Picha kwa Hisani ya gazeti la serikali la Daily News.
KITABIA, nafasi ya Makamu wa Rais katika nchi inayofuata mfumo wa uchaguzi wa Kimarekani – kama ilivyo kwa sehemu hapa kwetu Tanzania, ni nafasi iliyopoa na inayoboa.
Enzi nikiwa ripota, mara mbili niliwahi kutumwa na mhariri wangu kwenda kuandika kuhusu mkutano wa mmoja wa Makamu wa Rais waliopita lakini nikaomba kupangiwa sehemu nyingine. Nilijua hakutakuwa na stori. Kwa kawaida, Makamu wa Rais huwa ‘hasemi’ kitu.
Kuna sifa nyingine ambayo huwa haisemwi hadharani kuhusu nafasi ya Makamu wa Rais; sifa hiyo ni kwamba kwa vyovyote vile hatakiwi kung’ara kuliko bosi wake. Umaarufu wa Makamu wa Rais kumzidi bosi wake ni jambo linaloweza kuleta migongano katika taasisi zinazolinda Urais.
Sifa za mtu anayetakiwa kuwa Rais ndizo sifa hizo hizo zinazotakiwa kwa mtu anayewania kwa mgombea mwenza. Hilo liliwekwa hivyo kikatiba ikijulikana kwamba huyu ni mtu anayeweza kuwa Rais endapo jambo lolote litasababisha aliye madarakani kushindwa kuendelea na wadhifa wake.
Sifa ya ziada ya Makamu Rais wa Tanzania na ambayo haipo Marekani ni kwamba walau hapa kwetu inajulikana kuwa kama Rais atatoka upande mmoja wa Muungano, ni lazima Makamu atoke upande wa pili. Kama Rais anatoka Tanzania Bara, Makamu ni lazima atoke Zanzibar na kinyume chake.
Pengine hiyo ndiyo sifa namba moja na isiyobadilika katika mfumo wa demokrasia yetu linapokuja suala la Makamu wa Rais. Linapokuja suala la sifa binafsi za waliowahi kushika nafasi hiyo, wanasiasa watano waliowahi kuwa Makamu wa Rais hawafanani kitabia, kihistoria na kwa ushawishi.
Katika mazungumzo binafsi ambayo nimewahi kufanya na baadhi ya viongozi kuhusu maisha ya Makamu wa Kwanza wa Rais baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Dk. Omar Ali Juma, kuna jambo moja ambalo nililibaini.
Ni kama vile waliotaka Dk. Omar awe Makamu, walifikiri ni mtu ambaye angeweza kumrithi Benjamin Mkapa mara baada ya kumaliza muda wake wa uongozi. Kwao, nafasi ya Makamu ilikuwa ni kama maandalizi kwa mtu ambaye baadaye angekuja kuwa Rais. Hilo lingesaidia vitu viwili; Mosi mwendelezo wa sera za mtangulizi na pili kupokezana kwa marais baina ya Bara na Zanzibar.
Dk. Omar alifariki dunia ghafla Julai, 2001. Alikuwa katika awamu ya pili na Mkapa akiwa ameanza kumhusisha katika masuala ya kutafuta amani katika Nchi za Maziwa Makuu. Uelewa wa masuala ya diplomasia ilikuwa moja ya vigezo kwa aliyetaka kuwa Rais kupitia CCM.
Makamu huyu ndiye mwanasiasa aliyekuwa na wasifu mkubwa zaidi kisiasa kulinganisha na wenzake wengine waliokuja kushika wadhifa huo baadaye. Kabla ya kuwa Makamu, alikuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar kwenye utawala wa Rais Salmin Amour.
Alikuwa mwanasiasa anayekubalika na karibu makundi yote kwenye siasa za Zanzibar, akiwa anatoka Pemba ilikokuwa ngome ya kisiasa ya upinzani, msomi wa kiwango cha Shahada ya Uzamivu (PhD) kwenye Tiba ya Wanyama na aliyeaminiwa na Rais Mkapa na vyombo vyake.
Yeye alikuwa tofauti na mbadala wake, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye kutangazwa kwake kuliwashangaza wengi. Ni wachache walikuwa wakimfahamu Waziri huyo wa Afya wa zamani wa Zanzibar. Ingawa alikuwa Mpemba kama mtangulizi wake, hawakuwa daraja moja kisiasa.
Kwa nini Mkapa alimtaka Shein? Baadhi ya viongozi waliozungumza nami huko nyuma walinieleza kwamba kwanza Rais huyo wa tatu wa Tanzania aliyefariki mwaka 2020 alitaka nafasi hiyo ibaki Pemba kwa sababu ya muktadha wa kisiasa wa wakati ule.
Vurugu zilizosababishwa na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 zilisababisha mauaji na baadhi ya Wazanzibari – wengi wao Wapemba, kukimbilia ukimbizini. Dk. Omar alikuwa kama alama ya Wapemba serikalini, na kumpa nafasi mtu kutoka Unguja ingekuwa sawa na kuwatelekeza.
Ndani ya CCM Zanzibar mwaka 2001, mwanasiasa aliyekuwa na utulivu, usomi, mwenye asili ya Pemba na haiba ya kufanya kazi kama Makamu wa Rais wa Mkapa alikuwa Shein na hiyo ndiyo sababu iliyompandisha zaidi na kumpa nafasi hiyo.
Wakati Shein alipoenda kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) mwaka 2010, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilimpa nafasi Dk. Mohamed Ghalib Bilal, kuwa mgombea mwenza wa Rais Jakaya Kikwete – baada ya Uchaguzi Mkuu akawa Makamu wa Rais wa Tanzania.
Baada ya Shein kuwa mwanasiasa wa kwanza mwenye asili ya Pemba kuwa Rais wa SMZ – Kikwete hakuwa na changamoto alizokuwa nazo Mkapa mwaka 2001. Mwaka 2010, Bilal alikuwa mwanasiasa mwandamizi kwenye siasa za Zanzibar na uteuzi wake ulipunguza joto la kisiasa visiwani.
Uteuzi wa Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wa John Magufuli mwaka 2015 haukutarajiwa na wengi. Katika baadhi ya hotuba alizowahi kutoa hadharani, Magufuli mwenyewe alitamka kuwa chaguo lake la awali lilikuwa ni Dk. Hussein Mwinyi – Rais wa sasa wa SMZ.
Hata hivyo, Samia alikuwa na kete mbili kisiasa kumzidi Mwinyi kwa mujibu wa CCM ya mwaka 2015. Mosi, kisiasa alikuwa mwandamizi – akiwa amewahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kwa muda mrefu zaidi na mwenye mizizi zaidi kisiasa Zanzibar.
Pili, mazingira ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 yalimpa Samia faida kumzidi Mwinyi. Katika mchuano mzito baina ya Edward Lowassa wa Chadema iliyokuwa kinara wa upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), mgombea mwenza mwanamke alikuwa na uzito kuliko mwanamume.
Ikumbukwe kwamba sifa kuu kati ya Lowassa na Magufuli ilikuwa ni viongozi wenye “maamuzi magumu” na mgombea mwenza alihitajika mtu ambaye ni kinyume cha tabia hizo na mwanamke wa sifa hiyo angeongeza kura kutoka kundi hilo.
Makamu wa Rais wa sasa, Dk. Philip Isidor Mpango, ndiye wa kwanza kushika wadhifa huo kutoka Tanzania Bara. Uteuzi wake ulifuatia kifo cha ghafla cha Rais Magufuli mnamo Machi mwaka 2021.
Kabla ya uteuzi wake huo, si wengi waliokuwa wakilitaja jina lake miongoni mwa waliopewa nafasi kubwa. Dk. Mpango ni mmoja wa wachumi wa daraja la juu nchini Tanzania lakini kisiasa ni mwanasiasa mchanga – akigombea ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 2020.
Itaendelea wiki ijayo…….