Maelezo ya picha: Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya mamilionea wa Tanzania baada ya mkutano wa Kamati ya Okoa Maisha Somalia uliofanyika Ikulu mwaka 2011 kuhusu namna ya kuisaidia nchi ya Somalia kwa misaada ya kibinadamu. Kutoka kushoto ni Haruna Zakaria, Said Bakhresa, hayati Reginald Mengi, Kikwete, Gulam Dewji na Balozi Said Shamo.
Na Ezekiel Kamwaga
KWA mara nyingine tena, bilionea Aliko Dangote wa Nigeria ameonyesha njia barani Afrika kwa kufanya uwekezaji ndani ya taifa lake utakaookoa mabilioni ya fedha za kigeni ambayo nchi yake ingelipa kuagiza mafuta kutoka nje.
Mradi wa mkubwa wa kuchakata mafuta ghafi ulioko Lekki, Nigeria, wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 19 za Marekani (takribani shilingi trilioni 40) ndiyo utakuwa mradi mkubwa zaidi wa aina yake duniani na utasaidia si mafuta peke yake lakini utazalisha mbolea na umeme kwa Nigeria.
Nigeria ilitakiwa kuwa na mradi kama huu miaka 30 au 40 iliyopita. Hata hivyo, watawala wa taifa hilo – kwa sababu tofauti, walikuwa na mawazo mengine vichwani mwao. Kulikuwa na sababu nyingine pia, kwamba taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika halikuwa na tajiri mwenye misuli ya kiuchumi inayofanana na aliyonayo Dangote sasa.
Akili ya mfanyabiashara inafanya kazi haraka kuliko ya mwanasiasa. Kwa sehemu kubwa, akili ya wanasiasa inaishia kwenye namna ya kushika dola na kubaki madarakani. Akili ya mfanyabishara inawaza mara zote namna ya kuongeza mapato na fursa za kiuchumi katika mazingira yanayomzunguka.
Ndiyo sababu ni muhimu sana kwa nchi kutengeneza matajiri wakubwa watakaoisaidia kujenga uchumi na kupambana na changamoto za kimaisha zinazokabili wananchi wa kawaida. Duniani kote, matajiri wa aina ya Dangote huwa hawaibuki hivihivi. Ni lazima taifa husika lijenge mazingira ya kuwasaidia kufikia utajiri huo.
Hakuna mfano mzuri wa serikali kutengeneza matajiri kama mfano wa Aliko Dangote. Katika mahojiano aliyowahi kufanya miaka ya nyuma, Dangote alisimulia kwamba siri ya utajiri wake ni urais wa Olusegun Obasanjo. Kwamba kama Obasanjo asingefanya aliyoyafanya, yeye asingekuwa mtu mweusi tajiri zaidi duniani.
Obasanjo alimfanyia nini Dangote?
Kwa mujibu wa maelezo yake, mara tu baada ya kuingia madarakani siku moja mwanzoni mwa miaka ya 2000, Obasanjo – wakati huo akiwa Rais wa Nigeria, alimwita ofisini kwake na kumuuliza lipi likifanyika inaweza kufanya iwe rahisi kwa Nigeria kuacha kuagiza saruji kwa wingi kutoka nje na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kwa jambo hilo.
Dangote alimweleza Obasanjo kwamba ni nafuu kwa wafanyabiashara kuagiza saruji kutoka nje kuliko kuzalisha wenyewe kwa sababu ya unafuu wa gharama ya saruji (simenti) kutoka ughaibuni. Kama Nigeria ingezuia uingizaji wa saruji kutoka nje, ingekuwa rahisi kufanya uzalishaji wa ndani na kupata faida.
Kwa bahati nzuri, Obasanjo akawa msikivu na serikali yake ikaweka masharti magumu ya kuagiza saruji kutoka nje. Wakati huohuo, ikaweka vivutio vyote kwa Dangote kuanzisha kiwanda cha saruji nchini Nigeria na huo ndiyo ukawa mwanzo wa utajiri wa bilionea huyo. Ndiyo sababu Dangote haoni haya kusema utajiri wake unatokana na Obasanjo.
Na mfano huo haupo Nigeria peke yake. Ukitazama Russia, utaona mchango mkubwa wa utawala wa Rais Vladimir Putin kwenye kutengeneza mabilionea kama Roman Abramovich na Mikhail Khodorkovsky (ingawa huyu walikorofishana baadaye). Uhusiano huo ni mkubwa kiasi kwamba jina walilopewa mabilionea ni oligarchy (matajiri -dola).
Ni maoni yangu kwamba ukitazama matajiri wa Tanzania kama vile Said Bakhresa, Reginald Mengi, Rostam Aziz na wengine, utaona uhusiano mkubwa kati ya utajiri wao na serikali zilizokuwa madarakani wakati walipopata biashara yao kubwa ya kwanza.
Kimsingi, ukisoma historia na kuzungumza na wafanyabiashara wakongwe wa hapa nchini, unajifunza kuwa kabla ya utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, wengi wafanyabiashara matajiri walikuwa wanajihusisha na biashara za magendo na nyingine zisizo rasmi. Kazi ya utawala wa Mwinyi, na baadaye Mkapa na Jakaya Kikwete, ilikuwa ni kurasmisha na kuwaingiza katika mfumo rasmi wa uchumi.
Tunawezaje kuwapata akina Bakhresa, Rostam na Mengi wengine?
Tatizo kubwa zaidi kwenye jamii yetu sasa ni ukosefu wa ajira. Mamilioni ya vijana wanamaliza shule na vyuo mbalimbali lakini wanapoingia mtaani wanakuta hakuna ajira rasmi zinazowasubiri kama ilivyokuwa miaka 30 iliyopita. Serikali peke yake haiwezi kupambana na tatizo hili.
Namna mojawapo ya kupambana na hali hii ni kutengeneza mabilionea wengi kadri iwezekanavyo ili waweze kutengeneza ajira. Lakini ni kwa namna gani tunaweza kufanya hivyo. Ziko namna tofauti ambazo serikali inaweza kufanya.
Njia ya kwanza ni ile aliyotumia Obasanjo. Serikali inatakiwa kuangalia ni wapi ambako inatumia mamilioni ya fedha za kigeni kuagiza vitu kutoka ughaibuni. Ikishatambua maeneo hayo, ifanye maamuzi ya kupunguza uagizaji kwa kiasi kidogo kidogo na kuwapa fursa wazalendo kufanya uzalishaji. Tukifikia kiwango cha kujitosheleza, tupige marufuku kabisa uagizaji wa vitu hivyo.
Bahati nzuri ambayo Tanzania inayo ni kwamba bidhaa yoyote ambayo kwa sasa inatumia mamilioni ya dola kuagiza kutoka nje, ni bidhaa pia ambayo hata nchi nyingi jirani zinaagiza. Kama tutazalisha kwa wingi zaidi, kuna soko la uhakika katika nchi zinazotuzunguka. Kinachotakiwa kufanyika ni uamuzi kama alioufanya Obasanjo kwenye simenti nchini kwake.
Kuna maeneo ya wazi nayaona ambako nchi yetu inaweza kufanya uamuzi wa namna hiyo. Kwa mfano, nchi yetu inatumia zaidi ya dola milioni 400 (takribani shilingi trilioni moja) kuagiza mafuta kila mwaka. Serikali pia inatumia takribani kiasi kama hicho kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi.
Hata hivyo, tunaweza kupunguza uagizaji mafuta kutoka nje kwa kulima kimkakati mazao kama alizeti na mawese. Kama serikali ikimtafuta tajiri mmoja au mchanganyiko wa matajiri na kuwashawishi waingie kwa nguvu katika kilimo cha mawese na michikichi, kuna bilionea mwingine ataibuka ambaye si tu atapunguza matumizi ya fedha za kigeni, lakini ataajiri vijana wengi zaidi na kupunguza tatizo la ajira.
Tanzania pia ina malighafi ya kutosha ya mbolea ikiwemo gesi. Kama serikali itafanya uamuzi wa kuagiza mbolea kidogo kidogo na kutoa motisha kwa wawekezaji wa ndani kufanya hivyo, tutatengeneza bilione au mabilionea wetu na kutengeneza ajira nyingi pia.
Kuna mfano mmoja wa kusisimua umetokea Tanzania mwaka huu. Baada ya tajiri Bakhresa kuingia katika sekta ya uzalishaji wa miwa, nimeambiwa mwaka huu pengo kati ya matumizi na mahitaji ya sukari hapa nchini wakati huu limefikia kiasi cha tani 15,000 tu. Hii ni katika nchi ambayo huko nyuma ilikuwa ikiagiza mpaka tani 50,000 hadi 100,000 za sukari. Kwa mwendo huu, muda si mrefu Tanzania haitakuwa na haja ya kuagiza sukari kutoka nje.
Inawezekana yapo maeneo mengi mengine ya kuyafanyia kazi. Kinachotakiwa ni kwa serikali kutazama ni wapi tunatumia fedha nyingi kuagiza vitu na kufanya uamuzi kuwa tutatengeneza vitu hivyo hapa nyumbani kama uwezo wa kufanya hivyo. Tunaweza pia kuamua kuzalisha vitu vingine ambavyo jirani zetu wana shida navyo kwa lengo la kuuza nje.
Kuna matajiri naona wanaibuka na wengine wako Kariakoo tu. Kuna wafanyabiashara ambao wanaonekana kama waagizaji wa bidhaa kutoka nje lakini wanaweza kushawishiwa kuingiza fedha zao katika uzalishaji wa biashara hapa nchini. Nawaangalia watu wa aina ya Ghalib Mohamed maarufu kama GSM na wengine wengi ambao wana ukwasi lakini bado hawajaingia kindakindaki kwenye sekta ya uzalishaji.
Kama tutaamua, hata watu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) wanaweza kufanya kazi ya kuwatambua na kuwabaini wafanyabiashara ambao kama wakipewa mazingira mazuri, wanaweza kubadili mwelekeo wa kiuchumi wa nchi yetu kwenye muda mfupi ujao.
Kama tuna maofisa usalama katika wilaya zote hapa nchini, ina maana tunaweza kwanza kutengeneza orodha ya matajiri wakubwa wote waliopo nchini kwa sasa na kupitia orodha hiyo, tukajua nani tukimpa nini tunaweza kupiga hatua kutoka hapa tulipo.
Uwezo wa kuwatengeneza akina Dangote, Rostam na Mengi tunao. Lakini tunahitaji kufanya maamuzi ya kimkakati.
Mwisho