Joan Wicken, mwanamke aliyemjua Julius Nyerere

Picha: Nakala ya kitabu kilichoandikwa na Profesa Aili Mari Tripp kuhusu maisha ya Joan Wicken na uhusiano wake na Mwalimu Nyerere. Kitabu hicho kimechapwa na kampuni ya Mkuki na Nyota

 

Na Ahmed Rajab

 

KWA zaidi ya miaka 40, kila alasiri baada ya saa za kazi, Bi Joan Wicken alikuwa akikimbilia Msasani, Dar es Salaam, nyumbani kwa Mwalimu Julius Nyerere. Ulikuwa muda wao wa faragha.  Wakizungumza kwa saa nzima kuanzia saa kumi na moja hadi jua lilipokuwa likizama. Kama palikuwa na vinywaji, basi Wicken akipiga pombe kali ya Whiskey, aliyokuwa akiipenda, na Nyerere akibugia mvinyo wa Kireno wa Mateus Rosé, uliokuwa ukimchangamsha.

 

Sidhani kama kuna mwanamke — au mtu yeyote — aliyekuwa akimjua Nyerere zaidi ya bibi huyo, kwa upande wa siasa. Wapo waliomtilia shaka kwamba labda alikuwa mtu wake.

 

Na wapo waliokuwa wakisema, kwa uhakika, kwamba uhusiano wao ulikuwa wa aina hiyo. Miongoni mwao alikuwa Oscar Kambona, aliyewahi kuwa chanda na pete na Nyerere halafu, baada ya kukorofishana kuhusu sera, akamgeuka na kuwa adui yake. Mwaka 1967, Kambona alikimbilia uhamishoni London alikoishi hadi alipofariki Juni 3, 1997.

 

Baina ya 1986 na 1997, katibu mkuu huyo wa zamani wa TANU na waziri wa zamani wa Nyerere alikuwa na mazoea ya kunipitia ofisini kwangu kwenye jarida la Africa Analysis. Kila tulipokutana akinihadithia mengi kuhusu Nyerere. Mambo mawili alikuwa heshi kuyadhukuru.

 

La kwanza, kwamba Nyerere akiweka fedha zake nje ya Tanzania. Hilo sikuliamini. La pili, kwamba Nyerere na Miss Wicken (kama mwenyewe alivyopenda kuitwa) walikuwa na uhusiano maalum.  Hilo nikiliacha liingie sikio moja, litoke sikio jengine.

 

Uvumi kama huo, uliomhusisha Nyerere na mabanati kadhaa, nilishausikia ingawa nikiutia kwenye kikapu cha hadithi za “sadiki, ukipenda.” Katu sikuamini kuwa mtu kama Mwalimu alikuwa mpenda makoo au “ahli makoo,” kama tusemavyo mabarazani Unguja, Mjini.  Katika miaka ya hivi karibuni kuna profesa mmoja wa Kiingereza mwenye kufanya tafiti kuhusu Tanzania ambaye siku moja alinionesha nakala ya ripoti ya siri kuhusu Nyerere iliyoandikwa na jasusi, asiyetajwa jina, wa idara ya ujasusi wa ndani ya nchini Uingereza, MI5.

 

Ripoti hiyo, ingawa ni ya zamani, inadhihirisha mambo matatu. La kwanza, kwamba kila Nyerere alipokuwa akipiga simu Uingereza kutoka Tanganyika wakoloni wa Kiingereza wakizisikiliza simu zake.  La pili, kwamba kila alipokuwa akenda Uingereza akiandamwa na majasusi wa Uingereza. La tatu, kwamba kutokana na hizo simu na nyendo zake za Uingereza idara ya ujasusi ya Uingereza ilikuwa na orodha ya wanawake waliohusishwa naye Nyerere. Ripoti hiyo iliwataja wanawake hao. Haina haja ya kuwadhukuru hapa.

 

Mwaka jana, Eric Kabendera, mwandishi habari maarufu wa Tanzania, alinipa mswada wa kitabu chake niupitie.  Kitabu chenyewe, chenye anuwani ya “In the Name of the President,” hivi sasa kimo mitamboni na karibu kitachapishwa na Jacana Media. Humo, Kabendera amevifichua baadhi ya visa vilivyomhusisha Mwalimu na starehe zake au utundu wake.

 

Wicken daima akisisitiza kwamba uhusiano wake na Mwalimu ulikuwa wa kikazi. Hapakuwa na jengine zaidi ya kazi.  Nyerere alikuwa “bosi” wake. Walipokuwa wakikutana Msasani kwa Mwalimu saa za alasiri walikuwa wakibadilishana mawazo.

 

Wicken alikuwa kama pacha wa Mwalimu kifikra kwani mawazo yao yakifanana bila ya kiasi. Mwingereza mwengine, Ronald Brown, aliyekuwa mwanasheria mkuu wa kwanza wa serikali ya Tanganyika huru, alimueleza Wicken kuwa “kioo cha ubongo wa Julius Nyerere.”

 

Wicken ndiye aliyekuwa akiiandika miswada ya hotuba za Kiingereza za Mwalimu pamoja na ya vitabu vyake.  Kwa mujibu wa Anna Mwansasu aliyefanya naye kazi Ikulu akiwa msaidizi wa Nyerere, wakati mwingine Mwalimu akiirekebisha miswada hiyo lakini mara nyingine akiiachia hivyo hivyo kama ilivyochongwa na Wicken bila ya kubadili chochote. Ni wazi kwamba Wicken alikuwa na ushawishi mkubwa juu ya Nyerere na fikra zake. Walitofautiana kwa jambo moja la msingi: Nyerere alikuwa Mkatoliki aliyekuwa akihudhuria misa, lakini Wicken alikuwa haamini Mungu.

 

Pengine utajiuliza bibi huyo wa Kiingereza alizukia wapi?  Ilikwendakwendaje hata binti huyo wa ukoloni wa Kiingereza akaangukia kwa Nyerere, aliyepigania uhuru wa nchi yake ya Tanganyika kutoka Uingereza? Na sio tu kwamba mwanamke huyo wa Kiingereza aliangukia Ikulu ya Nyerere lakini alikuwa mshirika wake wa maisha.

 

Na kuna suala nyeti la utiifu: tuna uhakika gani kwamba Wicken alikuwa mtiifu asilimia moja kwa Tanganyika na, baadaye Tanzania, na Nyerere wake?

 

Tunajuaje iwapo Waingereza hawakumpachika Wicken kwa kusudi, kwa lengo la kumtumia, katika duru ya ndani kabisa ya Mwalimu? Hayo si maswali ya uchokozi.  Ni maswali ambayo lazima yampitikie mtu yeyote mwenye akili zake timamu na mwenye kuzitambua njama za mabeberu katika medani za siasa za kimataifa.

 

Naitoshe tukisema kwamba uhusiano wa Wicken na Nyerere ni kitendawili kinachusubiri kuteguliwa kwa utafiti wa kina.  Angalau kwa sasa, ya ndani kuhusu uhusiano huo hatuwezi kuyajua, lakini habari zote za juujuu za bibi huyu zimo kwenye kitabu kiitwacho “Joan Wicken: A Lifelong Collaboration with Mwalimu Nyerere.” (Joan Wicken: Ushirikiano wa Maisha na Mwalimu Nyerere).

 

Mwandishi wa kitabu hicho ni Aili Mari Tripp, Profesa wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison huko Marekani. Utangulizi wa kitabu chenyewe umeandikwa na Mwansasu. Mchapishaji wa kitabu hicho muhimu katika historia ya Tanzania ni Mkuki Na Nyota (www.mkukinanyota.com).

 

Sehemu kubwa ya kitabu hiki ni mahojiano ambayo Tripp alimfanyia Wicken kuhusu maisha yake na nyakati zake. Ni hadithi inayoanzia alikozaliwa katika umasikini wa kutupwa kwenye kiunga kimoja cha London, North Woolwich. Alilelewa zaidi na baba yake kwa vile mama yake alifariki akiwa mdogo.

 

Wicken alikuwa na mwamko wa kisiasa tangu utotoni mwake kwa vile alishiriki katika harakati za kuupinga ufashisti siku za Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Ingawa alisoma kwa taabu taabu hatimaye alifanikiwa kuwa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Oxford.  Alikuwa na bahati pia ya kupata kazi katika chama cha Labour cha Uingereza kwenye kitengo chake cha Jumuiya ya Madola.

 

Siku moja mnamo 1955, Julius Nyerere, mpigania uhuru kutoka Tanganyika, akiwa katika ziara yake ya mwanzo ya Uingereza alikwenda kwenye ofisi za chama cha Labour kukutana na bosi wake Wicken, John Hatch. Wakati huo, Hatch alikuwa safarini na ikamwangukia Wicken kumpokea Nyerere. Mkutano huo uliyabadili maisha ya Wicken.

 

Baada ya miaka kadhaa, alipelekwa Tanganyika kukiasisi chuo cha chama cha TANU cha Kivukoni.  Hapo ndipo uhusiano wake na Nyerere ulipoanza kushamiri.

 

Tutayarudia maisha ya washiriki hawa wawili katika wiki zijazo lakini kwa sasa, kwa kumalizia makala haya, napenda kuwasihi wachapishaji wa Mkuki Na Nyota wakifasiri kitabu hiki kwa Kiswahili ili Watanzania wengi na wazungumzaji wengine wa Kiswahili waweze kuyasoma maisha ya Wicken na ushirikiano wake wa maisha na Mwalimu Nyerere.

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; @ahmedrajab/X

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.

 

 

 

a