TAABINI YA MZEE ALI HASSAN MWINYI

TAABINI

Ali Hassan Mwinyi “Mzee Rukhsa”: (Mei 8,1925 – Februari 29, 2024)

Mtu wa watu aliyependwa na masharifu

ALHAJI Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia Dar es Salaam, Alhamisi iliyopita, siku 70 kabla ya kutimia miaka 99, aliushangaza ulimwengu alipoibuka kuwa Rais wa tatu wa Zanzibar 1984.

Mwinyi aliushangaza tena ulimwengu miezi kadhaa baadaye alipochomoza kuwa Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hadi sasa ni yeye tu aliyewahi kuwa Rais wa Zanzibar na wa Tanzania.

Alipoushika urais wa Zanzibar machepe wa mitaani wakisema kwamba urais huo ulimjia kama “riziki dudu”. Hakuulalia, hakuuamkia.

Kabla ya hapo huko huko Zanzibar, Mwinyi alikuwa mwalimu wa skuli, na mkuu wa chuo cha ualimu.

Mwinyi hakuwa mzawa wa Zanzibar. Alizaliwa Mkuranga, Tanganyika, na alipelekwa Mangapwani, Unguja, kusomeshwa dini akiwa na umri wa miaka mine.

Hata hivyo, waalimu wake, wengi wao wakiwa Waarabu, walimpenda kwa jitihada na umahiri wake.  Na ndio maana akapelekwa Uingereza 1954 kusomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Durham.

Zanzibar ilipopata uhuru Desemba 1963, serikali iliyoundwa na vyama vya ZNP na ZPPP ilikuwa imekwishampangia Mwinyi awe katibu wa kwanza katika ubalozi wa Zanzibar uliokuwa ufunguliwe Indonesia.

Lakini serikali hiyo ilipopinduliwa serikali ya mapinduzi ikamteua awe katibu mkuu wa wizara ya elimu na baadaye kaimu mkurugenzi wa shirika la biashara za nje (BIZANJE).

Ingawa aliwahi kushika nyadhifa za juu katika Serikali ya Mapinduzi, Mwinyi hakuwa miongoni mwa wapinduzi. Akiishi kwa hadhari kubwa. Ali Sultan Issa, aliyekuwa Waziri wa Elimu na mjumbe wa Baraza la Awali la Mapinduzi, aliwahi kunambia kwamba akimhofia Mwinyi alipokuwa Katibu Mkuu wake.

Sababu ya hofu yake ni kwamba Sheikh Abeid Karume, aliyekuwa Rais, hakuwa akimsema vizuri Mwinyi.  Ilikuwa kama alikuwa na chuki za kibinafsi dhidi ya Mwinyi na Ali Sultan alifikiri kwamba labda Mwinyi alikuwa Mshirazi.

“Siku moja nilimwita Mwinyi nikamuuliza, wewe Mshirazi?” Alinieleza Ali Sultan.

Mwinyi alimjibu kwa upole kwamba hakuwa Mshirazi, kwamba alizaliwa Bara na alipelekwa Unguja akiwa mtoto.  Ali Sultan alimueleza hofu zake na palipotokea nafasi katika Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA) alimpeleka Dar es Salaam.

“Mwinyi hakuisahau jamala hiyo na kila alipokuwa akija Zanzibar hata alipokuwa Rais wa Muungano akipita njiani akisimamisha gari na kunisalimia,” alinambia Ali Sultan.

Nakumbuka safari moja nikiwa likizoni Dar es Salaam, Abdulrahman Babu, aliyekuwa waziri katika serikali ya Muungano, alinambia kwamba Mwalimu Julius Nyerere atalibadilisha baraza lake la mawaziri siku ya pili yake.

Nilimuuliza alijuaje? Akanijibu kwamba Mwalimu alimtaka Karume ampe majina ya watu wawili kutoka Zanzibar ili amchague mmoja awe waziri.  Karume alimpa majina ya Ali Mwinyigogo na Ali Hassan Mwinyi lakini yeye alikuwa hawajui na alitaka ushauri wa Babu.

Swali langu lililofuata likawa: “Na wewe ulimpendekeza nani?” Akanijibu: Sheikh Ali Hassan.

Nikamuuliza tena: “Kwa nini?” Akanambia kwamba kwa sababu ni mtu mzima mwenye heshima na hahusiki na majungu ya kisiasa ya Zanzibar.

Siku hizo nilikuwa siyajui mengi kumhusu Mwinyi isipokuwa nikimkumbuka kwa mbali kwamba alikuwa mtu mtanashati na wa thakafa.

Katika utumishi wa serikali ya Muungano alikuwa waziri wa afya, waziri wa mambo ya ndani, balozi nchini Misri, waziri wa maliasili na utalii, na waziri wa nchi katika ofisi ya makamu wa pili wa Rais. Alipokuwa waziri wa mambo ya ndani ndipo alipochukua hatua ya kihistoria nchini Tanzania kwa kuwa waziri wa kwanza kujiuzulu kwa kosa la watumishi wa chini katika wizara yake — askari polisi waliowatesa watu waliotuhumiwa kwa uchawi na kusababisha  vifo vyao.

Wazanzibari walishusha pumzi Mwinyi alipoushika urais wa Zanzibar baada ya Nyerere kumpindua Aboud Jumbe, aliyekuwa Rais wa pili wa Zanzibar.

Kilichomchongea Jumbe kwa Nyerere ni kuonekana akiota pembe kwa kuanza ghafla kuitetea hadhi ya Zanzibar katika Muungano.

Hadithi ni ndefu lakini, kwa ufupi, Jumbe alivuliwa uwanachama wa CCM na, kwa hivyo, akapoteza sifa ya kuwa Rais wa Zanzibar. Jumbe akawekwa kizuizini nyumbani kwake Kigamboni, Dar es Salaam, alikoishi hadi alipofariki 2016 akiwa na umri wa miaka 96.

Mara baada ya Jumbe kubwagwa, Nyerere alimchomoa Mwinyi kutoka kwenye wizara ya nchi katika ofisi ya makamu wa Rais na akampachika kwenye urais wa Zanzibar.  Inasemekana kwamba Nyerere alishauriwa na Sheikh Thabit Kombo, kigogo wa siasa za Zanzibar aliyewahi kuwa katibu mkuu wa chama cha Afro-Shirazi Party (ASP).  Mwinyi akawa pia mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu mwenyekiti wa CCM.

Mwinyi alikuwa rais wa mwanzo wa Zanzibar  asiyekuwa mjumbe kwenye Baraza la awali la Mapinduzi lililoundwa Januari 1964. Wala hakuhusika kwa vyo vyote vile na mapinduzi.

Mei 1984, mwezi baada ya kuwa rais wa Zanzibar halmashauri kuu ya taifa ya CCM ilianza mchakato wa kuibadili Katiba ya Tanzania, na kuurejesha mfumo wa kuwa na makamu wa rais wawili, utaratibu ambao ulifutwa 1977.

Chini ya mfumo huo rais wa Tanzania huteua makamu wawili.  Mmoja wao huwa Rais wa Zanzibar na wa pili ndiye anayekuwa Waziri Mkuu wa serikali ya Tanzania.

Alipochaguliwa Rais wa Zanzibar, Mwinyi akawa pia makamu wa Rais wa Nyerere.  Utaratibu wa makamu wa rais wawili uliwekwa ili kuwadhihisha hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano. Badiliko hilo la kikatiba lilimjenga Mwinyi kisiasa.

Muda wote alipokuwa Rais wa Zanzibar, Mwinyi alikuwa akifanya kazi mkono kwa mkono na waziri kiongozi Seif Sharif Hamad.  Walionekana wakiwa na pupa ya kuijenga Zanzibar mpya kwa kuvifungua visiwa hivyo kwa wawekezaji wa kigeni na Wazanzibari walio ughaibuni.

Katika kipindi hicho, Wazanzibari waliokuwa wameihama nchi walianza kurudi kwa shughuli za kibiashara na kwa matembezi.  Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa wengi wao kuikanyaga Zanzibar tangu Mapinduzi.

Mwinyi alionesha ujasiri wa kujaribu kuleta mageuzi ya kisiasa kwa kushajiisha umoja na maridhiano ya Wazanzibari.

Mara tu baada ya Mwinyi kuwa Rais, Nyerere aliamrisha vigogo kadhaa waliokuwa karibu na Karume, wakamatwe.  Akiwaona kuwa wakorofi. Walifungwa gerezani au waliwekwa katika kizuizi cha nyumbani.

Miongoni mwao walikuwa wapinduzi Kanali Seif Bakari, Hafidh Suleiman na Ramadhani Haji, aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Jumbe.  Wote hao walikuwa wakitisha kwa wananchi.

Nyerere naye akiwaogopa kwa sababu akiwahusisha na mkakati wa Jumbe wa kutaka kuregeza kamba za Muungano. Jumbe, na wananchi wengi wa Zanzibar, wakiamini kwamba kamba hizo zikiikaba roho Zanzibar.  Wazanzibari walianza kuhoji iwapo Muungano ulikuwa na manufaa yoyote kwao kwa vile matatizo ya kiuchumi ya Tanzania yaliwaathiri vibaya.

Katika mazingira hayo magumu, Mwinyi alifanikiwa kwa kiwango kikubwa kuwatuliza Wazanzibari na kuwaondoshea hofu kwamba mamlaka yao yakizidi kumomonyoka kutokana na mageuzi ya kikatiba yaliyokuwa yakifanywa Bara.

Mwinyi na utawala wake wa Awamu ya Tatu walichukua hatua kadhaa za kuuimarisha utambulisho wa Kizanzibari.  Miongoni mwazo ni Katiba Mpya ya 1984, ambayo kwa mara ya kwanza, baada ya Mapinduzi, ilikuwa na Sheria ya Haki za Binadamu.

Kipengele hicho cha kisheria katika Katiba kilihakikisha kwamba kila mkaazi anakingiwa haki zake za kibinadamu zisikiukwe na anakahikishiwa uhuru na haki za kiraia.  Kila atayekiuka haki hizo aliweza kufikishwa mahakamani.

Hatua hiyo iliifaidi Tanzania nzima kwa hoja ya kwamba huwezi kuwa na Sheria ya Haki za Binadamu Zanzibar bila ya kuwa nayo Tanzania Bara. Matokeo yake ni kwamba sheria hiyo muhimu ikatumbukizwa pia katika Katiba ya Tanzania.

Fanikio jengine la Mwinyi Zanzibar ni kutungwa ile iitwayo “Sheria ya Zanzibar” iliyoainisha ni nani Mzanzibari kwa muktadha wa Katiba ya Zanzibar. Utambulisho huo ulikuwa tofauti na ule utambulisho wa uraia wa Muungano.

Hali kadhalika, serikali ya Mwinyi ilianzisha Nembo ya Taifa mahsusi kwa Zanzibar pamoja na bendera ya Rais wa Zanzibar. Pia ilichukua hatua kadhaa za kutanua demokrasia, angalau wananchi kuanza kujifaragua kwa kuwawezesha kutoa madukuduku yao kuhusu utawala bila ya hofu ya kukamatwa na kuteswa.

Hatua zote hizo zilimjenga Mwinyi katika nyoyo za Wazanzibari na alipoihama Ikulu ya Zanzibar 1985 kwenda Ikulu ya Dar es Salaam, Zanzibar iligeuka ikawa mithili ya yatima.

Mchakato uliompelekea Mwinyi amrithi Nyerere nimeuelezea kwa urefu katika jarida la Africa Events kwenye makala yenye ilani ya “A Tale of Two Presidents” (Hekaya ya Marais Wawili).  Nasikia makala hayo yalimkera Nyerere kiasi cha kumpandisha hamaki kwa sababu yalitoboa yaliyokuwa yakiendelea katika vikao vya siri vya Halmashauri Kuu ya Taifa pamoja na Kamati Kuu ya CCM.

Nyerere alifoka akitaka kumjua aliyenipasha habari hizo.

Nilipokutana naye Mwinyi London miezi kadhaa baadaye alinambia: “Umemtia matatani nduguyo Salim. Watu wengi wanafikiri yeye ndiye aliyekwambia habari zile. Mimi najua siye yeye.”

Vipi alijua, hadi leo sijui.  Kwa “nduguyo Salim” akimaanisha komredi mwenzangu Dkt. Salim Ahmed Salim aliyekuwa mshindani wake mkuu wa urais wa Tanzania ndani ya CCM na aliyesemekana kuwa ndiye aliyekuwa chaguo la Nyerere.  Hiyo ni dhana ambayo hivi sasa naitilia shaka.

Nilikutana naye Mwinyi baada ya kupigiwa simu na Anthony Nyakyi, aliyekuwa balozi wa Tanzania hapa Uingereza akinitaka nende kukutana na Rais mpya kwenye hoteli aliyoshukia.

Hapo ndipo nilipozidi kuitambua hulka yake ya unyenyekevu, upole na ucheshi.  Alipokuja tena London, niliutambua utu na uadilifu wake.  Nilidokezewa na afisa mmoja wa ubalozi wa Tanzania kwamba safari hiyo akiwa hotelini mwake alinitaja kwamba ninaipa taabu serikali yake. Akikusudia kwamba maandishi yangu ya ukosoaji kwenye magazeti ya ughaibuni yakiwakera.

Niliambiwa kwamba kuna mtu aliyekwenda kumtembelea Mwinyi aliyemwambia: “Nyiye mnajihangaisha bure. Subirini aje nyumbani, mumkamate mumtie ndani.”

Mwinyi aliruka na kumkanya akisema: “Lakini anafanya kazi yake.”

Alipoushika urais wa Tanzania, nchi ilikuwa imedamirika kwa dhiki nyingi za kiuchumi. Rafu za bidhaa madukani zilikuwa tupu. Ulaji rushwa na ufisadi ulikuwa wa hali ya juu.

Siasa pia zilikuwa zimefungika; watu hawakuweza kufurukuta kisiasa. Chama kinachotawala kiliikalia kichwani serikali. Vyombo vya habari vilibanwa.

Yote hayo Mwinyi aliyanyosha kwa kuanzisha mfumo wa soko huria, bila ya shaka kwa ridhaa ya Nyerere hata kama wakati mwingine akiridhia kichwa upande.

Unaweza kumfananisha Mwinyi na Deng Xiaoping wa Jamhuri ya Watu wa China, sio kwa umbo tu kwani wote walikuwa wafupi, lakini kwa jinsi walivyozibadili nchi zao kwa kuleta sera za mageuzi hasa katika nyanja za kiuchumi.  Mwinyi alifanikiwa kidogo zaidi ya Deng kwa kusimamia kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa wakati Deng, hata kama angetaka, asingefua dafu.

Tofauti nyingine kubwa baina yao ni kwamba Deng alifanya mageuzi baada ya kufariki Mao Zedong, aliyekuwa ameyahodhi madaraka yote nchini, wakati Mwinyi alianza kufanya mageuzi chini ya kivuli cha Nyerere wakati muasisi huyo wa Tanzania akiwa mwenyekiti wa chama pekee nchini.

Kuna wengi waliomshambulia Mwinyi kwa mageuzi ya uchumi aliyoyafanya. Walimvurumishia matusi mengi lakini hakuwa na tabia ya kusutana na kujibizana.  Alielewa kwamba anayetaka kukutukana hakuchagulii tusi.

Niliwahi kuandika katika gazeti la Raia Mwema jinsi siku moja Nyerere alipofanya dhihaka ya kutaka kunichapa kwa kifimbo chake. Kilichonichimba yalikuwa makala mafupi niliyoyaandika katika jarida la Africa Analysis na yaliyoashiria kwamba Mwalimu alivunjika moyo na baadhi ya hatua za Mwinyi.

“Kwa nini huniulizi? Kwa nini usinipigie simu kabla hujaandika?”  Nyerere aliniuliza kwa mkazo.

Ajabu ya mambo ni kwamba baadaye Nyerere aliandika kijitabu kiitwacho  Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania ambamo aliikosoa serikali ya Mwinyi.

Wengi wameeleza jinsi Mwinyi alivyokuwa mtu wa watu.  Walichokosa kusema ni kwamba alikuwa pia “mtu wa Mabwana,” yaani mtu wa masharifu.  Wenye kuzijua siri za tasaufu (“tasawwuf” kwa Kiarabu na “sufism” kwa Kiingereza) watafahamu nakusudia nini, na watamuelewa zaidi Mwinyi kwa kalima hiyo ya kwamba alikuwa mtu wa mabwana. Akiwapenda na wakimpenda.  Inavyoonesha alikuwa mtu wa tariqa ya Bani ‘Alawi ingawa akitabaruku pia na nyiradi za tariqa nyingine kama za Qadiriya na Rifa’iyah.

Safari moja nilishuhudia alaka baina yao nilipohudhuria Maulidi ya Lamu yanayoandaliwa kila mwaka na taasisi ya Msikiti wa Riyadha.

Ilisadifu kwamba mwaka huo Mwinyi pia alihudhuria na wakati wa chakula tuliwekwa chumba kimoja. Pamoja na Marehemu Sharif Hussein Badawy na mdogo wake Sayyid Ahmad bin Ahmad Badawy (Mwenyebaba) walikuwako pia masharifu kutoka Tarim Hadhramaut, Yemen, na kutoka nchi nyingine.  Hapo nilizidi kuuona unyenyekevu wake.

Nilipata fursa nyingine ya kumshuhudia Mwinyi akiingiliana na wanazuoni wa Kiisilamu mwanzoni mwa Aprili, 2018, katika kongamano la kimataifa lililofanywa Moroni, Comoro, kuadhimisha miaka 100 ya uzawa wa Sayyid Omar Abdallah (Mwinyi Baraka).

Huyu alikuwa miongoni mwa hao mabwana wa kisufi. Alikuwa “mu‘allem murshid” (mwalimu aliyekuwa akiongoza). Mwinyi Baraka, aliyezaliwa Unguja na kufia Comoro, alimsomesha alipokuwa mwanafunzi skuli ya Dole, kabla ya kwenda Uingereza kwa masomo.

Siku ya mwanzo ya kongamano hilo nilimwendea Mwinyi aliyekuwa ameketi kitini na miye nikichutama nikamnong’oneza yaliyonikaa moyoni kuhusu Rais wa Tanzania wa wakati huo, John Magufuli.

Alinisikiliza kwa usikivu mkubwa, kisha akanambia, “InshaAllah nitafanya hivyo.” Ilikuwa jawabu yake kwa ushauri nilioutoa. Pengine akinitoa njiani lakini — kama ilivyo kawaida ulipokuwa naye — nikijihisi “special” kwake, hapakuwa na mwengine kama mimi!

Siku moja nilikuwa nakwenda kuhudhuria mkutano fulani katika Bunge la Uingereza na nilipofika kwenye kituo cha treni ya chini ya ardhi karibu na hapo nilimkuta Mwinyi na walinzi wake wakinunua tiketi za kusafiria kwenye treni hiyo kama abiria wa kawaida.  Nilikwenda kumsalimia na alinambia kwamba alikuwa anatoka kwa daktari wake.

Nilifarijika Agosti 2002 alipofariki mzee wangu, kumuona Rais Mstaafu Mwinyi akiingizwa Msikiti Jibrili, Mkunazini, Unguja, na kuletwa kukaa nami wakati wa hitima.  Alimjia marehemu kwa sababu wakifahamiana tangu ujanani mwao. Huyo ndiye Mwinyi aliyekuwa mtu wa watu.

 

 Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; @ahmedrajab/X

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.