapo kabla lakini sasa ni muhimu kueleza kuhusu uimara wa demokrasia. Uimara wake uko kwenye uwezo wake wa kujirekebisha. Tunaweza kabisa kufanya vizuri kuliko tulivyo sasa.

 

 

Kwa mfano, tunaweza kukubaliana kwa pande zote kufanya siasa za kistaarabu zinazojali utu wa mtu pasipo kuangalia siasa zake. Tunaweza kuenenda katika siasa zinazoamini kwamba kuwa CCM au upinzani hakukufanyi kuwa mtu zaidi, mwenye akili zaidi, maarifa zaidi au mwenye uchungu zaidi na nchi?

 

 

Walio na pingu na bunduki, wanaweza kurejea kwenye imani kwamba zana hizo walipewa si kwa ajili ya kutesa na kuteka waliowapa bali kwa sababu ya kuwalinda? Huu ni wakati mwafaka kwa wenye pingu kutafakari nini kitatokea wakati wananchi watakapoanza kununua bunduki na pingu zao wenyewe ili wajilinde.

 

 

Uwajibikaji unatakiwa kuwa msingi muhimu wa demokrasia yetu. Kama watu hawawajibishwi kwa matendo yanayoathiri social contract iliyopo kati ya watawala na watawaliwa, mambo yataendelea kuwa mabaya. Na ubaya una pande mbili mara zote – unaweza kuwa kwetu au kwenu.

 

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Siasa za Maridhiano na ni Mhitimu wa Shahada ya Uzamili katika Siasa za Afrika (African Politics), aliyoipata katika Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza. Anapatikana kupitia email; ekamwaga57@gmail.com