Nikionacho Baraza Kivuli ACT Wazalendo

Picha: Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe. Picha kwa hisani ya Gazeti la Mwananchi

 

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

 

MWANZONI mwa wiki hii, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alitangaza Baraza Kivuli la Mawaziri la chama hicho lenye wajumbe 54 litakalokuwa na wajibu wa kusimamia na kuzungumzia utendaji wa serikali katika sekta tofauti za masuala yanayogusa maisha ya Watanzania.

 

Umekuwa ni utaratibu wa chama hiki kuunda baraza kivuli tangu kuasisiwa kwake takribani miaka tisa iliyopita. Hata hivyo, kulinganisha na miaka mingine, nimeliona baraza la safari hili likiwa tofauti kwa maana ya muundo wake, mwelekeo, uzingativu wa usawa katika jinsia na masuala ya Muungano, mchanganyiko wa uzoefu na upya na kubwa zaidi; kuona chama cha kisiasa kikifanya jitihada kubwa mbili ambazo hazifanywi na vyama vingi vilivyopo nchini – kupika viongozi wa kizazi kipya na kutengeneza kada ya viongozi ambao siasa ndiyo kazi yao.

 

Kwa miaka kadhaa sasa, nimekuwa na utaratibu wa kutathmini utendaji wa mawaziri walio katika Baraza rasmi la Mawaziri lakini sijawahi kufanya uchambuzi wa Baraza Kivuli. Kwa mara ya kwanza, ninalazimika kufanya uchambuzi wa baraza la ACT Wazalendo kwa lengo la kutazama mambo ya msingi kwa kulinganisha na wasifu wa baadhi ya wajumbe wa baraza hilo.

 

Siasa ni kazi

 

Mwaka 1919, msomi wa Kijerumani, Max Weber, aliandika insha yake maarufu, Politik als Beruf (Politics as a Vocation) ambayo kimsingi alijenga hoja kwamba kazi ya siasa inatakiwa kufanywa na kundi la watu wanaofikiri na kutenda tofauti na watu wa kawaida. Hili ni kundi la watu wanaoamua si kwa kutumia moyo au roho bali kwa kutumia vichwa vyao. Weber aliandika; “Politics is made with the head, not with the other parts of body, nor the soul.

 

Hii ni kwa sababu, mwanasiasa anaweza kupata madaraka makubwa yatakayompa mamlaka ya kutumia dola. Ukiwa Amiri Jeshi Mkuu, kuna siku utalazimika kupeleka watu wako vitani ukijua kuna wengine hawatarudi makwao wakiwa hai. Utalazimika kufanya mambo yanayoweza kuchukiza wapambe na ndugu zako lakini ni muhimu kwa maslahi ya nchi au taasisi. Haya si aina ya maamuzi ambayo kila mtu anaweza kufanya. Lakini unaweza kumjenga mtu akawa kiongozi mzuri kwa kuifanya siasa kama kazi yake.

 

Tazama mtu kama Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete. Mara alipotoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mara moja alikwenda kufanya kazi kwenye chama cha TANU. Kikwete hajawahi kufanya kazi nyingine nje ya siasa kwenye maisha yake yote ya utu uzima. Hata alipokuwa akitumikia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alifanya zaidi kama Kamisaa wa Siasa wa Jeshi. Huyu ndiye aina ya wanasiasa ambao Weber alikuwa anawazungumzia.

 

Ukitazama Baraza Kivuli la ACT Wazalendo, kuna vijana kama Abdul Nondo, Kulthum Mchuchuli, Idrisa Kweweta, Petro Ndolezi na wengine ambao ingawa ni wasomi, wametumia sehemu kubwa ya maisha yao kufanya kazi za siasa. Kimsingi, sijawahi kufahamu kazi nyingine ya ajira za kawaida ambayo wamewahi kuifanya zaidi ya siasa.

 

Ni muhimu kwa chama chochote cha siasa kujenga kada ya viongozi – kuanzia ngazi ya vijana, ambao kwao siasa ni kazi. Kufanya hivi kunawapa uzoefu mkubwa wa kuwafahamu watu wao, taifa lao, siasa zao, kushiriki katika vikao vikubwa vya maamuzi wangali wadogo na kuwajenga kama watu wanaotumia vichwa zaidi kuwaza na kuamua badala ya kusikiliza nafsi zao.

 

Ndiyo sababu, wakati nafanya uchambuzi wa chama chochote cha kisiasa ili kujua mwelekeo wake miaka michache ijayo, huwa naangalia kama kinajenga kada ya wanasiasa au viongozi wanaoamini kwamba siasa ni kazi na wajibu wa kipekee unaotakiwa kubebwa na baadhi ya watu katika jamii yetu. Ni dalili nzuri kwa ACT Wazalendo kwamba si kwamba wanao vijana wa aina hiyo tayari, lakini wameanza kuwapa majukumu ya kushiriki katika nafasi kama za mawaziri kivuli.

 

Uwiano wa Kijinsia

 

Katika mijadala mingi ya kisiasa kuhusu masuala ya uwiano wa kijinsia kwenye ugawanaji wa majukumu, suala ambalo lipo sasa si kuna idadi gani ya wanawake na wanaume kwenye baraza au chombo husika bali ni majukumu ya aina gani wahusika wamepewa.

 

Kwa mfano, kama serikali ina uwiano wa mawaziri wa asilimia 50 kwa 50 lakini wanawake wamepewa uwaziri katika wizara kama jinsia, michezo, sanaa, mazingira na nyingine za namna hiyo huku wanaume wakipewa fedha, ulinzi, mambo ya ndani, sheria, mambo ya nje na mengine ya namna hiyo, usawa huo huwa hauna maana.

 

Jicho la haraka haraka kwenye baraza hili la ACT Wazalendo linakupa picha ya mgawanyo wa madaraka unaozingatia jinsia na majukumu. Kwa mfano, asilimia 54 ya wajumbe wa Baraza Kivuli ni wanawake na hivyo uwepo wao ni mkubwa. Hata hivyo, nimevutiwa na wapi hasa wanawake hao wamewekwa.

 

Kwa kuanzia, Waziri Mkuu Kivuli, ambaye ndiye mratibu na msimamizi mkuu wa baraza hili, Dorothy Semu, ni mwanamke. Hii ni nafasi kubwa. Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ni Wakili Bonifasia Mapunda lakini yule wa Ulinzi ni Fatma Fereji, Wizara ya Maji imeangukia kwa Mwanaisha Mndeme huku Nasra Omar akiwa Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje. Katika mwendelezo huohuo, Esther Thomas amepewa wadhifa wa Waziri Kivuli wa Fedha. Kwa vyovyote vile, huu si aina ya uteuzi wenye lengo la kujaza majina ya wanawake pekee, lakini umetoa hasa majukumu na mamlaka kwa wahusika.

 

Kuzingatia weledi

 

Katika kazi zangu za uandishi wa habari, nimebaini jambo moja la wazi katika jamii yetu; kwamba michezo na siasa ndiyo zimebaki tasnia pekee ambako weledi au usomi huwa haupewi nafasi sana isipokuwa mambo mengine kama fitina, kujipendekeza, majungu, uongo na uzandiki. Nimejaribu kutazama baraza hili la mawaziri kivuli na jambo ambalo naliona sasa ni kwamba usomi na maarifa umepewa nafasi kubwa.

 

Chukulia kijana kama John Patrick Mbozu aliyeteuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano). Yeye kitaaluma ni msomi wa shahada ya kwanza ya sheria na sasa anafanya Shahada ya Uzamili katika Masuala ya Mafuta na Gesi. Yeye ni mmoja wa vijana walioingia katika siasa wangali na umri mdogo lakini pia ni wasomi.

 

Kuna maingizo ambayo Watanzania wengi hawayafahamu. Kwa mfano, Naibu Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu), Estazia Kangwa, ni msomi wa Masuala ya Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham nchini Uingereza na pia masuala ya Ujasiriamali kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia ni mmiliki wa mojawapo ya redio zilizoko Kanda ya Ziwa.

 

Waziri Kivuli wa Afya, Dk. Elizabeth Sanga na Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje, Dk. Nasra Omar kitaaluma ni madaktari wa magonjwa ya binadamu. Bonifasia ni wakili na sehemu kubwa ya wajumbe wa baraza hili ni wasomi wa kiwango cha shahada moja. Kuondoa elimu yake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Webiro Wassira (Wakazi), ni msanii maarufu na anayeheshimika katika uga huo.

 

Muungano

 

ACT Wazalendo ni chama cha kipekee miongoni mwa vyama vya upinzani nchini Tanzania. Ingawa kinazidiwa kwa ukubwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), lakini chenyewe kinaweza kujitapa kwamba ndicho pekee cha upinzani hapa nchini chenye uhakika – walau kwa sasa, wa kuwa na uwakilishi katika pande zote mbili za Muungano – yaani Tanzania Bara na Zanzibar.

 

Ndiyo sababu, wakati nilipoona taarifa ya baraza hili, jambo la kwanza nililoanza kulitazama lilihusu ni kwa vipi suala la Muungano limetazamwa katika uteuzi huu. Uchambuzi wa majina na nafasi nilioufanya umenionyesha kwamba Zitto amefanya mawili kwenye uteuzi huu; mosi ametoa nyadhifa zote za masuala ya Muungano kwa wanawake na na amefanya uteuzi ulio sawa kwa pande zote.

 

Wizara kuu zinazosimamia masuala ya Muungano ni Fedha, Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani na Ulinzi. Zanzibar imetoa mawaziri wawili; ulinzi na mambo ya nje huku Bara ikitoa mawaziri wa fedha na mambo ya ndani. Na pale ambapo waziri alikuwa anatoka upande mmoja wa Muungano, naibu anatoka upande mwingine.

Fursa sawa kwa wote

 

Chama cha siasa kinachotaka kukua kina wajibu wa kuonyesha kwamba kiko tayari kutoa fursa kwa wanachama wake wote pasipo kujali yupi kaingia wakati gani. Jambo la msingi ni kuona ingizo jipya litaleta athari gani chanya kwa chama. Lakini, ni muhimu pia kuelewa kuwa falsafa ya kuwa na Baraza Kivuli la Mawaziri ni kutoa nafasi ya watu kuonyesha uwezo wao kabla ya kupewa majukumu zaidi kwenye chama.

 

Unaweza kumjaribu mtu kuwa Waziri Kivuli wa Habari na Mawasiliano lakini kumfanya mtu kuwa Katibu Mwenezi wa chama ni hatua ya juu ya kumwamini mtu kwa uwezo wake, maarifa na utunzaji wake wa siri na masuala nyeti ya chama.

 

Katika baraza hili, kuna jina la Malaika Milinga ambaye ni Naibu Msemaji wa Masuala ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu. Huyu ni binti wa hayati Ntimbanjayo Milinga; mjamaa mashuhuri aliyepata kuongoza Mamlaka ya Ustawi wa Mkoa wa Ruvuma (RDA). Inawezekana kuna watu wamefahamika na kutumikia ACT Wazalendo kwa muda mrefu zaidi yake lakini katika muda mfupi aliokaa na viongozi wa chama hicho, ameonyesha ana kitu atakiongeza kwenye chama. Uteuzi huu ni ujumbe kwa wanachama wapya wengine kuwa fursa za namna hii haziangalia ugeni au wenyeji ndani ya chama bali kile ambacho unakileta.

 

 

Akina Mtutura na akina Shangwe

 

Katika mojawapo ya hotuba zake maarufu za kuaga wana CCM wakati akitangaza kung’atuka katika siasa, Baba wa Taifa, Julius Nyerere, aliwahi kuzungumzia furaha yake kuwa anaiacha CCM akiwa na furaha kwa sababu chama kina “Vikwete” (akimaanisha Kikwete) na “Vingunge” (akimaanisha Kingunge Ngombale Mwiru). Nyerere alimaanisha wazoefu na vijana ndani ya chama.

 

Uteuzi huu wa Zitto kwa Baraza Kivuli la ACT Wazalendo unatoa picha ya wazoefu wa siasa za Tanzania na maingizo mapya katika mchakamchaka wa siasa za ushindani hapa nchini. Watu kama Mtutura Mtutura, Riziki Shahali Mngwali, Ally Saleh na Mchuchuli ni wanasiasa wapevu tayari wakiwa wamewahi hadi kuwa wabunge katika Bunge la Tanzania. Mwanasiasa kama Hussein Ruhava amepata kuwa Meya wa Halmashauri ya Kigoma Ujiji.

 

Watu kama Semu, Kweweta, Mbarala Maharagande, Isihaka Mchinjita, Emmanuel Mvula, Monalisa Ndala na Nondo tayari wana uzoefu wa kutosha kuhusu siasa za Tanzania. Lakini wakati huohuo kuna maingizo mapya kama vile Shangwe Ayo, Estazia, Malaika na binti mdogo mwenye umri wa miaka 23, Salma Abdallah, ambao yote yanaonyesha chama kina mustakabali mzuri huko mbele ya safari.

 

Kuhusu kivuli

 

Mshairi mashuhuri wa Uingereza, William Shakespeare, alipata kuandika; “Kuna nini kwenye jina? Uwaridi litanukia harufu ileile hata lingeitwa kwa jina lingine”. Hata hivyo, kuna sababu ya baraza hili la Zitto kuitwa “kivuli”. Linaakisi ukweli kwamba tofauti na baraza halisi la mawaziri; hili la ACT halina posho, wafanyakazi wa ziada, magari ya kusaidia shughuli za kazi na mamlaka ya dola.

 

Wala usishangae siku moja kukutana na waziri kivuli wa ACT Wazalendo kwenye daladala. Haitakuwa jambo la ajabu pia kwamba kuna wengine hutawasikia mpaka pale yatakapofanyika mabadiliko madogo ya kuwaondoa kwenye nafasi zao.

 

Mazoea ya demokrasia ya kiliberali ni kwamba aina hii ya baraza ingefaa kwa chama kikuu cha upinzani ndani ya Bunge. Ukweli ni kwamba ACT Wazalendo si chama kikuu cha upinzani kwenye Bunge la Tanzania na hivyo wawakilishi hawa hawana hata zile fursa za kuzungumza bungeni au kufaidi rasilimali zinatolewa na chombo hicho kama inavyotakiwa kikanuni.

 

Walichonacho wateule hawa wapya ni elimu yao, ndoto zao za kuwa wanasiasa wakubwa na ujenzi wa jamii wanayoitaka ya Watanzania, mazingira ya kisiasa ya Tanzania yanayoruhusu upinzani kufanya kazi zao na kero nyingi za Watanzania zinazohitaji watu wa kuzisemea. Kama watazibaini kero hizo na kuwa wazungumzaji wake mahiri – maana hilo ndilo pekee lililo ndani ya uwezo wao, wanaweza kutimiza ndoto zao katika siasa. Kama sivyo, watakuwa walau wamejaribu kufanya kitu cha maana kwenye maisha yao.

 

Kwa ACT Wazalendo, hii ni hatua nzuri inayopaswa kuendelezwa. Vyama vya siasa vimeanzishwa kwa ajili ya lengo kuu la siku moja kushika dol ana kuongoza watu na ni muhimu kwa kila chama – wakati wote, kuhakikisha kina watu wa kutosha kushika dola katika siku ya kwanza watakayoingia madarakani. Majukumu kama haya ya Baraza Kivuli ni sehemu ya maandalizi hayo.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa  mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.