Na Ezekiel Kamwaga
“Maji kila mahali lakini hakuna hata tone moja la kunywa”
Samuel Taylor Coleridge, The Rime of the Ancient Mariner
MWANZO kabisa, napenda kutoa pole kwa Watanzania wenzangu ambao wameathirika kwa namna moja au nyingine na mvua hizi za El Nino zinazoendelea kunyesha.
Ninafanya kazi kwenye kituo cha televisheni na ninaona picha nyingi za maeneo tofauti ya Tanzania ambako watu wameathirika na mvua. Nimezaliwa, kukulia na bado naishi Dar es Salaam na hivyo nimeshuhudia pia kwa macho yangu kile kinachoendelea sasa kufuatia mvua zinazonyesha.
Ukweli mmoja wa wazi kuhusu Dar es Salaam, na Tanzania kwa ujumla, ni kwamba kila mvua zinaponyesha, unaweza kujua ni wapi na wapi kutakuwa na matatizo. Maeneo ni yaleyale, miundombinu inabadilika lakini sijawahi kuona kama kuna tofauti yoyote kulinganisha na ilivyokuwa miaka 30 iliyopita wakati nimeanza kupata akili ya utambuzi. Ningeweza kutumia muda mrefu kueleza kuhusu kutobadilika kwa namna tunavyojiandaa na mvua na namna hali ileile imekuwa ikijirudia palepale, kwa watu walewale na kwa mazingira yaleyale kila uchao.
Leo ninataka kuzungumzia kuhusu kitu ambacho pengine hatukijadili sana. Ni kuhusu ni kwa vipi sisi Watanzania tunatumia maji haya ya mvua inayoendelea. Nukuu yangu niliyoanza nayo kwenye makala haya inahusu mtu aliyeona maji ya bahari lakini akashindwa kuyanywa kwa sababu ya chumvi nyingi lakini nimeichukua kwa sababu yangu binafsi.
Kwamba inakuwaje baada ya mvua hizi kubwa, maji haya yote ya mvua inayoendelea, tutaanza kulalamika kuhusu ukosefu wa maji wiki au miezi michache tu baadaye?
Mwaka huu, mvua hii imekuwa na maana tofauti kwangu. Imekuja takribani mwezi mmoja baada ya kuwa nchini India na kumsikia Waziri Mkuu wa taifa hilo, Narendra Modi, akitueleza Watanzania namna alivyojenga zaidi ya mabwawa laki moja – narudia, mabwawa laki moja ya maji, kwa kutumia mbinu za kuvuna na kuhifadhi maji.
Maji ya mvua ni miongoni mwa vyanzo vya maji safi. Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizopo, katika maji yote yaliyopo duniani, maji safi ni asilimia tatu tu. Yanapatikana katika maeneo tofauti matatu; mito na maziwa, ya kuchimba ardhini (visima) na ya mvua. Kwa namna hiyo, kuondoa wale walio jirani na mito na maziwa, maji ya mvua ndiyo maji safi mengine ambayo ni rahisi kuyapata. Hata hivyo, uzoefu wangu na taifa langu – kuanzia kwa serikali hadi kwa sisi wananchi wa kawaida, maarifa yetu ya kuvuna na kuhifadhi maji ni madogo.
Sijui ni Watanzania wangapi ambao wamejenga nyumba na kuweka kinga maji za kuhakikisha wanaweza kuvuna maji wakati kama huu. Katika rafiki zangu wa karibu, ni mmoja tu ambaye ninafahamu ana mfumo wa kukusanya maji na ana tenki la maji la chini ya ardhi linalokusanya maji yote ya mvua yanayogusa bati la nyumba yake.
Kwa maelezo ya rafiki yangu huyo, maji anayokusanya wakati wa majira ya mvua pekee hutosha kwa matumizi ya nyumbani kwake kwa muda wa miezi mitatu. Alichonieleza ni kwamba kama ikitokea Dar es Salaam ikakauka maji kwa muda wa miezi mitatu, yeye ana uhakika wa kupata huduma hiyo kwa muda wote huo.
Huyo ni mtu mmoja. Ina maana kwenye nyumba zetu pekee tuna uwezo wa kuhifadhi maji ya walau mwezi mmoja mpaka miwili kama tutaweka mifumo ya kukinga maji. Hili si la kulisikia India, nimeliona mwenyewe hapa Dar es Salaam.
Nimekumbuka kuhusu maelfu ya shule za msingi na sekondari zilizojengwa vijijini. Kuna maeneo watoto wanalazimika kwenda kufuata maji visimani na kwenye mito kwa sababu ya ukosefu wa maji shuleni. Lakini unakuta shule nzima haina mfumo wa kuvuna na kuhifadhi maji wakati wa mvua.
Kama shule zitaweza kuwa na akiba ya maji ya kutosha miezi mitatu, ina maana wanafunzi hawatalazimishwa kwenda kufuata maji mbali na watapata muda mrefu wa kujisomea na kufanya shughuli nyingine. Lakini shule ina vyumba takribani 20 na hakuna mfumo wa kuvuna maji.
Naangalia pia maji yanayopita kuanzia Kinyerezi kupita Kigogo, Jangwani na kuishia Bahari ya Hindi kwa miaka yangu yote ya uhai. Hakuna hata sehemu moja hapo kati ambako tumeweka mfumo wa kuvuna na kuhifadhi maji.
Maji yote yanaelekea baharini na kuwa ya chumvi na kufanya yashindwe kutumika. Modi aliuambia ujumbe wa Tanzania kwamba tukitaka tunaweza kujenga mabwawa mengi zaidi kwa kuangalia tu njia ambako maji yanapita – yale ya mvua, na kujenga mabwawa.
Nafahamu kwamba ujenzi wa miundombinu hii ni gharama. Lakini gharama ni lazima ipimwe kwa kufanya mlinganisho na nini kinapotea. Kama maji yanasababisha mafuriko na uharibifu wa mali, hayana faida.
Na kimahesabu ipo mifano ya kuonyesha kwa nini kujenga miundombinu ya kuvuna na kuhifadhi maji kunaweza kuokoa fedha. Mwaka 2011, wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, uchumi wa Tanzania ulipanda kwa asilimia 6.4 badala ya makisio ya asilimia saba na sababu kubwa ikitajwa ni ukame uliosababishwa na ukosefu wa mvua.
Kwa viwango vya mwaka 2011, kusinyaa ukuaji uchumi kwa kiwango hiki cha asilimia 0.6 – kwa mujibu wa ripoti ya Water Resource Group ya mwaka 2014, kilikuwa sawa na dola za Marekani milioni 142 (karibu shilingi bilioni 350 kwa viwango vya sasa). Kama maji yangevunwa ipasavyo na kusaidia kwenye kilimo, maji safi na salama na kukata makali ya mgawo wa umeme, hasara isingefika huko.
Kama kiwango hicho kingeangaliwa kwa kuangalia kila mwananchi wa wakati huo ameathirika vipi, ina maana vipato vya watu 250,000 viliathirika na hali hiyo.
Ninachotaka kusema hapa ni kwamba suala la kuwa na mikakati ya kuvuna na kuhifadhi maji haliepukiki kama kweli tunataka kufaidi maji haya ambayo ni sawa na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwetu.
Kuna takwimu kuhusu Tanzania na namna tunavyopoteza maji safi zinahuzunisha. Kuna mahali niliwahi kusoma kwamba kwenye kilimo cha mpunga pekee, wakati nchi zilizoendelea zinapoteza maji walau asilimia 10, sisi tunapoteza maji kwa takribani asilimia 85.
Na ukiangalia miradi yetu ya maji wakati mwingine unaweza kuona tatizo lilipo. Kuna maeneo ambako ujenzi wa bwawa la kuhifadhi maji na mifumo ya kuvuna maji ingekuwa rahisi na haraka zaidi lakini utakuta miradi ina gharama kubwa za kutandaza mabomba kwa umbali mrefu na nyingine za uendeshaji.
Unakuta mradi wenye gharama ya shilingi bilioni moja, kuna gharama za shilingi milioni 300 kutandaza mabomba, 300 nyingine kununua gari aina ya shangingi kwa ajili ya watendaji, milioni 100 ya gharama za uendeshaji na milioni 200 pekee inahusu maji husika.
Matokeo yake ni kuwa na miradi ambayo mabomba yapo, ofisi zipo na watendaji wapo lakini maji hakuna. Mabomba mpaka yanachakaa na kupata kutu lakini maji hakuna.
Ni muhimu sana kama taifa tukajitafakari. Kuanzia serikali inayoona maji yanatiririka kila mwaka kuelekea baharini bila kuyavuna. Kwa maji yanayosababisha mafuriko na kufunga barabara wakati yanaweza kuvunwa na kutumika vizuri zaidi.
Kwa kujenga shule, hospitali na ofisi za umma ambazo hazina mifumo ya kinga maji. Ni kwa vipi jengo ambalo inajulikana watu wataishi na watahitaji maji lijengwe pasi na mfumo wa kuvuna maji?
Na kwa sisi wananchi wa Tanzania tunaojenga nyumba zetu na kuacha maji yaanguke ardhini na baada ya siku mbili tunalalamikia kukatika kwa maji majumbani kwetu. Nyumba iliyojengwa kwa thamani ya mamilioni ya shilingi, inakosaje mfumo wa kutunza maji wenye thamani ya walau milioni kadhaa? Hili si la serikali. Ni letu sisi wenyewe.
Tubadilike. Ni aibu kulalamika ukosefu wa maji wakati maji yote haya yametuzunguka.