Mrithi wa Makonda: CCM na revolvere  

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

NI kazi ngumu kubashiri uteuzi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho. Ukiangalia waliochukua nafasi hiyo kabla, huwezi kutunga uzi au shanga kuunganisha matukio.

 

Hakuna sababu ya waziwazi ya kusema kwa nini alimpa nafasi kwanza Shaka Hamdu Shaka. Aliyemfuatia Shaka, Sofia Mjema, hana sifa za kipekee kulinganisha na wana CCM wengine waliopo Tanzania. Mbadala wa Mjema, Paul Makonda, hakuwa na lolote la kumfananisha na watangulizi wake hao wawili zaidi ya kuwa wanachama wa chama tawala.

 

Hii maana yake ni kwamba mwana CCM yeyote – kwa kufuata utangulizi huo, anaweza kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho. Hili halifanyi kazi ya kubashiri mbadala wa Makonda anayetarajiwa kujulikana leo baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kuwa rahisi kwa vigezo vyovyote vile.

 

Lakini, ziko namna kadhaa ambazo ubashiri unaweza kufanyika. Nitaangalia maeneo ambayo huenda Mwenyekiti wa CCM na NEC watayazingatia wakati wakimtafuta mtu wa kushika wadhifa huo.

 

Mapinduzi Vs Mabadiliko

 

Imesadifu kwamba kirefu cha CCM ni Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tafsiri ya mapinduzi (revolution) inayotumika leo – ameandika Fareed Zakaria katika kitabu chake kipya cha Age of Revolutions (2024), si tafsiri ya awali iliyotumika wakati neno hilo lilipoanza kutumika.

 

Neno hilo lilianza kutumiwa na Wanasayansi kwa mara ya kwanza. Revolution, kwao, ni neno lililotokana na neno la lugha ya Kilatini, Revolvere, likimaanisha mzunguko kurejea katika hatua ya awali. Dunia kuzunguka jua au kujizungusha kwenye mhimili wake ilikuwa ni sehemu ya revolver. Mapinduzi yalikuwa ni jambo lenye utaratibu, asili, hali na yanayotabirika.

 

Hali hiyo ni tofauti kabisa na neno mapinduzi kama linavyotumika katika dunia ya sasa. Mapinduzi kisasa ni jambo linalofumua kabisa mfumo uliopo na kuleta mfumo mpya. Mapinduzi, yawe ya Zanzibar, Ufaransa, China, Urusi na kwingineko, si jambo linalotarabirika na kutakiwa kurejea katika hatua ya awali.

 

Uteuzi wa Makonda kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi ulielekea zaidi katika tafsiri ya sasa ya mapinduzi kuliko tafsiri ya awali ya utaratibu na kubashirika. Tabia na kauli za Makonda hayakufanana na matendo na kauli ulizotegemea kutoka kwa Katibu wa Uenezi wa CCM ya Rais Samia.

 

Kwa sababu ya asili ya mapinduzi kwa mujibu wa tafsiri ya sasa, haikuwa jambo la busara kuwa na kiongozi wa nama hiyo wakati chama kikiwa kinajitahidi kuwa kimoja kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Kila nikitazama, simwoni Mwenyekiti wa CCM akimpa tena nafasi mtu wa dizaini ya Makonda kuwa Katibu wa Uenezi. Naona CCM ikimpa nafasi mtu mwenye tabia za kimapinduzi kwa maana ya tafsiri ya kwanza ambayo inakirejesha chama katika tabia na misingi yake.

 

Kama walivyokuwa akina Shaka na Sofia, CCM itampa nafasi mtu ambaye anafahamika vema ndani ya chama lakini si mtu atakayetaka kukigeuza chama kwenye mwelekeo mpya katika nyakati ambazo kinajipanga na uchaguzi na kinataka kiwe na umoja na si minyukano.

 

Jicho kwa wapiga kura

 

Tanzania ni mojawapo ya nchi zenye vijana wengi na ni wazi kuwa uteuzi wa Shaka na Makonda ulizingatia hilo pia. Kwamba kwa vile Mwenezi ni mtu anayeonekana zaidi kwa wapiga kura kuliko kiongozi mwingine yeyote wa chama kuondoa Mwenyekiti, ni muhimu wajihi na tabia zake vikafanana na vijana wa kizazi kipya.

 

Sioni uwezekano wa kuwa na Katibu wa Uenezi mwenye umri wa zaidi ya miaka 50 la sivyo awe ni aina fulani ya watu ambao ingawa umri ni mkubwa lakini akili na maarifa yao yanafanya waonekane vijana.

 

Na ni wazi kuwa anaweza kuwa mtu ambaye tayari anafahamika miongoni mwa Watanzania badala ya kuwa na mtu ambaye chama ndiyo kitaanza kumpa umaarufu. Ninapozungumzia umaarufu ninazungumzia kujulikana na Watanzania. Kuna kutofautiana kujulikana lakini kuna wastani ambao angalau unajua huyu anajulikana.

Kama ambavyo ilikuwa rahisi kwa Makonda ku ‘connect’ na kundi la watu wanaoamini katika aina yake ya siasa, CCM itajitahidi pia kuwa na mwenezi ambaye mara tu baada ya uteuzi wake, ataweza ku ‘connect’ na base yake kisiasa.

 

Kumpa nguvu Katibu Mkuu Vs Kufurahisha Makundi

 

Katibu Mwenezi anatakiwa kufanya kazi chini ya Katibu Mkuu. Katika makundi yaliyo ndani ya CCM, Makonda na Katibu Mkuu wa CCM, Emmanuel Nchimbi, wanatoka katika makundi tofauti. Kitabia, kimakuzi na kiutendaji, wawili hawa pia wako tofauti.

 

CCM inaweza kumwongezea nguvu Katibu Mkuu kwa kumpa Katibu Mwenezi anayeendana na haiba ya Katibu Mkuu. Kwamba Mwenezi anaweza kufanya lolote hata akiwa amefumba macho lakini akajua Katibu Mkuu hatakuwa na tatizo kwa sababu wanafahamiana.

 

Lakini uteuzi wa Makonda ulimwongeza nguvu Rais Samia kwenye chama kwa sababu alimpa nafasi mtu wa kundi lingine ndani ya chama. Kwa kumwongezea nguvu Katibu Mkuu na kumpa mtu atakayemfaa, Mwenyekiti anaweza kujikuta anaongezea nguvu kundi moja huku akiliacha kundi lingine na unyonge.

 

Lakini kuna mpango wa pili. Nao ni wa kumpa nafasi mtu kutoka kundi lisilo la Katibu Mkuu, lakini atakayeweza kufiti vizuri na bosi wake huyo pasi na mikwaruzano. Kwa kufanya hivyo, atakuwa ameua ndege wawili kwa kundi moja; ameondoa misuguano lakini pia bado amebaki na makundi yote chini ya mbawa zake.

 

Anatakiwa mtu, lakini ni mtu gani hasa?

 

Kwa zaidi ya miaka 200, siasa za dunia zilikuwa zimegawanyika kati ya wale walioamini katika siasa za mrengo wa kushoto na wale wa mrengo wa kulia. Tangu mwaka 2006, nikinukuu maneno ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, dunia sasa ina makundi mawili; wale wanaoamini kwenye uwazi na wale wa kujifungia.

 

Tangu aingie madarakani, Rais Samia ameipambanua serikali yake kama inayoamini katika uwazi na si kujifungia kama ilivyokuwa kwa mtangulizi. Maana yake ni kwamba wapinzani wa chama na serikali yake wanaruhusiwa kushambulia kwa hoja na vioja ili mradi hawavunji sheria.

 

Kinachotakiwa kwa mtu anayebeba chapa ya chama katika mazingira ya aina aliyotengeneza Rais Samia ni kuwa mtu anayeweza kujibu hoja kwa hoja na kufafanua kwa lugha rahisi uamuzi au hatua zilizochukuliwa na chama au serikali kwa wakati mwafaka.

 

Katika mfumo wa kujifungia, a la Blair (closed system), hoja zinapigwa nyundo au wakosoaji wanaonekana kama maadui au wasio wazalendo. Hii si namna ambayo open system inatakiwa kufanya.

 

Katibu Mwenezi wa CCM ya Rais Samia anatakiwa kuwa mtu ambaye vyama vya upinzani vinamhofia kufanya naye mdahalo kwa sababu anaaminika zaidi, ana taarifa zaidi, ana maarifa zaidi na anajua kuwasilisha taarifa alizonazo.

Kwa kufanya hivyo, siyo tu atakonga nyoyo za Watanzania, lakini atakisaidia chama na viongozi wake wa juu kupata ushindi kwenye uchaguzi ujao.

 

Lakini, hili la mwisho ni la kwangu zaidi. Siyo lazima CCM ilione lina maana.

 

Mwandishi ni msomi wa masuala ya Maridhiano ya Kisiasa  mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza. Anapatikana kwa email ya; ekamwaga57@gmail.com