Nyakati za Samia na Hakainde

Na Ezekiel Kamwaga

 

Katika moja ya hotuba zake maarufu za zamani, Baba wa Taifa la Zambia, Dk. Kenneth Kaunda, alipata kuelezea uhusiano baina ya taifa lake na Tanzania kuwa sawa na ule wa pacha walioungana. Hakuna kilichokuwa kinaeleza uhusiano huo kama uhusiano baina yake na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

 

Wawili hawa walipendana kiasi kwamba Kaunda aliamua kumpa mmoja wa watoto zake jina la Kambarage – ambalo ni moja ya majina ya Mwalimu Nyerere.

 

Na hata wakati alipokuwa akipita katika wakati mgumu kwenye utawala wa mbadala wake, Frederick Chiluba, kiasi cha kususa kula, ni Mwalimu ndiye aliyekwenda Zambia kumbembeleza aache mgomo huo wa kula.

 

Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akianza ziara yake ya kitaifa ya siku tatu nchini Zambia leo, ni muhimu kutumia muktadha huu kumtazama yeye na Rais wa sasa wa Zambia, Hakainde Hichilema.

 

Wanafanana nini? Nyerere na Kaunda waliunganishwa na itikadi ya Ujamaa wa Kiafrika (Ubuntu). Samia na Hakainde ni waamini wa mfumo wa soko huria. Nyerere na Kaunda walikuwa wamepishana miaka miwili – Julius akiwa mkubwa kwa Keneth, na Samia na Hakainde pia wamepishana miaka miwili; wa Tanzania akiwa mkubwa kwa wa Zambia.

 

Wote wameingia madarakani wakati dunia ikiwa inapambana na janga la Uviko 19 huku wanasiasa wa siasa za kidikteta wakipanda chati na mfumo wa dunia ukibadilika kutoka ule unaoongozwa na nchi za Magharibi na kuwa wa pande tatu – China na India kwa upande mmoja na Russia kwa upande mwingine.

 

Wanafanana pia kwa mazingira yao ya kuongoza vyama vyao vya siasa. Hakainde alianza kuongoza chama chake cha UPND mwaka 2006 kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wake, Anderson Mazoka huku Samia akipata Uenyekiti kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli.

 

Wanatofautiana nini wawili hawa?  Mambo makubwa mawili – kwanza ni ukweli kuwa Hakainde ni mfanyabiashara aliyeingia kwenye siasa wakati Samia ni mwanasiasa ambaye hajawahi kuwa mfanyabiashara. La pili, na hili ni kubwa, ni kuwa Hakainde amewahi kuwa mwanasiasa wa upinzani wakati Samia ameishi katika nchi ambayo kwa muda wote imetawaliwa na chama kimoja cha siasa.

 

Samia na Hichilema kwenye macho ya dunia

 

Wakati likifanya uchambuzi wa mwaka mmoja madarakani wa Rais Hichilema, taasisi ya Chatham House ya Uingereza; ilimwita Rais huyo kwa jina la Meneja Masoko wa Zambia. Lakabu hiyo ilikuwa ikiakisi juhudi za kiongozi huyo kwenye kuhakikisha taifa lake linavutia wawekezaji na mitaji kutoka nje.

 

Hiyo pia ni lakabu aliyopewa Rais Samia wakati alipoamua yeye binafsi kutumia filamu ya Royal Tour kutangaza utalii wa Tanzania uliokuwa umeumizwa sana na changamoto ya Uviko 19.

 

Wawili hawa pia wanafahamika kwa kuelekeza sera za mambo ya nje ya mataifa yao kwenye kutofungamana na upande wowote na diplomasia ya uchumi. Wote wanavutia mitaji kutoka China, Marekani na kote kwingine kwenye fursa.

 

Wote wawili waliingia madarakania wakiwarithi viongozi ambao maridhiano ya kisiasa hayakuwa ajenda kuu kisiasa. Hakainde aliwahi kufunguliwa kesi ya uhaini na mara kadhaa kuwekwa ndani na mtangulizi wake, Edgar Lungu.

 

Samia kwa upande wake, alirithi nchi iliyogawanyika kutokana na utawala wa Magufuli na aliamua suala la maridhiano liwe ajenda kuu ya Urais wake mara tu alipoingia madarakani.

 

Wote wawili wanachukuliwa kuwa ni miongoni mwa viongozi wanaofanya mabadiliko makubwa ya kimifumo kuzifanya nchi zao za kidemokrasia zaidi katika bara ambalo udikteta na mapinduzi ya kijeshi vinaanza kupanda chati.

 

Fursa 

 

Pengine kuliko marais wengine wa Afrika, Samia na Hakainde wana fursa ya kusimika zaidi uhusiano wa nchi zao kwa sababu misingi tayari ipo. Reli ya Tazara na Bomba la Mafuta la Tazama ni ushahidi wa msingi ambao tayari umewekwa.

 

Miundombinu na nishati ni masuala mawili ambayo yanaunganisha nchi na watu kwa namna ya kipekee. Reli ya Tazara si tu inasafirisha mizigo, lakini ni jukwaa la kipekee kwa raia wa nchi hizi mbili kuchangamana, kutembelea na kukutana.

 

Bomba la mafuta linamaanisha nchi hizi zimeunganishwa kiunoni- nikiazima maneno ya hayati Kaunda wakati akifananisha Tanzania na Zambia na mapacha walioungana, na jambo ambalo wote wana maslahi ya pamoja ya kudumu.

 

Kinachotakiwa sasa ni kuambizana kuhusu ni kwa vipi Zambia itaendelea kutumia bandari ya Dar kwa miaka mingi zaidi, wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizi mbili wataunganishwa kifursa ili waweze kuwekeza miongoni mwao na kuruhusu watu na mitaji wahame kutoka nchi moja kwenda nyingine.

 

Biashara baina ya Zambia na Tanzania bado haijafika katika kiwango cha kuridhisha. Kiwango cha chini ya shilingi bilioni 300 ni kidogo kulinganishwa na umuhimu na ukaribu uliopo baina ya nchi hizi mbili.

 

Lakini walau dirisha la kufungua mahusiano mapana zaidi na yenye maana zaidi limeanza kufunguliwa. Baada ya ziara hii, nina maana kutakuwa na mengi ya kuzungumza.