Namna Move Forward walivyoshinda uchaguzi wa Thailand

Maelezo ya picha:

Mgombea wa chama cha Move Forward, Pita Limjaroenrat, (katikati) akiwashukuru wapiga kura wake kwenye eneo la Mnara wa Demokrasia jijini Bangkok, walipokusanyika kusherehekea ushindi wa chama chao kwenye uchaguzi uliofanyika Mei 15, mwaka huu. Picha kwa hisani ya gazeti la Times la Uingereza. 

 

Na Francesca Regalado, Bangkok

 

VYAMA vya upinzani vimepata ushindi usiotarajiwa katika Uchaguzi Mkuu wa Thailand uliofanyika Mei 15 mwaka huu. Ushindi wa chama cha Move Forward ilikuwa ni kauli thabiti dhidi ya siasa za kujuana na zinazoongozwa na ushawishi wa jeshi la nchi hiyo.

 

Chama hicho kilishinda kwa kufanya kampeni iliyokwenda kinyume na siasa zinazoongoza taifa hilo kwa muda mrefu na ndizo zilizokipa ushindi hata katika maeneo yaliyoonekana kuwa hayapenyeki kabla ya uchaguzi.

 

Kwa mfano, eneo lenye wapiga kura wengi la Kaskazini na Kaskazini Mashariki lilikuwa likionekana kama ngome ya chama tawala cha Pheu Thai huku eneo la Kusini mwa Thailand likichukuliwa kama ngome ya chama cha kihafidhina cha Democrat lakini kote huko Move Forward kimepata ushindi.

 

Katika uchaguzi huo, Move Forward kilipata viti 32 kati ya 33 katika mji wa Bangkok, unaojulikana kama ngome ya chama cha Democrat. Nako Kaskazini, kilishinda viti 19 – hadi katika mji alikozaliwa kiongozi wa chama cha Pheu Thai, Thaksin Shinawatra. Ilifanikiwa kushinda viti vyote vitatu katika eneo la Kusini la Phuket – ngome ya wahafidhina.

 

“Kuna mikakati kadhaa ilitumika iliyowezesha upinzani kushinda,” anasema Decharut Sukkumnoed, ambaye ni Mkurugenzi wa Sera wa Move Forward. “Kwanza, walikuwa na msimamo wa kisiasa ulioeleweka kirahisi. Pili walikuwa na sera zilizoshiba na mipango mikubwa ya mambo ya kufanya.”

 

Sasa, kampeni ngumu zaidi ya kushinda katika uchaguzi wa Seneti ambayo huteuliwa na Jeshi inaanza. Pamoja na wabunge wa kawaida 500, Katiba ya Thailand inataka pia maseneta 250 washiriki katika uchaguzi wa kumpitisha Waziri Mkuu. Muungano wa wapinzani wa Move Forward unatarajiwa kuwa na wabunge takribani 310. Hata hivyo, ili kiongozi wake mwenye umri wa miaka 42, Pita Limjaroenrat, awe Waziri Mkuu, anahitaji kura nyingine 70 kutoka kwa wabunge na maseneta.

 

Pasipo Muungano, Move Forward peke yao, walishinda viti 152 katika uchaguzi huo – ikiwa ni mara ya pili kushiriki uchaguzi tangu kilipoanzishwa mwaka 2018 wakati huo kikijulikana kwa jina la chama cha Future Forward. Waanzilishi wa chama hicho walikuwa ni mfanyabiashara bilionea, Thanathorn Juangroongruangkit, na mwanazuoni wa masuala ya sheria, Piyabutr Saengkanokkul. Kwenye uchaguzi wa mwaka 2019, chama hicho kilipata viti 81.

 

Chini ya mwaka mmoja baadaye, chama hicho kilifutwa kupitia uamuzi wa Mahakama ya Katiba na zaidi ya nusu ya wabunge wake walifutwa pia. Hata hivyo viongozi wa chama hicho hawakukata tamaa bali walijipanga upya na kuanzisha chama hiki cha sasa – wakishirikiana na taasisi ya Progressive Movement Foundation, inayotoa huduma za dawa, maji safi na miradi mingine ya kijamii. Huu ndiyo ushirikiano uliozaa matunda.

 

Jambo lingine lililokipa nguvu chama cha Move Forward kuelekea uchaguzi wa mwaka huu ni wabunge wake wachache waliosalia bungeni ambao walijipambanua kwa kuzungumzia masuala muhimu na nyeti katika taifa katika muda wote waliokaa bungeni.

 

Wengi wa waliokuwa wagombea wa chama hicho hawakuwa wanasiasa waliozoeleka na walikuwa wakifanya kampeni za kutembelea nyumba kwa nyumba kuelezea sera za chama chao. Kupitia kampeni hizo, wagombea hao walikuwa wakizungumza kukonga moyo wa yule waliyekuwa wakizungumza naye wakati huo badala ya ajenda za jumla.

 

Moja ya mbinu iliyofanikiwa zaidi kwenye kampeni hizo za uso kwa uso na wapiga kura ni kuwashawishi kuchagua ama mgombea au chama kulinganisha na mrengo aliokuwa akiuonyesha mpiga kura mtarajiwa.

 

“Kama mpiga kura akisema anapenda chama cha Pheu Thai, tulikuwa tunajaribu kumweleza kuwa kuna machaguo mawili mbele kwenye kupiga kura; anaweza kumpigia mgombea wa chama chake na anaweza kutupigia mgombea wetu kwenye nafasi nyingine,” anasema Charas Koonkainam, mbunge wa Move Forward kutoka jimbo la Chonburi.

 

Kikifahamu kwamba kina fedha za kampeni kidogo kulinganisha na vyama vikongwe, kampeni za Move Forward zilijikita kwenye maeneo ya mjini zaidi kwenye kila jimbo. “Tulijikita kwenye maeneo ya mijini na vyuo vikuu. Tulifahahamu kwamba kama wanafunzi wangetuelewa, wangewashawishi wazazi wao watupigie kura,” anasema Nitipon Piwmow, aliyeongoza kampeni za chama hicho Kaskazini mwa taifa hilo.

 

Changamoto kubwa iliyokuwa inakikabili chama hicho ilikuwa ni madai kutoka kwa baadhi ya wazee na watu wazima kuwa chama hicho kilikuwa na mrengo mkali unaovunja mil ana desturi za taifa hilo. Moja ya mambo yenye utata yaliyozungumzwa na chama hicho ilikuwa ni kuahidi kupunguza adhabu kwa watu wenye kesi za kumkashifu Mfalme wa Taifa hilo na pia kupendekeza Mfalme mwenyewe ndiye ashitaki kama anaona ametukanwa.

 

Pia chama hicho kilipata bahati ya kuwa na mgombea mwenye mvuto na uwezo wa kujieleza mbele za watu. Umaarufu wake uliongezeka zaidi pia kwa vile viongozi wa vyama vingine walikuwa wakimkwepa kwenye midahalo na kumpa yeye nafasi kubwa ya kuzungumza na kusambaza vipande vya sauti vya hoja zake za msingi.

Makala haya yalichapwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Nikkei Asia na hii ni tafsiri isiyo rasmi ya lugha ya Kiswahili. Unaweza kuisoma katika lugha ya Kiingereza kupitia https://asia.nikkei.com/Politics/Thai-election/How-Move-Forward-shocked-Thailand-s-old-guard.