Mkataba wa Bandari umeonesha rangi zao

Picha: Sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam

 

Na Ahmed Rajab

 

KUMEKUWA na mijadala ya kushangaza nchini Tanzania tangu ibainike kwamba serikali yake inawasilisha bungeni Azimio la kujadili mkataba unaotarajiwa kutiwa saini baina yake na kampuni ya kimataifa ya DP World inayomilikiwa na serikali ya Dubai. Kiini cha mkataba huo ni Bandari ya Dar es Salaam na nyinginezo zilizo Bara ambayo kampuni hiyo inatarajiwa kuziendesha.

 

Si dhamiri yangu kuujadili wala kuuhukumu huo mkataba. Sitofanya hivyo kwa sababu sikuuona na siyajui yaliyomo ndani yake.  Naufata ule wasia maarufu wa Mao Zedong, aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha Kikomunisti cha China.  Wasia wake unasema: “kama hujafanya utafiti, huna haki ya kusema.”

 

Kuna jambo moja lakini ninaloweza kulisema ingawa halihusiki moja kwa moja na mkataba wenyewe. Linahusika, kwa jumla, na ushirikiano au miamala kama hii inayofanywa katika haya yaitwayo mazingira ya utandawazi.  Kwa kawaida, miamala hii hufuata kanuni na taratibu za ubepari uliopevuka. Na ubepari wa aina hiyo huwa na harufu ya ubeberu ambao ndio daraja ya juu ya ukoloni. Ndio maana kuna haja kubwa ya kuipiga darubini na kuichunguza vilivyo mikataba aina hiyo isije ikawa ni ya kuzikaba na kuzitia kwapani nchi kama zetu.

 

Tusisahau jinsi ukoloni ulivyoanza.  Ulikotoka na ulipofika.  Makampuni kutoka nchi za Ulaya yalikwenda katika nchi za wengine kusaka bidhaa kama dhahabu, madini ya fedha, karafuu na kungumanga; mwishowe ikazitawala nchi hizo. Kampuni ya Uingereza ya East India Company, kwa mfano, ilihodhi biashara katika nchi za Asia na ikaishia kuzihodhi nchi hizo kiutawala, kwa kuzitamalaki na kuzigeuza koloni. Huo ndio uliokuwa ukoloni asilia. Siku hizi za utandawazi unajigeuza gamba na kuwa ukoloni mamboleo.

 

Tangu wiki iliyopita mitandao ya kijamii imegeuzwa majaa ya kutupia lawama dhidi ya serikali ya Tanzania kwa kisingizio cha kuukosoa huo mkataba wa bandari.  Kwa ninayoyasikia inaonesha kwamba kweli kuna baadhi ya mambo yasiyokaa sawa katika mkataba huo na yanabidi yarekebishwe.  Lakini kusema kweli lawama nyingi zinazovurumishwa dhidi ya huo mkataba ni za upotoshaji.  Tena wa makusudi.

 

DP World, kwa mfano, si kampuni mburu mbatara, chambilecho jamaa wa barazani.  Ni jikampuni lenye uzoefu mkubwa sana wa shughuli za bandarini.  Miongoni mwa kazi zake ni kusimamia utaratibu wa ugavi na usafirishaji wa watu na vitu vikiwa pamoja na mazao yanayouzwa nchi za nje. Jikampuni hilo limekuwa likiendesha shughuli zake kimataifa na lina kampuni tanzu kadhaa katika nchi mbali mbali.

 

Tangu 2010 DP World imekuwa ya tatu kwa ukubwa duniani miongoni mwa makampuni yenye kuendesha bandari.  Kwa hivyo, uzoefu wake wa shughuli za bandarini umevuka bahari ya Dubai na umetia gati katika bandari za sehemu tafauti duniani.

 

Hapa ningependa kuwakosoa wakosoaji wa mkataba wa DP World kwa kusema kwamba sio kweli kuwa kuna vilio katika nchi ambazo DP World imewekeza.  Bila ya shaka kumekuwako watu waliokuwa wakilalama lakini sio wenye kulia. Kuna tafauti kubwa baina ya kulalamika na kuangua vilio.  Kweli kumekuwako na malalamiko kuhusu uwezekaji huo katika nchi zao.

 

Hilo ni jambo la kawaida katika utekelezaji wa mikataba ya kiuchumi ya kimataifa. Na ndio maana tumeshuhudia kesi zikifunguliwa katika nchi mbali mbali za kuishitaki DP World kuhusu masharti ya ushirikiano wake na nchi hizo.  Kutokana na hayo ni sahihi kabisa kuwa Tanzania iwe na hadhari ili mkataba huo usiwe na masharti yatayoipendelea kampuni ya DP World na kuionea Tanzania. Panahitajika uangalifu mkubwa.

 

Tusisahau pia kwamba DP World nayo imefungua kesi kadhaa dhidi ya wabia wao katika baadhi ya nchi.

 

Mwenyekiti na mkuu wa kampuni hii ni mfanyabiashara mashuhuri wa Dubai, Sultan Ahmed bin Sulayem.  Kwa muda mrefu babake alikuwa mshauri wa aila ya kifalme ya Dubai.

Sulayem ana shahada ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Temple kilicho Philadelphia, Marekani.  Alihitimu katika miaka ya mwisho ya mwongo wa 1970 na aliporudi kwao alianza kazi akiwa afisa wa forodha.

 

La kuhuzunisha kutokana na mijadala ya mitandaoni kuhusika na kadhia hii ni kujitokeza tena kwa chuki na ubaguzi wa kikabila na kidini.  Ilivyo ni kwamba baadhi ya Watanzania wenye msimamo sahihi wa kupinga ubaguzi wanapofanyiwa Waafrika, huona ni sawa na haki yao kuwabagua watu wa makabila mengine.

 

Ubaguzi huo haukuibuka tu vivi hivyi.  Tuseme kweli: ubaguzi huo umo ndani ya nyoyo za Watanzania wengi hasa miongoni mwa wanasiasa wa Bara na wale wanaojiita wasomi. Baadhi yetu hatukushangaa kwa sababu tumetambua zamani kwamba kuna ukabila wa kukirihisha Tanzania.

 

Baadhi ya wanasiasa wakuu wa Tanganyika wamekuwa wakiutumia ubaguzi kutufitinisha sisi wanaotuita ndugu zao wa Zanzibar. Furaha yao ni kutuona tukipapurana sisi kwa sisi. Wanaifuata mbinu ya wakoloni ya kuwagawa watu wa taifa moja ili iwe rahisi kuwatawala.

 

Wenye kutoa matamshi ya kibaguzi si watu ambao ndimi zao ziliteleza.  Walijua wanasema nini, kwa mintarafu gani na kwa faida ya nani.

 

Kuna bibi mmoja alihoji kwamba Tanzania inarudi utumwani. Alifika hadi ya kuthubutu kusema “tunarudi kwenye utawala wa kisultani…angalau tunaweza kutawaliwa na mzungu lakini tusitawaliwe na Mwarabu.”

 

Ilivyo ni kwamba huyo bibi anajitia mwenyewe utumwani. Kuhiari ukoloni wa taifa moja kwa kuukataa wa taifa jengine ni kuwa na fikra za kitumwa, za kuridhia na kukubali kutawaliwa na wengine.  Mzalendo halisi hupinga ukoloni wa aina zote, wa rangi zote na wa kabila zote.  Na hupinga isimu ya ukoloni kwa kutumia njia au nyenzo zozote alizonazo kwa kufanya kinachohitajika.

 

Tamko la kwamba afadhali tutawaliwe na mzungu lakini tusitawaliwe na Mwarabu ni tamko lisilo na hata chembe ya uzalendo. Ni ulaanifu wa kibaguzi wenye kuitusi historia yetu na kututukana sote.  Inasikitisha, tena sana, kuwasikiliza wenye kujigamba kwamba ni wasomi na wanaharakati wenye kupigania haki wakiropokwa namna hivyo.

 

Tamko hilo linatukumbusha maneno yaliyojaa ubaguzi wa kikabila na udini yaliyowahi kutamkwa hadharani katika nyakati tafauti na waziri wa zamani William Lukuvi pamoja na Samuel Sitta, aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.  Wanachofanya wakosoaji hao ni kuwatetanisha Watanganyika na Wazanzibari. Na huko huko Tanganyika kwenyewe kuleta mtafaruku baina ya Wakristo na Waislamu.

 

Badala ya kuwa makini na kutoa hoja zenye mashiko ya kimantiki wakosoaji hawa wamekurupuka na, kwa pupa, bila ya kuutalii walianza kuuponda huo mkataba unaotarajiwa baina ya DP World na Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa kutumia upotoshaji badala ya ukweli katika utetezi wao.

 

Panaweza pakawa na sababu za kweli za kuukosoa mkataba huo na kila mwenye kuona taksiri zozote katika masharti ya ushirikiano huo ana kila haki ya kulitoa joto lake. Lakini afanye hivyo kwa hoja zenye kujikita juu ya yaliyo kweli. Si kwa kujitia jazba za ubaguzi.

 

Wasomi ndio tunaowataraji wawe safu ya mbele kuwapiga darubini watawala na kuwakosoa wanapostahiki kukosolewa.  Wanapomuona mtawala yuko hadharani bila ya nguo wanatakiwa wawe na ujasiri wa kupaza sauti na kumwambia, kinagaubaga, kwamba yuko uchi.  Lakini wanatakiwa wafanye hivyo pakiwa na ushahidi.

 

Maswali ya kujiuliza ni kwa nini wakajigeuza wehu na wakacharukwa hivyo? Kwa nini wakachuna nyuso wakaona ni sawa na ni haki yao kuupinda na kuupotosha ukweli? Kwa nini wakatumia lugha ya kibaguzi?

 

Hawa ni watu wanaojiona kuwa ni wasomi.  Ingefaa tuwaonee huruma lau wangelikuwa wanayasema wayasemayo kutokana na ujinga wa kutoujua uhalisia wa mkataba wenyewe.  Lakini hawa hawamo katika kaumu hiyo.

 

Hawa ni maafiriti. Ni maluuni wenye ajenda nyingine iliyo kubwa na ovu na wanayoiengaenga isije ikavuja hadharani na mapema.  Mijicho yao imelenga mbali.  Inauangalia mwaka 2025 na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanywa mwaka huo nchini Tanzania.

 

Inavyoonesha ni kwamba wamevinjari kufanya juu chini ili Rais Samia Suluhu Hassan asiwe mgombea wa urais wa chama kinachotawala cha CCM.  Na kama watashindwa katika njama hiyo basi wanataka kuhakikisha pasiwepo tena Rais wa Muungano atayetoka Zanzibar.

 

Ajabu ya mambo ni kuona mlingano wa dhamira baina ya wanaCCM wenye kumchimba Rais wao na wengine walio nje ya CCM wenye kuicheza ngoma isiyo yao.  Wote wanatumia ubaguzi wa kikabila na udini. Kwao, hili ni jambo la kufa au kupona, la pata potea.

 

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

 

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.