#Siasa

Kamari ya Rais Samia kwa Nchimbi

Picha: Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan akiteta na Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, Emmanuel Nchimbi, mara baada ya kupewa majukumu hayo mjini Zanzibar wiki hii. Picha kwa hisani ya CCM. 

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

KUCHAGULIWA kwa Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumeibua swali moja kubwa kwa watu wengi; kwa nini  yeye? Tangu CCM kitangaze kwamba kimempa nafasi hiyo, nimeona wachambuzi na wadadisi wengi wakieleza na kujibu swali hilo la kwanza.

 

Nimeamua kwamba sitajielekeza kujibu swali hilo na badala yake nitaangazia upande mwingine ambao haujajadiliwa sana kwenye mjadala mzima wa suala hilo. Kwangu, naamini kwamba Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, amecheza kamari ya kisiasa kwenye maeneo takribani matano kwenye hatua hii aliyochukua.

 

Hivyo, lengo la makala hii ni kuelezea kamari hiyo na mtanziko wake katika picha kubwa ya kisiasa ya CCM kuanzia kutoka ilipoanzishwa na kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025 na mbali zaidi. Natumai neno kamari kwa tahadhari kubwa nikifahamu taathira yake ya lugha lakini nimekosa neno zuri zaidi kulitumia katika muktadha wa ninachotakia kuzungumzia.

 

Ni kamari zipi hizo?

 

Kuchagua kundi la uaminifu

 

CCM kwa sasa ina makundi makubwa matatu – na mengine madogo madogo. Kundi la kwanza ni lile linalofahamika kama CCM Asili. Hili ni kundi linalohusishwa zaidi na wana CCM wa aina ya Jakaya Kikwete na Abdulrahman Kinana. Lina mchanganyiko wa makundi mengine madogo lakini wengi ni watu ambao wana historia na chama hicho, wamekulia humo na wamekifanyia kazi kwa muda mrefu.

 

Kundi la pili limepewa lakabu maarufu ya Sukuma Gang. Hili ni kundi ambalo limehusishwa sana na Rais wa Tano wa Tanzania, hayati John Magufuli. Wengi wa wanaohusishwa na kundi hili ni watu ambao wanaonekana walikuwa vipenzi vya Magufuli na kupewa nyadhifa kubwa wakati huo.

 

Kundi la tatu ni lile linalohusishwa na kundi la Mtandao ambalo kinara wake alikuwa Edward Lowassa – Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, kabla hajahamia chama cha upinzani cha Chadema. Wengi wa walio katika kundi hili hawakuhama na chama kumfuata Lowassa lakini bado walikuwa wamoja hata leo.

 

Sifa za watu wa kundi la kwanza na la tatu zinafanana. Tofauti yao pekee ilikuja wakati wa mchakato wa kutafuta mrithi wa Kikwete mwaka 2015. Kundi hili linaamini Kikwete na Kinana ndiyo waliosababisha Lowassa asipewe tiketi ya kuwania urais. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mpasuko na mgawanyiko wao.

 

Nchimbi anatoka katika kundi hili la tatu. Mara baada ya Lowassa kuhama CCM, yeye ndiye alikuwa akijulikana kama kiranja au kaka wa kundi hili. Mpaka sasa, hakuna shaka kwamba kwenye kundi hili, Nchimbi ndiye namba moja.

 

Nchimbi amechukua nafasi ya Daniel Chongolo aliyejiuzulu wadhifa huo. Kwenye siasa hizi za makundi ndani ya CCM, Chongolo anahusishwa zaidi na kundi la kwanza – ingawa si monolithic kama ambavyo nalieleza hapa.

 

Kwa kumpa nafasi Nchimbi, Samia amecheza kamari ya kuchagua mtu kutoka katika mojawapo ya makundi ya ndani ya CCM. Kwa nini ameamua kucheza kamari hii? Kwa uelewa wangu wa siasa za CCM na namna Rais Samia anavyofanya uteuzi, kamari hii imechagizwa na kitu kimoja tu; uaminifu.

 

Katika makundi makubwa matatu ya ndani ya CCM, kundi la wana mtandao limejipambanua kama lenye watu waaminifu kwa kundi kuliko mengine. Kilele cha hiki kilikuwa ni tukio la mwaka 2015 wakati Nchimbi na wana mtandao wenzake, Sofia Simba na Adam Kimbisa, walipopinga waziwazi hatua ya CCM kumpitisha Magufuli kuwa mgombea wake badala ya Lowassa.

 

Ukitaka kujua ukaribu na udugu wa kundi hili, angalia hata wakati mwenzao anapopata msiba au tatizo lolote popote. Utaona makumi kwa mamia ya wenzake wakishirikiana naye kwa faraja au kutafuta namna ya kutatua tatizo. Na ingawa hawakumfuata Lowassa alipokwenda Chadema – kwa sababu tofauti, wengi bado walibaki pamoja.

 

Ni wazi Samia ameamua kucheza kamari ya kwanza kwa kumpa nafasi mtu kutoka katika kundi linalojulikana kwa uaminifu na kutogeukana. Na hili si jambo la ajabu kwa sababu kama unafuatilia uteuzi unaofanywa na Rais, utaona kwamba jambo la uaminifu na kutokuwa ‘snichi’ analipa umuhimu sana.

 

Upande mmoja wa shilingi kwenye kamari hii ni kwamba Rais amemchagua kada mahiri wa chama, mtu wa ndani, mwaminifu, anayekubalika ndani ya chama na anayeleta chini ya Mwenyekiti mojawapo ya makundi muhimu ndani ya chama.

 

Upande wa pili wa shilingi unahusu makundi mengine makubwa yaliyobaki na namna yatakavyotazama nafasi yao baada ya kada mwandamizi wa kundi kinzani kupewa nafasi hiyo nyeti kwenye chama. Watahofu? Wataona upendeleo kwa kambi yake kwa kila hatua itakayochukuliwa naye akianza kutimiza majukumu yake?

 

Yalikuwepo majina mengine ya watu waliokuwa wakitajwa kuchukua nafasi iliyoachwa na Chongolo kutoka katika makundi mengine lakini Mwenyekiti aliamua kuchukua njia hiyo.

 

Ukweli mchungu ni kwamba wengi wa wafuasi wa kundi lililokuwa likihusishwa na Magufuli wanaonekana kama “wakuja” ndani ya chama huku kundi la kwanza halisifiki kwa uaminifu na uvumilivu. Mwenyekiti kaamua kuamini kundi la watu analoamini linamwamini na halitamgeuka huko mbele ya safari.

 

Katibu Mkuu mwenye ngome

 

Kuna utaratibu ambao haujaandikwa popote kwenye Katiba ya CCM lakini inajulikana kwamba mara nyingi kwamba ngome ya kisiasa ya Katibu Mkuu wa chama hicho huwa ni Mwenyekiti. Kwamba Katibu Mkuu ni mtu ambaye nguvu na ushawishi wake unategemea nguvu ya Mwenyekiti wake.

 

Baada ya Uhuru, Katibu Mkuu wa TANU alikuwa Oscar Kambona na alikuwa mwanasiasa kipenzi na mwenye ushawishi binafsi ndani ya chama na serikali. Inaonekana Baba wa Taifa, Julius Nyerere, alijifunza kitu baada ya kutofautiana na kuamua kuwa chama hakitakuwa tena na Katibu Mkuu mwenye nguvu na ushawishi wa kushindana na Mwenyekiti.

 

Katibu Mtendaji wa kwanza wa CCM baada ya TANU kuungana na ASP ya Zanzibar alikuwa Pius Msekwa ambaye wengi wanamwona kama “kijana” wa Mwalimu. Wengine waliofuatia wa aina ya Rashid Kawawa, Daudi Mwakawago na wengine walikuwa wanasiasa watiifu kwa Nyerere.

 

Rais Ali Hassan Mwinyi alijaribu kwa kumpa nafasi Horace Kolimba. Kiongozi huyu alikuwa na ngome yake kisiasa kupitia Jumuiya ya Wafanyakazi (JUWATA) alikotokea. Kuna nyakati hali ilikuwa mbaya kisiasa kiasi kwamba mwisho wake kwenye nafasi hiyo haukuwa mzuri.

 

Benjamin Mkapa alibaki na Philip Mangula kwa miaka yake yote kumi ya Uenyekiti wake. Mangula siyo kwamba hakuwa na nguvu na ushawishi kwenye chama, lakini kwenye maisha yake hakuwahi kuwania nafasi yoyote ya kisiasa na kushinda. Nguvu yake kisiasa ilikuwa nguvu ya Mkapa.

 

Kikwete alianza na Yusuph Makamba ambaye walikuwa naye kwenye kundi moja la kisiasa. Hata alipombadili, alimchukua Wilson Mkama ambaye naye hakuwa na ushawishi mkubwa. Abdulrahman Kinana alikuwa na ushawishi kwenye jamii lakini hakuwa na kundi maalumu aliloweza kuliita ngome yake kisiasa kwenye chama. Nguvu yake ilikuwa heshima na hadhi yake ndani ya chama na kwenye vyombo vya ulinzi na usalama nchini.

 

Haikuwa ajabu pia kwamba Magufuli aliamua kumpa nafasi Dk. Bashiru Ally Lyakurwa, ambaye hakuwa na ushawishi wala nguvu ya kisiasa ndani na nje ya chama. Kama Bashiru alikuwa na ushawishi wowote kwenye wadhifa wake huo, nguvu yake ilikuwa ni nguvu ya Magufuli mwenyewe.

 

Nchimbi, kipekee kabisa, ndiye pengine Katibu Mkuu wa kwanza katika miongo mitatu iliyopita ambaye anajulikana ana nguvu na ushawishi kisiasa ambao hautokani na Mwenyekiti wake. Kupewa kwake Ukatibu Mkuu kunamaanisha uwezekano wa kuwepo kwa nguzo mbili za mamlaka ndani ya chama – jambo ambalo watangulizi wa Samia walikuwa wakiliogopa.

 

Kuwa na Katibu Mkuu mwenye ngome yake ya kisiasa kuna faida ya kwamba kundi hilo lote moja kwa moja linakuwa kundi la Mwenyekiti. Lakini, tatizo linakuja pale ambapo kundi hilo inapotokea likatofautiana na Mwenyekiti. Ni kamari, na kama zilivyo kamari nyingine, zinaweza kulipa au kutolipa.

 

Misimamo ya Katibu Mkuu

 

Katika hotuba yake ya kwanza tangu apewe Ukatibu Mkuu, Nchimbi amezungumza kitu ambacho sikuwahi kukisikia kwa mtu mwengine aliyewahi kupewa wadhifa huo kwenye miaka ya karibuni. Alitangaza hadharani kwamba yeye ni mtu mwenye misimamo na kwamba yuko tayari kufukuzwa hata katika siku yake ya kwanza kazini kwa sababu hiyo.

 

Nchimbi hakuwa anapiga porojo kwa maneno yake hayo. Historia inaonyesha kwamba mwaka 2015 aliwahi kuonesha msimamo wake dhidi ya CCM wakati kilipompitisha Magufuli. Na kwa ukweli huu, inaonekana yuko tayari kufanya tena endapo mazingira ya kufanya hivyo yatajitokeza tena.

 

Kamari ya Rais Samia kwenye hili ni kwamba amemchagua mtu ambaye ana misimamo ambayo haiwezi kupindishwa. Katika mazingira haya, neno pekee ambalo naweza kulisema ni kwamba tuombe Mungu lisije kutokea jambo ambalo likasababisha wawili waende njia tofauti.

 

Kwa sababu, ni jambo moja kwa mwanachama mfuasi wa kiongozi mmoja kutofautiana na chama kwenye jambo la msingi. Lakini ni jambo tofauti kabisa kwa Mwenyekiti na Katibu Mkuu kutofautiana katika jambo la msingi.

 

 

Kupingana na chama hadharani

 

Hii ni kamari nyingine ya Rais Samia inayofanana kidogo na ile iliyotangulia hapo juu. Mwaka 2015, Nchimbi alifanya kile ambacho hakijawahi kufanywa na mwana CCM mwingine kwenye miaka ya karibuni – kupinga hadharani uamuzi wa vikao vya juu vya CCM.

 

Kwenye vyama vya aina ya CCM, kosa kama hilo mara nyingi adhabu yake huwa ngumu kusameheka. Hata kama mhusika ametoa hoja za maana, uamuzi wa chama huwa uko juu ya maamuzi binafsi ya wanachama wake. Ndiyo sababu wapo walioandika taazia ya kisiasa ya Nchimbi mara tu baada ya tukio lile.

 

Na wiki hii, Rais Samia aligusia kuhusu jambo hilo. Hata hivyo, alihusisha jambo lile na utoto akisema Katibu Mkuu huyo mpya wa CCM hawezi kufanya jambo kama lile tena kwa vile sasa “amekua”.

 

Kamari ya hili ni kwamba ali mradi Nchimbi amesamehewa, “watoto” wengine ambao “hawajakua” bado, wanaweza kufanya vitendo vya kumpinga Mwenyekiti au chama hadharani kwa sababu tayari kuna historia ya mtu ambaye alipinga uamuzi wa vikao vya juu vya chama na bado akapanda hadi ngazi za juu miaka ya baadaye.

 

Inawezekana hakuna taarifa za kutosha kuhusu nini hasa kilitokea usiku ule ambapo Nchimbi na akina Kimbisa waliamua kutoka hadharani kuzungumza walichozungumza. Labda ni jambo ambalo chama inalielewa vizuri zaidi kuliko wengi wetu.

 

Chama Cha Mapinduzi kinafanana kidogo na Chama cha Kikomunisti cha China kwenye masuala ya kiitikadi na ukitaka kufahamu nini hutokea pale mwanachama mwandamizi wa chama anapokwenda kinyume cha maamuzi ya vikao vya chama,  unatakiwa kusoma maandishi ya watu kama Chen Boda na Gao Wengiang kujua nini kilikuwa kinatokea China kwenye miaka ya 1950, 1960 na 1970.

 

Upande mmoja wa shilingi unaeleza kuhusu namna chama kilivyo tayari kusamehe makada wake wanaokwenda kinyume na msimamo wa chama lakini upande mwingine unatoa picha ya chama kisichoamini katika kile ambacho vyama kama FRELIMO viliamini – kwa lugha ya Kireno, kama alinhar correcta “mstari sahihi wa chama”.

 

Kuhusu ushawishi wa mitandaoni

 

Waandishi mahiri wa masuala ya siasa kama Rory Stewart wanaeleza kuwa nguvu hasa ya mitandao ya kijamii kwenye siasa ilianza kuonekana baada ya mwaka 2010, hasa kuanzia mwaka 2012 na hakuna ushahidi mzuri kuhusu hilo kama ile Arab Spring ilipoanza mwaka 2013.

 

Kwenye hotuba yake ya kwanza tangu apewe Ukatibu Mkuu, Nchimbi alisema wadhifa wa Katibu Mkuu wa CCM tangu mwaka 1982 unahitaji mtu mwenye sifa mbili; mwanasiasa na mtendaji. Lakini, kama ilivyosema taasisi ya Democracy in Africa miaka mitatu iliyopita, mitandao ya kijamii ni sehemu muhimu ya siasa za Afrika.

 

Katika wanasiasa wote wa umri wake, Nchimbi ndiye pekee ambaye hayupo katika mitandao ya kijamii. Inawezekana ana akaunti mitandaoni lakini hana umaarufu wa kiwango cha akina Mwigulu Nchemba, Ummy Mwalimu, January Makamba, Zitto Kabwe, Nape Nnauye na wengine.

 

Mtu anaweza kusema John Magufuli pia hakuwa kwenye mitandao ya kijamii lakini bado alikuwa na ushawishi mkubwa kwenye jamii. Lakini Magufuli alikuwa maarufu kwa sababu alijua kutumia vyombo vya habari vilivyokuwepo na kufanya mambo yaliyomfanya kuwa maarufu.

 

Changamoto ya Nchimbi ni kuwa ana nguvu na ushawishi wa kutosha ndani ya chama chake lakini haulingani na ule alionao nje ya chama. Na kwa sababu Tanzania ni taifa lenye vijana wengi wanaotumia mitandao ya kijamii ambako mbunge huyu wa zamani wa Songea Mjini haonekani, si mengi yanajulikana kumhusu.

 

Katika eneo hili la Afrika, chama cha siasa chenye hadhi na ushawishi kinachofanana na CCM pengine ni ANC cha Afrika Kusini. Katika miaka ya karibuni, kimekuwa na Makatibu wakuu wawili; Gwede Mantashe na Fikile Mbalula. Ukiingia kwenye mtandao wa twitter, Gwede ana wafuasi zaidi ya laki tano lakini huyu wa sasa, Fikile, ana wafuasi milioni tatu.

 

Kuwa na Katibu Mkuu wa aina ya Nchimbi ambaye hajulikani sana mitandaoni ni jambo la kama kwenye siasa za kisasa. Inawezekana kwamba upande wa pili wa kamari hii ni kwamba chama kinajua kwamba faida zake nyingine zinazidi faida ya kuwa na umashuhuri mitandaoni.

 

Nyongeza

 

Swali ambalo nimeulizwa na rafiki zangu tangu Nchimbi atangazwe ni kuwa je kwa nafasi hii mpya, mbunge huyu za zamani wa Songea Mjini ana nafasi zaidi ya kuwa mrithi wa Rais Samia  mwaka 2030 – endapo atashinda uchaguzi wa mwaka 2025, au la?

 

Nina majibu mawili kuhusu swali hili. Jibu la kwanza ni kwamba mwaka 2030 ni mbali sana na mambo mengi yanaweza kutokea hapa katikati. Hatuwezi hata kujihakikishia kwamba wote wanaotajwa sasa watakuwa hai wakati huo.

 

Lakini la pili, na la muhimu zaidi, linahusu mwaka 2027. CCM kitafanya uchaguzi wake wa ndani wakati huo. Kama Nchimbi ataendelea kuwa Katibu Mkuu baada ya hapo, maana yake ni kwamba hataweza kuwa mgombea urais wa chama. Huwezi kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama na wakati huohuo mgombea.

 

Lakini, kama Nchimbi ataacha kuwa Katibu Mkuu wa CCM na kumwachia mwengine wajibu huo, nipigie wakati huo kuniuliza. In Sha Allah.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza. Anapatikana kupitia email: ekamwaga57@gmail.com

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *