Utamjuaje Magufuli, Netanyahu au AMLO?

AKIANDIKA katika gazeti maarufu nchini Israel la Haaretz hivi karibuni, mwanahistoria maarufu, Yuval Harari, alieleza kwamba katika historia, kuna mapinduzi ya namna mbili; yale ya kutoka juu na mengine ya kutoka chini.

 

Mapinduzi ya kutokea chini ni yale ambayo yamezoeleka zaidi. Mwanajeshi anaongoza kikosi cha askari wenzake kupindua serikali iliyoko madarakani. Au wananchi wanachukua silaha dhidi ya serikali dhalimu na kuiondosha madarakani.

 

Barani Afrika, Asia na Amerika Kusini hili lilikuwa jambo la kawaida katika karne iliyopita. Wananchi wanaamka asubuhi au usiku wa manane na kusikia sauti ya askari wanayemsikia kwa mara ya kwanza akiwaambia serikali imebadilika.

 

Mapinduzi ya aina ya pili – yale ya kutokea juu, hayajazoeleka sana lakini ndiyo yameanza kuwa ya kawaida katika siku za karibuni. Haya hutokea pale ambapo serikali iliyoingia kihalali madarakani, huanza mamlaka yake kufanya mapinduzi kwenye taasisi za umma.

Hiki ndicho, kwa maneno ya Harari, kinachotokea Israel hivi sasa. Mara baada ya kuingia madarakani kupitia Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo, serikali ya Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, inataka kufanya mabadiliko ya kisheria yaliyoanza kupingwa na wananchi.

 

Kwa mfano, Netanyahu anataka kufanya mabadiliko yatakayolipa Bunge la Israel uwezo wa kutengua uamuzi uliofanywa na Mahakama ya Juu ya taifa hilo. Washabiki wake wanadai wanataka watu waliopewa dhamana kwa njia ya kura ndiyo wawe waamuzi wa mwisho.

 

Kwamba kwa sababu majaji hawapigiwi kura na wananchi, hawawezi kuwa wa mwisho wa kuamua mambo ya wananchi. Wanaompinga wanajua kwamba lengo la Netanyahu ni kutaka kutawala bila kuwekewa mipaka na taasisi nyingine.

 

Kwa muda mrefu, sifa kubwa ya mfumo wa kidemokrasia ya kiliberali ilikuwa ni uwezo wake wa kuweka vyombo vinavyoweka ukomo wa mamlaka ya walio madarakani.

 

Kwamba kutakuwa na Serikali, Bunge na Mahakama. Kila kimoja kitakuwa kinafanya mambo yake kwa mujibu wa mipaka yake. Na hata serikalini, kunakuwa na taasisi za uwajibikaji ambazo hazitakiwi kuingiliwa.

Anachofanya Netanyahu sasa si kigeni. Marais wengine wawili duniani; hayati John Magufuli wa Tanzania na Andres Manuel Lopez Obrador (AMLO) wa Mexico wamepita katika njia hiyo wakiwa madarakani.

 

OMLO na Mexico yake

 

AMLO ni mwanasiasa mkongwe ambaye chama chake cha Morena kilishinda uchaguzi wa mwaka 2018 na anatarajiwa kukaa madarakani hadi mwaka 2024. Ni aina ya wanasiasa wanaojitambulisha kama watetezi wa watu wa hali ya chini na ndiko alikojijengea umaarufu.

 

Chama tawala cha Partido Nacional Revolucionario (PRI) kiliitawala Mexico kwa takribani miaka 70 hadi kiliposhindwa kwa mara ya kwanza mwaka 2000. Minyukano ndani ya chama hicho ndiyo ilimpa fursa AMLO ya kuanzisha chama kinachotawala nchi hiyo sasa.

 

Hata hivyo, kwa muda mrefu, ushindi wa PRI ulikuwa ukielezwa kuwa wa kubebwa na viongozi waliokuja baada ya uchaguzi wa mwaka 2000 walihakikisha Tume ya Uchaguzi ya Mexico inakuwa imara kiasi kwamba tafiti za miaka ya karibuni zinaitaja kama ya pili kwa kuheshimika baada ya Jeshi la Mexico.

 

Baada ya kuingia madarakani, kazi ya kwanza ya AMLO ilikuwa ni kupunguza bajeti ya tume hiyo ili kuikata makali, kubana asasi za kiraia na ‘kuwashughulikia’ wale wote anaoona hawaungi mkono utawala wake.

 

Jambo kubwa zaidi alilofanya ni kuitumia Mahakama kama silaha dhidi ya wapinzani wake – wakifikishwa mahakamani na kufunguliwa mashitaka yasiyo na kichwa wala miguu.

 

Magufuli na Tanzania yake

 

Rais Magufuli alikuwa Rais wa Tanzania kwa muda mfupi wa miaka sita tu kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2021. Maneno yake kwenye majukwaa ya kisiasa yalikuwa ni kujitanabaisha kama mtetezi wa wanyonge na mwenye kufuata sheria.

 

Hata hivyo, wakati kulipoanza tuhuma za matumizi ya fedha za serikali bila kufuata utaratibu ikiwemo ununuzi wa ndege bila kupitia Bunge, Magufuli aliamua kufunga midomo wale ambao wangeweza kupiga kelele.

 

Mojawapo ya hatua zake za awali zake za awali ilikuwa ni kupunguza bajeti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa takribani shilingi bilioni nane kutoka shilingi bilioni 69 mpaka bilioni 61.

 

Kama Watanzania walivyosikia katika siku za karibuni, Mahakama – kama Mexico, zilitumika kama silaha dhidi ya wapinzani wake. Zipo kesi kadhaa zilizofunguliwa dhidi ya watu walioonekana kama wapinzani wa utawala wake.

 

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, baadhi ya watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), walisikika hadharani wakitoa matamshi yaliyoashiria upendeleo wa waziwazi dhidi ya chama tawala.

 

Changamoto ya demokrasia ya kilberali

 

Ni rahisi kumwona Magufuli, Netanyahu au AMLO kama ni watu pekee kwenye dunia yao lakini ukweli ni kwamba wao ni zao la siasa za kidunia zinazotawala sasa.

 

Ningeweza kuacha kutumia mfano wa Magufuli na AMLO na nikatumia mifano ya Narendra Modi wa India au Viktor Orban wa Hungary na bado ungeona mwelekeo huohuo.

 

Dunia ya sasa ina mifano mingi ya viongozi ambao ingawa waliingia madarakani kwa kufuata sheria, wanatumia vyeo vyao kuharibu mfumo uliokuwepo na ni kama vile wanafanya mapinduzi.

 

Tatizo ni nini? Kwa mujibu wa wasomi mbalimbali wa sayansi ya siasa, inaonekana mfumo unaotamba sasa wa demokrasia ya kiliberali umeshindwa kutatua changamoto nyingi zinazowakabili masikini duniani.

 

Maneno yanayoanza kutamalaki sasa ni kwamba demokrasia imeshindwa kuweka chakula mezani kwa watu. Na kama demokrasia imeshindwa kutatua kero za wananchi, kiu ya kuwa na kiongozi anayeweza kutatua kero hizo hata kwa kufuata mifumo ya kidikteta imeanza kuongezeka.

 

Swali kubwa ambalo wana demokrasia ya kisasa na viongozi waliopo wanatakiwa kujiuliza ni kuhusu kwa vipi wataendeleza mfumo huu huku wakijibu changamoto za wananchi.

 

Utawajuaje?

 

Kwenye kuzuia aina ya viongozi wenye kutaka kufanya mapinduzi kutokea juu, kuna namna kadhaa za kufanya. Zipo namna za kuzuia kupitia mifumo na nyingine kuhusu wagombea wenyewe.

Kwenye mifumo, mfano mzuri zaidi uko kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM). Inajulikana kuwa chama hicho kikongwe zaidi hapa nchini kimejiwekea sifa takribani 13 kwa ajili ya yeyote anayetaka kuwa Rais wa Tanzania kupitia chama hicho.

 

Inajulikana kwamba Magufuli hakuwa na baadhi ya vigezo vinavyotakiwa – kikiwemo kile cha upeo (exposure) kwenye masuala ya kimataifa, lakini chama hicho kiliamua kumpa nafasi hiyo kwa sababu ya mazingira yaliyokuwepo wakati huo.

 

Hivyo Magufuli akawa mgombea mwenye majibu ya nyakati husika – kama ilivyokuwa kwa Modi, Orban na AMLO kwenye nchi zao ambao kuingia kwao madarakani kulikuwa kwenye nyakati zinazofanana.

 

Kama CCM ingeamua kufuata taratibu ilizojiwekea na kuchagua mtu mwenye vigezo ilivyoviweka badala ya yule waliyeona atawafaa kwenye uchaguzi, huenda historia ya Tanzania leo isingekuwa hii tuliyonayo.

 

Tatizo la kumchagua mtu kwa sababu ya kushinda uchaguzi ndiyo tatizo la kwenye hekaya za Esopo za miaka mingi nyuma. Kwenye ule mkasa wa farasi na mpandaji, Esopo alieleza namna alivyoitumia shida ya muda mfupi ya farasi kumpanda kwenye maisha yake yote duniani.

Mgombea yeyote akijua kwamba mlimpa nafasi kwa vile bila yeye msingepata kitu, atataka uhusiano baina yake na wale waliompa nafasi ubaki kuwa namna hiyo. Na ndiyo sababu ni muhimu vyama vikaweka sifa mahususi kwa watu wanaotakiwa kuwa viongozi wa juu.

 

Mfumo pia unaweza kujitazama upya. Kwa mfano, kwa nini mfumo huu wa demokrasia ya kiliberali unaweka nje maelfu kwa maelfu ya watu nje ya mfumo rasmi wa ajira, fursa za kiuchumi na kuwaongezea walichonacho?

 

Jambo ambalo tumejifunza katika kipindi cha miaka 20 iliyopita ni kwamba kama demokrasia imeshindwa kuweka chakula mezani na fursa sawa kwa wote – wananchi watamwamini yeyote atakayewaahidi pepo hapa duniani.

 

Unapokuwa na kiongozi kama Modi ambaye kwa vigezo vyote vya kidemokrasia anafeli lakini India inaanza kupata mafanikio kiuchumi – ni muhimu kutazama kama kuna kitu kinaweza kufanyika ili demokrasia imaanishe mafanikio kwa wote.

 

Changamoto kubwa kabisa ya kizazi cha sasa cha viongozi ni kutazama ni namna gani demokrasia yetu inatatua shida za wananchi hasa wale wa hali ya chini. Kumsifia mtu kwa kuwa mwanademokrasia katika nchi yenye njaa na matumaini hafifu ni jambo lisilo na afya.

 

Kuondoa mifumo, ni muhimu kuwaangalia wale wanaotaka kuwania nafasi za juu kwa jicho la kidadisi. Kwa mfano, kwa namna ilivyo sasa, mtu yeyote anayewania nafasi za juu na kutamka mara kwa mara maneno kama kujitoa sadaka, kutetea wanyonge na maadili mema ya jamii ni mgombea wa kutazamwa kwa jicho la karibu.

 

Sifa moja kubwa ambayo tumeiona kwa wanasiasa wa dizaini ya akina Magufuli, AMLO na Orban ni kutengeneza makundi baina ya wao na sisi au wenye nacho na wasio nacho. Wafuasi wakishalewa na ubaguzi huo, kiongozi hupata fursa ya kuwatweza wengine vile apendavyo.