Netanyahu na wenzake ni chui wa karatasi

 

Na Ahmed Rajab

 

NILIPOWASILI Gaza kwa mara ya kwanza Mei 2009 nilikuwa na hamu kubwa ya kukutana na Ismail Haniyeh, kiongozi wa Hamas (ufupisho wa Harakah al-Muqawamah al-Islamiyyah) na aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Palestina.  Hamas ni chama cha kisiasa chenye muelekeo wa Kiislamu; wafuasi wake wanafuata madhehebu ya Sunni.

 

Chama hicho kimekuwa kikiliendesha eneo la Gaza tangu 2007, mwaka mmoja baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa Bunge la Palestina.  Katika uchaguzi huo Hamas kilikibwaga chama cha Fatah, chama kikubwa cha Wapalestina kinachoongozwa na Mahmoud Abbas.

 

Hamas si shetani wa Fatah. Wala si shetani wa Israel. Sasa ni miaka 17 tangu serikali ya Israel ilizingire eneo zima la Gaza — hakuna kinachoingia humo wala kinachotoka bila ya idhini yake. Si vyakula, si madawa.  Si kwa njia ya baharini, nchi kavu wala ya angani.  Hutokosea ukisema kwamba Israel imewashika mateka wakaazi wote wa Gaza.  Zaidi ya hayo, hali za maisha katika Gaza ni duni.

 

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, hatua ya Israel ya kuizingira Gaza inazikiuka haki za binadamu na ni sawa na kuwatia adabu wakaazi wote wa Gaza kwa pamoja.

 

Nilikwenda Gaza nikitokea Jerusalem nilikokuwako kwa takriban wiki mbili na kupata fursa ya kuitembelea miji kadhaa ya Israel ikiwa pamoja na Tel Aviv, Haifa, Sderot na Jangwa la Negev ambako nilikutana na jamii za Wapalestina wenye asili ya Kiafrika.

 

Siku hizo nikifanya kazi Dubai nilikokuwa Mkuu wa Ofisi ya Mashariki ya Kati na Asia ya lililokuwa Shirika la Habari la Umoja wa Mataifa, IRIN.  Nilikwenda Gaza na Ramallah, katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, na maeneo mengine yanayokaliwa kwa nguvu na Israel kukutana na waandishi wetu na kuitathmini hali ya mambo ilivyokuwa baada ya Israel kuishambulia Gaza tangu Desemba 2008 hadi mwishoni mwa Januari 2009.

 

Miezi michache kabla, mwandishi Serene Assir, aliyekuwa akituletea ripoti kutoka Cairo na baadaye kutoka kwao Beirut, alifika Gaza na alikutana na Haniyeh. Katika picha waliopiga, nilimuona binti huyo wa Kilebanon, kwa mara ya kwanza, akiwa amevaa buibui akiheshimu maadili ya Kiislamu.

 

Mwandishi wa Kipalestina Nahedh Abdelwahed, aliyekuwa akijuana na baadhi ya viongozi wa Hamas alijitahidi sana kunisaidia kumfikia Haniyeh. Bahati mbaya juhudi zake hazikufua dafu.  Kwa sababu za kiusalama katika wakati huo tete, Haniyeh hakuwa akitulia mahala pamoja. Hata ilikuwa haijulikani wakati wa usiku atalala wapi.

 

Nikitamani sana kukutana na Haniyeh sio tu kwa sababu ni kiongozi wa Hamas lakini pia kwa sababu nyingine nyepesi: nikitaka kuzungumza naye kuhusu fasihi ya Kiarabu aliyosomea Chuo Kikuu cha Kiislamu huko Gaza.  Kadhalika, nilidokezwa kwamba alipokuwa mwanafunzi alikuwa shabiki wa soka akichezea timu ya Jumuiya ya Kiislamu katika chuo kikuu.  Nikitaka kuongeza “cha huko kwao Gaza” lakini nikakumbuka kwamba Gaza sio kwao Haniyeh.

 

Ingawa alizaliwa Gaza katika kambi ya wakimbizi ya Al-Shati kwao hasa ni mji ambao siku hizi unaitwa Ashkelon ulio ndani ya taifa ambalo tangu 1948 linaitwa Israel.  Wazazi wake walikuwa wakimbizi baada ya mji wao kutekwa katika vita vya mwaka huo, vilivyokuwa vya mwanzo baina ya Waarabu na Wayahudi. Wazazi wake Haniyeh walikuwa miongoni mwa waliokimbia makwao na walioishia katika kambi za wakimbizi.  Wayahudi waliokuwa wakitumia mbinu za kigaidi walishinda katika vita hivyo.

 

Wayahudi wanaviita vita hivyo kuwa ni Vita vya Uhuru kwa sababu ushindi wao uliwapa uwezo wa kuunda taifa la Israel Mei, 1948.  Wapalestina, kwa upande wao, wanauelezea ushindi huo wa Wayahudi kuwa ni “nakba” — neno la Kiarabu lenye maana ya “maafa,” “nakama” au “msiba”.

 

Sababu ya kuitwa hivyo ni kwamba wakati wa mapigano na baada ya Wayahudi kuanzisha dola la Israel, Wapalestina wasiopungua 700,000 ama walibidi wakimbie kutoka makwao au walifukuzwa kwa mitutu ya bunduki. Nyumba zao, ardhi zao na mashamba yao yakatwaliwa na Wayahudi.  Mpaka sasa kuna visa vinavyotokea vya walowezi Wakizayuni wanaoingia katika nyumba za Wapalestina na kuwatoa wenye nyumba kwa nguvu na kuingia wao kuishi.

 

Hiyo ni sehemu ya historia ngumu ya Israel — historia sio tu ya wizi wa mali za Wapalestina na roho zao lakini pia wizi wa ukweli.

 

Hicho ndicho chanzo cha mgogoro huu unaoendelea kwa miaka 75 baina ya Wayahudi na Wapalestina.  Israel inawanyima haki ya kurudi makwao Wapalestina wote waliokimbia nchi pamoja na wanaoishi katika kambi za wakimbizi.  Hiyo ndiyo sababu iliyomfanya Mwalimu Julius Nyerere, alipokuwa Rais wa Tanzania, avunje uhusiano wa nchi yake na Israel Oktoba 1973 baada ya vita vya Yom Kippur.  Tanzania ikawa safu ya mbele miongoni mwa nchi za Kiafrika zilizokuwa zikiwaunga mkono Wapalestine na Nyerere akawa na uhusiano wa kidugu na Yasser Arafat, aliyekuwa kiongozi wa chama kikuu cha Ukombozi wa Palestina (PLO).

 

“Hatujawahi kusita kuunga mkono haki ya Palestina kuwa na ardhi yao wenyewe,” ni moja ya semi maarufu za Nyerere.  Kadhalika, Tanzania ikipinga vikali uhusiano mkubwa uliokuwako kati ya Israel na utawala wa kibaguzi wa makaburu wa Afrika Kusini.

 

Israel imekuwa ikijifanyia itakavyo katika kuwakandamiza Wapalestina, walio Waislamu na Wakristo.  Katika ardhi iliyo kwenye Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, Israel imekuwa ikipora ardhi za Wapalestina na kujenga makazi ya Wayahudi, kinyume na sheria za kimataifa.

 

Hivi karibuni Wayahudi wakisaidiwa na polisi wamekuwa wakiingia kwa nguvu katika Msikiti wa Al-Aqsa na kuwapiga Waislamu. Nyakati nyingine Wayahudi wamekuwa wakiwabughudhi Wakristo na kuwatemea mate barabarani.

 

Nilifika Gaza wakati mgumu kwa wakaazi wote wa eneo hilo na mgumu zaidi kwa viongozi wa Hamas.

 

Gaza ni eneo la ukanda mwembamba kwenye mwambao wa mashariki wa Bahari ya Mediterranean lakini pia ni jina la jiji la ukanda huo.  Kuna namna nyingine ya kuielezea Gaza. Kuwa ukanda si ukanda, jiji si jiji bali kuwa Gaza nzima ni gereza. Ni gereza lililo wazi lenye wakaazi wasiopungua milioni mbili — zaidi ya nusu wakiwa watoto. Ni gereza lenye msongamano mkubwa wa watu na majengo ambayo, katika baadhi ya sehemu, huwa kama yaliyopandana na ambayo kila baada ya miaka michache hutwangwa kwa mabomu ya Israeli na kugeuzwa kuwa unga, vifusi na magofu.

 

Hiyo ndiyo hali niliyoikuta Gaza. Inataka uwe na moyo usitokwe na machozi. Nikisema nilikutana na maangamizi pengine sitokuwa nikiielezea kwa usahihi hali halisi ilivyokuwa.  Niliyoyakuta yalikuwa zaidi ya maangamizi  — yalikuwa mithili ya jahanamu ya duniani.  Wiki sita kabla ya kuwasili kwangu ndege za kivita za Israel ziliitwanga Gaza.  Mabomu na makombora yalianguka kama mvua.  Nilipofika nililikuta jiji zima la Gaza likiwa limevunjwavunjwa.  Skuli zilihujumiwa pamoja na misikiti, vituo vya polisi na hospitali kuu ya Al-Shifa.

 

Mambo mawili yalinishangaza: la kwanza, marikiti yao iliyokuwa imejaa vyakula. La pili, nyuso za wakaazi wa Gaza.  Nyuso zao zilijawa na bashasha na, mara kwa mara, wakiangua vicheko. Nikijiuliza: wanawezaje hawa kucheka? Wanawezaje kucheka watu walio katika janga la maangamizi? Watu waliofikwa na nakama, wasio na mbele wala nyuma?

 

Nilivifikiri sana vicheko vyao. Ilinichukua muda mrefu kutambua kwamba vicheko hivyo havikuwa vicheko vya kawaida. Vilikuwa vicheko vya kujihami na vya kuvisitiri vilio. Havikuwa vicheko vya kusalimu amri, vya kuyaacha yaliyojiri yapite.  Vilikuwa vicheko vya kuzihifadhi kumbukumbu za maumivu, fikira za uonevu na hisia za kudhalilishwa. Ndani ya nyoyo zao waathiriwa hao wa Gaza wakiungulika, wakisononeka.

Henri Lopes, waziri mkuu wa zamani na balozi mstaafu wa Congo-Brazzaville na ambaye pia ni mwandishi wa riwaya, ameiita riwaya yake moja: “Le Pleurer-Rire.” Kwa tafsiri isiyo rasmi tunaweza kuiita riwaya hiyo “Kicheko cha Kulia.”  Hicho ndo aina ya kicheko walichokuwa wakicheka wakaazi wa Gaza.

 

Tunapaswa kuyaangalia kwa muktadha huo mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya Israel alfajiri ya Jumamosi iliyopita.  Mashambulizi hayo ya Hamas na wenzao yaliishitua Israel kwa sababu kamwe haikuyatarajia.  Baada ya saa chache ilikuwa wazi kwamba Israel ilishindwa.

 

Wakati wa vita vya Vietnam (1955-1975), ambapo Marekani ikipigana na wazalendo wa Vietnam ya Kaskazini wakiongozwa na Ho Chi Minh, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha China, Mao Zedong, akipenda kuielezea Marekani kuwa ni “chui wa karatasi.”  Mao akimaanisha kwamba juu ya silaha nzito ilizokuwa nazo Marekani, taifa hilo halikuwa na uwezo wa kuwashinda wazalendo wa Vietnam.  Marekani na mshirika wake, Vietnam ya Kusini, zikiwa na silaha nzito wazalendo wa Vietnam walikuwa na imani ndani ya nyoyo zao.

 

Mashambulizi haya ya sasa ya Israel yataposita — na kuna siku yatasita ijapokuwa hayatokwisha kabisa — nina hakika kwamba serikali ya Netanyahu itaporomoka na huenda hata yeye mwenyewe akapandishwa kizimbani katika mahakama ya Israel.  Pamoja na mashitaka mingine ya ufisadi yanayomkabili anaweza pia akashitakiwa kwa uzembe.  Historia itapokuwa tayari kumhukumu ninaamini kwamba itamhukumu kuwa ni kiongozi ovyo kabisa Israel iliyowahi kumpata.

 

Uzembe wa majeshi na wa vyombo vya ulinzi vya Israel uliishangaza dunia. Tunasikia kwamba katika mkesha wa kuamkia alfajiri ya mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel, wakuu wa ulinzi wa Israel, walipata fununu kwamba Hamas ikiandaa kitu. Mara mbili palifanywa mazungumzo ya simu baina ya wakuu wa Shin Bet, idara ya ujasusi ya Israel, kitengo kinachosimamia jimbo la kusini mwa nchi hiyo, pamoja na wakuu wa idara ya ujasusi ya majeshi ya Israel. Mkuu wa majeshi hayo, Herzl Halevi, alielezwa kuhusu mazungumzo hayo.  Wakuu hao wa ulinzi wa Israel wakidhani kwamba wanamgambo wa Hamas wakifanya mazoezi.

 

Sasa Marekani na Israel zinajua kwamba wapiganaji wa Hamas wa Brigedi za Al-Qassam walikuwa na siri nyingi za kijeshi za Israel. Kwa mfano, wakijua wapi kilipo kituo maalum cha ujasusi cha Israel ambacho kinajulikana tu na wafanyakazi wa kituo hicho. Wakijua wapi ilipo mitandao ya mawasiliano katika baadhi ya kambi za kijeshi za Israel na wakitambua wapi jeshi la Israel lilipokuwa na udhaifu.

 

Ni wazi kwamba Israel, yenye uwezo wa kinyuklia, imeshindwa katika duru hii ya vita baina yake na Hamas. Waisraeli hawatolisahau hilo.

 

Hamas sasa inapambana sio tu na Israel lakini pia na Marekani ambayo juzi ilipeleka manowari zake mashariki mwa bahari ya Mediterranean.  Vikosi maalum vya Marekani navyo vimewasili vikishirikiana na majeshi ya Israel.

 

Israel imekuwa ikisema kwamba lengo la mashambulizi yake ya kulipizia kisasi yale ya Hamas ni kukifyeka kabisa chama hicho na kuibadili ramani ya Mashariki ya Kati. Hamas, kwa upande wake, pamoja na chama cha Hizbullah cha Lebanon vimesema kwamba navyo pia vitaibadili ramani hiyo endapo Israel itajaribu kukifyeka Hamas.

 

Hivi sasa Waisraeli wanaishambulia Gaza lakini lengo lao hasa huenda likawa ni kulitamalaki eneo zima la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, linalotawaliwa na Mamlaka ya Palestina yakiongozwa na Mahmoud Abbas. Hizo ndizo njama inazozipanga.

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.