Chawa ni nani?

Tajiri Elon Musk wa Marekani (kushoto) katika picha na mgombea urais wa chama cha Republican, Donald Trump. Picha kwa hisani ya IBTimesUK

 

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

 

KWA wafuatiliaji wa siasa za Marekani kuelekea uchaguzi wao wa Novemba mwaka huu, watakuwa wamebaini namna Elon Musk; mmoja wa matajiri wakubwa duniani, anavyomuunga mkono mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump.

 

 

Kama Musk angekuwa Tanzania, pasi na shaka yoyote angepachikwa jina la Chawa. Kwenye siasa zetu, neno chawa limekuwa likinasibishwa na ufuasi wa mtu kwa wanasiasa au viongozi.

 

 

Lakini swali ambalo nitajaribu kulijibu kupitia makala haya ni kama kweli Musk anaweza kuingia kwenye kundi hilo la chawa. Au, kwa lugha nyepesi kabisa, chawa ni nani?

 

 

Ni muhimu kuanzia na asili ya neno lenyewe. Katika lugha ya Kiswahili, jina chawa linamaanisha mdudu anayeishi mwilini mwa mwanadamu au kwenye nguo na ambaye uhai au uwepo wake unategemea uhai au uwepo wa mtu au nguo hiyo.

 

 

Kuna mambo mawili ya msingi hapa. La kwanza ni kwamba chawa hawezi kuishi pasipo huyo host (mwanadamu au nguo) na pili ni kwamba huyo mwanadamu hafaidiki chochote na uwepo wa chawa huyo. Ndiyo kusema, kama akijua ana chawa na akatumia dawa au kufanya usafi wa eneo husika, chawa atakufa na mwanadamu atabaki salama.

 

 

Katika elimu ya viumbe, chawa anatokea katika kundi la wanyama wanaoitwa kwa lugha ya Kiswahili vimelea au parasites kwa Kiingereza. Ikrari, neno hili asili yake si Kiingereza bali linatokana na neno la lugha ya Kilatini parasitos. Tafsiri ya neno parasitos ni mtu anayekula kwenye meza ya mwingine. Jambo la maana kulipata hapa ni kwamba chawa – kwa maana ya parasitos mtu anayetakiwa kupata riziki yake kupitia kwa mwingine.

 

 

Narudi nilipoanzia. Je, Elon Musk ni chawa wa Trump? Kabla hujajibu swali hili, kuna vigezo vitatu vya kutazama; cha kwanza – bila ya Trump, Musk atabaki na utajiri wake? La pili, Trump anamhitaji Musk? Kwamba Trump atapata athari yoyote akimkosa Musk? Na hoja ya tatu ni je, riziki ya Musk inatoka kwa Musk?

 

 

Ni rahisi kujibu swali hili kwa kutumika mtandao wa Google tu. Ukitafiti, utaona Musk alikuwa bilionea mwaka 2012 wakati Barack Obama akiwa Rais wa Marekani. Mwaka 2021 – wakati Rais wa Marekani akiwa Joe Biden, Musk alitangazwa na jarida la Forbes kuwa tajiri namba moja duniani. Kwa hiyo hoja kwamba Musk anamtegemea Trump kuwa tajiri haipo.

 

 

Je, Trump hamtegemei Musk? Jibu la swali unalipata kirahisi pia. Mosi ni kwamba siasa za Marekani zinahitaji matumizi makubwa ya fedha na Trump anahitaji michango ya kifedha ya watu wenye ukwasi kama Musk kushinda urais. Lakini kubwa zaidi, Musk anamiliki mtandao wa X (zamani twitter) ambao sasa ni uwanda muhimu kwenye mapambano ya kisiasa. Hakuna mwanasiasa anayetaka urais ambaye hatapenda kuwa rafiki wa mmiliki wa silaha hii kubwa kisiasa.

 

 

Hivyo Musk si chawa wa Trump kwa maana ya neno lenyewe. Lakini kwa nini anamsifia? Haijulikani vema kwa sasa lakini inaonekana kuna aina ya dili ambayo wawili hawa wameingia itakayofanya Musk apate anachotaka na Trump apate pia. Huenda dili ya Musk imekataliwa na watu wa chama cha Democratic na ameamua kufanya anachokifanya kupata anachokitaka au kuwakomesha waliomkatalia.

 

 

Hili ndilo ambalo linafanyika duniani kote. Kwa kawaida, binadamu ni kiumbe mbinafsi na mar azote atafanya mengi ya anayoyafanya kwa sababu ya faida yake binafsi kwanza kabla ya mambo mengine.

 

 

Ninaamini kwamba neno chawa au uchawa hapa kwetu linatumika vibaya na kupitiliza matumizi yake ya kawaida yanayopaswa. Mambo mengi huwa yanarundikwa kwa pamoja na neno chawa linatumika kuyakusanya yote na kuyaweka fungu moja.

 

 

Nitatoa mfano mmoja wa tukio lililotokea hivi karibuni. Baada ya Dk. Faustine Ndugulile kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, kuna video zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, zikionyesha wabunge na ujumbe wa Tanzania uliokuwa kwenye mkutano ukiimba nyimbo za kumsifu Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushindi huo.

 

 

Mmoja wa rafiki zangu katika mojawapo ya makundi sogozi niliyopo, aliituma video hiyo na kusema “Huu ni uchawa. Kashinda Ndugulile sasa inakuwaje wanaimba kumsifu Samia? Uchawa sasa ni tatizo kubwa zaidi hapa kwetu.” Niliposoma tu ujumbe ule, wazo la kuandika makala haya likanijia kwa sababu kadhaa.

 

 

Kwanza, rafiki yule aliamua kufanya hitimisho kwa kutumika picha jongefu (video) moja tu aliyoiona. Kama angetazama nyimbo tofauti zilizoimbwa, angeona pia video za nyimbo za Kinyakyusa, wimbo wa Tanzania Nakupenda kwa Moyo Wote, nyimbo za kumsifu Ndugulile na nyingine walizoimba. Ni bahati mbaya alifanya hitimisho kwa kutumika video moja ya dakika chache.

 

 

La pili na ambalo ni la muhimu zaidi, ni kwamba muktadha ni muhimu katika mambo haya. Ni miaka michache tu iliyopita, wapo viongozi wa Tanzania waliokuwa na sifa za kushika nyadhifa kubwa kwenye taasisi za kimataifa lakini hawakupata fursa hiyo kwa sababu ya kukataliwa na mamlaka za juu – hasa Rais.

 

 

Kwenye kuchaguliwa kwa Ndugulile, kuna ushahidi wa kutosha kwamba Rais Samia alitumia rasilimali fedha, ushawishi wa nchi na rasilimali watu ya kutosha kuhakikisha Mtanzania huyo anapata nafasi hiyo. Kama watu waliimba kumpongeza – walau katika hili, ilikuwa sahihi kwa sababu ni kweli Rais alifanya kazi kubwa.

 

 

Ningeelewa kama rafiki yule angeona mtu anamsifia Rais kwa sababu ya mvua kunyesha au watu kuamka asubuhi. Lakini kwa muktadha wa uchaguzi wa Ndugulile, haikuwa sahihi kutumika neno hilo. Muktadha ni muhimu kwenye nyakati kama hizi.

 

 

Ikanikumbusha rafiki yangu mmoja ambaye aliwahi kunipigia simu na kusema anataka kunipa kazi kwenye chombo cha habari anachokianzisha lakini anashindwa kwa sababu siku hizi nimekuwa chawa na hivyo siwezi tena kuwaandika au kuzungumza kwa uwazi mabaya ya serikali kama ilivyokuwa miaka 10 au 15 iliyopita.

 

 

Tulicheka lakini ilibidi niweke rekodi mbili tatu sawa. La kwanza ni kwamba hadi sasa, hakuna mtu au taasisi yoyote ambayo umuhimu wake kwangu ulikuwa kwamba ukifa nami nimekufa. Ajira zote ambazo nimewahi kupata, narudia ZOTE, zimetokana na waajiri kuona kwamba nina uwezo wa kufanya kazi ninayotakiwa kuifanya.

 

 

Watu wengine wamewahi kuzungumzia uhusiano wangu binafsi na baadhi ya viongozi mashuhuri nchini na kuona ni uhusiano wa chawa na host. Ukweli ni kwamba wengi wa viongozi. Baadhi ya viongozi tuna urafiki tangu shuleni, wengine nimejuana nao wakiwa wanafunzi na mimi ndiye mwenye hela. Wengine kwa sababu kwa majukumu yao, walihitaji mtu makini kwenye tasnia ya habari kwa ajili ya ushauri.

 

 

Uhusiano ni kama wa Trump na Musk ingawa ni katika kiwango cha chini. Kila mwanasiasa mkubwa au kiongozi duniani kote anahitaji kuwa na rafiki mwenye ushawishi miongoni mwa wanahabari na mifano iko mingi. Na mwanahabari yeyote makini, anahitaji kuwa na aina fulani ya uhusiano na viongozi au watu wenye ushawishi ili kufanya kazi zake vizuri.

 

 

Siku hizi naona viongozi na watu wenye ushawishi wakilalamika kuwa uchawa ni tatizo kubwa hapa nchini. Ukitaka kuonekana una maarifa na akili nyingi kwenye siku za karibuni, kemea tu tabia za kichawa na utaona makofi unayopigiwa. Lakini, ni kweli kwamba tatizo letu ni uchawa na kwamba umeanza nyakati hizi? Si kweli.

 

 

Baba wa Taifa, Julius Nyerere, alipata kuzungumza kwamba kuna watu wake wa karibu walikuwa wanamtaka asiachie ngazi kwa sababu nchi bado inamhitaji. Akasema baadaye, akabaini wahusika walikuwa wakililia maslahi yao na si ya nchi. Sina shaka kwamba wale waliokuwa wakimpa Mwalimu ushauri huo, ndiyo walipaswa kuitwa chawa. Hii ni kwa sababu, maisha yao na nafasi walizokuwa wakishikilia, zilikuwa zikitegemea uwepo wa Mwalimu madarakani.

 

 

Baadhi ya wale wanaotajwa kuwa walikuwa sehemu ya waliokuwa wanamshawishi Mwalimu abaki madarakani, ndiyo hao wanaolalamikia uchawa kwenye taifa letu!! Chawa wa namna hii ndiyo hatari kwa taifa kuliko chawa wa aina ya Mwijaku na Baba Levo ambao wanasemwa kila siku. Hawa wengine wameona fursa kwenye maisha na wameamua kuitumia. Hawa wanaomwambia kiongozi asifuate Katiba, ndiyo tatizo kubwa zaidi kwa nchi.

 

 

Ninaamini tuna shida ya namna tunavyoandaa na kupata viongozi wetu, tuna shida kwenye mifumo yetu ya elimu na kuna mtanziko kwenye suala zima la maadili na malezi kwenye jamii. Uchawa, kwa maoni yangu, unatumika kuficha matatizo makubwa zaidi ambayo tunayo lakini tunashambulia au kukipa maana kitu ambacho kwa hakika ni kidogo sana.

 

 

Kama mimi namsifia mtu kwa mambo anayofanya, inawezekana nafanya kwa sababu ni rafiki yangu ambaye namtia shime afanye vizuri zaidi, kwa sababu ninafaidika na uongozi wake kwa namna moja au nyingine na yeye anaendelea na urafiki na mimi kwa sababu nina mchango kwenye kufanikiwa kwake kwenye majukumu yake.

 

 

Kabla hujamwita mtu chawa au kuzungumzia ubaya wa uchawa kwa taifa letu, ni muhimu kuangalia muktadha wa anachoandika, kuzungumza na kutenda. Na mambo ya msingi ni matatu; la kwanza, maisha yake yanategemea kuwepo au kutokuwepo kwa huyo anayeonekana kumsifu? La pili, huyo anayesifiwa hafaidiki chochote na huyo aitwaye chawa? Na tatu – na hili ni la muhimu sana, riziki ya huyo aitwaye chawa inatoka kwa host?

 

 

Kama majibu ni hapana, hapo hakuna chawa. Labda litafutwe jina lingine.

 

 

Mwandishi ni msomi wa masuala ya Maridhiano ya Kisiasa  mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza. Anapatikana kwa email; ekamwaga57@gmail.com