Pingpong porini na Savimbi

 Mwandishi wa makala haya, Ahmed Rajab, akiwa kwenye handaki eneo la Jamba, Angola, ilikokuwa kambi ya kijeshi ya kundi la waasi la UNITA. Kunradhi kwa mwonekano wa picha. Mazingira ya ndani ya handaki yamefinya mwonekano. Picha kwa hisani ya Ahmed Rajab. 

 

Na Ahmed Rajab

 

ILIKUWA alasiri Januari 1991 na nilikuwa nimejikalia kivivu ofisini mwangu London kwenye jarida la Africa Analysis, nililokuwa nikilihariri.  Mara ikalia simu ambayo hatimaye ilinifikisha kwa Jonas Savimbi na jeshi lake la waasi katika pori la Angola.

 

Aliyepiga simu alijitambulisha kuwa ni Isaias Samakuva, aliyekuwa mwakilishi wa London wa chama cha União Nacional para a Independência Total de Angola (Unita). Hatujawahi kukutana.  Ingawa alijaribu kuzungumza kwa upole, nikihisi alikuwa na lake, aliazimia kunishutumu.

 

Siku hizo chama cha Unita, kikisaidiwa kwa hali na mali na serikali ya makaburu wa Afrika Kusini pamoja na Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, kilikuwa vitani kikipigana na chama cha Movimento Popular de Libertação de Angola (MPLA) kilichokuwa kikitawala, na ambacho hadi leo kinatawala, Angola.

 

Waafrika wengi waliokuwa na msimamo wa kizalendo walielemea upande wa MPLA, chama kilichoungwa na Muungano wa Sovieti na Cuba.

 

Katika ulingo wa siasa za ushindani wa kimataifa, vita hivyo vilikuwa mfano mzuri wa vita vya mawakala. Vilikuwa vita vya pande mbili zilizokuwa mbali na medani halisi ya mapigano yenyewe. Pande hizo zilikuwa Marekani na Muungano wa Sovieti.

 

MPLA ilikuwa ikinasibishwa na Wasovieti na Unita ikionekana kuwa kibaraka wa Wamarekani.

 

Tulipokuwa tunazungumza kwa simu. Samakuva alinilaumu kuwa nikikiponda chama chake bila ya kujitahidi kukutana na kuwasikiliza viongozi wake. Ili kurekebisha mambo alinialika chakula cha mchana.

 

Siku chache baadaye tulikutana hoteli kwenye mtaa wa kitajiri wa Mayfair.  Nilipomuangalia kwa mara ya kwanza nilimuona kuwa kakaa kama kasisi wa kijijini.  Alikuwa mpole na, mara kwa mara, akitabasamu ingawa akionesha kama akionaona haya.  Machoni mwangu uso wake ulikuwa mgumu.

 

Baadaye kuna mtu alinambia kuwa sijakosea, kwamba Samakuva aliwahi kuwa kasisi wa kiinjili huku akipanda vyeo katika Unita.  Aliwahi hata kuisimamia ofisi ya Savimbi.

 

Alipokuwa akinilaumu kuwa nikiudharau msimamo wa Unita alikuwa hajui kwamba kama miongo miwili kabla ya hapo miye pamoja na masahibu wangu wawili, wote kutoka Zimbabwe — Chen Chimutengwende na Alfred Mutasa — tulikuwa tukishirikiana na Jorge Sangumba, mwakilishi wa Unita wa miaka hiyo jijini London pamoja na msaidizi wake, Ernesto Mulato.  Wakati huo nilikuwa nimeshapata fununu kwamba Sangumba alikuwa ameuliwa na Savimbi.

 

Chen, Alfred na mimi tulikuwa wafuasi wa siasa za Kimarx za mrengo wa China. Tukiitwa na tukijiita “Maoist”, wafuasi wa itikadi ya Kimao, iliyoanzishwa na Mao Zedong, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha China.   Wakati huo Unita nayo ilikuwa ikizifuata siasa hizo hizo za Kimao. Ndiyo maana Savimbi na wapiganaji wake wakikaribishwa China walikofunzwa mbinu za kupigana katika vita vya porini. Mlingano huo wa kiitikadi ndio uliotufanya wakati huo tuliunge mkono vuguvugu la Unita.

 

Ni muhimu kuyaeleza hayo kwa sababu kila hali lazima ieleweke kwa muktadha wa historia yake.

 

Tulipokuwa tunakula Samakuva aliniasa kuwa kwa vile nilikuwa nikiandika sana kuhusu siasa na vita vya Angola ni muhimu niwe na ufahamu mzuri wa vuguvugu lao.  Akanialika nende Jamba kwenye makao makuu yao na ambako, mwezi Februari mwaka huo wa 1991, Unita kilikuwa kifanye mkutano wake mkuu wa saba.

 

Mji wa Jamba uko katika mkoa wa Angola wa Cuando Cubango, kaskazini kidogo ya mpaka wa Namibia katika eneo la Caprivi. Kufika huko ilibidi mtu kwanza ende Afrika Kusini iliyokuwa bado ikitawaliwa na makaburu ingawa utawala wao ulikuwa mahututi, ukivuta pumzi zake za mwisho.

 

Magharibi ya siku ya pili ya kuwasili Johannesburg miye pamoja na wageni wengine wa kimataifa tulipelekwa kwenye kiwanja cha ndege kidogo kwa safari ya kwenda Jamba.  Nakumbuka mtu mmoja alisema safari yetu lazima iwe ya usiku kwa sababu tutaruka bila ya ruhusa juu ya anga ya Namibia kabla ya kuingia Angola.

 

Ndege ilipopaa tu nilimsikia Mmarekani mmoja akimnong’oneza mwengine: “Unamuona yule? Ni João Soares, mtoto wa Rais Mario Soares wa Ureno.”

 

Nilipogeuka na kumuangalia Soares moyo ulinipwaya. Nikajiuliza: balaa gani tena hili?

 

Nilikumbuka kwamba 1989 João Soares, aliyekuwa mbunge wa Kisoshalisti Ureno, alikwenda Jamba pamoja na wabunge wenzake wawili na mwandishi wa Kijerumani. Walipokuwa wanarudi ndege yao ilianguka ilipokuwa inajaribu kuruka.  Alijeruhiwa vibaya sana.  Nikajiuliza: si nuksi kusafiri naye huyu?

 

Kila muda ukipita nikiona hatufiki. Hatimaye, ndege yetu ilitua Jamba usiku wa manane katika eneo lililokaa kama konde.  Pembezoni, kulia na kushoto mlikuwa mienge.  Tulipokelewa na giza totoro na kimya cha kushtusha kilichovunjwa kwa sauti kali za nyenje.

 

Tulifululiza kwenye banda lililoezekewa makuti ambalo Unita ikilitumia kama idara ya uhamiaji na forodha.

 

Mapokezi yalikuwa mema. Yalijaa tabasamu, chai, kahawa na soda. Kulikuwako pia vitafunio vilivyokuwa na sura ya mandazi lakini vilivyokuwa na utamu wa mahamri yasiyo na hamira.

 

Tuliambiwa tujaze fomu zilizouliza iwapo tulikuwa na silaha.  Baada ya kuzijaza tulipakiwa kwenye magari tukapelekwa tulikokuwa tushukie.  Baadhi yetu tulipelekwa kwenye kambi ya Kwame Nkrumah.  Kambi kadhaa nyingine zilipewa majina ya viongozi asilia wa vuguvuvu la Umajumui wa Afrika.

 

 

Kwa vile tulikuwa Jamba siku za mkutano mkuu wa Unita, Jamba nzima ikinuka Savimbi.  Kila ulipoangalia uso wa Savimbi ukikutumbulia macho: kwenye miti, kwenye milingoti, hata kwenye makalio ya wanawake waliojifunga vibwebwe vitambaa vilivyokuwa na chapa ya Savimbi.  Alikuwa hakimbiliki hata kama ungetaka.

 

Mkutano mkuu wa Unita uliendelea kwa wiki nzima.  Takriban kila siku nikihojiwa na kipindi cha BBC cha Focus on Africa kuhusu mkutano huo.

 

Jamba siku hizo ilikuwa kama ina tamasha. Asubuhi na mchana vikao vya mkutano vikiendelea na wapiganaji wa Unita wakionesha misuli yao ya kivita kwa magwaride na maonesho ya silaha nzito, pamoja na vifaru vya kijeshi.  Usiku pakimoromoshwa dansa na tafrija nyingine.  Kila wakati wa mlo ulikuwa wakati wa dhifa.

 

Mkutano mkuu ulipomalizika Savimbi alikutana na waandishi wa habari. Na hapo alijimwaya. Ulimi wake mmoja ulikuwa na kipaji cha ufasaha wa lisani, au ndimi, nyingi. Akizungumza lugha sita za Kiafrika zikiwa pamoja na lugha yake asilia ya Umbundu, Chokwe na Luvale. Hali kadhalika akizungumza lugha nne za kizungu: Kireno, Kijerumani, Kifaransa na Kiingereza. Akikifahamu pia Kihispania.

 

Ulipomalizika tu mkutano huo wa waandishi wa habari mkuu mmoja wa Unita alinijia akanambia kwamba Savimbi atakutana na waandishi maalum wa habari za usiku na kwamba miye nitakuwa mmojawao.

 

Jioni nikaamua kunyosha miguu.  Nikatembea kuwaendea wanakijiji waliokuwa kisimani. Ghafla nikashtukia gari la kijeshi likiwa nyuma yangu; lilipakia wapiganaji waliokuwa na silaha nzito. Walinambia nilipotea njia. Nikawaambia sijapotea njia. Wakashikilia kuwa nilipotea na kwamba njia ya ninakokaa ilikuwa nyuma yangu sio mbele niendako.  Nilitambua kwamba hawakutaka nikazungumze na wanakijiji.

 

Nikageuza njia kurejea nilikotoka.  Baada ya kupiga hatua mbili tatu nikasikia sauti ikiniita kwa kelele: “Comrade Rajab, comrade Rajab.”  Nilipogeuka nilishangaa kumuona Ernesto Mulato. Tulisalimiana na tukaanza kukumbushana ya London.  Alitaka kujua walipo Chen Chimutengwende na waziri wa zamani wa Tanzania Abdulrahman Babu niliyemjulisha naye London mwaka 1971.

 

Katika miaka ya mwanzo ya Unita Babu alikuwa na maingiliano na Savimbi.  Hata Kanali Ali Mahfoudh, Mzanzibari aliyepata umaarufu katika vita vya ukombozi wa Msumbiji, aliwahi kunambia kwamba zamani naye pia alikuwa na uhusiano na Unita.

 

Katika mazungumzo yangu na Mulato, nilimuuliza Jorge Sangumba alifikwa na nini? Akanambia kwamba alikuwa nje ya Angola na aliporudi aliambiwa kwamba Sangumba aliuawa vitani.

 

“Maskini Jorge”, nilisema. “Maskini Jorge,” akaungama Mulato.

 

Jawabu yake ilithibitisha kwamba Sangumba alikuwa amekufa. Lakini sikuamini kwamba aliuawa katika mapigano.  Nilidokezwa kabla ya kuondoka London kwamba Savimbi alikuwa akiwaua baadhi ya wapinzani wake akiwasingizia kuwa wachawi.

 

Nilighadhibika na nikasema tutapokutana na Savimbi usiku nitamuuliza yaliyomfika Sangumba.

 

Savimbi akitisha. Angekutokea ghafla gizani lazima ungeshtuka. Alikuwa mweusi kama gogo la mpingo na alikuwa na macho makubwa yaliyokuwa yakimulika mithili ya kandili yenye nuru kali. Katika giza lililotanda ni mwanga mkali wa macho yake tu ndo ukionekana.

 

Tulikuja kuchukuliwa milango ya saa sita za usiku kwenda kumuona.  Wenzangu wengine waliwakilisha shirika la utangazaji la BBC (Idhaa za Kireno na Kifaransa) pamoja na waandishi kutoka Ubelgiji, Marekani na Afrika Kusini.

 

Tuliposhuka garini tulijikuta porini. Tulikikuta kikundi cha wapiganaji wa Unita wakiwa na silaha.  Ikanijia hofu.  Si ya kushambuliwa majeshi ya serikali lakini niliwaza endapo hao wapiganaji wa Unita wangepigana wenyewe kwa wenyewe sisi tungekimbilia wapi.

 

Tukajikuta tunateremka ngazi kwenye handaki kubwa. Tulipofika chini ya ardhi tukakuta ramani kadhaa zimetundikwa zikiwa na pini za rangi mbali mbali zikionesha maeneo ya vita. Tulikuwa ndani ya chumba cha operesheni za kivita.  Upande wa kulia kulikuwa meza kubwa ambapo Savimbi na viongozi wenzake walikaa. Wengine walisimama nyuma yao.

 

Baada ya kukaribishwa kukaa, miye ndiye niliyekuwa wa mwanzo kufungua mdomo. Nayakumbuka niliyoyasema:

 

“Ningependa kuanza mimi kwa sababu alikuwa rafiki yangu. Yu wapi Jorge Sangumba?”

 

Savimbi alivimba, akanuna.  Alizikusanya hasira zake akazitia kwenye mkono wake wa kulia, akaunyanyua na akaupiga kwa nguvu mezani huku akinguruma: “Sangumba, Sangumba, kila ajaye humuuliza Sangumba. Mtamuona wakati utapofika.”

 

Kimya kilitanda. Hakuna aliyesema hata “kwi”.  Niliuangalia uso wake. Ulijaa ghadhabu.  Niliuangalia mkono wake. Ulijaa maguvu.  Angenipiga konde usoni uso wangu ungekuwa vumbi.  Savimbi lilikuwa jibaba la mtu. Alikuwa na tambo la mwenye kustaftahi, kufungua kinywa asubuhi, kwa kula mbuzi mzima.

 

Kwa upole nikamuuliza: “Yaani una maana yu hai?”

 

Alinitolea macho. Na bila ya kuyapepesa akajibu kwa ukali: “Ndio. Naam.”

 

Waandishi wenzangu walikaa kimya wakiniachia fursa ya kucheza “pingpong” (mpira wa meza) na Savimbi kuhusu Sangumba.

 

Nadhani Savimbi akifikiri nilikuwa na swali jengine kama msumari kwa sababu swali langu la tatu lilimbabaisha.

 

“Unafanya nini kwa kupumzika?”

 

Hakunisikia. Au labda hakunifahamu.

 

“O que? [Nini?]”

Nikauliza tena kwa Kireno nikisaidiwa na watu wake: “Como você relaxa?”

 

Na nikaongeza “kwa sababu nasikia zama zako ulikuwa mwingi wa dansa.”

 

Uso wake ukakunjuka, pumzi zikamshuka, akaangua kicheko.  Baadhi ya wafuasi wake nao wakacheka.

 

“Ah, siku hizi sina wakati, mapigano hayaruhusu,” alisema.

 

Akatufungulia mlango wa kumuuliza maswali kuhusu vita baina ya Unita na jeshi la serikali ya Angola.

 

Tulipomaliza tulipanda juu kutoka chini ya ardhi. Walinzi wa Unita walikuwa wamesimama na silaha nzito. Kimoyomoyo nikajiuliza swali la kujitisha: wakianza hawa kutwangana wenyewe kwa wenyewe tutakimbilia wapi?

 

Kwa mbali niliyasikia majogoo ya Jamba yakianza kuwika.  Tukapandishwa kwenye magari na kurudishwa kwenye kambi ya Kwame Nkrumah.

 

Nilimuona tena Savimbi miezi michache baadaye alipozuru London na kukutana na waandishi wa habari.  Kulifanywa majaribio zaidi ya sita ya kutaka kumuua na kulitolewa taarifa za uwongo mara 17 kwamba alikufa.  Hatimaye, alifariki Februari 22, mwaka 2002 alipokuwa akipigana na wanajeshi wa serikali ya Angola katika jimbo la Moxico alikozaliwa.  Majeshi ya Angola yalisaidiwa na Waisraeli.  Wakitumia teknolojia yao ya kijasusi Waisraeli ndio waliogundua alikuwa wapi walipoinasa simu yake ya mkononi.  Alipofariki alikuwa na umri wa miaka 67.

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.