Na Ezekiel Kamwaga
KATIKA kipindi cha takribani miaka 60 ya nchi yetu – na pengine duniani kwa ujumla, P mbili; Perfomance and Politics (Siasa na Utendaji), zimeamua uwepo wa waziri au mawaziri kwenye Baraza la Mawaziri.
Rais anaweza kumbadili au kubadili mawaziri kwa sababu ya utendaji wao mbovu au kwa sababu za kisiasa. Wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete – kwa mfano, kuna mawaziri mpaka waliitwa majina ya “mizigo” kwa sababu ya utendaji wao usioridhisha na waliondolewa kwenye baraza.
Wakati huohuo wa Kikwete, alilazimika kukubali kujiuzulu kwa Edward Lowassa kama Waziri Mkuu ingawa wakati huo alikuwa mmoja wa mawaziri waliokuwa wakijulikana kwa utendaji usio na shaka. Utendaji uliondoa ‘mawaziri mizigo’ wakati huo wa JK na siasa za wakati ule zilimwondoa Lowassa.
Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan wiki hii hayana tofauti na mengine yaliyofanywa na watangulizi wake kwenye historia ya nchi yetu. Vigezo ni hizo P mbili tu.
Pamoja na mabadiliko haya ya karibuni kugusa takribani mawaziri watano – January Makamba, Nape Nnauye, Deo Ndejembi, Jerry Silaa na Ridhiwani Kikwete, majina mawili ya kwanza ndiyo ambayo yametawala mijadala inayoendelea.
Niseme vitu viwili kabla sijazama mbali kwenye uchambuzi wangu. La kwanza ni kwamba Makamba aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, ni rafiki yangu. Na pili ni kwamba shingo upande ninaandika nikijua ni rahisi watu kutanguliza urafiki wangu naye badala ya kusoma kilicho kati ya maandishi.
Lakini baada ya kusoma baadhi ya chambuzi zilizofanywa na baadhi ya waandishi wenzangu – hasa ule wa Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), naamini wasomaji wana haki ya kupata taarifa sahihi.
Katika miezi 10 ya January kwenye wizara hii, niliona mambo mengi nikiwa kwenye viti vya mbele kabisa. Mengi ambayo nitaeleza humu ni yale ambayo niliyashuhudia kwa macho yangu au kuyasikia yakizungumzwa .
Swali ambalo nitajaribu kulijibu humu ni moja; Je, mabadiliko yaliyotokea hivi karibuni – hasa kwenye Wizara ya Mambo ya Nje, yametokana na utendaji au siasa?
Jambo moja muhimu la kulisema mapema ni kwamba nitakachofanya hapa ni kuchambua tu kutokana na hoja zilizo mezani lakini anayejua sababu hasa ya kufanya mabadiliko ni Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe. Yeye anasikia na kuona vitu vingi kuliko mtu mwingine yeyote hapa nchini na ana mamlaka ya kufanya mabadiliko pale anapoona inafaa. Ni haki yake.
UTENDAJI
Katika uchambuzi wake alioupa kichwa cha habari cha “Rais Samia ana maamuzi magumu” (www.jamhurimedia.co.tz/rais-samia-ana-maamuzi-magumu), Balile ametoa sababu kubwa mbili za kuonyesha kwa nini January ameondolewa. Mosi, kwamba hakuwa akitangaza ziara za Rais nje ya nchi na pili, tabia ya kupenda ukuu na kujitukuza.
Balile amefananisha utendaji wa mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Uingereza; Antony Blinken na David Lammy, kama kielelezo cha January kutotimiza vema majukumu yake. Balile ameenda mbali kwa kusema January alitakiwa awe anafanya mikutano hata mitatu kwa siku na waandishi kwenye ziara za Rais.
Kuna vitu kadhaa vya upotoshaji kwenye sababu hizi za Balile. Kwanza, ni kuwa January ndiye waziri wa kwanza wa mambo ya nje kwenye serikali ya Rais Samia – na pengine kwenye serikali iliyotangulia — kuweka utaratibu wa kuzungumza na waandishi wa habari kueleza kuhusu kila ziara.
Ukiingia mtandaoni kumbukumbu ziko za kutosha. Mkutano wa kwanza ulikuwa ni Oktoba 5 mwaka huu wakati alipotangaza ziara ya kitaifa ya Rais Samia nchini India (www.habarileo.co.tz/rais-samia-kufanya-ziara-india), ambayo ndiyo ilikuwa ya kwanza tangu January apewe wizara hiyo.
Inaonekana ni mbali kidogo lakini ni muhimu kuwa na muktadha. Kabla ya kwenda India, Rais alikuwa na ziara nyingine Qatar ambayo haikutangazwa kabisa kabla na ilishuhudiwa tu Rais akiwa huko. Huo ni wakati ambao kila ziara za Rais zilianza kuzungumzwa vibaya kuwa hazina faida.
Ninaamini January aliamua kuweka utaratibu wa kuzungumza kabla kwa lengo la kutoa sababu na kuonyesha faida za ziara za Rais. Ilikuwa bahati nzuri ni India ambako Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu na Wizara ya Mambo ya Nje zilikuwa na timu za waandishi zilizoifanya ziara hiyo kuwa ya mafanikio makubwa kihabari.
Sina hakika kama kuna ziara ya Rais Samia ughaibuni ambayo ilitangazwa na kuzungumzwa vizuri kuliko ziara yake hiyo ya India. Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, alipambania sana suala la waandishi kuwemo kwenye ziara za Rais lakini kwa sababu za kirasimu jambo hilo halikuanza mapema. Serikali ya Magufuli ilikuwa na hali ya kutoamini waandishi wa habari na hayo ndiyo mazingira aliyoyakuta Zuhura wakati anaingia Ikulu.
Ni muhimu kueleza mchango wa Waziri Rajabu ambaye alipoteuliwa kuwa Katibu wa Rais na kuingia Ikulu, ndipo urasimu ulipoanza kuondoka na mambo kwenda kwa kasi inayotakiwa. Ni yeye ndiye aliyewezesha kutimia kwa ndoto ya Zuhura na kuwezekana kwa waandishi kusafiri na Rais.
Kila nchi ambayo Rais alikwenda, January alihakikisha Watanzania wanafahamu kwa nini anakwenda huko lakini hakuishia hapo pekee, alikuwa akitangulia mapema kuhakikisha vyombo vya habari vya nchi husika – hasa vile vikubwa, vinafahamu na kuripoti kwa kina.
Na nje ya nchi, January alikuwa anahakikisha waandishi wa Tanzania wanaandika matukio yanayomhusu Rais tu na si vinginevyo. Tukiwa India, kwa mfano, ni January aliyeniambia kwamba waziri muhimu wa kuzungumza naye baada ya ziara ni Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kwa vile wizara yake ndiyo imefanikisha biashara ile kubwa ya mbaazi.
Nina uhakika, kama January angekuwa anafanya mikutano mitatu kwa siku na waandishi wakati wa ziara za Rais ughaibuni, Balile angetumia hilo kama mfano wa namna waziri huyo wa zamani alivyokuwa anatumia ziara hizo kwa manufaa yake binafsi.
January pengine ndiye mwanasiasa pekee wa Tanzania ambaye anahukumiwa kwa mambo ambayo ameyafanya na yale ambayo hajayafanya.
Lakini nini kimetokea wizarani wakati January akiwepo? Kwanza wizara imefanya upembuzi yakinifu wa majukumu yake kwa kuangalia mapungufu na namna ya kuyaboresha. Wizara pia imeanza utaratibu wa kuunda Sera Mpya ya Mambo ya Nje inayokidhi mahitaji ya sasa. Mikutano ya maboresho ya sera hiyo ilifanyika hadharani katika mikoa tofauti ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar.
Kukamilika kwa mambo haya, kutaifanya wizara na nchi kufuata mwelekeo wa muda mrefu ambao utasaidia nchi miaka mingi baada ya uwepo wa Rais Samia, ambaye ndiye mwanadiplomasia namba moja, na January mwenyewe.
Wizara pia imeanza mkakati kabambe wa kutumia rasilimali zake zilizo nje ya nchi kuongeza mapato ya nchi badala ya kuhudumiwa na serikali kama ilivyo sasa. Mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya Tanzania Tower ni mfano mmojawapo wa mwelekeo mpya wa nchi yetu.
Ni katika wakati wa January akiwa waziri ndipo Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson, alipochaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika kampeni ambazo Rais mwenyewe alimtuma January kuongeza nguvu – hasa katika hatua za mwisho nchini Angola.
January aliondolewa kwenye uwaziri akiwa ametoka Accra, nchini Ghana, ambako aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye kumwombea kura Dk. Faustine Ndugulile, awe Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti mwaka huu.
Hii maana yake ni kuwa hadhi ya Tanzania katika uga wa diplomasia kimataifa imeanza kupanda na kurejea katika hadhi yake. Rais Samia ndiye namba moja lakini January alifanikiwa kutekeleza kwa vitendo maono ya bosi wake.
Kwa hiyo, si kweli kwamba January hakumtangaza Rais au Tanzania kama ilivyopaswa bali ukweli ni kuwa alimtangaza bosi wake na nchi yake pakubwa pengine kuliko waziri mwingine yeyote aliyewahi kushika wadhifa huo kwenye miaka ya karibuni.
Kwa hiyo, kwa ile P ya kwanza – ya utendaji, naamini January alifaulu vizuri.
SIASA
Naamini kwamba sababu kubwa ya kuondolewa kwa January na Nape inaingia kwenye kundi hili. Neno siasa linamaanisha vitu vingi – kuanzia kwenye kuiokoa serikali, kutoweza kukaa pamoja, kuadhibu, kutoa mfano na kurekebisha.
Naamini kwamba uamuzi uliochukuliwa na Rais haukuwa mwepesi. Ninafahamu kwamba Rais Samia anawapenda vijana hawa. Hadharani, amewahi kuwaita watoto wake. Wakati anaingia madarakani, January na Nape walikuwa wabunge wa kawaida na “watoto waliotengwa”. Ni yeye ndiye ‘aliyewarudisha mjini’.
Ninafahamu pia kwamba Nape, January na marafiki zao walikuwa watu wa kwanza kumuunga mkono Rais Samia wakati anaingia madarakani kufuatia kifo cha Rais John Magufuli. Nakumbuka ni January aliyepenyeza nukuu maarufu kwenye vyombo vya kimataifa ya “fair but firm on issues” na “the most underestimated politician in Tanzania” wakati vikijaribu kudodosa kuhusu Rais mpya wa taifa letu.
Wengi wa watu wanaojitokeza kama watetezi au watu wanaompenda sana Rais hivi sasa, walikuwa na maoni tofauti mwaka 2021 na miaka ya mwanzoni ya utawala wa Samia. Nape na January walikuwa upande wake kuanzia siku ya kwanza na siamini kama hilo limebadilika.
Na nakubali kwamba wawili hawa – hasa January, si watu rahisi kuelewana nao na kufanya nao kazi. Ni rahisi sana mtu kutoelewana au kupishana na January kuliko kupatana naye. Kuna matukio mawili ambayo naweza kueleza kwa urahisi kuhusu tabia yake.
Mwaka 2015, CCM iliandaa tukio la kumtambulisha kwa wasanii aliyekuwa mgombea urais wake, John Magufuli, katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Msanii mmoja mrembo alimfuata January kutaka wacheze naye na mbunge huyo wa Bumbuli alimjibu kwa mkato; “I don’t dance”.
Mrembo yule alikuja kulalamika kwangu kwamba January amemringia kwa kumwambia maneno yale. Pengine angeweza kutumia lugha tamu kukataa kucheza naye lakini ni kweli kuwa January huwa hachezi muziki. Anapenda kusikiliza lakini hachezi.
La pili, linahusu tabia yake ya kuamini kutumia muda fulani wa siku akiwa peke yake. Mara kadhaa amewahi kuniambia kwamba anaamini kiongozi anahitaji muda wa kukaa peke yake – kusoma au kutafakari tu kila siku; na kuachana na kelele za maisha za kila siku.
Hii ni tabia ambayo imejenga dhana kwamba ni mtu anayependa kujitenga na asiyependa kukaa na watu. Katika uchambuzi wake, Balile ameandika kuwa January hakukutana na waandishi ughaibuni kwenye ziara za Rais hadi pale walipomwomba. Kwa watu wanaoamini kwneye elimu ya nyota, watafahamu kuwa tatizo la January ni nyota yake. Tabia zake – za kufikiri kwa picha kubwa, kupenda kufanya mambo bila kuangalia wengine wanajisikiaje na kuonekana mshaufu, zote hizo ni sifa za watu wa nyota yake ya ndoo (aquarius).
Sababu ya hili inaweza kuwa tabia ya kutaka kukaa peke yake kutafakari na pili ni kujiepusha kukaa na watu na kuzungumza kauli ambazo baadaye hunukuliwa vibaya. Balile anamwona January kuwa ni mtu anayeringa, mimi namwona kuwa ni mtu anayejichunga akijua anawindwa na mishale mingi.
Bahati mbaya ya siasa za Tanzania ni kwamba kila wakati, kuna mwanasiasa mmoja hutafutwa na kugeuzwa kuwa adui wa Rais aliye madarakani. Wakati wa Benjamin Mkapa, mzigo huu ulibebwa na John Malecela. Wakati wa Kikwete, ilikuwa zamu ya Lowassa na January – kwa maoni yangu, ndiye anayebebeshwa safari hii.
Kwa Lowassa, sababu ilikuwa mbio za mwaka 2010 ikidaiwa alikuwa anataka Kikwete aongoze kwa muda wa muhula mmoja tu na asingeweza kusubiri hadi mwaka 2015.
Kila nikisikia ya January na 2025, nakumbuka ya Lowassa ya 2010. Naamini siasa zilizomuondoa January kwenye Baraza la Mawaziri ni siasa zinazohusu uchaguzi wa 2025 na kinyang’anyiro cha 2030.
Inajulikana kwamba yule atakayemsaidia Rais Samia kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi wa mwakani, atakuwa anatazamwa na mamlaka kwa jicho pendwa ifikapo mwaka 2030. Kama January akiwa nje ya picha mwaka 2025, maana yake nafasi yake kwa 2030 itakuwa finyu. Hesabu ziko hapo.
Naamini pia huenda kuna kitu kilikwenda kombo kuhusu uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Jina la January lilianza kutajwa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa kelele kuanzia nje ya nchi na naamini kuna wakati waziri huyo wa zamani alianza kufikiria kujitosa.
Sifahamu mamlaka zilipokea vipi jambo hilo na huenda ndani ya kuondolewa huko kwenye Baraza la Mawaziri, kuna kitu kinahusiana na uchaguzi wa Kamisheni ya AU. Lakini kama nilivyosema awali, hili ni jambo ambalo mamlaka za uteuzi zinafahamu zaidi kuliko akina sisi.
Rais Samia ni mtu mzuri, muungwana na anawajua vijana wake – mazuri yao na mapungufu yao. Na ninafahamu pia kwamba January, Nape na wengine wa aina yao, hawana chuki na Rais wao. Labda sisi wa nje hawawezi kutuambia lakini najua wao wenyewe wanafahamu nini hasa kimewatokea.
Kama wakiendelea kumuunga mkono Rais wao kutoka hapa walipo sasa, na muda ukatoa majibu ambayo sasa hayapo, naamini tutawaona tena kwenye majukumu mapya si muda mrefu kutoka sasa. Bahati nzuri kwa January ni kwamba yeye na Rais wanapishana siku moja ya kuzaliwa kwenye kalenda ya mwezi. Pengine Rais Samia
anamwelewa vizuri kijana wake huyu kuzidi sisi wengine. Nyota yao ni moja.
Kama visemavyo vitabu vitakatifu; “Wamejaaliwa wale wenye subra”.