Magufuli alishinda au Lowassa alipoteza 2015?  

Picha: Hayati Rais John Magufuli akisalimiana na Edward Lowassa katika mojawapo ya matukio ya kitaifa. Picha ya Ikulu

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

MAJUZI nilikuwa nasikiliza Podcast ya The Rest is Politics kutoka nchini Uingereza na mada iliyozungumzwa ilinivutia. Watangazaji wa kipindi hicho, Alastair Campbell na Rory Stewart waliulizana swali moja; Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1997 nchini kwao, Tony Blair alishinda uchaguzi au John Major alishindwa?

 

Mwishoni walikubaliana kwamba Tony alishinda uchaguzi ule kwa sababu kwa mazingira ya wakati ule yalivyokuwa, haingekuwa rahisi kwa Major kushinda. Ni bahati nzuri pia kwamba kwenye mahojiano ya wawili hao na Major mwenyewe kwenye Podcast ya LEADING, Major mwenyewe alikubaliana na uchambuzi wa wawili hao.

 

Jambo hilo lilinikumbusha Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2015 uliomwingiza madarakani hayati Rais John Magufuli. Katika uchaguzi huo – pengine mkali zaidi katika historia ya uchaguzi wa vyama vingi nchini kwetu, Magufuli alishindana na Edward Lowassa aliyewania nafasi hiyo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

 

Baada ya kumalizika kusikiliza Podcast ile, nilijiuliza swali moja papo hapo; kwamba, je ni Magufuli aliyeshinda uchaguzi ule au Lowassa aliyepoteza? Hili ni swali ambalo makala haya yatajaribu kulijibu na kutoa hitimisho langu mwishoni.

 

Nadhani ni muhimu nikafafanua kuhusu uteuzi huu wa maneno ya kushindwa au kupoteza uchaguzi. Mgombea aliyeshinda uchaguzi ni yule ambaye vigezo vyote vya uchaguzi vilimpa nafasi ya kushinda na kwamba hakukuwa na uwezekano wa kushindwa. Upande mwingine wa sarafu ni yule aliyepoteza ambapo kwangu ni yule ambaye alikuwa na uwezekano wa kushinda lakini kwa sababu ya mapungufu fulani, akashindwa kwenye uchaguzi.

 

Safari ya Magufuli

 

Mwezi Januari mwaka 2015, niliandika habari exclusive kwenye gazeti la Raia Mwema, kueleza kwamba Magufuli ana mpango wa kuwania Urais kupitia CCM mwaka huo. Nakumbuka mmoja wa marafiki zangu waliokuwa na nyadhifa kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais wakati ule, alinipinga hadharani kupitia mtandao wa facebook akisema habari ile ilikuwa ya kutunga.

 

Kwa maelezo yake, Raia Mwema – wakati ule, ilikuwa inatafuta wagombea wa ‘kutunga’ ili tu kuzuia Lowassa asiwe mgombea wa CCM. Ambacho hakufahamu ni kwamba taarifa ile ilitoka katika vyanzo vyangu vya kuaminika nchini Kenya na kimsingi taarifa zile nilizipata kwa bahati tu kwa vile hazikupaswa kutolewa hadharani wakati ule.

 

Nakumbuka Magufuli mwenyewe alinipigia simu – enzi hizo akiwa Waziri wa Ujenzi, kuniuliza ilikuwaje tukaandika habari ya mazungumzo ambayo sisi hatukuwepo. Nikamwambia mtandao wetu ni mpana sana kiasi kwamba tupo kila mahali alipo. Aliishia kucheka tu lakini haikuwa ajabu pia kwamba sisi tukawa sehemu ya magazeti mawili tu ya Tanzania ambayo aliyapa mapema taarifa za siku aliyokuwa anakwenda kuchukua fomu Dodoma.

 

Mpaka wakati ule, wengi wa wafuatiliaji wa siasa za Tanzania walikuwa wakimwona Magufuli kama mtu aliyekuwa anajipanga kuwa Waziri Mkuu ajaye wa Tanzania. Ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) majina yaliyokuwa yanapewa nafasi zaidi ni Lowassa – kabla hajahamia Chadema baada ya kukatwa kwenye kinyang’anyiro cha chama hicho, hayati Bernard Membe, Profesa Mark Mwandosya, January Makamba na wengine walioonekana kuwa na nguvu ndani ya chama tawala.

 

Hata wakati ilipoonekana waziwazi kuwa Magufuli atapitishwa na CCM kuwa mgombea wake, Mwandosya aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akihoji ni kwa vipi chama hicho kitakuwa na mgombea ambaye hakuwahi hata kuwa kiongozi wa kata wa chama hicho? Mpaka leo, naamini kwamba kama CCM isingekata jina la Lowassa, hakungekuwa na mwana CCM mwingine wa kushindana naye ndani ya chama hicho kwa kura. Namna pekee ya kuzuia Lowassa asiwe mgombea wa chama hicho wakati ule ilikuwa ni kumkata jina lake. Kwa maana hiyo, Magufuli alikuwa ni mnufaika wa kukatwa kwa Lowassa.

 

Safari ya Lowassa

 

Kuondoa Jakaya Kikwete mwaka 2005, hakujawahi kuwa na mgombea urais katika historia ya Tanzania kupitia CCM aliyewahi kuwa amejiandaa kuwania nafasi hiyo kumzidi Lowassa. Maajabu ya aina ya siasa za mbunge huyo wa zamani wa Monduli yalikuwa kwamba hata baada ya ajali ya kisiasa ya Richmond na kujiuzulu kwake Uwaziri Mkuu, alibaki kuwa na nguvu na ushawishi pasipo cheo chochote.

 

Siku ile kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mwaka 2015 ambapo nilikuwa ukumbini kama sehemu ya waandishi wa habari tulioalikwa, Lowassa aliyeimbwa na wajumbe “Tuna Imani na Lowassa” hakuwa na cheo chochote kikubwa serikalini. Kimsingi ule ulikuwa ni uasi dhidi ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania wakati ule, Jakaya Kikwete.

 

Wakati wanasiasa wengine wangekuwa wamemalizwa kisiasa baada ya tukio kubwa kama Richmond, Lowassa – taratibu, alibadili aina ya ufanyaji wake wa siasa, akitumia muda wake mwingi kutengeneza mtandao wake wa kisiasa uliohusisha hadi watu wasio wanasiasa wakiwamo viongozi wa kidini. Kuelekea Mkutano Mkuu wa CCM mwaka 2015, Urais ulikuwa mikononi mwa Lowassa.

 

Lowassa alikuwa na faida kadhaa ambazo washindani wake hawakuwa nazo. Mosi, alikuwa tayari na mtandao wa kisiasa waliouanzisha na Kikwete tangu walipotaka kuwania urais kwa mara ya kwanza mwaka 1995. Kwa kiasi kikubwa, timu ya kampeni iliyomwingiza madarakani Kikwete mwaka 2005 ilikuwa na uhusiano wa karibu zaidi na Lowassa kuliko hat ana Kikwete.

 

Ni timu hiihii ambayo – kwa kiasi kikubwa ilibaki naye, ndiyo ambayo ilikuwa naye kuelekea 2015. Tofauti na wanasiasa wengine wa kizazi chake, Lowassa alikuwa na kipaji kikubwa cha kudumu na marafiki zake wa kisiasa. Kama ulikuwa upande wake mwaka 2000, mara nyingi bado ungebaki kwake mwaka 2020. Kama kuna sifa ya kipekee ya Lowassa kisiasa, sifa hiyo ni uwezo wake wa kuatamia watu au kundi lake kisiasa.

 

Jambo la pili lililomfanya Lowassa awe na faida kulinganisha na wenzake ni uwezo wake wa kukusanya fedha kutoka kwa rafiki zake. Lowassa binafsi si mtu fukara lakini hakuwa mfadhili wa kampeni zake za kisiasa. Katika wigo wake wa ushawishi, alihakikisha ana marafiki wanaoweza kuchangia kiasi kikubwa cha fedha kulinganisha na wengi wa washindani wake.

 

Faida ya tatu ilikuwa ni kukifahamu chama, serikali na nchi kwa ujumla ipasavyo. Lowassa ni kada halisi wa CCM kwa mafunzo na kwa kukitumikia. Kukulia kwake kuanzia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), utumishi wake Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na utumishi wake serikalini kufikia cheo cha Waziri Mkuu, kulimfanya awe na sifa za kipekee kulinganisha na washindani wake wote wengine.

 

Kushinda na kupoteza

 

Ndani ya CCM, Lowassa alikuwa na kura za kutosha kushinda. Kama CCM ingempitisha Lowassa kuwa mgombea wake, nina uhakika bado CCM ingeshinda katika uchaguzi wa mwaka 2015. Sheria za uchaguzi zilizopo, Katiba iliyopo, mifumo ya kisiasa iliyopo na taasisi za kusimamia uchaguzi zilizopo Tanzania wakati ule na sasa bado zinaipa faida CCM kuliko upinzani.

 

Ndani ya CCM, Magufuli hakuwa na kura za kutosha lakini angeweza tu kushinda endapo mazingira yangehitaji “mgombea wa mwafaka” – mtu ambaye pande mbili hasimu hazina shida naye. Baada ya Lowassa kukatwa na wafuasi wake kuamua kwamba hawatampa Membe kura kwa madai kuwa ndiye alikuwa chaguo la Kikwete, mlango ulikuwa wazi kwa Magufuli.

 

Kwa mantiki hii, ili aupate urais wa Tanzania, Lowassa alitakiwa ashinde kwanza vita yake ndani ya CCM iliyochemka kwa takribani muongo mmoja ili jina lake lipitishwe. Kwa Magufuli, hakukuwa na namna ya yeye kupenya isipokuwa kwa kutamani walio juu yake wavurugane ili yeye apenye kati.

 

Kwa Lowassa, kuna vitu viwili naamini vilichangia kushindwa kwake ndani ya CCM; mosi ni uhusiano wake mbaya na Rais Kikwete na pili ni kushindwa kuweka mezani dili la kisiasa ambalo waliokuwa hawamtaki ndani ya chama chake na kwenye “mfumo” wangeshindwa kulikataa. Rais wa Tanzania anayemaliza muda wake huwa hana ushawishi wa kutosha kumweka amtakaye achukue nafasi yake lakini akisema “yeyote apate isipokuwa huyu” hilo huwa ni tatizo kubwa.

 

Katika vitu ambavyo bado naendelea kuvitafiti hata wakati nikiandika makala haya, ni kwamba ilikuwaje kwa mtu ambaye amelelewa na CCM, akawa Ofisa wa Jeshi, akawa mtumishi wa serikali na kupanda kisiasa hadi kuwa Waziri Mkuu, alishindwa kuweka mezani dili ambayo ingekuwa ngumu kukataliwa hata na wale waliokuwa hawamtaki?

 

Labda kuna baadhi ya tabia za watu wa karibu yake zilianza kuwatisha wale wanaoendesha nchi yetu nyuma ya pazia? Kulikuwa na tishio la kuharibika kwa utulivu au utangamano wa kisiasa endapo angekuwa Rais? Au baadhi ya maamuzi yake magumu aliyochukua kisiasa hayakufanywa kwa wakati sahihi? Pengine alihama chama kwa kuchelewa? Pengine angetumia muda aliokaa nje ya serikali baada ya kujiuzulu Uwaziri Mkuu kuengaenga uhusiano wake na Kikwete na wengine walio nyuma ya pazia kwenye dola yetu?

 

Hitimisho langu mimi ni kwamba Lowassa alipoteza mwenyewe urais kupitia kinyang’anyiro cha ndani ya CCM. Urais ulikuwa mkononi mwake na yeye ndiye aliyekuwa namba moja kwenye mstari kufikia Julai 2015. Kwa minajili hii, alipoteza nafasi ya urais kama tutazingatia mchakato wa ndani ya CCM.

 

Lakini, kama tutaangalia uchaguzi wa 2015 kati yake na Magufuli, mshindi alikuwa ni mgombea wa CCM. Hii ni kwa sababu, kwa mazingira ya Tanzania – tofauti na ilivyo Uingereza ya 1997 au sasa, mgombea wa chama tawala ana nafasi kubwa ya kushinda kumzidi yule wa upinzani.

 

Huo ndiyo ukweli wa hizi nchi zetu zinazoitwa – katika lugha ya wasomi wa Sayansi ya Siasa, Competitive Authoritarian, kwamba ingawa ni nchi za kidemokrasia kwa vigezo vya kimagharibi, ukweli ni kwamba mzani unaelemea upande wa chama kilicho madarakani.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa  mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha SOAS nchini Uingereza.