Picha: Prighozin na vikosi vya Wagner barani Afrika. Picha ya jarida la Foreign Affairs
Na Ahmed Rajab
PAKIZUKA zahama kama zile za Jumamosi iliyopita zilizozushwa na Yevgeny Prigozhin, kiongozi wa Kundi la Wagner, si uzuri mtu kukurukupwa na kuanza kusema asiyoyajua. Ni kheri auzuie mdomo wake au kalamu yake mpaka vumbi litapotulia.
Nasema hivi kwa sababu aghalabu pakizuka ghafla sokomoko kama hilo tuyaonayo siyo hali halisi ya mambo yalivyo. Kwa mfano, kuna uwezekano kwamba sakata lote hili ni kiini macho cha Vladimir Putin, Rais wa Urussi, la kuwawekea mtego NATO pamoja na maadui zake waliojificha ndani ya Urussi kwenyewe. Miongoni mwao ni wale walio katika ngazi za juu za utawala.
Kwa ufupi, inawezekana Putin akitaka kubaini nani miongoni mwa walio ndani ya duru yake wataoanza kucharukwa kwa furaha ikionekana kana vile karibu atavunjika miguu ya uongozi.
Kuna mifano mingi ya tamthilia za kisiasa za namna hii katika historia. Mifano ya viongozi waliowatega wapinzani wao wa siri walio karibu nao. Hujifanya dhaifu na nusura wapinduliwe ili waweze kuwafichua na kuwachukulia hatua kali.
Vyombo vya habari vya nchi za Magharibi vilipata fursa ya kuzidi kumkebehi Putin. Kwao yeye ni adui mkubwa. Shirika la utangazaji la CNN, tukiutaja mfano mmoja, halikuweza kujizuia. Lilianza kufafaruka na kuropokwa kwamba Putin yumo hatarini, kwamba madaraka yanamponyoka na kwamba saa 24 zijazo (yaani kufikia Jumapili) ni muhimu kwani zitaamua mbivu na mbichi.
Kuna wasemao kwamba hivi ni vita vya ndani kati ya genge la Putin la St. Petersburg na lile la Moscow la kina Vitaly Gerasimov, mkuu wa majeshi, na Sergei Shoigu, waziri wa ulinzi. Hawa wawili ni maadui wakubwa wa Prigozhin.
Na kuna wasemao kwamba huu ni mwanzo wa kampeni ya uchaguzi ya Putin anayetaka achaguliwe tena katika uchaguzi ujao wa Machi, 2024. Kwamba Putin anamtumia kibaraka wake Prigozhin kujidai kwamba amechoka na jinsi kina Gerasimov na Shoigu wanavyokorofesha ushindi katika vita vya Ukraine. Wanatafuta vijisababu vya kuwasingizia kwa Urussi kutopata ushindi wa haraka Ukraine.
Zote hizo ni dhana. Minghairi ya Prigozhin na Putin hakuna mwenye hakika ya nini hasa kilichotokea.
Swali linalozuka ni: nani atakwenda na maji?
Hamna shaka kwamba Vladimir Putin anayeiongoza Urussi kwa miaka 23 sasa, ameumizwa na Prigozhin kwa hatua yake ya kuandamana na wapiganaji wake, akionesha kwamba analiasi jeshi la Urussi. Walitiana ndaro lakini, kwa sasa, wote wawili wamesalimika. Wameumizana lakini hawajauana. Wote wawili wamepata majaraha ya kisaikolojia.
Mahna iliyozushwa na Prigozhin haikuwa ndogo. Huu ulikuwa mgogoro mkubwa wa kisiasa lakini hadi sasa ni mapema mno nadhani kusema nani kati yao wawili aliyeumizwa vibaya. Tukiangalia juu juu bila ya kupiga mbizi kwenye bahari kuu ya mgogoro huu tunaweza tukafikiri kwamba Prigozhin ndiye aliyepoteza mengi.
Wakati wapinzani wa Putin walipokuwa wakishangilia matukio ya Jumamosi iliyopita nchini Urussi, jijini Moscow walikuwepo waliokuwa hamkani lakini kwa jumla, wengi wa wakaazi wa Moscow wakiendelea na shughuli zao bukheiri wa khamsini.
Prigozhin alifinyangwa na Putin. Inasemekana kwamba kwamba hata kundi lake la wapiganaji wa mamluki la Wagner liliasisiwa ndani ya wizara ya mambo ya ulinzi mwaka 2014. Alipokuwa akiwabembeleza wakuu wa wizara wamkubalie aliwaambia kwamba mradi huo una baraka za “Papa” (baba), yaani Putin.
Baada ya kumfinyanga Prigozhin, Putin akamtia ufunguo na kumtumia atakavyo hususan katika nchi kadhaa za Afrika (Mali, Jamhuri ya Afrika Kati, Libya, Sudan na, kwa kipindi kifupi, Msumbiji), na pia Syria na Ukraine. Jumamosi iliyopita sanamu hilo lilimgeukia mwenyewe Putin na lilitaka kumtia adabu.
Sijui wazimu gani ulimuingia kichwani Prigozhin akadhani kwamba ataweza kufanikiwa kuingia Moscow na kushinda katika mapigano baina ya mamluki wake na wanajeshi wa serikali. Alikabiliwa na vikwazo vingi.
Si rahisi hivyo kupenya kwenye ulinzi mkali wa Moscow. Vikosi kadhaa vya kijeshi vimeuzunguka mji huo. Na kuna idara tafauti za kiusalama zinazopigana darubini zikichunguzana.
Prigozhin alisema azma yake ilikuwa kuandamana kupigania haki na kuupinga ufisadi na uzembe katika wizara ya ulinzi ya Urussi.
Prigozhin hajawahi kuwa mtu wa duru za ndani za Putin. Sana sana alikuwa kama ni tarishi wa Putin lakini hakuwa mwenza wake mwenye hadhi sawa naye.
Kwao ni kumoja, mji wa St. Petersburg ambao zamani ukiitwa Leningrad. Kwa kila hali hawa ni watoto wa mjini. Mmoja ni jambazi aliyegeuka akawa tajiri wa kutupwa; mwengine ni jasusi aliyegeuka akawa Rais. Kila mmoja alimtumia mwenzake kwa matilaba na maslahi yake.
Prigozhin ana mdomo mchafu wenye kumsibu mtu kama yeye mwenye historia ya uhuni. Wapiganaji wake ni wahuni na majambazi kama yeye: wezi, wabakaji, wauaji na wahalifu wa makosa mengine. Aliwafungua kutoka jela na akawaingiza katika jeshi lake kwenda kupigana Ukraine kuyasaidia majeshi ya Urussi. Kati yao aliwahi kuwamo kijana wa Kitanzania Nemes Tarimo na aliyeambiwa achague ama aselelelee gerezani au aachiwe huru lakini aingizwe kwenye jeshi la Wagner ende kupigana Ukraine. Alichagua kuwa huru; muda si mrefu aliuliwa katika mji wa Ukraine wa Bakhmut kulikokuwa mapigano makali. Maiti ya Tarimo ilirudishwa nyumbani kuzikwa. Kuna na raia wa Zambia aliyekufa kama yeye.
Nchini Mali mamluki wa Wagner hawajitokezi sana Bamako, mji mkuu wa nchi hiyo. Warussi wenye kuonekana jijini humo ni wakufunzi wa kijeshi wenye kuwafunza wanajeshi wa Mali. Wakufunzi hao huvaa sare za kijeshi za Kirussi. Lakini miongoni mwao mna mamluki wa Wagner na wengine wako sehemu za kati za nchi hiyo ambako wanayasaidia majeshi ya Mali kupambana na magaidi Wakijihadi.
Kuna ushahidi kuwa mamluki wa Wagner wamekuwa wakipora madini ya Mali na kwamba walihusika na visa visivyopungua sita vya mauaji ya kinyama ya watu wasio na hatia. Umoja wa Mataifa umewatuhumu kwamba waliwakusanya mamia ya watu wakawaamrisha wachimbe makaburi yao halafu wakawapiga risasi.
Mamluki wa Wagner wameshutumiwa pia kwamba wamekuwa wakiwanyanyasa, kuwatesa na kuwaua raia wasio na hatia katika Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu 2019.
Tangu Agosti 2020, Mali imekuwa chini ya utawala wa baraza la wanajeshi. Watawala hao wa kijeshi wameyavunja makubaliano ya muda mrefu baina ya Mali na Ufaransa pamoja na washirika wengine wa nchi za Magharibi katika mapigano dhidi ya magaidi wenye itikadi ya kijihadi. Wafaransa wananuka Mali na wanachukiwa na wananchi wa kawaida na hasa na wanajeshi.
Baada ya kuwaacha mkono Wafaransa na wenzao wa Magharibi, watawala wa kijeshi wa Mali wameigeukia Urussi iwasaidie kijeshi.
Kazi kubwa ilimuangukia Balozi wa Urussi nchini humo, Igor Gromyko, ambaye pia anaiwakilisha Urussi nchini Niger. Nchi hizo zina uhusiano mzuri. Wiki iliyopita tu, Gromyko alikuwa Niamey, mji mkuu wa Niger, alikopokewa na Rais Mohamed Bazoum.
Igor Gromyko ni mwanadiplomasia wa muda mrefu na ni mjukuu wa Andrei Gromyko, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Muungano wa Sovieti kwa muda wa miaka 28.
Mali ilipokea zana za kijeshi kutoka Urussi mwezi Machi na tena Agosti mwaka 2022, na mwezi Januari mwaka huu. Mwezi uliopita, jeshi la Mali lilipokea ndege kadhaa za kivita kutoka Urussi na droni kutoka Uturuki.
Licha ya tuhuma za uporaji wa madini na mauaji ya ovyo ya watu wasio na hatia dhidi ya mamluki wa Wagner, Warussi, kwa jumla, wanapendwa katika eneo la Sahel kwa sababu moja kubwa. Nayo ni kwamba wameweza kuwafata magaidi na kupigana nao huko huko waliko kwenye ngome zao.
“Eneo la Sahel linahitaji mkakati wa kivita kama huo”, ametueleza mchambuzi mmoja wa mambo ya usalama anayefuatilia matukio ya vita dhidi ya ugaidi katika kanda za Sahel na Sahara.
Tangu Wafaransa wafurushwe Mali, Warussi wameyachonga upya majeshi ya nchi hiyo. Wameyawezesha, kwa mfano, kupata mafunzo zaidi pamoja na silaha zaidi na zana nyingine za kijeshi. Kwa kufanya hivyo, majeshi ya Mali yamepata uwezo wa kuwasaka magaidi, kuwafuatia na kuwafikia katika ngome zao katika eneo la Sahel.
Balozi mmoja wa Kiafrika anayeiwakilisha nchi yake mjini Bamako, juzi aliliambia Gazeti la Dunia kutoka Mali kwamba katika miezi ya hivi karibuni, wanajeshi wa Mali wamekuwa wakishirikiana kwa kiwango kikubwa na jeshi la Burkina Faso.
“Ushirikiano huo umeyapa majeshi ya Mali uwezo wa kuwashambulia magaidi kwa masafa ya kilomita zipatazo 150 ndani ya ardhi ya Burkina Faso,” balozi huyo alitueleza.
Inakisiwa kuwa tangu Mali ipate uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1960 si chini ya asilimia 80 ya wakuu wa kijeshi wa nchi hiyo wamepatiwa mafunzo ya kijeshi katika Muungano wa Sovieti na baadaye Urussi.
Katika miaka ya hivi karibuni, China nayo haijajiweka nyuma katika kuiuzia Mali silaha na zana zingine za kivita. Kwa kawaida, siku hizi China hutoa misaada ya kijeshi kwa nadra. Lakini mapema mwezi huu iliipatia Mali silaha za kijeshi zilizopakuliwa katika bandari ya Conakry, Guinea.
Katikati ya mwezi huu Mali ilipokea mzigo wa pili wa zana za kivita kutoka China zikiwa pamoja na vifaru 70 vya kupigana vitani, vya aina ya WZ-551 na VP11 MRAP. China ilivionesha kwa mara ya kwanza hadharani vifaru hivi vya VP11 MRAP mwaka 2014. Vifaru hivyo ni sugu kwa mabomu ya kuzikwa ardhini.
China iliyapatia majeshi ya Mali aina nyingine ya silaha nzito nzito pamoja na wakufunzi wa kijeshi.
Kuzipata silaha hizo kumeyapa majeshi ya Mali ufanisi mkubwa katika mapigano yao dhidi ya waasi na magaidi. Kwa kupatiwa teknolojia ya kivita ya kisasa kabisa, majeshi hayo yatakuwa na uwezo wa kuvikabili vitisho kwa haraka zaidi na kwa uthabiti mkubwa.
Ununuzi wa silaha hizo ni sehemu ya mkakati mkuu wa kuimarisha uwezo wa jeshi la Mali wa kupambana na waasi baada ya kuwafukuza wanajeshi wa Kifaransa na wa nchi nyingine za Magharibi.
Mali inajivunia kuwa na aina kwa aina ya vifaru vya kivita. Nchi za kigeni ndizo zilizoipa Mali vingi vya vifaru hivyo ili kuisaidia kupambana na ugaidi katika ukanda huo.
Kwa upande wa Burkina Faso, jeshi la huko nalo pia limepata mafanikio na hivi sasa magaidi wanateremka upande wa kusini kuelekea kaskazini mwa Ghana, Togo na Benin.
Kinyume na walivyotarajia wengi katika nchi za Magharibi, Prigozhin hakuweza kufua dafu alipokabiliwa na majeshi ya Urussi. Tishio lake lilififirika na mwenyewe akaja matao ya chini na akakubali kukimbilia Belarus. Huku nyuma lazima kundi lake la Wagner litabadilika, walau kwa sura. Mustakabali wake katika nchi za Kiafrika nao pia utakuwa mashakani. Na marais wa Kiafrika wanaolindwa na kundi hilo lazima nao wamo hamkani.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab