#Siasa

Kupotea: Kazi ya kwanza ya dola ni kutulinda

Na Ezekiel Kamwaga

KABLA ya kuandika kile nilichotaka kuandika, ni muhimu sana kuweka msingi. Na msingi wenyewe, kwa kukosa mifano ya karibuni sana, itabidi nirudi nyuma takribani miaka 365.  Mwaka 1659, kitabu cha Leviathan cha Thomas Hobbes kilichapwa kwa mara ya kwanza. Hoja yake kubwa ilikuwa kwamba wananchi wanatakiwa kuipa dola nguvu isiyo ya kawaida na mamlaka juu yao kwa malipo ya wao kuwa salama.

 

Binadamu waliamua kuwa na serikali yenye viongozi wanaoishi kwa kuhudumiwa na umma kwa sababu moja kubwa, wananchi wawe salama. Wananchi wamekubali kujengwa kwa magereza, nchi kununua magari ya kuwasha, bunduki, virungu na silaha nyingine zote dhidi yao lakini lengo kuu liwe usalama wao.

 

Wananchi wanapokuwa hawako salama ndani ya nchi yao, kunakuwa hakuna sababu ya kuwa na serikali wala dola. Ndiyo sababu, katika masomo ya sayansi ya siasa, kuna kitu kinaitwa “Failed States” yaani nchi ambazo wananchi wake wanaweza kuishi pasipo kutegemea serikali. Kila mtu na lwake.

 

Kwa nini Hobbes aliona umuhimu wa kuwa na dola yenye nguvu? Ni kwa sababu kwa asili binadamu ni mtu mgumu kudhibitika. Ana tamaa, ana mahitaji, ana shauku, ana utashi ana mambo mengine yanayoendana na asili yetu kama binadamu. Wakati mwingine, mawazo yetu, tamaa zetu, shauku zetu na utashi wetu unaweza usiendane na maslahi ya pamoja kama taifa. Dola sasa ndiyo inatakiwa iwe msimamizi wa kuona watu hawaishi kama mbuzi waliokata kamba.

 

Ndiyo sababu, mimi ni mmoja wa watu wanaoendelea kushtushwa na vitendo vinavyoonekana kuanza kuzoeleka vya watu kupotea/ kupotezwa, katika mazingira ya kutatanisha na hakuna maelezo yanayotolewa ya kutosha – na vyombo vya dola, kuhusu nini hasa kinaendelea.

 

Mimi ni mwandishi wa habari na katika siku za karibuni nimezungumza na familia  mbili tatu za watu ambao wamepotea katika mazingira kutatanisha. Hakuna kitu kigumu kwa mwandishi wa habari kama kupigiwa simu za mfululizo na familia za watu ambao wapendwa wao wametekwa na hawaoni mtu wa kumpigia simu awasaidie. Wamefanya jitihada za kwenda polisi kulalamika lakini mwishowe wameambiwa watulie tu kwani uchunguzi unaendelea.

 

Kuna kesi moja ambayo inanyima usingizi hadi sasa. Watu watatu wa mkoa mmoja walifunga safari kuja Dar es Salaam. Hapo katikati, wakapoteza mawasiliano. Familia ikatoa ripoti polisi kwenye mkoa walikotoka. Kwenye maelezo kwa polisi, wakasema mara ya mwisho walipigiwa simu kuwa mhusika alikuwa Morogoro . Hapohapo, Polisi wa mkoa huo wakasema kama wahusika walikuwa Morogoro, jambo hilo liko nje ya mkoa wao na hivyo haliwahusu tena.

 

Walipopiga simu kutaka maelezo kutoka Morogoro, Polisi nao wakawaambia kuwa zaidi ya simu, kuna ushahidi gani wahusika walikuwa Morogoro wakati huo? Kwa hiyo watu watatu wa familia moja wamepotea kama moshi na kila Polisi wa mkoa hawahusiki na suala hilo!

 

Sasa huyu mwananchi ambaye kapotelewa na baba, mama, mtoto au mume, akimbilie wapi katika mazingira ya namna hii? Waende kwa nani? Si walikubali kwamba sehemu ya mapato yao itatumiwa kuwalipa watumishi wa dola ili wawalinde? Kama Polisi wa Morogoro hawahusiki na watu wa Singida, Ruvuma au Kigoma, wananchi hawa waende wapi?

 

Nilitikisa kichwa siku moja wakati nilipomsikia Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) mmoja katika mkoa ambao kuna familia imepotelewa na ndugu zao ambapo mbele ya waandishi wa habari, kamanda alisema “Hata sisi tumepata taarifa kama ninyi mlivyozipata”. Inawezekana alizungumza ukweli lakini si kauli ambayo watu waliopotelewa na wapendwa wao wanataka kuisikia kutoka kwa Polisi.

 

Katika makala haya, nimeambatanisha picha ya ukurasa wa kwanza wa gazeti la Mwananchi iliyoonyesha makumi ya watu ambao wamepotea na hakujawahi kutolewa taarifa ya maana kuhusu waliko. Ukisoma stori ile kwa undani, utapata picha ya nini familia za waathirika wa hali zinapitia sasa.

 

Ni muhimu kusema kwamba hali hii si ya Kitanzania? Kwa miaka mingi baada ya uhuru, hofu pekee tuliyokuwa nayo sisi wananchi ilikuwa ni ujambazi na wizi wa vibaka. Kwamba unajua kama unatembea mitaa ya Manzese kwa Mfuga Mbwa saa nane usiku ukiwa peke yako, ujue unahatarisha maisha yako.

 

Waliokuwa wakisafiri kwa magari usiku, walikuwa wanajua kuna hatari ya kukutana na majambazi walioweka magogo barabarani. Lakini hatari zote hizo kwa watu kwa kiasi kikubwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeshughulika navyo na kama kuna wizi au ujambazi unatokea, ni wa hapa na pale.

 

Hili la watu kutekwa lina umri wa labda miaka saba au nane hivi. Ninayeandika hivi ni mtu ambaye nina marafiki, jamaa na wana taaluma wenzangu waliowahi kupotea/kutekwa – wengine walipatikana baadaye na wengine hawajaonekana hadi leo.  Nikisikia mtu katekwa au kaponea linakuwa ni suala binafsi kwangu kwa sababu najua nini hutokea kwa familia na marafiki.

 

Tatizo la kuteka au kupoteza watu likimea litatuletea hasara kubwa mbili. Hasara ya kwanza ni kwamba litasababisha watu kuanza kupoteza imani na vyombo vya dola. Wataona kwamba hawawezi kulindwa tena na vyombo vilivyopo na hivyo watalazimika kutafuta ulinzi kwingineko.

 

Tabia hii ya binadamu kutafuta ulinzi kwingineko, ndiyo tabia iliyoyaibua makundi kama ya Mafia kule Italia na akina Pablo Escobar kule Amerika Kusini. Mafia walitumia hali ya kukosekana kwa ulinzi wa dola kwa wao kugeuka kuwa serikali. Kama ukienda Colombia leo, wapo watu wanaoamini kuwa Escobar alikuwa muhimu kwao kwa sababu aliwalinda na waovu wengine.

 

Watu wanaweza kuamua kutengeneza vikundi vyao vya ulinzi, kwanza kama sungusungu na mgambo na baadaye wakapata silaha. Tukifikia hatua hii, tujue kwamba muda si mrefu tutaelekea kuwa katika hali ile ya kutambulika kama nchi isiyo iliyoshindikana. Hatujafika huko lakini kama watu wataendelea kutekwa na kupotea kwa sababu zozote zile, njia ya kuelekea huko itakuwa inapaliliwa.

 

Jambo la pili ambalo ni la hatari kwa nchi kwa hali ni kuhusu nini itakuwa mwisho wa hili? Kwa sasa, wengi wa wanaotekwa na kupotea pengine ni watu wa chini. Lakini vipi ikianza kwa watu kuanza kutumia fursa kutimiza mambo yao ya kiovu? Kama mtu anamchukia mtu kwa sababu ya shida zao kazini, majumbani au kwenye mahusiano ya kijamii, wanaweza kutumia ombwe hili kufanya mambo maovu.

 

Tutaanza kuwa taifa la hatari kama watu wataona kuwa namna bora ya kumaliza tofauti zao na wenzao ni kwa kuwateka na kuwapoteza badala ya kufuata mfumo uliopo wa kuendesha nchi. Ikifika hatua hii, hakuna kati yetu atakayekuwa salama. Hata wale ambao wanasema “jambo la Morogoro halinihusu” nao pia watakuwa hatarini kwa sababu ya majukumu yao.

 

Nini tunahitaji kufanya? La kwanza kama jamii ni kuonyesha kwamba maisha ya yeyote yana thamani. Kama mtu mmoja amepotea na taarifa zimefika Polisi, ni muhimu yakatolewa matangaza kwa umma yanayoonyesha sura za wahusika na kwamba hawaonekani na wanatafutwa.

 

Kama wanashikiliwa na polisi na vyombo vingine vya usalama, ni muhimu ikaelezwa haraka iwezekanavyo. Hii ni kwa sababu ni sisi wenyewe wananchi ndiyo tumeipa dola nguvu ya kutukamata na kutuchukulia hatua. Kuna ubaya gani kwa taarifa kutoka kwamba tunamshikilia mtu X kwa sababu hii na ile na tutamtoa wakati tutakapokamilisha uchunguzi wetu?

 

Kama shida ni teknolojia, kuna haja ya Jeshi la Polisi na vyombo vingine kusema ni vigumu kufuatilia mazungumzo na mienendo ya wahalifu au watekaji kwa sababu kuna vitu hatuna. Kwa kufanya hivyo, nchi inaweza kuamua kuingia gharama ya kununua vitu na pengine kuweka kamera kwenye maeneo fulani ya kimkakati kiusalama ili ijulikane wahusika walipita wapi.

 

Namna ya kupambana na kuondokana na hali hii ni kwa dola kuonyesha kwamba inajali uhai wa raia wake hata mmoja. Ni muhimu taarifa ikatolewa mapema kuhusu watu waliopotea umma ukiombwa usaidie wapatikane. Kama wanashikiliwa, taarifa itolewe kwa wanafamilia kwamba mtu au watu wenu wako kwenye mikono salama lakini wanachunguzwa kuhusu hili na lile. Na kama utekwaji unakua kwa sababu kuna ombwe la teknolojia, ni muhimu wahusika wakasema ili ombwe hili lizibwe.

 

Lakini Tanzania haiwezi kuwa – nikinukuu maneno ya mwanafalsafa wa Cameroon, Achile Mbembe, taifa ambalo Necropolitics inashika mizizi yake. Kwamba wapo watu wanaoweza kuamua uhai wa nani ni muhimu kuliko wa mwingine. Tunaishi katika nchi ambayo mji wake mkuu wa biashara una jina la bandari salama.

 

Usalama wetu ndiyo Utanzania wetu na haiwezi kuwa vinginevyo.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza. Anapatikana kupitia email: ekamwaga57@gmail.com

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kupotea: Kazi ya kwanza ya dola ni kutulinda

TAABINI YA MZEE ALI HASSAN MWINYI

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *