Na Ezekiel Kamwaga
MWAKA 2015, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilipata mafanikio makubwa katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania. Kilipata takribani asilimia 40 ya kura zote zilizopigwa – kiwango ambacho kilikuwa hakijawahi kufikiwa na chama chochote cha upinzani katika historia ya taifa letu.
Kulikuwa na mambo mawili katika ushindi huo wa CHADEMA. Mosi ilikuwa ni ukweli kuwa kilishinda chini ya mwavuli wa UKAWA na pili kikawa chama cha kwanza cha upinzani kujikuta kina mawaziri wakuu wawili wastaafu ndani ya Kamati Kuu yake.
Nyuma ya ushindi ule mkubwa alikuwa ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe. Ni yeye ndiye aliyekubali chama kimpokee aliyekuja kuwa mgombea urais wake, Edward Lowassa, na ni yeye pia aliyekuwa tayari kuruhusu kuingia makubaliano na vyama vya CUF, NCCR Mageuzi na NLD kuunda UKAWA.
Kulikuwa na tatizo moja kwenye mafanikio hayo makubwa ya CHADEMA na Mbowe. Kwa kuruhusu Lowassa – ambaye viongozi wa chama hicho walitumia takribani muongo mzima kumshutumu kwa tuhuma za ufisadi, kuwa mgombea wake, kilikuwa kimejiondolea kuaminika kwa baadhi ya watu.
Katika andishi lake mashuhuri la Political Decay la mwaka 1965, Profesa Samuel P. Huntington, ameandika vizuri sana kuhusu ukuaji wa taasisi kisiasa. Kwamba kuna mambo ambayo taasisi (soma chama cha siasa) yanaweza kusaidia kujenga chama lakini yakabomoa upande mwingine. Au yakabomoa kwingine na kujenga kwingine.
Mafanikio ya CHADEMA ya mwaka 2015 kwa kumtumia Lowassa yaliwaongezea kura na ushawishi kwa upande mwingine lakini yalibomoa upande mwingine. Na hakuna ushahidi wa wazi wa kubomoka kama kitendo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa, kuamua kujiondoa kwenye chama hicho.
Baada ya uchaguzi ule, Mbowe alitakiwa kufanya mambo yafuatayo. Mosi alitakiwa kuachia Uenyekiti wa chama na kuchukua nafasi nyingine kama ya Ukatibu Mkuu. Ilitakiwa chama – wakati ule, ampe Lowassa aliyekuwa mgombea urais wakati wa mafanikio makubwa ya chama hicho.
Kumpa Lowassa kulikuwa na faida mbili; mosi Mbowe angekuwa ameachia ngazi katika wakati wa juu kabisa kwa chama chake akiwa na heshima na hadhi ya kipekee. Lakini angekuwa ametoa fursa kwa Lowassa na wageni wengine walioingia CHADEMA kujiona si wakuja.
CHADEMA ya mwaka 2017 ilitakiwa kuwa na Mwenyekiti Lowassa, Katibu Mkuu Mbowe na pengine ingemfanya Halima Mdee kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama. Ingawa wote wanatoka Kaskazini mwa Tanzania, naamini hilo lisingeifanya CHADEMA kuonekana ya kikabila kwa sababu viongozi hao wamevuka siasa za kikabila.
Naamini kwamba kama Lowassa angekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, angetafuta jukumu na namna ambayo ingemfanya Sumaye abaki CHADEMA. Na kwa vyovyote vile, haingekuwa rahisi kwa yeye kushindwa kuelewana na Maalim Seif Shariff Hamad ili ahamie kwenye chama chake badala ya ACT Wazalendo baada ya maji kukorogeka ndani ya CUF.
Isivyo bahati ni kwamba Mbowe aliamua kuendelea kuwa Mwenyekiti na badala ya kuwakumbatia akina Lowassa, alifanikisha wanasiasa hao kushindwa maisha ya upinzani na hatimaye kurejea CCM. Mbaya zaidi alishindwa kumshawishi Maalim Seif ahamie CHADEMA.
Pengine swali ambalo unaweza kuwa unajiuliza sasa ni kwamba kwa nini Mbowe alifanya makosa. Naamini kuwa Mbowe ana shida na watu anaomini wanaweza kuwa wanatishia nafasi yake ya uongoi ndani ya chama hicho.
Udhaifu huo haukuwa unafahamika hadi wakati aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, alipoamua kuwania nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho dhidi yake. Mbowe alitumia cheo na ushawishi wake wote kuhakikisha Zitto siyo tu hashindani naye tena mwaka 2014, lakini asiwe hata ndani ya CHADEMA wakati huo.
Niliwahi kuambiwa kwamba Mbowe aliahidi baadhi ya wazee wa CHADEMA kwamba atashikilia wadhifa huo hadi mwaka 2014 na angemwachia Zitto au mwengine aliyefaa wakati huo. Hakufanya hivyo na ndiyo sababu Tundu Lissu hawezi kuamini kuwa Mbowe ataachia ngazi mwaka 2029 kama alivyoahidi wiki hii.
Anachojua Lissu kwa sasa ni kwamba mara baada ya kukamilika kwa uchaguzi huu, Mbowe atafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba Lissu hatampa taabu tena mwaka 2029 – awe ndani ya CHADEMA au akihama. Ameona yaliyompata Zitto huko nyuma.
Udhaifu huu wa Mbowe – au tuseme woga, ulionekana pia mwaka 2016. Mara baada ya Slaa kuachia Ukatibu Mkuu na wana CHADEMA wakiwa na majina kadhaa kichwani ya watu waliokuwa wanaweza kupewa nafasi hiyo, Mbowe aliibuka na jina la Dk. Vincent Mashinji.
Mashinji hakuwa na umaarufu wowote nje ya CHADEMA. Kwa chama ambacho Katibu Mkuu wake aliyepita alikuwa na sifa ya kuwa mgombea urais, ilitarajiwa kuwa nafasi ya Slaa ingejazwa na mtu mwingine maarufu ndani na nje ya chama.
Uteuzi wa Mashinji ulitoa ujumbe mmoja tu kwa wana CHADEMA, kwamba Mwenyekiti hakuwa anataka tena kuwa na Katibu Mkuu ambaye watu wangemwona kama mbadala wake au mwenye sifa za kuwa mgombea urais kupitia chama hicho.
Hilo, pasi na shaka, pengine ndiyo sababu iliyofanya iwe ngumu kwa Sumaye na Lowassa kudumu ndani ya CHADEMA. Na pengine ndiyo sababu inayofanya watu wengi wenye maarifa na uwezo mkubwa kutoshika nyadhifa kubwa au kuwa karibu na Mbowe kwenye miaka ya karibuni.
Kuporomoka kwa taasisi
Mwanafunzi wa Huntington, Francis Fukuyama, naye amefanya maboresho ya profesa wake huyo kwa kuandika kiundani pia kuhusu kuoza au kuporomoka kwa taasisi za kisiasa. Kwa mujibu wa Fukuyama, ukitaka kujua kama taasisi inapanda au kuporomoka unatakiwa kutazama mambo matatu ambayo mimi huziita C tatu; competence, credibility and corruption. Utaona hali ya Chadema kwa kuangalia vigezo hiyo.
Katika competence, Fukuyama ameandika unapaswa kuangalia je taasisi inaongozwa na watu walio bora kiakili na kimaarifa kuliko zamani? Kwa CHADEMA, unatakiwa kurudi miaka 15 nyuma na kuangalia nani walikuwa wanamzunguka Mbowe kwenye Kamati Kuu.
Kamati Kuu ya Mbowe, Lissu, Zitto, Prof. Kitila Mkumbo, Prof. Mwesiga Baregu, John Mnyika, Prof. Abdallah Safari, Slaa na wengine wa namna hiyo inafanana na Kamati Kuu ya sasa ya CHADEMA?
Katika credibility, Fukuyama ameandika kuhusu kama maneno ya viongozi wa chama hicho yanaaminika kwa wanaowasikiliza. Je, imani ya wananchi na wanachama kwa CHADEMA inafanana na imani yao miaka kumi au hata mitano tu iliyopita?
Katika corruption, Fukuyama anazungumzia rushwa kugubika taasisi. Ni hivi karibuni tu, Lissu alitoa tuhuma kuhusu chama hicho kugubikwa na rushwa kwa viongozi wa ngazi za juu kabisa. Taasisi iliyogubikwa na rushwa, ni taasisi inayoporomoka.
Kinachoendelea sasa CHADEMA kwenye uchaguzi huu kina nasaba za moja kwa moja na makosa ambayo Mbowe ameyafanya katika kipindi cha miaka 20 ya uongozi wake – hasa kumi iliyopita.
Ezekiel Kamwaga ni Mwandishi wa Habari na Mchambuzi wa Masuala ya Siasa. Ana Shahada ya Uzamili katika Siasa za Afrika (MSc Politics of Africa) aliyoipata katika Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS)