Tafakuri za ghafla juu ya Muungano

 

Na Ahmed Rajab

 

KUTIMU miaka 60 ya Muungano wa Tanzania mnamo 26 Aprili, 2024, kumezidi kuwasisimua na kuwatia jazba baadhi ya waumini wa Umajumui wa Afrika. Mhemuko wao umewafanya wausukume na wajaribu kuufikisha mbinguni Muungano huo. Wanauelezea kuwa ni mfano thabiti wa umoja halisi wa Afrika.

 

 

Mashabiki hao wa Muungano wanasisitiza kwamba lazima Muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar uangaliwe kwa mtazamo mpana. Wanahoji kwamba fahari na uzito wake wapaswa kuzingatiwa katika muktadha wa historia ya Afrika na mafanikio ya Waafrika katika kupambana na kuushinda ukoloni, ubeberu na itikadi za kibaguzi.

 

 

Hayo ni maneno yenye kuutukuza Muungano. Yanaufanya uonekane kama ulikuwa na malengo adhimu, hata kama waasisi wake hawakuwa na dhamira hizo.

 

 

Taarifa za siri za serikali za Marekani na Uingereza ambazo sasa ni ruhusa mtu kuzipitia, zinaonesha kwamba Muungano ulikuwa mkakati wa kuikaba roho Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyoibuka baada ya Mapinduzi ya 1964.

 

 

Hizo zilikuwa zama za “Vita Baridi” baina ya dola za Magharibi na zile za Mashariki zilizokuwa zikiongozwa na Muungano wa Jamhuri za Kisovieti za Kisoshalisti (USSR). Zanzibar mpya ilionekana ikielemea upande wa Mashariki.

 

 

Jirani zake, Kenya, Tanganyika na Uganda, zilikuwa upande wa Magharibi.

 

 

Wakati huo, Zanzibar ikijigamba kuwa ikitaka kuleta usawa kwa wananchi wake wote.  Na ni kweli kwamba katika miezi ya mwanzo baada ya mapinduzi hapakuwa na mambo ya kijingajinga ya ubaguzi.

 

 

Zanzibar ilijititimua iwe mfano mwema kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki.  Ujerumani ya Mashariki ilipeleka Zanzibar mastadi wa uchumi kuisaidia kuandaa Mpango wake wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitatu.

 

 

Kwa kuwa ilisusiwa na nchi za Magharibi, Zanzibar ikitegemea kupata ruzuku na misaada isiyo na masharti kutoka nchi za Kikomunisti. Yote hayo yaliwafanya viongozi wa Zanzibar wawe na matumaini makubwa ya kuviendeleza visiwa vyao.

 

 

Ni matumaini hayo yaliyozitia hofu nchi za Magharibi.  Hazikutaka Zanzibar iwe nchi ya kupigiwa mfano katika ukanda wa Afrika Mashariki.

 

 

Ndio maana Marekani ikaanza kuisema Zanzibar kuwa ni “Cuba ya Afrika”.  Nia yake ilikuwa kuzitia hofu nchi jirani ziione Zanzibar kuwa ni ya kikomunisti.  Marekani ikiamini kwamba lau Zanzibar ingefanikiwa basi ingekuwa mfano mbaya kwa nchi jirani.

 

 

Marekani na Uingereza zikausuka mkakati wa kuisambaratisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

 

 

Mambo yalianza kwenda kombo Zanzibar ilipounganishwa na Tanganyika miezi minne baada ya Mapinduzi. Ule Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitatu ulitupiliwa mbali na Zanzibar ikapoteza dira.

 

 

Si kwamba nia ya kuungana ilikuwa mbaya. Lakini Muungano uliingia nuksi kwa namna ulivyoasisiwa, kwa papara, kwa malengo yasiyotukuka na bila ya ridhaa ya wananchi wa Tanganyika na wa Zanzibar.

 

 

Pia, Nyerere hakuwa na insafu aliposhauri nchi hizo ziungane, kila moja ikiwa na serikali yake. Sasa tunajua, kwa yaliyotokea, kwamba nia yake ilikuwa baadaye serikali ya Zanzibar iyayuke na pabaki serikali moja tu ya Muungano.  Mpango ulikuwa pawe na serikali mbili kuelekea moja.

 

 

Hadi sasa wapo baadhi ya wafuasi wa Nyerere na viongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi kinachotawala wenye kuona kuwa njia hiyo ya kuelekea serikali moja ndiyo njia sahihi ya kuuhifadhi Muungano.

 

 

Wazanzibari wanaiona dhana hiyo kuwa ni njama ya kuimeza nchi yao na kuigeuza iwe mkoa.

 

 

Nyerere hakuwa na pupa kutimiza lengo lake.  Aliwavumilia Wazanzibari huku taratibu akiyadokoa mamlaka yao na kuyaingiza katika orodha ya yale yaitwayo “mambo ya Muungano”.

 

 

Hivi sasa imesalia miaka 40 kabla ya kutimu karne nzima tangu Muungano uundwe. Maswali kadhaa yanajichomoza yaliyonifanya niwe na tafakuri za ghafla juu ya Muungano.

 

 

Tafakuri yangu ya kwanza ni juu ya uhai wa Muungano wenyewe na uwezekano wa kuvunjika bila ya kuvunjwa kwa kusudi.

 

 

Licha ya kudumu kwa miaka 60, Muungano hauko shuwari, japokuwa watawala wanajikaza kwa kusema kuwa ni imara — hauyumbi wala hauwezi kuyumbishwa.

 

 

Hapa tunapaswa kujikumbusha kwamba Muungano uliokuwa na nguvu zaidi ya huu wa Tanzania ulikuwa ule wa USSR. Muungano huo ulizaliwa 1922 na ulikufa 1991 – ukiwa na umri wa miaka 69.

 

 

Muungano wa USSR ulijifia baada ya kujipasukia ndani kwa ndani.  Mpasuko huo ulisababishwa na mchanganyiko wa sababu, za ndani na nje. Lakini za ndani ndizo zinazoyashabihi mazingira ya Tanzania na ndizo nitazozitaja hapa.

 

 

Kwanza, katika USSR kulikuwa na shida za maisha zilizosababishwa na uzorotaji wa uchumi, ufisadi na kuanguka kwa hali za wananchi. Hayo yapo Tanzania.

 

 

Pili, kulikuwa na ukandamizaji na kukosekana kwa uhuru wa kisiasa. Wananchi walizidi kutoridhika na wakiiona serikali kwamba haikuwa na uhalali wa kutawala. Kelele kama hizo tunazisikia Tanzania.

 

 

Tatu, kulikuwa na manung’uniko makubwa ndani ya jamhuri zilizounda Muungano huo kutaka usawa na kampeni za kutaka kujitenga zilipamba moto.  Kelele za Wazanzibari zenye kudai mamlaka kamili ni mithili ya hayo yaliyokuwa yakitokea katika Muungano wa USSR.

 

 

Nne, kiongozi wa USSR Mikhail Gorbachev alijaribu kuleta mageuzi kwa dhana zake za ‘glasnost’ (uwazi) na ‘perestroika’ (kuunda upya mifumo ya siasa na uchumi).  Jitihada kama hizo zinajaribiwa Tanzania.

 

 

Gorbachev alifanikiwa kwa kiwango fulani lakini, mageuzi hayo yaliugeukia utawala wake kwani yalichochea hisia zaidi za kutaka kujitenga kwa jamhuri za Muungano na zilizusha taharuki kubwa za kisiasa na kijamii.

 

 

Hatimaye, mageuzi ya Gorbachev yaliudhoofisha udhibiti wa serikali kuu na wakosoaji wa serikali wakapata mwanya wa kufurukuta.

 

 

Ingawa walikuwepo wachambuzi walioamini kwamba Muungano wa USSR utasambaratika, sidhani kama kuna waliofikiria kwamba ungeporomoka, kwa ghafla na kwa kasi, kama ilivyotokea 1991.

 

 

Kusambaratika na kuporomoka kwa USSR ni funzo kwa Muungano wa Tanzania.

 

 

Tafakuri ya pili iliyonijia ghafla ni iwapo kuna linaloweza kufanywa kuwatuliza roho Wazanzibari na Watanganyika.

 

 

Watanganyika wana dukuduku kwa kuhisi kuwa nchi yao imetoweka, na hawana utambulisho. Na kuna wahisio kwamba Zanzibar inapendelewa, hasa katika uwakilishi bungeni, kwa vile ni kijinchi kidogo ikilinganishwa na Tanganyika.

 

 

Wazanzibari nao wanakumbusha kwamba Zanzibar iliyokuwa na mamlaka kamili kabla ya Muungano, sasa imebaki kama kifuu. Haina inaloweza kulifanya ikiwa halitakiwi na serikali ya Tanganyika inayojivisha koti la serikali ya Muungano.

 

 

Kuna miradi kadhaa ya Zanzibar iliyokwamishwa na Serikali ya Muungano. Miradi hiyo ikihitaji kusainiwa na serikali ya Muungano lakini serikali hiyo ilikataa kusaini.

 

 

Mara nyingi serikali ya Muungano imekuwa ikijifanyia mambo kana kwamba Zanzibar inapaswa kudhibitiwa au ni “koloni” la Tanganyika.

 

 

Katika miaka yote hii 60 hapajafanywa jitihada za dhati za kuufanya Muungano wa Tanzania uwe wa usawa baina ya nchi mbili huru na zilizokuwa na mamlaka kamili.

 

 

Kwa miongo yote sita, Zanzibar ilidumaa kiuchumi. Haikuwa na maendeleo ya maana ambayo serikali ingeweza kujivunia.

 

 

Yapo mambo kadhaa ambayo lau yakitekelezwa yanaweza kutuliza roho za wapinga Muungano, ingawa siamini kwamba kutuliza roho kutazizima kelele zinazozidi kupaa dhidi ya Muungano.

 

 

Miongoni mwa mambo hayo ni: kugawana kwa usawa mali za Tanzania; kuwarejeshea Watanganyika utambulisho wao; kuipa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mamlaka zaidi ya utawala bila ya kuingiliwa na Dodoma; kufanywa uchaguzi wa haki na kuyakubali matokeo; kuuheshimu na kuuhifadhi utambulisho na utamaduni wa Zanzibar na kuhakikisha kwamba maslahi yake yanalindwa.

 

 

Na ni muhimu pia kwamba malalamiko ya Zanzibar tangu Muungano uundwe, yazingatiwe.

 

 

Tafakuri inayokwenda sambamba na hiyo ni ya kutaka kujua ni njia gani zitumiwe ili Muungano, kama una faida, uendelee kudumu kwa miaka 60 mingine au zaidi?

 

 

Nafikiri kwamba njia pekee ya kuudumisha na kuzivutia nchi nyingine zijiunge nao kwa msingi wa Umajumui wa Afrika ni kuubadili muundo wake. Badili ya kuwa na Muungano wa serikali mbili au hata wa serikali tatu naamini kwamba Muungano utaokuwa endelevu na imara ni ule utaoundwa juu ya msingi wa Mkataba.

 

 

Tanganyika na Zanzibar ziufumue muundo wao wa sasa wa Muungano na ziufume tena kwa kuzifanya nchi hizo mbili ziungane kwa Mkataba.  Na kwa wale wanaousifia Muungano kuwa ni hatua ya kwendea kwenye Umajumui wa Afrika, basi kuweko na kifungu katika Mkataba huo cha kuziruhusu nchi nyengine za Afrika zitakazotaka kujiunga nao,

 

 

Tafakuri yangu ya tatu imechochewa na swali lililo nyeti. Nalo ni kwamba, kama tutakubaliana ya kuwa Muungano umeshindwa, na hauna dawa, basi njia gani zitumiwe kuuvunja, kwa amani?

 

 

Endapo hali itafika hapo, pande mbili za Muungano zinaweza zikakubaliana juu ya mchakato wa kupatikana talaka ya amani. Panaweza, kwa mfano, pakapigwa kura ya maoni juu ya suala hilo.

 

 

Kwa vile idadi ya Wazanzibari ni ndogo sana ikilinganishwa na ya Watanganyika, lazima patumike mfumo utakaohakikisha kwamba sauti za Wazanzibari hazitafudikizwa na sauti za Watanganyika.  Au kura hiyo iwe kwa Wazanzibari peke yao kwa vile wengi wao ndio wenye kuushuku Muungano kwa shida zao.

 

 

Njia nyingine ni ya kufanya mabadiliko katika katiba za Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar ili zirejeshwe dola mbili huru za Tanganyika na Zanzibar.

 

 

Pamoja na tafakuri hizo juu ya Muungano, nimekuwa pia nikiitafakari Zanzibar na watu wake.  Zanzibar imekuwa ikiteseka na ikijitesa kisiasa kwa takriban miaka 70 tangu zianze ziitwazo zama za siasa.  Mipasuko katika jamii imetufikisha hapa tulipofika.

 

 

Vizazi vipya vya Wazanzibari vina shauku ya kuijua historia ya kisiasa ya nchi yao. Wanataka kujua walikotoka ili wajirudi wasirejelee makosa ya wazee wao.

 

 

Wazanzibari wanahitaji kuwa na umoja ulio imara.  Lakini ili wawe na umoja huo kuna mambo mawili muhimu wanayopaswa kufanya. Kwanza, wale wenye kuupinga uhuru wa Zanzibar wa Desemba 10, 1963 waukubali ukweli huo wa kihistoria na waache siasa za kitoto za kuukana.

 

 

Pili, kuna haja ya kuyatathmini upya Mapinduzi ya 1964.  Wazanzibari wayatafakari kwa kujitenga na hisia walizokuwa nazo au walizolishwa na wazee wao – wa kifamilia au wa kisiasa. Yanayostahili kupongezwa yapongezwe; yanayostahiki kupondwa yapondwe.

 

 

Pakizuka suitafahamu na kutokubaliana kwa machache basi pawepo na uvumilivu wakukubaliana kutokubaliana. Lengo liwe kuimarisha umoja.

 

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; @ahmedrajab/X.

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.