TAABINI: Salum Badar (1938 -2024), kielezo cha historia ya Zanzibar

Picha. Salum Badar

 

Na Ahmed Rajab

 

SALUM Badar aliyefariki dunia mjini Malmo, Kusini mwa Sweden, Agosti 13, 2024, akiwa na umri wa miaka 86 alikuwa miongoni mwa Wazanzibari washupavu waliochangia katika harakati za ukombozi bila ya kujigamba au kutambulika au hata kujulikana.

 

 

Katika siasa za Zanzibar, Salum Badar alikuwa wa mrengo wa kushoto. Akimuunga mkono Abdulrahman Babu aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha Umma Party, kilichokuwa kikifuata falsafa ya Umarx.  Utiifu wake kwa Babu haukuyumba hata siku moja na alikuwa mfano wa mtu wa tabaka la juu la kimaisha aliyetetea, kwa hali na mali, maslahi ya walio chini.

 

Siasa zikimwenda ndani ya damu yake kwani alizaliwa katika ukoo wa kisiasa.  Ukiuangalia wasifu wake utadhani kama vile aliibeba historia ya siasa za Zanzibar mabegani mwake.

 

Mamake, Bibi Kadhiya binti Muhsin, alikuwa ndugu kwa baba na Sheikh Ali Muhsin Barwani, aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP au Hizbu) na waziri wa mambo ya nje wa serikali iliyopinduliwa Januari 12, 1964.

 

Salum pia alikuwa mtoto wa mjomba na shangazi na Mohamed Humud, aliyemuua kwa kumpiga kisu Inspekta Sultan Ahmed Mugheiry mnamo Desemba, 1955.  Mauaji ya Mugheiry yalikuwa ya kisiasa na yalikuwa ya kwanza katika historia ya karibuni ya Zanzibar.  Ingawa nilikuwa mdogo, naikumbuka vizuri kadhia hiyo.  Mugheiry alituhumiwa na wazalendo kuwa akisambaratisha harakati za kudai uhuru.

 

Miaka 11 baada ya tukio hilo, mtoto wa Mohamed Humud, aliyeitwa Humud, na niliyesoma naye darasa moja katika skuli ya Darajani, alimpiga risasi na kumuua Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Aprili 7, 1972.  Humud aliyekuwa luteni katika jeshi la Tanzania alikuwa katika kaumu yetu, makomredi, waliokuwa wanachama wa zamani au wafuasi wa Umma Party.

 

Katika kaumu hiyo alikuwemo pia Salum Badar, mjomba wake Humud.  Komredi mwengine alikuwa shemeji yake, Hamed Hilal, aliyekuwa mwanajeshi wa cheo cha kapteni.  Salum alikuwa binamu yake Hamed na pia mkwewe kwa vile alikuwa mjombake mkewe.  Hivyo ndivyo ukoo wa Salum Badar ulivyoshikamana kwa karibu sana kwa damu.  Lakini ndani yake mlikuwamo mpasuko wa kisiasa.

 

Mabarwani wana historia kubwa Zanzibar na mtu anaweza kuandika kitabu kizima kuwahusu na siasa za kwetu. Wakati wa zama za siasa, Mabarwani wengi, na takriban ukoo mzima wa akina Salum Badar, walikuwa Mahizbu, yaani wafuasi wa chama cha ZNP.  Baba yake mzazi alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya ZNP.  Mmoja wa kaka zake, Said, na ami yao Sheikh Hilal, walikimbilia Uingereza pamoja na Seyyid Jamshid, sultani aliyepinduliwa. Wakiwa uhamishoni walishirikiana na Sheikh Ahmed Seif Kharusi, kiongozi wa Zanzibar Organisation, jumuiya iliyokuwa na nia ya kuipindua serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.

 

Kinyume na Mabarwani wengine, Salum, Hamed na Humud walikuwa wafuasi wa Umma Party na waliyaunga mkono mapinduzi.

 

Salum alizaliwa tarehe Februari 3, 1938. Jina lake rasmi ni Salim Badar Mohammed al-Barwani lakini mwenyewe akijiita, na akishikilia aitwe, Salum Badru badili ya Salim Badar.   Wengi lakini wanamjua kwa jina la Salum Badar.

 

Napakumbuka kwao alikozaliwa kwenye jumba kubwa lililokuwa na lango la matovu ya shaba katika mtaa wa Kajificheni, pua na mdomo na palipo sasa baraza ya kisiasa ya Jaw’s Corner na palipokuwa ule mkahawa maarufu wa Tamim na karibu sana na Vuga, nilikozaliwa.

 

Ninamkumbuka vilivyo baba yake, Sheikh Badar Mohammed, mcha Mungu aliyekuwa hatoki Msikiti Gofu.  Alikuwa mrefu, akiwa na sharafa za ndevu zilizonyunyizwa mvi, macho makali na haiba iliyozidi kukozwa kwa mavazi yake maridadi ya kanzu, koti na kofia ya mkono.   Salum aliurithi urefu wa baba yake, ingawa yeye, hasa alipokuwa shababi, alikuwa mwembamba zaidi.

 

Simkumbuki Sheikh Badar kufanya kazi. Nikijua tu kwamba alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakijiweza, waliokuwa na ulwa katika mitaa yetu.  Akionekana kama bwanyenye. Yeye na nduguye Sheikh Hilal Mohammed, baba wa komredi Hamed Hilal, walirithi mashamba mengi ya baba yao na ndiyo yaliyokuwa yakiwapatia riziki.

 

Ndugu hao walikuwa wasasi na Sheikh Badar alikuwa mkubwa wa chama cha wasasi wa Zanzibar, wadhifa ambao baadaye ulishikwa na mtu wa shamba, Maalim Maksudi.  Bwana huyu, aliyekuwa mwenyeji wa sehemu za Jendele na Chwaka, alikuwa miongoni mwa waasisi na viongozi wakuu wa ZNP. Walikuwa sana wakisaka paa na nguruwe mwitu.  Msasi mwenzao, aliyekuwa mdogo wao kwa umri, alikuwa Seyyid Jamshid bin Abdallah, aliyejaaliwa na historia awe sultani wa mwisho wa Zanzibar.

 

Nawakumbuka pia kaka zake Salum. Kaka yao mkubwa Maalim Mohammed Badar, alinisomesha katika skuli ya Darajani.  Tukimwita “madasta” kwa sababu akihamaki akimrushia dasta mwanafunzi aliyemuudhi. Kaka zake wawili, Suleiman na Muhsin, waliuliwa na wapinduzi katika mapinduzi ya Januari 1964.  Ingawa mauaji ya kaka zake yakimuuma, Salum hakuwa na tabia ya kuyadhukuru.

 

Masomo ya mwanzo ya Salum yalikuwa chuoni  (madrasa) mtaani Vuga alikosomeshwa Kur-ani asubuhi. Saa za magharibi akihudhuria darsa za Sharifu Alawi bin Abdulwahab kwenye msikiti ulio nyuma ya sinema ya Majestic hapo hapo Vuga.

 

Mwenzake aliyekuwa akihudhuria naye darsa hizo alikuwa Yahya Ashraf Hujjat, ambaye tangu ujanani aliangukia kuwa komredi mwenzake na uzeeni wakiishi jirani katika mji wa Malmo, Sweden.

 

Salum Badar alianza masomo ya skuli katika Skuli ya Mashimoni, palipo sasa uwanja wa Mao Zedong, na baadaye Pemba alikochukuliwa na kaka yake Maalim Mohamed Badar alipohamishwa huko.  Kaka yake alimchukuwa kwa utundu wake uliokuwa hausemeki.

 

Salum alikuwa heshi kutoroka skuli.  Akiwa nyumbani alikuwa hachoki kuwatia wazimu wazee wake kwa utundu wake.  Mara nyingi akitiwa adabu kwa kufungwa katika chumba cha giza kwao chini.  Siku moja alfajiri yeye alimfungia baba yake ndani kwa kutia kufuli nje ya chumba na hivyo kumzuia asiweze kwenda msikitini kuswali.

 

Kupelekwa Pemba kwa muda kulikuwa kama dawa yake kwani aliporudi akili zake zilikuwa zimetua, akaanza kuwa mpole na kuwa na bidii na masomo.

 

Kama ilivyokuwa kawaida ya watoto watokao Pemba, aliporudi Unguja Salum alipelekwa Beit el Ras, nje kidogo ya Mjini.  Baadaye aliingia skuli ya sekondari ya Government Secondary School iliyokuwa Mnazi Mmoja palipo sasa skuli ya Ben Bella.

 

Salum wa skuli ya sekondari alikuwa Salum mwengine. Aliibuka kuwa hodari kiasi cha kuchaguliwa kuingia kidato cha tano katika King George VI Memorial Secondary School (ambayo siku hizi inaitwa Skuli ya Lumumba).  Huko alisoma pamoja na mwanahistoria Profesa Abdul Sheriff.

 

Tabia alizokuwa nazo skuli ndo zile zile alizokuwa nazo utu uzimani. Alikuwa mpole, mkimya, akipenda kusikiliza maoni ya wenzake kwa usikivu mkubwa, huku akikodoa macho kabla ya kutoa maoni yake.  Mara nyingi alikuwa na misimamo mikali lakini aliipamba kwa mizaha na vicheko.  Bado alikuwa na mabaki ya ukaidi wake wa utotoni kwa sababu haikuwa rahisi kumburura kwa hoja za kiitikadi alipokuwa hakubaliani nazo.

 

Mwamko wake wa kisiasa ulianza kutanuka akiwa skuli na ulimfanya azikumbatie siasa za kimaendeleo —  za kuupinga ukoloni, ubeberu na zilizokuwa zikihubiri mshikamano wa wenye kutawaliwa kote ulimwenguni.

 

Wanafunzi waliosoma naye katika skuli ya sekondari wanavikumbuka visa viwili vinavyomhusu.

 

Cha kwanza, kilihusika na picha.  Mwalimu wao mmoja wa Kizungu, aliyekuwa kijana na jeuri, akipenda kuwatukana wanafunzi.  Safari moja alipachika mapicha ya wafalme wa Kiingereza katika ukuta wa kidato cha pili, darasa lake Salum.  Aliwaambia kwamba kwa kuziweka picha hizo ati alikuwa akiwafundisha ‘ustaarabu’.

 

Siku ya pili, picha hizo zilionekana zimechanwachanwa.  Pakazuka sokomoko darasani na mwalimu alitaka kujua nani aliyezichana. Hakuna aliyethubutu kumtaja. Lakini ilijulikana kwamba alikuwa Salum Badar.

 

Profesa Sheriff amenambia kwamba kisa cha pili kilihusika na mtihani wa fasihi ya Kiingereza.  Badala ya kujibu maswali yaliyoulizwa kuhusu fasihi ya Kiingereza, Salum aliandika insha nzima kuulaani msimamo wa serikali ya Uingereza katika mgogoro wa Vita vya Suez vya mwaka 1956 pale Misri ilipovamiwa na majeshi ya Uingereza, Ufaransa na Israel.

 

Kwa sababu ya visa hivyo viwili Salum alifelishwa na alifukuzwa kwa muda skuli mpaka alipoingilia kati mjombake Sheikh Ali Muhsin Barwani.

 

Salum alishirikiana na vijana wenzake wa Mjini, Unguja, katika harakati za Umoja wa Vijana wa Kiislamu (Young Muslim League). Kati yao alikuwa Farouk Topan, ambaye siku hizi ni profesa mstaafu wa fasihi ya Kiswahili.  Salum alikuwa miongoni mwa vijana waliokuwa wakikusanyika kwenye baraza zilizokuwa karibu na mkahawa wa Tamim katika sehemu iliyo maarufu siku hizi kwa jina la Jaw’s Corner.

 

Vijana, na watu wazima, wakikusanyika hapo kusikiliza redio za kigeni kama vile Idhaa ya Kiswahili ya BBC kutoka London na hasa Sauti ya Afrika kutoka Cairo iliyokuwa iking’uruma dhidi ya ukoloni.

 

Vijana wa mkahawa wa Tamim wakijiita “Moscow Boys”. Miongoni mwao walikuwa Salum Badar, binami yake Hamed Hilal, Said Hamoud Mugheiry, Ahmed Ali Riyami na Salum Ali Riyami.  Moscow Boys walikuwa wakitiwa mori na wanaharakati Ahmed Lemki na Abdulrahman Mohamed Hamdani (Guy).

 

Lemki aliwahi kufungwa Misri alipokuwa mwanafunzi wakati wa enzi ya Mfalme Farouk, kwa shitaka la kwamba alikuwa Mkomunisti.  Abdulrahman ‘Guy’ naye katika miaka ya mwanzo ya 1960 alifungua chama cha Kikomunisti cha Zanzibar na akawa katibu wake mkuu.

 

Mwaka 1957 vijana wa Moscow Boys walikisaidia chama cha ZNP wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwanzo visiwani humo.  Baada ya muda Moscow Boys walijiunga na kikundi kipya kilichoitwa Zanzibar Action Group (ZAG), kilichojipanga kuyahujumu majengo ya serikali ya kikoloni ya Uingereza na ya serikali ya Marekani. Pia walikuwa wakibandika kwenye kuta za Mjini vikaratasi viliyoupinga ukoloni na ubeberu.

 

Lilipoundwa tawi la vijana la ZNP, Youths’ Own Union (YOU), takriban vijana wote wa Moscow Boys walijiunga nalo. YOU, iliyokuwa jumuiya ya mwanzo ya kisiasa ya vijana visiwani Zanzibar, iliasisiwa na Babu alipokuwa katibu mkuu wa ZNP.  Salum alichaguliwa katika kamati kuu ya YOU.

 

Kwa sababu ya mwamko wake wa kisiasa, Salum hakutaka kumaliza masomo ya kidato cha sita na badala yake mwaka 1961 alikubali msaada wa kwenda kusomea sheria Prague, Czechoslovakia. Msaada huo ulipatikana kwa jitihada za komredi Ali Sultan Issa.  Salum aliingia katika Chuo Kikuu  cha Charles, kilicho maarufu na chenye hadhi nchini Czechoslovakia.

 

Rafiki yake mkubwa alipokuwa huko alikuwa Dkt. Miraji Issa aliyekianzisha Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU).

 

Akiwa Prague, Salum Badar alipata mtoto mmoja wa kiume, Tomasi.  Baadaye alipohamia Sweden alimuoa Bi Nadhira Farsy, binti wa mwanachuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Abdallah Saleh Farsy, aliyewahi kuwa Kadhi Mkuu wa Kenya.  Walijaaliwa watoto wawili, Hamoud na Amina. Aliimaliza miaka yake ya mwisho akiuguzwa na kuangaliwa na chuo chake cha tatu, Bi Maryam binti Khatib.

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; @ahmedrajab/X

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.