Na Ezekiel Kamwaga
MAJUZI nilihudhuria harusi moja jijini Dar es Salaam na wakati muda wa kwenda kula ulipofika, MC akatania “wakati tunapokwenda kupakua chakula, msisahau ushauri wa Profesa Janabi”. Ukumbi mzima ulilipuka kwa vicheko. Ni kama kila mtu alikuwa anamjua Profesa Mohamed Janabi na ujumbe wake kwa jamii yake.
Kwa hakika, katika mwaka 2023, hakuna mwanataaluma wa Kitanzania ambaye amejulikana kazi yake na kugusa maisha ya watu kumzidi Profesa Janabi. Mkurugenzi Mtendaji huyu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) amejipambanua kwa mafunzo na ushauri wake kuhusu umuhimu wa watu kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanayoharibu maisha ya Watanzania na dunia kwa ujumla.
Siku ile kwenye harusi, nilijiuliza swali moja, itakuwa vipi kama tungekuwa na akina Janabi kwenye masuala mengine muhimu? Vipi kama tungekuwa na mtu kama Janabi kwenye kilimo – anayezungumza lugha ambayo wakulima na wasio wakulima wangemuelewa na kufanya kinachotakiwa?
Kama tungekuwa na kiongozi wa aina ya Janabi aliyejitolea kufanya hivyo kwenye masuala ya kufundisha watu kuweka akiba na kuwekeza, kama angekuwepo wa aina yake kwenye kufunza watoto malezi ya kuwa watu wenye maarifa na umakini, naamini tungekuwa mbali kama nchi.
Na kuna watu wanaamini pengine Janabi anadhihakiwa kwenye mitandao ya kijamii kupitia vikatuni na maneno mbalimbali. Mimi naamini tofauti. Naamini Janabi ameeleweka kwa Watanzania. Anapendwa na kuwa kampeni yake imeanza kubadili utaratibu wa kula na kulinda afya zetu. Pengine ni vigumu kupima kwa kiasi gani lakini ukweli uko wazi, daktari huyu ameeleweka na kuwa na faida kwenye jamii yetu.
La mwisho ni kuwa MNH inazidi kupanda hadhi chini ya uongozi wake. Muhimbili inazidi kubadilika kuanzia mwonekano wake, huduma, ubobezi na ufanisi. Maneno yake mdomoni, yanaendana na vitendo vyake kazini.