Kraken ameachiwa

Na Ezekiel Kamwaga

KATIKA  filamu maarufu ya Clash of the Titans ya mwaka 2010, Liam Neeson – akiigiza kama mungu wa hekaya  za Kigiriki Zeus, alitamka maneno “Release the Kraken”. Kraken ni lidubwana lisilo na huruma ambalo Zeus aliagiza lifungiwe baharini, chini ya ulinzi wa Poseidon – mtawala wa baharini kwenye hekaya hizohizo, ili asidhuru wanadamu. Zeus – kwa kutimiza matakwa ya mdogo wake, Hades, aliamua Kraken afunguliwe kufanya uharibu kwa vile wanadamu walikuwa wamekosea miungu hiyo.

 

Ni stori ndefu lakini mwishowe Kraken hakufanikiwa kuumiza wanadamu kwa sababu alizuiwa na mwanadamu aliyekuwa na sifa ya kuwa nusu mungu na nusu mtu, akiitwa Parseus.

 

Nimekumbuka maneno ya Neeson kumhusu Kraken wakati nikiangalia hotuba ya jana ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, kwenye maadhimisho ya miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Sokoine.

 

Kuna mambo makubwa matatu ambayo yalinisumbua wakati akizungumza na baada ya kumalizika kwa tukio zima la kumbukuzi ya Sokoine.

 

La kwanza ni tuhuma alizotoa kuwa kuna baadhi ya mawaziri wanatumia mitandao ya kijamii kumhujumu Rais Samia Suluhu Hassan. Alitishia kwamba atawataja mawaziri hao kwa majina endapo wataendea na tabia yao.

 

Nilijiuliza maswali machache baada ya tuhuma hizo. Kama mawaziri hao anawajua, kwa nini asubiri waendelee kufanya hivyo mpaka Jumatatu ijayo ndiyo awataje? Kwa nini asiwataje kabla hawajafanya madhara zaidi kwa taasisi ya Rais ambayo ina heshima kubwa hapa nchini?

 

Swali la pili lilihusu nafasi ya Baraza la Mawaziri lenyewe. Kwamba kuanzia dakika ile Makonda ametoa tuhuma zile, mawaziri wote wa Rais Samia ni watuhumiwa. Kama hakuna jina lililotolewa, maana yake wote wanahusika.

 

Kama ikifika Jumatatu na Makonda asitaje majina, itakuwa baraza lote la mawaziri lina watuhumiwa wa kumkashifu au kumhujumu Rais mpaka wakati litakapovunjwa. Hii si afya kwa mawaziri, serikali nzima na ustawi wa dola.

 

Kama mawaziri wote ni watuhumiwa, watazungumza nini na Rais kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri? Watamshauri nini? Na kama mawaziri wote ni watuhumiwa, Rais atashauriwa na nani? Atashauriwa na mkuu huyo wa mkoa ambaye sasa anajipambanua kama “mtoto pekee wa Rais?”.

 

Nilisumbuliwa pia na tukio lenyewe. Jana tukio lilimhusu marehemu Sokoine. Mgeni rasmi alikuwa Rais. Kwa kawaida ya matukio ya kumbukumbu kama haya, ujumbe mkuu ulikuwa utoke kwa Rais na uwe unahusu mtu aliyekuwa anakumbukwa siku hiyo.

 

Baada ya hotuba ya Makonda, tukio lote likabadilika. Sijui kama watu wanakumbuka chochote kuhusu Sokoine kupitia tukio lile – ikiwemo hotuba ya Rais. Hata mimi siandiki kitu kuhusu Sokoine hapa na naandika kuhusu Makonda.

 

Kama mtu niliyefanya kazi kwenye sekta ya habari kwa zaidi ya miaka 20, sikumbuki hata mara moja tukio ambalo alikuwepo Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Rais mstaafu na bado Mkuu wa Mkoa ndiyo akawa stori.

 

Sidhani kama wahusika wanaona hili ni jambo la kawaida. Kesho, mkuu wa wilaya mwenye tatizo na waziri au mkuu wake wa mkoa anaweza kutumia mkutano wa Rais kufikisha ujumbe wake. Na waziri. Na mjumbe wa mkutano mkuu. Na IGP. Na CDF. Naona inajengwa barabara ambayo mwisho wake hautakuwa mzuri.

 

La tatu ambalo sikulifurahia ni hatua ya Makonda kuzungumza hadharani kwamba watu wote wanajua Rais ni mama yake. Sioni shida ya mtu kumwita Rais Samia kwa jina la Mama. Wengi wetu tunamwita hivyo.

 

Lakini, kwa mtazamo wangu, ni makosa kuhusisha u-Mama na Urais. Nakumbuka sana maneno ya Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo, aliyezungumzia utata uliokuwepo wa kumwita Rais Mwanamke Amiri Jeshi au Amirat na mwisho ikaangukia kwenye Amiri Jeshi. Ukuu wa Nchi hauna jinsia. Rais ni Rais tu.

 

Sasa anapotokea mwanasiasa mmoja na kusema Rais ni mama yake na ikazoeleka hivyo, ni hatari kwa Urais. Kwanza kwa sababu tu ya historia ya nyuma, Makonda si aina ya mtu ambaye Rais au Urais inatakiwa kujihusisha moja kwa moja naye.

 

Urais hauna ubia. Na Rais mwenyewe ameshasema kwamba yeye watoto wake wote ni wake. Huyu mmoja anayetaka kuaminisha umma kuwa Rais ni mama yake yeye ni wazi anacheza mchezo anaoujua vizuri ingawa inawezekana wengine hatujausoma.

 

Kraken kaachiwa: Part II

 

Baada ya matokeo ya Urais wa Marekani mwaka 2020 kutoka, Rais Donald Trump alipinga ushindi wa Joe Biden akidai matokeo yamechakachuliwa.

 

Mmoja wa wanasheria waliokuwa wakiunga mkono madai hayo ya uongo, Sidney Powell, alidai kuwa yuko mbioni ku “release the Kraken”, kwa kuja na ushahidi wa kura zaidi ya laki moja kuonyesha uchakachuaji huo. Hakuweza kufanya hivyo hadi leo.

 

Kuanzia mwaka 2020 na kauli hiyo ya Powell, neno Release the Kraken limeanza kutumika kama hatua ya kutengeneza madai au tuhuma zisizo za kuaminika (consipiracy theories) dhidi ya wapinzani wako.

 

Miongoni mwa mbinu kubwa inayotumiwa na wanasiasa walaghai – populist, wa kizazi cha sasa duniani kote ni uwezo mkubwa wa kutengeneza conspiracy theories dhidi ya wabaya wa nchi, viongozi au serikali.

 

Wabaya wa Hitler walikuwa Wayahudi. Wabaya wa Narendra Modi ni Waislamu na wabaya wa Trump ni watu wa tabaka la viongozi na wageni kutoka nje. Kila aina ya uzushi unatengenezwa kupitia madui hao wa kuchongwa.

 

Kraken kaachiwa, nini kifanyike?

 

Sijui ni vigezo vipi vilitumika kumrejesha Makonda kwenye uongozi na nani alichukua nafasi ya Hades kumshawishi Zeus amfungulie Kraken.  Hilo ni suala lililo juu ya uwezo wangu. Lakini angalau najua lipi la kutarajiwa wakati Kraken anapoachiwa kufanya uharibifu.

 

Lakini nafahamu kwamba tunaishi katika zama hatari kisiasa duniani. Msomi Fareed Zakaria anaeleza hili vizuri sana kwenye kitabu chake kipya cha Age of Revolutions. Wanasiasa wa aina ya Makonda si wa kuwadharau.

 

Namna pekee ya kuepuka kurejea tulikotoka kati ya 2016 – 2021 ni kwa wanasiasa na viongozi wasio na siasa za kilaghai kuwa kitu kimoja na kusema “Never Again”. Ni kwa kuungana wakijua kwamba upande wa pili umeungana na uko tayari kwa mapambano.

 

Ninafahamu kuwa kuna mgawanyiko miongoni mwa viongozi ambao waliumizwa pamoja katika kipindi nilichokitaja hapo juu. Baada ya Rais Samia kuingia madarakani, ilibidi kundi hili liwe moja kulinda maslahi yake na kutengeneza ngoma dhidi ya viongozi na wanasiasa laghai.

 

Lakini kwa sababu ambazo sijazielewa hadi sasa, kundi hili limegawanyika na haliko pamoja. Hatari kubwa iliyopo mbele yao ni kwamba wasipokuwa wamoja, Kraken atawala – mmoja baada ya mwingine. Usalama wao ni kuwa wamoja kwakujitambua na kufahamu hali yao na wanachosimamia.

 

Nina habari mbaya. Kraken hana huruma. Ameachiwa na macho yake yote yako kwao. Anawajua wote – mmoja mmoja. Kwa sababu hakuna Perseus miongoni mwenu, umoja wenu ndiyo utakuwa kinga yenu.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.