ANC, BJP, CCM na Zama za Mseto

Picha kwa hisani ya tovuti ya Al Jazeera

 

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

 

NILIPIGA kura kwa mara ya kwanza mwaka 2000 na jambo moja nililolishuhudia wakati ule halijatoka kichwani kwangu hadi leo. Wakati naingia kupiga kura, nilikutana na wasimamizi wawili waliokuwa na mazungumzo ya ajabu kidogo.

 

 

Mmoja alisema; “Eti hawa wapinzani wanataka kuitoa CCM madarakani. Hii tusikubali, watatuletea vita”. Wakati ule, ingawa nilikuwa mwanafunzi wa kidato cha tano, sikuwaonea haya, niliwaambia kwamba hakuna vita yoyote itakayoletwa na upinzani. Walipigwa na butwaa. Naamini hawakutegemea mwanafunzi kuwaambia maneno yale.

 

 

Nimeyakumbuka maneno yale wakati nikimsoma mmoja wa wachambuzi maarufu wa siasa za Afrika Kusini, William Gumede, kuhusu uchaguzi uliomalizika hivi karibuni wa taifa hilo. Gumede anaamini kwamba tatizo kubwa la nchi zetu za Afrika ni kuamini kwamba mpinzani wako kisiasa ni adui yake.

 

 

Anaamini hilo halijabadilika tangu mwaka 1847 wakati Liberia lilipokuwa taifa huru la kwanza la Afrika. Kwa kupigilia msumari wa mwisho, Gumede anasema kama tutaendelea hivihivi, hakutakuwa na mabadiliko yoyote barani Afrika kwa miaka mingine 177 ijayo.

 

 

Ni kwa sababu ya kuamini kwamba mpinzani wako kisiasa ni adui yako – na si mtu ambaye mnapishana kimawazo kuhusu namna bora ya kuiendeleza nchi yenu, ndiyo sababu siasa sasa zimekuwa za chuki, wivu, ubaguzi na hisia zaidi kuhusu ukweli na uhalisia.

 

 

Hivi ni kweli kwamba aina hii ya siasa, ya kuchukiana, kubaguana na kutwezana ndiyo siasa ambayo tunataraji itatufikisha mbali au kutufikisha kutimiza ndoto zetu za kuwa mataifa yaliyoendelea?

 

 

Uchaguzi uliomalizika wa Afrika Kusini unatakiwa kutupa picha halisi ya nini hasa nchi zetu za Afrika zinatakiwa kufanya kutoka sasa. Kama ANC ikikubali kuungana na chama cha Democratic Alliance na vingine vilivyo tayari kujenga taifa lililo imara zaidi ni afadhali kufanya hivyo.

 

 

Zaidi ya nusu ya wapiga kura wa Afrika Kusini wameikataa ANC. Uamuzi wa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa ni uamuzi sahihi kwa sababu utawafanya ANC na DA kukaa pamoja kwa maslahi ya taifa lao. Hata kama Inkatha Freedom (IFK), EFF na MK nao wakikubali, huo ndiyo utakuwa uamuzi sahihi.

 

 

Tangu awali, mimi ni muumini mkubwa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK). Imani yangu inajengwa na msingi kwamba si sahihi kwa taifa ambalo ni kama limegawanyika nusu kwa nusu baina ya wafuasi wa CCM na ACT Wazalendo, kuongozwa na chama kimoja cha siasa.

 

 

Jambo pekee ambalo nimewahi kuliandikia kwa muda sasa ni kwenye kuona kwamba wabia hao kwenye kuendesha SUK Zanzibar ni kupeana nguvu na mamlaka yanayowafanya wote wawili wajihisi wana la kufanya kwenye kujenga Zbar wanayoitaka.

 

 

Hii kuona wapinzani ni maadui imerudisha nyuma nchi nyingi za Afrika. Akina Elly Anangisye na Wilfrem Mwakitwangwe walionekana maadui mwaka 1968 kwa vile tu walikuwa na mawazo tofauti kuhusu mwenendo wa nchi yetu.

 

 

Kwenye maisha yangu ya utu uzima, nimeshuhudia wanasiasa wa upinzani kama vile Augustine Mrema, Ibrahim Lipumba, Seif Shariff Hamad, Ismail Jussa, Nassor Mazrui na mbaya zaidi, Tundu Lissu, wakifanyiwa mambo mabaya kabisa na yasiyo na utu kwa sababu ni wapinzani.

 

 

Nimetazama Uganda. Angalia namna serikali ya Rais Yoweri Museveni ilivyokuwa inamtenda Kizza Besigye na sasa Bobi Wine. Siku moja, nilishuhudia askari wa Uganda wakimvurumishia Besigye maji ya pilipili za kuwasha machoni na mwilini kwake kwa sababu alikuwa anaandamana.

 

 

Huyu ni Besigye ambaye miongo michache iliyopita alikuwa msituni na Rais Museveni kuipambania Uganda iliyo bora zaidi. Baadhi ya waliokuwa wakimmwagia Kizza pilipili ni wanufaika wa Uganda ambayo daktarin huyu alihatarisha maisha yake. Lakini kosa hasa la Besigye ni lipi? Ni kwa sababu alikuwa mmoja wa wanasiasa wa kwanza kukataa Rais Museveni ajiongezee mihula zaidi ya kutawala.

 

 

Ukienda Zambia, hali si tofauti pia. Huyu Rais wa sasa, Hakainde Hichilema, alifanyiwa vitendo vingi visivyo vya utu enzi akiwa mpinzani. Katika miezi ya karibuni, naona naye ameanza kushughulika na Edgar Lungu, aliyekuwa Rais wakati Hakainde akiwa mpinzani.

 

Hizi ni siasa ambazo hazijaifikisha Afrika kokote kwenye miaka 177 iliyopita. Na kama kuna kitu naendelea kujifunza mwaka huu, ni kwamba zile zama cha chama kimoja kushika hatamu ya kuongoza dola zimepita. Hizi ni zama za kuwa na serikali jumuishi ambazo si za chama au mrengo mmoja bali uwakilishi wa makundi mbalimbali.

 

Tazama India. Wakati wengi wakiamini kwamba Waziri Mkuu, Narendra Modi, angepata ushindi wa kishindo, raia wa India wamesema hapana. Modi sasa atalazimika kuunda serikali akishirikiana na wengine.

 

 

Nikiangalia Marekani, sioni ni kwa vipi mshindi wa uchaguzi wa mwaka huu wa taifa hilo, anaweza kuunda serikali ya peke yake katika mazingira ya sasa. Mgawanyiko ni mkubwa kiasi kwamba kazi ya kwanza inatakiwa ni kujenga taifa moja.

 

 

Ni bahati kwamba Tanzania tayari Zanzibar imetuonyesha kitu. Kama ingekuwa ni mapenzi yangu, natamani sana kwamba yeyote atakayeshinda uchaguzi wa mwaka 2025, atafute namna ya kuwa na watu wa vyama vingine kwenye serikali yake.

 

 

Katika nchi ambayo watu wenye taaluma na stadi muhimu za kazi hawafiki hata asilimia 15 ya nchi nzima, tuna sababu kweli ya kuacha kundi kubwa kabisa la watu nje ya serikali kwa sababu tu kwenye uchaguzi – tena ambao hauna vigezo vya kuitwa huru na wa haki, chama kimoja kilitangazwa kushinda.

 

 

 

Chukulia mfano wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. UKAWA walipata takribani asilimia 40 ya kura zote huku CCM ikipata 40. Binafsi, niliwahi kumsikia aliyekuwa mgombea wa UKAWA, Edward Lowassa, akisema kwamba alikuwa tayari kumteua Zitto Kabwe, kuwa Waziri Mkuu wake, endapo angekuwa Rais. Wakati huo, Zitto alikuwa kiongozi wa chama kingine, ACT Wazalendo.

 

 

Aliyeshinda kwenye uchaguzi ule, John Magufuli wa CCM, hakuwa na mawazo hayo. Na ingawa watu walihama vyama vyao na kujiunga na CCM kwenye utawala wake, walihama kwanza vyama vyao kabla ya kupokewa na kupewa vyeo na chama kilichoshinda.

 

 

Ninaamini kwamba kama taifa, tulipoteza fursa adhimu mwaka 2015. Ninafahamu kwamba Magufuli alikuwa anaungwa mkono na baadhi ya watu waliokuwa vyama vya upinzani. Kama Magufuli angekubali kuunda serikali yenye vyama vya upinzani na kufanya kazi kwa pamoja, naamini sumu iliyokuja kujitokeza baadaye isingekuwepo.

 

 

Naamini Tanzania tuna uhitaji mkubwa wa akili na maarifa ya Zitto na Freeman Mbowe. Tunahitaji maarifa ya watu kama Tundu Lissu, Reggie Munisi, Halima Mdee, Dorothy Semu na wengine wengi wa aina hiyo.

 

 

Fikiria kama wakati ule wa Magufuli angekuwa na washauri wa pembeni yake kama Lissu, Fatma Karume, Zitto, Lowassa, Mbowe na wengine ndani ya baraza lake, si tungeweza kupata dili zuri zaidi kwenye mikataba ya madini? Si tungepata njia nzuri zaidi ya kufadhili miradi kama ya SGR na Bwawa la Mwalimu Nyerere?

 

 

Katika kitabu chake kipya cha Age of Revolutions, Fareed Zakaria, amejenga hoja kwamba katika zama hizi, kitu muhimu zaidi kwenye siasa ni hisia kuliko uhalisia wa mambo.

 

 

Mimi naziona hizi kama Zama za Serikali za Mseto. Kwa sababu ya aina ya siasa zinazoendelea sasa duniani, hakuna sababu ya kuwa na chama kimoja madarakani chenye nguvu na mamlaka yote. Nguvu ya serikali, itakuwa nguvu ya umoja wa wale walio ndani yake.

 

 

Na katika hili, ni muhimu zaidi Afrika kuliko kote kwingine.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.