Na Ahmed Rajab
Sura ya nje ya kitabu cha Mtazamo wa Kifikra wa “Sauti ya Dhiki” ya Abdilatif Abdalla. Mashairi yamefasiriwa kwa Kiingereza na Ken Walibora Waliaula na kitabu kizima kimehaririwa na Annmarie Drury. Kitabu hicho chenye kurasa 344 kimechapishwa na University of Michigan Press na Afrika kimechapishwa na Mkuki na Nyota Publishers, Dar es Salaam, Tanzania.
KITABU hichi tunachokihakiki kimekusanya mengi yenye kukifanya kiwe tunu kwa wasomaji wa aina mbalimbali. Tena ni cha kihistoria kwa sababu ni kitabu cha kwanza chenye tafsiri ya Kiingereza ya diwani nzima ya “Sauti ya Dhiki”, mkusanyiko wa mashairi uliompatia umaarufu mkubwa Abdilatif Abdalla, bingwa wa tungo za Kiswahili na gwiji wa lugha ya Kiswahili.
Tafsiri hii ya “Sauti ya Dhiki” imetolewa ukumbi zaidi kidogo ya nusu karne baada ya diwani yenyewe kuchapishwa mwaka 1973 na inafuata nyayo za tafsiri nyingine muhimu ya kazi ya fasihi inayonasibishwa na Afrika ya Mashariki. Nayo ni tafsiri ya Ida Hadjivayanis ya riwaya ya Abdulrazak Gurnah “Paradise”. Gurnah ametunga riwaya zaidi ya kumi na zote amezitunga kwa Kiingereza. “Paradise” ndiyo riwaya pekee iliyofasiriwa kwa lugha yake ya Kiswahili na kupewa jina la “Peponi”.
Tafsiri za kazi hizo mbili za fasihi zinathibitisha jinsi mandhari za kifasihi za Afrika Mashariki zinavyomeremeta. Tafsiri hizo za kazi za magwiji hao wawili wa fasihi walio wazawa wa Uswahilini — Abdilatif akiwa mzawa wa Mombasa, Kenya, na Gurnah wa Zanzibar — zinaonyesha jinsi fikra za ubunifu wa kifasihi zinavyochanua na kuoana katika akili au ufahamu wa Mswahili.
Insha zilizomo ndani ya kitabu hiki zinamsifu na kumpamba Abdilatif Abdalla na, kwa kweli, anastahili kusifiwa hivyo. Abdilatif ni msomi au mwanazuoni wa umma, mwenye maajabu mengi. Yeye ni miongoni mwa watunzi wa safu ya mbele walio waanzilishi wa mashairi ya Kiswahili ya kisasa akitumia zaidi lahaja ya kwao ya Kimvita.
Kadhalika ana sifa ya kipekee ya kuwa mtu wa kwanza nchini Kenya kufungwa kwa sababu za kisiasa baada ya nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1963. “Sauti ya Dhiki” ni ushahidi wa jinsi alivyosimama imara alipokuwa akizitunga tungo hizo akiwa kifungoni katika gereza la Shimo la Tewa na lile Gereza Kuu la Kamiti akizihifadhi na, apatapo wasaa, kuziandika kwenye karatasi za chooni za kujisafisha baada ya kwenda haja.
Historia imewashuhudia washairi wengi waliokuwa wamefungwa gerezani. Na katika karne hii ya 21 bado washairi wanaandika kuhusu maudhui ya uhuru wa ubunifu au uhuru wa kifikra.
Washairi pia hujitamba kwa kuthubutu kuyatamka au kuyaandika yasiyosemeka au yasiyoandikika. Huwa na ujasiri au ujabari wa kusema kweli hata wa kuwaambia kweli watawala madhalimu. Kuna mifano mingi ya washairi wanaofungwa na serikali kwa sababu ya mashairi yao. Mfano mmoja ni mshairi wa Kipalastina Dareen Tatour. Dareen ni mwanamke shujaa aliyekamatwa 2015 kwa shairi aliloliandika liitwalo ‘Qawem Ya Shaabi, Qawemahum’ (Pambaneni Umma wangu, Pambaneni nao). Baada ya kukaa gerezani pamoja na kwenye kizuizi cha nyumbani, hatimaye Julai 2018, alihukumiwa kifungo cha miezi mitano.
Kuna na wanaofungwa gerezani kwa sababu zisizohusika na utungaji wa mashairi. Na wanapokuwa korokoroni ndipo wanapotunga tungo zisizosahaulika. Abdilatif Abdalla ni mmojawao.
Abdilatif amefika hapa alipofika baada ya safari ndefu ya kusaka ilimu na maarifa. Aliitambua nyota yake na akaisafiria.
Aliingizwa chuoni yaani madrasa kusoma Kuruani na dini. Pia aliingizwa skuli lakini huko skuli, ingawa hakuwa pocho, hakuweza kuendelea na masomo ya sekondari. Aliambiwa hakufaulu mtihani wa kuchupa kutoka masomo ya msingi kuingia ya sekondari.
Alijikaza kutaka kuyajua mambo na akawa na hamu kubwa ya kusoma vitabu. Natija aliyopata ni kwamba ukubwani aliibuka akishika nyadhifa nzito katika vyuo vikuu na katika tasnia za uandishi habari na utangazaji wa redio.
Kitabu hiki ni kama kito adhimu chenye thamani kubwa kwa wapenzi wa tungo za sasa za Kiswahili. Hakiwapi wasomaji wa Kiingereza tafsiri tu za maandishi ya Abdilatif na ya yaliyoandikwa juu yake, lakini pia yanatudodesha mengi kuhusu maisha yake na maono yake.
Katika Dibaji yake ya tafsiri ya “Sauti ya Dhiki”, Ngugi wa Thiong’o amemyanyua Abdilatif na kumpachika kwenye shubaka la majagina ya fasihi yaliyopambana na udhalimu kwa kutumia ubunifu wao. Ajabu ya mambo ni kwamba Ngugi pamoja na Abdilatif, wote wawili, wamejipambanua kuwa mabingwa wa mapambano dhidi ya udhalimu nchini Kenya.
Mfasiri wa “Sauti ya Dhiki”, Ken Waliaula, anastahiki kupongezwa kwa jitihada zake za kuyatafsiri mashairi hayo kwa Kiingereza, ijapokuwa alikabiliwa na kibarua kikubwa cha kuyahaulisha katika Kiingereza mahadhi, midundo na mbwembwe za mashairi yenyewe.
Mhariri wa kitabu hiki, Annemarie Drury, ameandika utangulizi mwanana juu ya mtazamo wa kifikra wa Abdilatif. Utangulizi huo umeranda na kutanda ukigusia mengi ya Abdilatif toka msimamo wake wa kisiasa, falsafa, maudhui ya tungo zake na namna anavyotumia lugha. Yeye zaidi hutunga kwa lahaja ya kikwao ya Kimvita lakini ameonyesha uwezo wa kutunga hata kwa lahaja ya Kigunya (Kitikuu).
Katika insha yake ya kiuchambuzi, Ann Biersteker anaueleza umuhimu wa “Sauti ya Dhiki” katika fasihi ya Kiswahili na ya Afrika Mashariki, hususan umuhimu wake katika kuifahamu historia ya kisiasa na ya kitamaduni ya eneo hilo. Tashwishi za Kiislamu na za kisoshalisti zinaonekana wazi katika tungo hizi.
Alamin Mazrui, naye katika insha yake, ameandika maelezo yenye kugusa moyo juu ya uhusiano wake na Abdilatif na jukumu lao la ubia la kuyatumia mashairi kama silaha ya kujikomboa. Alamin, ambaye ni profesa katika Chuo Kikuu cha Rutgers, Marekani, anafanana kwa mambo kadhaa na Abdilatif. Yeye pia ni mzawa wa Mombasa, mshairi wa Kiswahili, mwanaharakati wa kupigania haki na aliwahi pia kutiwa gerezani kwao kwa sababu za kisiasa.
Sina shaka kwamba wasomaji wa Kiingereza wanaposoma tafsiri ya Meg Arenberg ya “mashairi mane ya Abdilatif yenye Vina na Mizani” wanapata ladha ya ustadi wa kiufundi wa Abdilatif Abdalla wa kuyafinyanga mashairi.
Kitabu hiki pia kina sehemu inayoangazia “Sauti ya Dhiki” katika muktadha wa wakati wake wa kihistoria. Sehemu hiyo ina tafsiri za matini za kimsingi na maelezo ya wasomi yenye kumpa msomaji ufahamu mpana zaidi. Miongoni mwa matini hizo ni tafsiri ya Kai Kresse ya makala ya “Kenya: Twendapi?” yaliyomchongea Abdilatif akatumbukizwa korokoroni na akaibuka na hazina ya tungo za “Sauti ya Dhiki”. Hiyo ni tafsiri ya kwanza ya Kiingereza ya makala hayo ya kihistoria. Matini nyingine ni tafsiri ya utangulizi wa chapisho la 1973 la “Sauti ya Dhiki” ulioandikwa na gwiji wa historia ya Kiswahili Shihabuddin Chiraghdin.
“Sauti ya Dhiki” ni diwani adhimu yenye kuhifadhi urathi wa Abdilatif Abdalla na kuendeleza masomo ya fasihi na historia ya Afrika Mashariki. Ni hazina, isiyoweza kusongwa, ya taamuli, tafakuri na fikira zenye kuonyesha kwamba mashairi yana uwezo na nguvu ya kudumu ya kutumika kama silaha ya mapambano na ukombozi.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; X/@ahmedrajab
Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.