Bahati na kupanda kwa Dk. Tulia Ackson

Picha: Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) akizungumza baada ya kupokewa katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma mara baada ya kurejea nchini akitokea nchini Angola alikoshinda uchaguzi wa taasisi hiyo ya mabunge duniani. Picha kwa hisani ya mtandao wa Zanzinews.

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

WAKATI Ikulu ilipotoa taarifa Septemba 14 mwaka 2015 kuwa Rais Jakaya Kikwete amemteua Mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Tulia Ackson, kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wengi walipokea taarifa hiyo kwa mshangao.

 

Sababu kubwa zilikuwa mbili; mosi kwamba kwa nini Rais aliamua kuteua mtu kushika nafasi hiyo ikiwa imebaki takribani mwezi mmoja tu kabla hajaondoka madarakani na pili ilihusu wasifu wa aliyepewa nafasi hiyo.

 

Kihistoria, Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinafahamika kwa kutoa wasomi maarufu ambao jamii inawafahamu. Katika wale waliokuwa wakionekana kama nyota wa UDSM kwenye kitivo hicho, jina la Dk. Tulia halikuwemo – walau nje ya viunga vya chuo hicho.

 

Nyota wa kitivo hicho nyakati hizo walikuwa watu kama maprofesa Palamagamba Kabudi, Hamudi Majamba, Gamaliel Mgongo Fimbo, Issa Shivji na wengine wa namna hiyo. Wakati huo nilikuwa nahariri gazeti la Kiswahili la kila wiki la Raia Mwema na hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kusikia jina la Tulia Ackson.

 

Katika nyota waliokuwa wazoefu zaidi, wasomi zaidi na maarufu zaidi kumzidi pale UDSM, jicho la Rais Kikwete lilimwona anafaa na kumpa wadhifa huo. Kikwete hajawahi kuzungumza hadharani kuhusu ni kwa nini alifanya uteuzi huo katika dakika za ‘lala salama’ za utawala wake na kwa nini alimteua mwanasheria huyo miongoni mwa wengi wengine waliokuwa wakifanya naye kazi UDSM.

 

Lakini kinachojulikana ni kuwa miezi miwili baadaye – Novemba 2015, Rais John Magufuli alimteua Tulia kuwa Mbunge wa Viti Maalumu; akiwa mbunge wa kwanza kuteuliwa kupitia nafasi 10 anazopewa Rais kuteua wabunge anaowataka.

 

Rais anaweza kumteua yeyote amtakaye kuwa mbunge lakini kitu kisicho cha kawaida kilichotokea kilikuwa ni hatua ya Tulia kuteuliwa kuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa nafasi ya Naibu Spika na hatimaye kushinda nafasi hiyo.

 

Kwa nini CCM kumpitisha Tulia hakikuwa kitu cha kawaida? Kuweka msingi wa hoja hii, ni muhimu kuangalia ni akina nani waliwahi kushika wadhifa huo kabla yake.  Na badala ya kurudi nyuma miaka mingi, tutazame tu Bunge la Tanzania tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi takribani miaka 30 iliyopita.

 

Bunge la Tanzania katika mfumo wa vyama vingi limewahi kuwa na manaibu spika wafuatao; Juma Akukweti, Philip Marmo, Anne Makinda, Job Ndugai, Tulia na Mussa Zungu. Karibu wote hao – ukiondoa Tulia, walikuwa na muda wa walau miaka 10 bungeni kabla ya kushika wadhifa huo.

 

Tulia – kwa bahati yake, hakuwahi kuwa mbunge kwa kuingia bungeni na kushiriki vikao walau kwa miezi mitatu kabla hajashika wadhifa huo. Hilo halikuwa jambo la kawaida na ilikuwa mara ya kwanza kutokea bungeni. Ilikuwa wazi kwamba kulikuwa na nguvu nje ya Bunge iliyotaka nafasi hiyo apewe mwanasiasa huyo.

 

Wakati alipokuwa Naibu Spika, likatokea pia tukio lingine ambalo halikuwa la kawaida kwa wengine waliopata kushika wadhifa wake. Miezi michache tangu kuanza kwa Bunge la 11, aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipata maradhi yaliyosababisha kwa kipindi kirefu alazwe hospitali nchini India.

 

Katika muda wote ambao Ndugai alikuwa India akijiuguza, Tulia ni kama alikuwa Spika kamili wa Bunge – kuna nyakati akihudhuria vikao vya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM); jambo ambalo waliomtangulia hawakuwahi kulipitia. Spika wa Bunge huhudhuria vikao vya Kamati Kuu kwa kupitia cheo chake hicho na hawezi kukasimu madaraka yake kwa msaidizi au mtu mwingine. Kwa watangulizi wake, nafasi ya Naibu Spika ilikuwa ni cheo tu cha kukaa kwenye kiti katika zile mara chache ambazo Spika mwenyewe ataamua kukuachia kiti wakati wa vikao vya Bunge au akiwa na dharura.

 

Kuna jambo lingine lisilo la kawaida ambalo limemtokea Tulia katika kupanda kwake madaraka ambalo si la kawaida. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, alijitosa kuwania ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini. Nchini Tanzania, Jimbo la Mbeya Mjini ni miongoni mwa majimbo yanayofahamika kwa kuunga mkono upinzani. Aliyekuwa anashikilia nafasi ya ubunge kwenye jimbo hilo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, alikuwa anaonekana mwenye nguvu jimboni kwake kuelekea uchaguzi ule.

 

Kilichotokea ni kwamba uchaguzi wa mwaka 2020 ulivurugwa sana kiasi kwamba kwa sasa hatuwezi kujua kwa hakika kama matokeo ya Mbeya Mjini – na kwingineko Tanzania, yangekuwa kama yalivyotokea endapo Rais asingekuwa Magufuli au vinginevyo. Uchaguzi ujao wa mwaka 2025 unaweza kuwa kipimo kizuri endapo Rais Samia Suluhu Hassan ataamua kusimama katika R zake nne.

 

Na wiki iliyopita, Tulia aliibuka kidedea katika uchaguzi wa kutafuta Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Kwa ambao tunafuatilia uchaguzi wa aina ya ule uliofanyika Luanda, Angola na kumpa Mtanzania huyo ushindi, ingekuwa vigumu kwa Tanzania kushinda endapo Rais angekuwa Magufuli.

 

Ili ushinde kwenye chaguzi za namna hii unahitaji kuwa na Rais anayetoka na mwenye mahusiano mazuri na wenzake. Unahitaji kutoka katika taifa linalokubali kuwa kwenye chaguzi za namna hiyo, kuna wakati unakubali kushindwa ili ashinde mwenzako ambaye naye atakuja kulipa wema wako wakati utakapomhitaji. Enzi za Magufuli, Watanzania kama Bernard Membe na Dk. Servacius Likwelile, waliwahi kukosa nafasi za kuwania katika taasisi za kimataifa kwa sababu serikali yetu wakati huo haikuwa na ‘mzuka’ na masuala ya uhusiano wa kimataifa.

 

Nikifupisha, ili Tulia awe Rais wa IPU leo, ilibidi mambo kadhaa yakae kwenye mstari mmoja kwa ajili yake. Kwanza Tanzania iwe na Rais aliyeamini katika vijana na asiye na woga wa kufanya uteuzi wa nafasi kubwa hata katika mwezi wake wa mwisho madarakani kama Kikwete, kuwe na Rais aliyemwamini na kumtaka awe Naibu Spika kwa gharama yoyote kama ilivyokuwa kwa Magufuli mwaka 2015 na pia Tanzania iwe na Rais ambaye aina yake ya diplomasia inaruhusu na inaunga mkono Watanzania wanaotaka kuwania nafasi kubwa katika vyombo vya kimataifa kama ilivyo kwa Samia.

 

Ni kama vile nyota zimejipanga zenyewe kwa Tulia katika wakati mwafaka; kwamba wakati IPU iko tayari kuongozwa na mwanamke kutoka Afrika – ikatokea kuwa yeye ni mgombea mwanamke kutoka katika nchi ambayo sasa imeanza kurejea katika zama zake kwenye duru za kimataifa.

 

Ni bahati peke yake?

 

Si haki kusema kwamba bahati pekee imemfikisha Tulia hapa alipo kisiasa wakati huu. Jambo la kwanza ni kwamba bila shaka ni mtu mwenye akili na maarifa na ndiyo sababu amefaulu katika ngazi zake zote kielimu mpaka kufika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 

Ili afike UDSM na kuonyesha uwezo wake kiasi cha kuonwa na mamlaka za uteuzi, Tulia alitakiwa kufaulu katika kila mitihani ya kitaaluma aliyokutana nayo kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu. Hajafika hadhi ya kuwa na PhD kwenye sheria kwa sababu ya bahati.

 

Lakini katika maisha yake mapya kama mwanasiasa, Tulia amejipambanua kama mpambanaji aliye tayari kuingia vitani na washindani wake. Si kazi rahisi kupambana na ‘Sugu’ katika mkoa ambao mfume dume umetamalaki kama Mbeya.

 

Mkoa wa Mbeya si mwepesi kwa wanawake. Kukupa usuli tu wa jambo hili, Tulia ndiye mbunge pekee mwanamke aliyeshinda uchaguzi kwa kupigiwa kura na wananchi katika mkoa huo kwenye uchaguzi wa mwaka 2020. Katika maisha yangu ya utu uzima, na nimejaribu kuangalia mitandaoni kujiridhisha, ni Tulia na Bahati Ndingo wa Mbarali aliyeshinda hivi karibuni, ndiyo wabunge wa Mbeya wanawake walioshinda uchaguzi kwenye majimbo.

 

Mwandishi ni msomi wa masuala ya Maridhiano ya Kisiasa  mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza. Anapatikana kwa email ya; ekamwaga57@gmail.com