Othman: SUK, Rais Mwinyi, Maalim Seif, Muungano na ajira Zanzibar

Picha: Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud (kulia), akizungumza na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Dunia, Ezekiel Kamwaga, kwenye mahojiano maalumu ofisini kwake kuhusu tathmini ya Nusu Muhula wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baina ya vyama vya CCM na ACT Wazalendo visiwani humo. Picha na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

 

Na Ezekiel Kamwaga

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud, amesema kwamba uhusiano wake kikazi na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, ni mzuri na ndiyo umefanikisha kutopanda kwa joto la kisiasa visiwani humo – ingawa hata hivyo amebainisha zipo changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi kwenye muundo wa serikali hiyo.

 

Othman aliyasema hayo kwenye mahojiano maalumu na Gazeti la Dunia yaliyofanyika ofisini kwake, Migombani, Unguja kueleza kuhusu mafanikio, changamoto na mwenendo wa siasa za Zanzibar wakati Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ikitimiza takribani miaka miwili na nusu tangu kuundwa kwake kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

 

Othman ambaye alichukua wadhifa huo kufuatia kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad Januari mwaka juzi, alisema ingawa yeye na Mwinyi hawakuwa wakifahamiana sana kabla ya yeye kuchukua wadhifa wao, wamejitahidi kwa kadri inavyowezekana kuhakikisha SUK inakwenda vizuri kukidhi uwepo wake.

 

” Mimi na Rais Mwinyi hatukuwa na uhusiano wowote binafsi kabla ya mimi kuwa Makamu wa Rais. Tumefahamiana vizuri zaidi sasa. Kwa hiyo uhusiano wetu ni wa kikazi zaidi na ninashukuru kwamba hadi sasa uhusiano wetu ni mzuri. Kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri natoa mchango wangu ipasavyo na yapo majukumu ya Rais ambayo huwa ananipa kumwakilisha katika nyakati tofauti ikionyesha kwamba tunaaminiana. Nadhani hili ni jambo la muhimu,” alisema Othman.

 

Alisema lengo kubwa la kuwa na SUK ni kujenga Umoja wa Kitaifa na kuondoa misuguano ya kisiasa inayohatarisha umoja na maendeleo ya taifa hilo na kwamba hadi sasa, uwepo wa SUK umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza joto la kisiasa na maisha ya Wazanzibari yanaendelea kama kawaida pamoja na changamoto za kiuchumi zinazoendelea.

 

Hata hivyo, alisema yako mapungufu katika muundo mzima wa SUK ambayo haitoi majukumu ya waziwazi kwa mtu wa wadhifa kama wake – zaidi ya hiyo ya kumshauri na kumwakilisha Rais wa SMZ pale inatokea, na kwamba jambo hilo linaweza kutoa picha ya kuwa madarakani kwa ajili ya cheo tu lakini kukosa nguvu za kimamlaka kutimiza majukumu yake.

 

“Umeniuliza hapa, katika mazingira ya namna hii, ikifika uchaguzi wa mwaka 2025 nitawaambia Wazanzibari nimefanya nini? Jibu langu ni kwamba Wazanzibari ni watu werevu, wanajua nafanya nini hivi sasa na watajua la kufanya kwenye sanduku la kura. Werevu wa Wazanzibari unajulikana. Tumewahi kuweka rekodi ya dunia ya uchaguzi ambao mtu alishinda kwa kura moja tu. Sina wasiwasi kabisa na hilo. Wazanzibari ni werevu,” alisema Othman.

 

Othman alijijengea heshima kubwa visiwani Zanzibar kama mwanasheria mahiri na mwadilifu na kuingia kwake kwenye siasa kuvaa viatu vya gwiji wa siasa za Zanzibar kungewatetemesha watu wengi. Lakini kwenye mazungumzo yake na Gazeti la Dunia (GD) ambayo yatarushwa yote kupitia podcast ya Ezekiel Kamwaga Show mwishoni mwa wiki hii, Othman alisema kinachompa nguvu ni kuamini kwamba, kimsingi, hakuna mwanasiasa wa Zanzibar, sasa na pengine milele, atakayekuwa kama Maalim.

 

“Tangu siku ya kwanza niliwaambia watu kuwa mimi si Maalim Seif. Maalim Seif alikuwa mmoja tu, hakujawahi kuwa na mwingine na huenda asitokee mwingine tena kama yeye. Aina yake ya siasa ilitokana na makuzi yake, mapitio yake na changamoto za watu wa kizazi chake. Kitu pekee ninachoweza kufuata ni ndoto zake na kile alichopigania kwa Wazanzibari wote. Kwa hiyo siwezi kuwa Maalim Seif, lakini mimi na wenzangu tuliobaki tunaweza kutimiza ndoto zake,” alisema.

 

Katika mahojiano haya yaliyojikita pia kwenye masuala ya kisheria na kiuchumi, Othman alizungumzia kwa kina kuhusu suala la Muungano kwa kusisitiza kuwa tatizo la zinazoitwa Kero za Muungano linatokana na muundo wa Mkataba wenyewe wa Muungano ulivyo. Alisema wakati kukiwa na mjadala mkubwa kuhusu suala la uwekezaji wa Bandari, mkataba usiofaa zaidi kuwahi kuingiwa Tanzania ni mkataba wa Muungano.

 

Kuhusu uchumi wa Zanzibar, Othman alisema wanashukuru Mungu kwamba changamoto ya ugonjwa wa Covid 19 sasa imemalizika na wako tayari kufanya jitihada zote kuzimua uchumi wa visiwa hivyo uliyoathiriwa sana na ugonjwa huo. Sekta muhimu ya utalii ni miongoni mwa zilizoathirika sana na ugonjwa huo.

 

Kwenye changamoto ya ajira kwa Wazanzibari, Othman alifichua kwamba ingawa tatizo la ajira lipo visiwani humo, lakini kunahitajika mabadiliko makubwa ya kifikra na kimtazamo kwenye kukabiliana na tatizo hilo. Akitoa mfano kwa kutumia takwimu halisi za wastani, alisema Serikali ya Zanzibar imeajiri watu wengi zaidi kuliko hata Tanzania.

 

Alisema SMZ ina watumishi takribani 40,000 wanaolipwa jumla ya shilingi bilioni 600 kwa mwaka. Serikali ya Muungano, kwa upande mwingine, inatumia takribani shilingi trilioni 11 kwa ajili ya kulipa mishahara kwa mwaka. Kama ukipiga hesabu ya kiwango ambacho kila mwananchi anamlipa mtumishi wa serikali, Tanzania wanalipa shilingi 15,000 wakati Mzanzibari analipia shilingi 32,000 kwa kila mtumishi wa SMZ.

 

“Kwa lugha nyingine, naweza kusema kwamba SMZ imevimbiwa kwa sasa, ina obesity kwenye suala hili la ajira. Mzanzibari wa kawaida analipa zaidi ya asilimia 100 kulinganisha na wenzao wa Serikali ya Muungano. Fikiria kwamba Zanzibar hatulipii majeshi wala masuala mengine ya Muungano ambayo yangeongeza bajeti zaidi. Hii maana yake ni kwamba tunatakiwa kuangalia jambo hili kwa jicho tofauti.

 

” Kuna haja ya kuwaambia watu wetu ukweli kuwa hii ndiyo hali tuliyonayo. Ni muhimu kuangalia nje ya boksi. Angalia eneo la utalii kwa mfano. Zanzibar leo tuna hoteli takribani 600 za kitalii lakini asilimia 80 ya kuku wanaotumika huko tunaagiza kutoka nje. Tunatakiwa kuangalia ni kwa vipi tunaweza kuhudumia soko hilo kubwa kutoka nje. Lakini hata kwa vijana wetu walioelimika, ni kwa vipi ujuzi wao utatumika kukidhi mahitaji ya soko kwenye uchumi wetu. Ziko fursa kwenye uchumi wa buluu.

 

” Tanzania na Zanzibar zina fursa nyingi ambazo hatujaamua kuzitumia. Angalia mfano wa Tanga na Rwanda. Ukipima kwa maeneo, zina eneo linalofanana kwa ukubwa. Lakini angalia wapi Rwanda ipo na angalia Tanga iko wapi kiuchumi. Tunatakiwa kufahamu tofauti ya kusaidia kijamii na kuwezesha watu. Tunatakiwa kuwezesha watu. Tunahitaji uongozi wenye maono. Siongoi haya mambo kama naota tu. Ipo mifano ya nchi ambazo zimefanikiwa kwa sababu ya maono sahihi,” alisema.

Mahojiano kamili kwenye Ezekiel Kamwaga Show