Niger: Yaliyomo ndani na nje

Picha: Viongozi wa wanajeshi waliopindua serikali ya Niger wakitoa taarifa rasmi kwa wananchi kuhusu jambo hilo. Picha kwa hisani ya tovuti ya Al Jazeera

 

Na Ahmed Rajab

 

TANGU Jumatano iliyopita wakati Rais Mohamed Bazoum alipopinduliwa nchini Niger hadi leo Gazeti la Dunia linapoingia mtandaoni, hakuna mwenye hakika iwapo Niger imeponyoka kutoka mikononi mwa Ufaransa.  Au ikiwa imebaki ikining’inia tu kwenye makucha ya huyo mkoloni wake wa zamani.

 

Hata hivyo, ni wazi kwamba Ufaransa pamoja na Marekani zimepata pigo kubwa kwa kuangushwa kwa Bazoum.  Kinachodhihirika ni kwamba sera za Ufaransa zinazohusiana na ukanda mzima wa nchi za Sahel zinaporomoka.  Sera hizo zimekuwa mithili ya nyumba iliyojengwa kwa karata na haraka haraka karata hizo zinaanguka, moja baada ya moja, na nyumba nzima inabomoka.

 

Hiyo ndiyo taswira moja inayochomoza katika mapinduzi hayo na tutarejelea kuiangalia baada ya kuyaangalia ya ndani Niger kwenyewe.

 

Tukiyaangalia hayo ya ndani, inatujia taswira nyingine. Nayo ni ya mikono ya Rais wa zamani wa Niger, Mahamadou Issoufou. Ukiingia kwenye jiko la siasa za Niger, licha ya moshi mkali na mvuke mnene uliozagaa humo, ukifikicha macho utaiona mikono ya Rais wa zamani Mahamadou Issoufou ikilikoroga jungu lililoyapika hayo mapinduzi ya kijeshi.

 

Hizo ni taswira mbili unazoweza kuziona kwa haraka haraka: taswira ya Ufaransa inayovunjika miguu na ya Issoufou asiyejulikana yuko upande gani.

 

Lakini nyuma ya taswira hizo kuna maswali mengi yanayozidi kuibuka katika machafuko yaliyoko Niamey, mji mkuu wa Niger.

 

Bazoum na Issoufou ni wa chama kimoja, Chama cha Niger cha Demokrasia na Usoshalisti, Tarayya, kwa ufupi PNDS. Kiongozi wa chama ni Issoufou. Bazoum aliurithi urais wa nchi kutoka Issoufou mwaka 2022.  Issoufou hakuweza kuendelea kuwa rais kwa sababu baada ya kuwa rais kwa mihula miwili katiba ya nchi haikumruhusu. Ndipo chama chao kilipomsimamisha Bazoum kwenye uchaguzi wa mwaka jana na akashinda.

 

Jambo lililokuwa dhahiri kwa wenye kufuatilizia siasa za Niger ni kwamba Bazoum tangu aushike urais hakuwa na udhibiti wa chama chao. Turufu zote alikuwa nazo Issoufou. Ilishangaza kuona kwamba Issoufou hakusikika kwa siku nne baada ya Bazoum kung’olewa madarakani.  Siku nne ni muda mrefu sana kwa mtu wa hadhi kama ya Issoufou kuubana mdomo wakati wa tukio kama la mapinduzi ya kijeshi.

 

Na Issoufou alipoibuka aliibuka kwenye mitandao ya kijamii.  Wala kauli zake hazikuonesha kuwa ni za mtu aliyefadhaishwa na yaliyojiri.  Alisema tu kwamba alijitahidi kwa njia mbali mbali kutafuta suluhisho la mgogoro huo na hasa kuachiwa kwa Bazoum na kurejeshewa madaraka yake.  “Nitaendelea na njia hii madhali kuna tumaini la kupatikana suluhisho,” alisema.  Huko si kuyalaani mapinduzi.  Wala si kuwalaani waliopindua.

 

Tuseme ya kweli. Ilikuwa muhali kwa Issoufou kumlaani kiongozi wa mapinduzi hayo, Jenerali Abdourahamane Tchiani.  Ni yeye aliyemteua awe kamanda wa kikosi cha ulinzi wa Rais chenye wanajeshi 700 na silaha nzito nzito zilizo nyingi mno laisa kiasi.  Alipokuwa Rais katika muda wake wote wa mihula miwili (2011-2021), Issoufou akitambua kwamba hakuwa akipendwa na majeshi.  Kwa hivyo, aliona umuhimu wa kuwa na kikosi kitachokuwa kitiifu kwake, kitachomlinda na kumhifadhi asipinduliwe.

 

Alipouacha Urais, Issoufou alimtaka Bazoum asimuondoshe Tchiani.  Walio karibu na Bazoum wanamlaumu kuwa hakujitahidi kujitoa kwenye makucha ya Issoufou na wala hakujaribu kuivunja mitandao ya ufisadi iliyotia mizizi Niger.

 

Tunasikia kwamba takriban jamaa zake wote Issoufou walio Niamey wanalindwa.  Lakini la kushangaza zaidi ni kwamba mwanawe Mahamane Sani Mahamadou Issoufou, aliyekuwa waziri wa petroli na nishati, na anayejulikana sana kwa jina la ‘Aba’, alionekana akenda hospitali akilindwa na wanajeshi wa kikosi cha ulinzi wa urais.

 

Jambo jengine la kushangaza ni kwamba watawala wepya wamechukua hatua madhubuti za kumhifadhi Malika, aliyekuwa mke wa Issoufou, pamoja na jamaa zake.  Nilipoyasikia hayo nilimkumbuka Aissa Diori, aliyekuwa pia akijulikana kwa jina la Aïchatou Diori na aliyekuwa mke wa Rais wa kwanza wa Niger, Diori Hamani, aliyepinduliwa mwaka 1974 katika mapinduzi ya mwanzo nchini humo.  Mapinduzi hayo hayakumwaga damu yoyote isipokuwa ya Aissa aliyekuwa pekee aliyeuawa.

 

Inasemekana kwamba Aissa alikuwa na mtandao mpana wa kifisadi na kwamba alikuwa na utajiri uliopindukia mipaka, akimiliki majumba ya fahari chungu nzima mjini Niamey na kwingineko.

 

Swali linaloulizwa kumhusu Malika na jamaa zake ni kwa nini wapinduzi wanawalinda? Chama cha PNDS cha kina Issoufou na Bazoum kinachukiwa sana Niger, hasa mjini Niamey.  Waandamanaji waliomiminika barabarani mwishoni mwa wiki iliyopita hawakuilenga mali ya Bazoum lakini waliichoma moto mali ya chama cha PNDS.

 

Mapinduzi haya ya Niger yana mengi ya kushangaza.  Jengine ni kwamba nasikia mwishoni mwa wiki iliyopita, Issoufou alikutana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Niamey. Walizungumza kwa muda mrefu na ninavyosikia ni kwamba Issoufou alijaribu kumkinga Tchiani akimueleza kuwa ni mtu aliyevunjwa sana moyo na Bazoum.

 

Pengine unajiuliza ilikwenda kwendaje hata Issoufou akamgeuka mrithi wake, Bazoum? Alisaidia apinduliwe ili arudi tena madarakani? Labda kuna kitu amekisahau Ikulu au analiwa na uchu wa kutaka mwanawe, Aba, auonje urais?  Minong’ono kwenye mikahawa ya Niamey inasema hivyo.

 

Au pengine labda Issoufou akihisi Bazoum akijifanyia atakavyo bila ya kumshauri yeye au kumsikiliza, kinyume na alivyo Tchiani. Ni ari iliyomfanya amuendee kinyume Bazoum?

 

Halafu tusiwasahau wale wenye kuwachunguza viongozi nje ndani.  Miongoni mwao kuna wasemao kwamba Issoufou kwa hulka yake, kwa alivyo kama alivyo, si mtu wa kuaminika.  Wanakumbusha kwamba mwaka 1993 alipokuwa waziri mkuu wa Rais Mahamane Ousmane, Issoufou huyu huyu alimwendea kinyume na akakifanya chama chake kiwe na uchache wa wabunge katika Bunge la nchi hiyo.

 

Si siri kwamba hadhi anayoitamani hasa Issoufou ni kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa baada ya kumalizika muda wa katibu mkuu wa sasa António Guterres mwaka 2026.  Wafaransa ndio wanaompigia chapuo, kwa siri kubwa. Naye anaicheza ngoma.

 

Yanayozuka Niger ni mambo ya ndani ya taifa hilo lililo kwenye mpaka baina ya jangwa la Sahara na nchi zilizo kusini ya jangwa hilo.  Hata hivyo, lazima yanayozuka huko yaangaliwe kwa darubini la siasa za kimataifa, siasa za kimkakati zinazohusisha jiografia, maliasili na hata vita.

 

Hizi ni siasa zinazochezwa na madola makubwa. Madola hayo ni mipapa katika bahari kuu ya vitimbi na magube ya kimataifa. Niger, kama zilivyo nchi nyingine za kwenye ukanda wa Sahel, ni kijidagaa.  Lakini ni kijidagaa ambacho tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1960 kimekuwa kikitumiwa, hususan na Ufaransa, kama chambo cha kuupapia ukwasi mkubwa sana wa eneo hilo.

 

Niger ni nchi yenye hazina kubwa ya madini ya urani. Tena madini yake yanasifika kuwa ya hali ya juu. Inakisiwa kwamba Niger ni nchi ya sita yenye kuchimba kwa wingi madini hayo ya urani duniani.

 

Kampuni ya nishati ya Areva inayomilikiwa na serikali ya Ufaransa imekuwa ikichimba urani Niger tangu miaka ya 1970.  Zaidi ya thuluthi moja ya urani inayotengenezwa na Areva inachimbwa Niger.  Asilimia kama 75% ya umeme wa Ufaransa unafuliwa kutokana na nishati ya nuklia, na takriban urani yote inayoendesha vinu vya kinuklia vya Ufaransa inachimbwa Arlit, mji wa kaskazini mwa Niger.

 

Katika miaka ya karibu kumezuka suitafahamu baina ya kampuni ya Areva na Niger kuhusu malipo ya urani inayochimbwa.  Niger inataka malipo zaidi kwa urani yake.

 

Kiwango kikubwa cha mahitaji ya nishati ya Ufaransa kinategemea urani kutoka Niger. Inasemekana kwamba Ufaransa ina akiba ya miaka miwili tu ya urani.  Hiyo ni sababu moja kubwa inayoifanya Niger iwe na umuhimu mkubwa kwa Ufaransa. Lakini Ufaransa si taifa pekee la kigeni lenye kuchimba urani Niger. Yako mengine pia yakiwa pamoja na Uhispania.

 

Pamoja na kuwako Niger kwa shughuli za uchimbaji wa urani, Ufaransa pia ina wanajeshi wake nchini humo wasiopungua 1,500.  Hilo ni jambo linalowakera na kuwaghadhibisha wananchi wengi wa Niger. Septemba mwaka jana maelfu ya wananchi hao walimiminika kwenye barabara za Niamey wakipinga kuwako wanajeshi wa Ufaransa nchini mwao.

 

Ufaransa ina wanajeshi na kambi za kijeshi Niger. Ujerumani, Italia na Canada zina wanajeshi wao wenye kuyafunza majeshi maalum ya Niger yenye kupambana na magaidi.

 

Marekani nayo ina wanajeshi wasiopungua elfu moja na kambi za kijeshi pamoja na ile kambi yao kubwa ya droni iliyogharimu dola za Marekani milioni mia moja kuijenga ($100m) kila mwaka kambi hiyo inahitaji si chini ya $30 milioni kuiendesha.  Mwaka huu Marekani ilikuwa imepanga iipe Niger $233 milioni, Muungano wa Ulaya (EU), kwa upande wake, imeweka kando bajeti ya $2.5 bilioni kuipa Niger.

 

Hizo si fedha kidogo. Kwa miaka fedha hizo za ‘misaada’ zimekuwa zikiingia katika mifuko ya serikali ya Niger.  Sehemu kubwa ya fedha hizo huwa zinalengwa kusaidia sekta muhimu za afya, elimu na maendeleo ya jamii lakini kwa bahati mbaya hupotea njiani na haziwafikii wananchi wanaokusudiwa kusaidiwa.  Matokeo yake ni kwamba ufukara bado ungali unawasumbua wakaazi wengi wa nchin hiyo.  Kwa hakika, ukifika Niamey kwa ndege basi utokapo tu uwanja wa ndege wa kimataifa wa Diori Hamani utauona ufukara uliokithiri ukikutumbulia macho.

 

Wananchi taabani, wamechoka. Na wanamlaumu mkoloni wao wa zamani, Ufaransa, kwa masaibu yote yanayowafika — ya kijamii, ya kiuchumi, ya demokrasia isiyo imara na ya usalama.

 

Wananchi wanasema kwamba Ufaransa imeshindwa kusaidia katika nyanja zote hizo za maisha. Imeshindwa pia kupata mafanikio ya kudumu katika vita dhidi ya magaidi wa Dola la Kiislamu katika Sahara Kubwa (ISGS) na wa Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM), wenye kufungamana na magaidi wa Al-Qa’eda.

 

Wananchi wa Niger wanakubaliana na viongozi wao wapya pamoja na wananchi wenzao wa ukanda mzima wa nchi za Sahel wenye kutaka majeshi ya Ufaransa yarudi kwao.

 

Inavyoonesha ni kwamba sasa hata baadhi ya wasomi wa Ufaransa nao pia wanaona afadhali warudi.  Mmojawao ni Gérard Araud. Huyu ni mtu wa kusikilizwa. Aliwahi kuwa Balozi wa Ufaransa nchini Marekani, Mkurugenzi Mkuu wa Mambo ya Siasa na Usalama katika wizara ya mambo ya nje, jijini Paris, na Mwakilishi wa Kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa.

 

Tarehe Mosi Agosti aliandika makala kwenye gazeti la Ufaransa liitwalo Le Point akikumbusha kwamba miezi 18 iliyopita alishauri kwenye gazeti hilo hilo kwamba Ufaransa iondoshe wanajeshi wake na izifunge kambi zake za kijeshi zilizo Afrika. Kadhalika, alipendekeza pafanywe uchunguzi wa kina wa sera ya Ufaransa katika ukanda mzima wa Sahel.  Wakati huo Ufaransa ilikuwa ishatimuliwa kutoka Mali na Burkina Faso. Na sasa inaonesha ni zamu ya Niger kuifukuza.

 

Balozi Araud ameitahadharisha serikali ya Ufaransa isilirejelee kosa hilo Senegal na Côte d’Ivoire. Kuna vuguvugu nchini Niger liitwalo Vuguvugu la M62 la asasi za kiraia ambalo ndilo lililoyaratibu maandamano hayo ya kuwapinga Wafaransa.

 

Hisia dhidi ya kuwako majeshi ya kigeni katika ardhi ya Afrika zimepamba moto katika sehemu nyingine pia za Afrika si katika ukanda wa Sahel peke yake.

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com: X:@ahmedrajab

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.