Septemba 23 isiwe maafa, uwe mwanzo mpya

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

KESHO, Septemba 23, 2024, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepanga kufanya maandamano hapa nchini kupinga vitendo vya utekaji na mauaji vinavyoonekana kukithiri hapa nchini hivi sasa.

 

Mpaka wakati naandika makala haya, ninafahamu kwamba CHADEMA wameamua kesho watafanya maandamano hayo. Na mpaka wakati huu, Polisi hawajatoa taarifa yoyote kuruhusu kufanyika kwa maandamano hayo. Taarifa iliyopo ni kwamba maandamano hayo hayataruhusiwa.

 

Mimi ni mwanafunzi wa siasa za hapa nyumbani na za bara letu la Afrika. Kwa hapa tulipofika sasa, sioni uwezekano wa jambo hili kumalizika kwa amani endapo busara haitatamalaki kutoka upande mmoja au zote.

 

Siasa si mchezo wa amani. Mapambano ya kisiasa mara kadhaa yamezua mauaji, uhasama na maafa mengine kwa sababu asili ya mchezo wenyewe ni tofauti zilizo baina yetu.

 

Kwenye mazingira ambayo naandika makala haya, jambo la muhimu kuliko yote ni kwa mtu, mamlaka au taasisi moja ya kitaifa iwe juu ya tofauti hizi za kisiasa, kimantiki na kiwajibikaji ambazo ni wazi zinatupeleka kusiko.

 

Mtu au taasisi hiyo iseme kwamba hatuwezi kwenda mahali pabaya kuliko hapa tulipo sasa. Tunatakiwa kurudi tulikotoka – kwenye nchi ambayo watu wake ni wamoja, waungwana, wenye upendo na wanaoshirikiana.

 

Kama CHADEMA wakiandamana kesho kama walivyoamua na kama Polisi na vyombo vingine vya dola vikiamua kubakia na msimamo wake wa kuzuia, kwa vyovyote vile siku ya kesho inaweza kujikuta ikikumbukwa sawa na siku ile ya Januari 27, 2001 ambako watu walipoteza maisha visiwani Zanzibar kwa sababu za kisiasa.

 

Kama pande zote mbili zitaamua kukingiana ngumi, itakayopoteza ni Tanzania na si upande wowote. Tayari nimeona katika Bunge la Kenya mbunge mmoja akitumia taifa letu kama mfano mbaya wa matukio ya kuteka na kuua watu.

 

Kama kesho pande zote zitabaki na misimamo yao, Tanzania itaingia katika historia nyingine ambayo haitafutika kirahisi katika miaka inayokuja.

 

Nini kinahitaji kufanyika?

 

Kabla ya kusema nini kinahitaji kufanyika kutoka hapa tulipo, nataka kusema mambo mawili kwa faida ya pande zote mbili zinazokinzana hivi sasa.

 

Kwa serikali, hakuna yeyote atakayefaidika kwa kubaki na kumbukumbu ya kumwaga damu ya Watanzania wenzake katika wakati usio wa vita. Nchi haiko vitani na hakuna sababu ya yeyote kupoteza uhai au kupata ulemavu kwa sababu ya mambo ambayo utatuzi wake uko ndani ya uwezo wetu.

 

Kubwa zaidi, Tanzania ni nchi ya kidemokrasia. Kama nchi yetu ni ya kidemokrasia, hakuna sababu ya kuelekeza mitutu kwa watu wanaondamana. Hiyo ndiyo gharama ya kuwa taifa la kidemokrasia.

 

Kwa wafuasi wa upinzani, kwa kadri hali ilivyo sasa, kama hali itakuwa hii mbaya ninayoiona sasa kabla ya kesho (Septemba 23), itabidi mwelekeo wa nchi yetu ubadilike. Hatutakuwa tena taifa la maridhiano na maelewano bali tutarejea kwenye zama za giza.

 

Kihistoria, vyama vya upinzani nchini Tanzania vimefanya vizuri zaidi – walau Tanzania Bara, katika uchaguzi wa 1995 na 2015. Ukiniuliza sababu ya kufanya vizuri miaka hiyo, nitasema ndiyo nyakati ambazo walau uchaguzi ulifuata misingi ya kidemokrasia.

 

Hata Zanzibar, Wazanzibari wengi wanaamini nyakati bora kwao kisiasa ilikuwa wakati wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kati ya mwaka 2010 hadi 2015. Uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2015 unaaminika ndiyo ulikipa matokeo mazuri zaidi katika historia ya vyama vingi – ingawa ZEC na wasiojulikana walifuta uchaguzi ule.

 

Mwaka 2005 na 2020 ambako vyama vya upinzani havikufanya vizuri, aina ya utawala haikuwa ya kidemokrasia kulinganisha na 2015 na 1995.

 

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, aliyekuwa Mkuu wa Polisi, Omar Mahita, alifanya mkutano na waandishi wa habari ambako alionyesha silaha kama vile mapanga alivyodai vimeingizwa nchini na kilichokuwa chama kikuu cha upinzani wakati ule – Chama cha Wananchi (CUF), kwa ajili ya kuharibu amani ya nchi. Hiyo ndiyo ilikuwa demokrasia yetu wakati ule! Mahita akasema kama CUF ni Ngangari, basi Polisi ni Ngunguri.

 

Nini ninachotaka kusema hapa? Ni kwamba vyama vya upinzani hapa nchini vinakuwa imara na kukaribia kushinda uchaguzi wakati utawala wa kidemokrasia unapokuwa na afueni. Kwa hiyo, kama nchi ikisererekea kuelekea kule tulikokuwa miaka mitano nyuma, faida haitakuwa kwao.

 

Kama viongozi wa upinzani hawatadhibiti mwenendo wa siasa za nchi yetu, kuna uwezekano wa makundi mengine kuchukua fursa hiyo. Tumeona Sudan na tumeona Bangladesh hivi karibuni.

 

Kwa muktadha wetu, naiona Sudan zaidi kuliko Bangladesh. Mimi ni mmoja wa wanaotamani kwamba safari yetu ya mabadiliko ibebwe na vyama vya siasa badala ya kuacha makundi mengine ambayo hayajajipanga kutwaa madaraka kushika hatamu.

 

Jambo linalopaswa kufanyika sasa ni kwa taasisi moja ya juu kuchukua udhibiti wa mambo. Pasipo kufanya hivyo, huku chini kila mmoja atachukua hatua anayodhani inafaa.

 

Lingine la muhimu ni kwa kufunguliwa kwa mlango wa mawasiliano baina ya viongozi wa upinzani na mamlaka zinazoongoza nchi.

 

Wanaweza kuwa watu wawili au watatu ambao watakuwa wanapeleka na kufikisha ujumbe kwa mamlaka zote kuhusu nini kinaweza kufanyika kutuondoa hapa. Na watu hao si lazima wawe wanasiasa bali hata watu wanaoheshimika katika jamii yetu wakiwemo viongozi wa dini.

 

Mlango huo wa mawasiliano utaanza kwanza kwa kurejesha kuaminiana baina ya viongozi wa pande zote mbili na kufikia mwafaka wa kuondoa dosari zilizotufanya tufike hapa tulipo sasa.

 

Na haya si mambo magumu. Ni suala la kupiga simu mbili tatu na gari itakuwa imekaa barabarani.

 

Hii ni Tanzania yetu sote.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa  mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza. Anapatikana kupitia email: ekamwaga57@gmail.com