Sheikh Abbas Idi, pumzika kwa amani Janat Firdaus

Picha: Sehemu ya umati wa wananchi  waliojitokeza kwenye mazishi ya Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Abbas Idi Noboka, Agosti 29, 2023. Picha kwa hisani ya Zitto Kabwe. 

 

Na Zitto Kabwe

 

Sheikh Abbas Idi Noboka, Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Mjumbe wa Baraza la Masheikh Mkoa na Sheikh wa Kata ya Mwanga alifariki dunia mnamo Agosti 28, 2023 na kuzikwa  siku moja baadaye katika makaburi ya Lubengera yaliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji. Sheikh Abbas aliugua kwa muda mfupi na kufanyiwa operesheni ya kukata utumbo. Baada ya operesheni alipata shinikizo kali la moyo ( massive heart attack) na kupoteza maisha.

 

Mazishi yake yalikuwa makubwa sana. Maandamano ya kuelekea malaloni (makaburini) yalikuwa makubwa kwa urefu wa kilometa moja. Nilipewa heshima ya kuwa miongoni mwa watu wachache walioingia katika kaburi kumhifadhi sheikh wetu. Watu wengi walizungumza maneno mazuri kuhusu wema wa Sheikh Abbas kwa waumini wa Kiislamu na wasio Waislamu. Katika Maisha yake alikuwa pia Mjumbe wa Bodi ya Parole katika Mkoa wa Kigoma na hivyo kufanya kazi kubwa ya kijamii katika kutoa misamaha kwa wafungwa.

 

Nilimfahamu Sheikh Abbas nikiwa kijana mdogo wa miaka sita hivi. Babu yangu upande wa mama yangu Almarhum Salum Mohammed alinipeleka madrasa (Shule ya dini ya Kiislamu) kama ilivyo ada ya watoto katika jamii za Kiislamu. Tukiwa darasani tuliletewa mwalimu mpya baada ya kutokuwa na mwalimu kwa wiki chache. Wakati huo tukimwita Mwalimu Abbas, ndiye aliyeanza kutufundisha Kurani Tukufu. Chuo chetu kiliitwa Madrasat Idhihar.

 

Sheikh Abbas ni mzaliwa wa Kijiji cha Bugamba, Kata ya Mwamgongo. Alianza kusoma masomo wa dini kijijini Bugamba, kijiji kilicho milimani kutoka mwambao wa Ziwa Tanganyika. Baadaye alisoma kwa Sheikh Khalfan Kiumbe katika Mji wa Ujiji na kuanza kusomesha dini katika mji wa Mwandiga kabla ya kuhamia Mwanga kuja kutusomesha sisi.

 

Nilipoanza masomo ya ‘kizungu’ katika Shule ya Msingi Kigoma, mwalimu Abbas Idi tayari alikuwa amekuwa Sheikh baada ya kumrithi sheikh Idrisa Athumani aliyefariki dunia mwanzoni mwa miaka ya 1980. Niliendelea na masomo ya madrasa nikiwa naendelea na Shule ya Msingi na vile vile nikihudumu katika Msikiti wa Mwanga ambao Abbas alikuwa Kiongozi wake. Kumbukumbu kubwa ya watu wengi wa Kigoma ni wajibu aliotupa mimi na mwenzangu, Jumanne Feruzi, kusoma nyiradi siku za mwezi wa Ramadhani katika sala za tarawehe.

 

Nilipomaliza masomo mpaka vyuo vikuu na hatimaye kuingia katika maisha na kazi za siasa, niliendelea kuwa karibu na Sheikh Abbas kwa malezi ya kiroho.

 

Tangu mama yangu mzazi Hajjat Shida Salum afariki dunia, Sheikh Abbas alikuwa nguzo ya kisomo ninachofanya kila mwaka kumwombea dua mama na wazee wetu wa mji wa Kigoma Ujiji. Vilevile tangu nimekuwa mtu mzima yeye ndiye amekuwa akisimamia zakat fitr zangu kila mwezi wa Ramadhan Kwa mujibu wa mila na desturi za dini yetu.

 

Alikuwa mtu mwaminifu sana. Alikuwa kimbilio la watu wengi katika mji wa Mwanga kwa shida zao mbalimbali. Vilevile aliongoza msikiti wetu wa Quds, Mwanga kwa uadilifu mkubwa kiasi kwamba hatujawahi kusikia mgogoro wowote wa uongozi katika miaka 40 ya utumishi wake.

 

Sheikh Abbas alikuwa kiongozi wangu wa kiroho mpaka mauti yalipomkuta. Kabla hajaingia chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Maweni kufanyiwa operesheni ya utumbo, Sheikh alimwagiza kijana wake wa kiume, Nurdin, anipigie simu.
Sheikh alipoteza maisha siku moja baadaye kutokana na shambulio kali la moyo lililotokana na shinikizo la damu la muda mrefu. Licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Maweni, Allah alikuwa ameshapitisha hukumu yake.
Inna lillah waina ilaih raajiun.

 

Siku ya mazishi yake nilisoma shairi hili. Nimeona niliweke wazi kwa heshima yake.

 

Sheikh Abbas Idi Noboka, roho yako ipumzike kwa amani,
Ulikuwa nuru ya elimu, mwanga wa dini yetu,
Ulinifundisha Qur’an, ulinifundisha njia ya imani,
Kijana mdogo ulipewa usheikh, baada ya Sheikh Idrissa kuondoka.

 

Wazee wa Mwanga, walikupenda na kukuheshimu,
Kwa hekima yako na busara, uliwaongoza kwa umakini,
Ulikuwa kiongozi wangu wa kiroho, mlinzi wa roho yangu,
Kwa muda wote wa maisha yangu, ulikuwa karibu nami.

 

Mama Idi, mke wako mpendwa, alikufa miezi michache iliyopita,
Moyo wako ulijaa huzuni, lakini ulimshukuru Mola,
Sasa anakutazamia kutoka pepo ya milele,
Wewe na yeye mtakutana tena, kwa furaha tele.

 

Sheikh Abbas Idi Noboka, utaungana nao kwa amani,
Katika pepo ya milele, pamoja na wazee wako wapendwa,
Mzee Hilal Mahuba, Mzee Omar Ng’ongo,
Mzee Abdallah Said, Mzee Feruzi Hanzuruni,
Mzee Khamis Kauke, Mwalimu Miraji, na Mzee Rashid Lukandamila.

 

Ulipendwa na viongozi wako, Sheikh Hassan Idi Kiburwa,
Sheikh wetu wa Mkoa, alikukaimisha kila wakati,
Akiwa nje ya mkoa, akiamini utakuwa mrithi wake mwema,
Lakini leo yupo hapa, anakuaga umetangulia,
Ni majonzi hayana kifani, machozi yanatiririka.

 

Tutakukumbuka kwa uongozi wako thabiti,
Kwa kujitoa kwako kwa ajili ya jamii yetu,
Ulikuwa mfano wa unyenyekevu na subira,
Sheikh Abbas Idi Noboka, roho yako ipumzike kwa amani.

 

Tunamuomba Mola akupokee kwa rehema zake,
Akusamehe makosa yako na kukusamehe,
Na akupe thawabu tele kwa kazi yako njema,
Sheikh Abbas Idi Noboka, roho yako ipumzike kwa amani.

 

Kwa kila jina lililotajwa, kwa kila kumbukumbu nzuri,
Sheikh Abbas Idi Noboka, tutakukumbuka kwa milele,
Kama nyota angani, utaendelea kung’ara,
Katika nyoyo zetu, daima utakuwa hai.

 

Allah amsamehe makosa yake na amuweke Janat Firdaus, sheikh wetu mwema.

 

Mwandishi wa makala haya ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na amepata kuwa mbunge wa majimbo tofauti ya mkoa wa Kigoma kwa vipindi vitatu mfululizo.